FIQHI : MLANGO WA UDHU

Nini Udhu?

Kilugha udhu ni unadhifu, au kujinadhifisha; Kisharia ni kutumia maji kwenye viungo maalum kwa kuanzia nia na kuwa khaasa kwa viungo hivyo.

Kuthibiti Kuamrishwa Udhu

Udhu umeamarishwa kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
 
“Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundo, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundo.........". (Al Maida : 6).

Shuruti, Fardhi, Sunna na Yenye Kuba'tilisha Udhu

Udhu una shuruti zake, fardhi zake, suna zake, na una yale yenye kuba'tlisha udhu.

Shuruti za Udhu

Shuruti za kusihi udhu ni kuwa Muislam, mukalaf, yaani baalegh na mwenye akili timam, maji yawe yenye kujuzu ku'tahirishia, kutokuwepo juu ya sehemu ya kiungo cha udhu kitu kinachozuia maji kufika kwenye ngozi ya sehemu hio ya kiwiliwili, na kutokuwa ndani ya hedhi au nifasi.
Vilevile kwa yule mwenye maradhi kama vile damu ya (hedhi) ya kudumu, kikojozi, au kujamba, wao inashurutishwa kuingia wakati wa ile Sala wanayotaka kuisali ndio watie udhu, sio kabla yake. Hivi ni kwa sababu udhu wa watu hawa ni udhu wa dharura, si udhu wa kawaida; na kusihi udhu wa dharura sharti yake ni kufika wakati wa lile la dharura nalo ni wakati wa ile Sala anayotaka kuisali.

Fardhi za Udhu

Fardhi za udhu ni sita:
Ya Kwanza, kutia nia; hivi ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:     “Hakika (kusihi) ibada ni kwa (kupatikana) nia”. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Wakati wa kutia nia ni pale unapoosha sehemu ya mwanzo ya uso huku ukikusudia kuondoa hadathi ndogo  au kujuzu kusali,  au kutekeleza fardhi ya udhu .
Ya Pili, kuosha uso; kulingana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “……..osheni nyuso zenu,” (Al Maaida : 6).
Uso kwa urefu ni tangu maoteo ya nywele mpaka kidevu, na kwa upana ni tangu sikio mpaka sikio. Kuosha uso ni kuosha kila sehemu ya uso pamoja na nywele ziliomo pembezoni mwa uso na kidevuni. Ikiwa ni chache hizo nywele yaani inabainika ngozi, basi ni lazima kufikisha maji mpaka kwenye ngozi, ama ikiwa ni nyingi basi hutosha kwa kupaka maji juu yake.
Ya Tatu, kuosha mikono miwili pamoja na vifundo viwili; kulingana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “..na mikono yenu mpaka vifundo…” (Al Maaida : 6). Neno mpaka maana yake ni pamoja na, yaani kukosha mikono pamoja na vifundo vya mikono. Hivi inathibiti kwa qauli ya Jabir r.a. kuwa amemuona Mtume wetu Mpenzi s.a.w. anazungushia maji juu ya vifundo vyake vya mikono. (Imepokewa na Darqu’tni na Al Baihaqy).
Na katika Hadithi yao walioipokea kutoka kwa Jabir vilevile kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alizungushia maji juu ya vifundo vyake vya mikono na akasema:
  “Huu ndio udhu, hakubali Mwenyezi Mungu Mtukufu Sala ila kwa udhu kama huu”.
Na ni lazima ili kutimia udhu kufikisha maji katika unywele na ngozi ya kiungo cha udhu. Ikiwa kwenye kucha kuna uchafu au juu ya ngozi kuna kitu kinachozuia maji kufika juu ya ngozi, kama vile lami, mafuta, utomvu, basi udhu hausihi, kwa hivyo Sala yake haisihi.
Ya Nne, kupaka maji kichwani (sehemu ya kichwa); kulingana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “. na mpake vichwa vyenu…” (Al Maaida : 6).
Kupaka maji kichwani huwa kwa maji mengi au kidogo, hivi ni kutokana na Hadithi ya Al Mughaira r.a. kwamba: “Mtume wetu Mpenzi s.a.w. ametia udhu na akapaka maji sehemu ya juu ya kipaji cha uso na juu ya kilemba chake na juu ya khufaini*”. (Imepokewa na Muslim).
Lau kama ni fardhi kupaka maji kichwa chote, basi Mtume wetu Mpenzi .s.a.w. asingalipaka maji juu ya sehemu ya kipaji cha uso tu (juu ya nywele).
Ya Tano, kuwosha miguu miwili pamoja na vifundo vyake; kulingana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: …na osheni miguu yenu mpaka vifundo…". (Al Maida : 6).
Ya Sita, kufululiza na kufuatiza; haya yamethibitika kutokana na hii Aya iliofunza juu ya udhu - Al Maida : 6, kwani “wau”  , yaani "na" iliomo kwenye Aya hii ni yenye kueleza juu ya mpangilizio. Pia haikupokewa kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amewahi kutia udhu bila ya mpangilizio kama ulivyokuja kwenye Aya hii.
Vilevile Mtume wetu mpenzi s.a.w. alisema baada ya kukamilisha kutia udhu maneno yenye maana kama hivi: “Huu ndio udhu, hakubali Mwenyezi Mungu Mtukufu Sala ila kwa udhu kama huu”. (Imehadithiwa na Al Bukhari).
Hadithi hii imetangulia kutajwa hapo juu.
Vilevile ameeleza Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  “Anzieni kwa alivyoanzia Mwenyezi Mungu Mtukufu”. (Imehadithiwa na Al Nissaai).

