February 3, 2008

001-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Utangulizi Wa Mfasiri

Utangulizi Wa Mfasiri


بسم الله الرحمن الرحيم

Hakika shukurani ni Zake Allaah (سبحانه وتعالى), tunamshukuru Yeye, na kumtaka msaada, na tunamuomba Yeye msamaha. Tunamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Atulinde na shari za nafsi zetu na ubaya wa matendo yetu. Anayeongozwa na Allaah (سبحانه وتعالى) hakuna wa kumpoteza, na anayepotezwa na Allaah (سبحانه وتعالى) basi hakuna wa kumuongoza.

Na nashuhudia kuwa hakuna apasaye kuabudiwa ila Allaah (سبحانه وتعالى), Ni Mmoja tu Asiye na mshirika. Na nashuhudia kuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni mja Wake na ni Mjumbe Wake. Swalah na Salaam za Allaah zimshukie yeye, jamaa zake, Swahaba zake, na wote waliotangulia kwa wema hadi siku ya mwisho.

Ama ba’ad,
Namshukuru tena Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kuniwezesha kukamilisha kazi hii kwa Lugha ya Kiswahili, kazi ambayo naamini sana kuwa itawanufaisha sana Waislam wazungumzaji wa lugha hii na kuweza kuwasaidia kupata mafunzo sahihi ya 'Ibaadah hii adhimu ambayo itakuwa ni jambo la kwanza kabisa kwa mja kuulizwa kwalo siku ya Hesabu.

Umuhimu wa kitabu hiki ni mkubwa sana, haswa kwa kuwa ni kitabu kilichoelezea ‘Ibaadah hii ya Swalah kwa mapana na marefu na kwa dalili sahihi zilizothibiti kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم). Ni kitabu kwa mwenye kutaka kujua ilivyokuwa Swalah ya kipenzi chetu (صلى الله عليه وآله وسلم) kama alivyosema: ((Swalini kama mlivyoniona nikiswali)) [Al-Bukhaariy]. Basi anapaswa kuwa nacho kwenye nyumba yake.

Hiki ni kitabu cha Swalah kilichoenea na kuuzika kwa wingi sana labda kuliko vitabu vyote vya Swalah vilivyowahi kuandikwa. Ni kitabu chenye mauzo makubwa katika nchi za Kiarabu kwa mujibu wa wachapishaji wa kitabu hicho. Hali kadhalika kimetafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kimeuzwa na kinaendelea kuuzika kwa wingi katika nchi za Ulaya na haswa Uingereza. Nimeonelea manufaa hayo yasiwaenee tu wenye kuzungumza Kiarabu na Kiingereza pekee, bali na jamii yetu ya wazungumzao Kiswahili.

Swalah ina fadhila kubwa sana, hivyo kukosa kuswali ni kosa kubwa. Swalah ni 'amali ya kwanza itakayokaguliwa Siku ya Qiyaamah na ndio ufunguo wa Pepo. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
((’Amali ya mwanzo atakayoulizwa Muislamu Siku ya Qiyaamah kuwa kaitekeleza–na kaitekeleza vilivyo–ni Swalah. Ikiwa aliitekeleza vilivyo basi kunatarajiwa atafaulu. Ikiwa hakuitekeleza au kaitekeleza, lakini sivyo ndivyo, basi itatazamwa Swalah za Sunnah, kama alizitekeleza vilivyo. Ama ikiwa hana hata Sunnah au kaitekeleza sivyo ndivyo, basi keshapata khasara)) [Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].
Amesema tena (صلى الله عليه وآله وسلم):
((Funguo za kufungulia milango ya Peponi ni Swalah)) [Muslim].

Ubaya wa kuacha Swalah ni mkubwa sana kwani Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلاَةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا  
((Lakini wakaja baada yao walio wabaya, wakaacha Swalah, na wakafuata matamanio. Basi watakuja kuta adhabu ya moto)) [19: 59].

Na kadhalika Anasema tena Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutaja habari za wasioswali pindi watakapoulizwa sababu yao ya kuwepo motoni:

مَا سَلَكَكُمْ فِي سَقَرَ  . قَالُوا لَمْ نَكُ مِنَ الْمُصَلِّينَ  

((Ni nini kilichokupelekeni motoni? Waseme: Hatukuwa miongoni waliokuwa wakiswali))  [74: 42 -43].

Na Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
((Kizuizi kilichoko baina ya mtu na ukafiri ni Swalah)) [Muslim].

Kadhalika akaeleza ubaya wa mtu kutokuswali na kumfananisha na kafiri:
((Tofauti baina yetu Waislamu na wasio Waislamu ni Swalah)) [Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah].

Baada ya kujua masuala hayo muhimu kutoka katika Kitaab na Sunnah, ndivyo vilevile tutaona umuhimu wa kuijua ‘Ibaadah hiyo vilivyo ili tuweze kuitekeleza ipasavyo. Na kwa mintarafu hiyo, tutaona kuna ulazima wa kupata mafunzo hayo kutoka katika chanzo kilichokamilika kwa dalili thaabit kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba zake. Na ndio nikakichagua kitabu hiki kukitafsiri ili kumuwezesha Muislam mwenye kusoma Kiswahili anufaike na aweze kuinoa na kuiboresha Swalah yake ili aweze kufikia makusudio yaliyotajwa katika Aayah na Hadiyth mbalimbali nilizotanguliza hapo juu, na pia ili aweze kuepukana na sifa na adhabu nilizotangulia kutaja.

Nisiwe mbakhili wa fadhila na mchache wa shukurani kwa wale waliotoa mchango wao mkubwa kabisa katika kazi hii tukufu. Nawaombea wote malipo kamili kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) yanayotokana na kazi hii, bila kukosa thawaab za wale wote watakaonufaika kutokana na ‘amali hii.

Shukurani zangu za dhati na du’aa zangu ni kwa dada yangu Ummu Iyyaad ambaye kwa juhudi zake zisizo mithali kazi hii imeweza kukamilika na pia ushirikiano wake mkuu wa dhati. Pia Al-Akh 'Abdullaah Mu'awiyyah na Al-Akh Fayswal ‘Abdul-‘Aziyz, kwa kujitolea wakati mkubwa kuipitia kazi hii. Pamoja na ndugu yangu mpenzi Sa’iyd Baawaziyr kwa kupitia vilevile na kuchangia maoni mbalimbali. Bila kusahau mchango mkubwa wa upitiaji na mawazo wa Al-Akh Muhammad Faraj As-Sa’ay. Hali kadhalika Al-Ukht Ummu ‘Abdir-Rahmaan kwa mchango wake.

Na shukurani nyingi kwa tashji’i kubwa na uvumilivu wa hali ya juu kutoka kwa mke wangu Ummu ‘Abdillaah ambaye amenisaidia kwa kiasi kikubwa na amenipa fursa ya kutosha ya kushughulika na majukumu haya matukufu bila kuchoshwa wala kuvunjika moyo. Namuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Amlipe yeye na wote duniani na Akhera. Aamiyn


Abu ‘Abdillaah Muhammad Baawaziyr
Swafar 1429 H – Februari 2008 M

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only