Sunna za Udhu

Sunna za udhu ni kumi na moja:
Ya Kwanza, kusomaa Bismillahi  wakati wa kuanza kutia udhu; haya ni kwa yaliopokewa na Al Baihaqy r.a. kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alitia mkono wake kwenye chombo chenye maji na akawaambia Masahaba zake r.a.:    “Tieni udhu kwa Bismillahi.
Na kwa Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
   “Kila jambo lenye faida lisipoanzwa kwa Bismillahi basi hilo lina upugufu na halina barka”.
Ya Pili, kuosha viganja viwili vya mikono kabla ya kuvichovya kwenye chombo chenye maji ya kutilia udhu, hivi ndivyo ilivyopokewa kuwa hivi ndivyo namna ya kutia udhu Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Vilevile ndivyo ilivyopokewa kutoka kwa Ausi bin Ausi Al Thaqafi:
      “Nimemuona Mtume wetu Mpenzi s.a.w. wakati anatia udhu anakosha viganja vyake viwili vya mikono mara tatu". (Imehadithiwa na Ahmad).
Vilevile imepokewa kutoka kwa Sayyidna Othaman r.a. kuwa kasema:
   “Akamiminia (maji) juu ya viganja vyake mara tatu akivikosha”.
Na haya yamethibiti kutokana na Masahaba mbali mbali r.a.
Ya Tatu Na Nne, kusukutua na kuvutia maji puwani; hivi ni kama ilivyoonekana akifanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w., na kwa qauli yake Mtume wetu Mpenzi s.a.w. yenye maneno na maana kama hivi:  (mambo) kumi ni katika suna”, ikahisabiwa miongoni mwa kumi hayo ni kusukutuwa na kuvutia maji puwani. (Imepokewa na Muslim).
Kutanguliza kusukutuwa kabla ya kuvutia maji puwani ni sharti ya kupatikana suna hii. Inapendekezwa kufanya mno hivi kwa asiekuwa kafunga, ama aliefunga ni karaha kwake kufanya hivi, (kuogopewa yasimponyoke maji yakaingia tumboni, akafungua).
Ya Tano, kupaka maji kichwa chote; hivi ni kama ilivyoonekana akifanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w., na pia kuepukana na tafauti za rai. Na ni suna kuanza kwenye kipaji cha uso na kuipeleka mikono miwili mpaka mwisho wa kichwa na kuirejesha mpaka ulipoanzia. Imepokewa hivi kutoka kwa Abdulla bin Zaid r.a. akieleza namna ya kutia udhu kwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. (Imehadithiwa na Jamaa wapokeaji Hadithi).
Ya Sita, kuosha masikio nje na ndani kwa maji mepya. Ameeleza Bwana Abdulla bin Zaid r.a. kuwa amemuona Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akitia udhu, akachukuwa maji mepya mbali na yale aliopangusia kichwa akaoshea masiakio. (Imehadithiwa na Al Hakim na Al Baihaqy).
Hufanya hivi kuosha masikio kwa kutia maji mepya mikononi kisha kutia vidole vya shahada masikioni na vidole vya gumba nje ya masikio na kuvizungusha polepole.
Ya Saba, kuesua (kupapachua) ndevu nyingi, (ndevu nyingi ni zile ambazo ngozi ya kidevu haionekani). Haya kama ilivyopokewa kutoka kwa Ibni 'Abbas r.a. ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alikuwa anapotia udhu hupapachua ndevu zake kwa vidole vyake. (Imehadithiwa na Ibnu Majah).
Na imepokewa kutoka kwa Ibni 'Abbas vilevile kuwa: “Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alikuwa akipapachua ndevu zake”.
Amesema Al Bukhari: “Hivi ni sahihi zaidi ilivyo kwenye mlango wa udhu na Hadithi ya Ibni 'Abbas r.a. kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alikuwa anapotia udhu hupapachua ndevu zake kwa vidole vyake kwa kuanzia chini ya kidevu. (Imehadithiwa na Ibnu Maajah).
Ya Nane, kuesua (kupapachua) vidole vya viganja pamoja na vidole vya miguu. Haya ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  “Ukitia udhu esua (papachua) vidole vyako vya mikono na miguu”. (Imehadithiwa na Ibnu Maajah na Al Tirmidhy).
Kuesua (kupapachua) vidole vya miguu ni kwa kupitisha kidole kidogo cha mkono wa kushoto kwa kuanzia chini ya kidole kidogo cha mguu wa kulia na kumalizia kidole kidogo cha mguu wa kushoto. Ama kupapachua vidole vya viganja ni kwa kupitisha baina ya vidole.
Ya Tisa, kutanguliza kulia kabla ya kushoto. Haya ni kwa Hadithi ya Mtume wetu mpenzi s.a.w.:   “Mkitia udhu anzieni kwa vya kuliani vyenu”. (Imehadithiwa na Abu Daud na Ibnu Maajah, na Ibnu Khuzaimah na Ibnu Hibban wameipa darja ya Hadithi sahihi).
Ya Kumi, kuosha mara tatu tatu; hivi ni kwa Hadith ya Sayyidna Othman r.a. kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akitia udhu kwa kuosha mara tatu tatu. (Imepokelewa na Muslim). Na kwa ilivyopokewa na Abu Daud r.a. kutoka kwa Sayyidna Othman r.a. ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amepangusa kichwa chake mara tatu. Na ilivyosimuliwa na Ibn Maajah r.a. kwamba Sayyidna 'Ali r.a. ametia udhu kwa kuosha mara tatu tatu; na akasema Sayyidna 'Ali r.a.: "Huu ndio udhu wa Mtume s.a.w.".
Kumi na Moja, kufululiza na kufuatiza; hivi ni kama alivyofanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na kufanya hivi ni kuepukana na khilafu za wanazuoni. Inapendekezwa ukikamilisha kutia udhu asikunute wala usifute mikono yako, hivi ni kutokana na Hadith ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
   "Mkitia udhu (mkikamilisha kutia udhu) musikunute (musipanguse) mikono yenu kwani maji ya udhu ni kikimbizo cha she'tani". (Imehadithiwa na Ibnu Abi Haatim na wengineo).
Kwani hivi kukunuta mikono baada ya kukamilisha kutia udhu huwa ni kama kujikunuta kutokana na hii ibada ya kutia udhu. Na inapendekezwa aongeze baada ya Bismillah kwa kusema:
  "Mwenyezi Mungu Mtukufu nighufirie makosa yangu, na uniwasi'ishie katika nyumba yangu, na unibarikie katika riziki yangu". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy kutoka kwa Abi Hureira).
Na aizungushe pete ikiwa maji yanafika chini ya hio pete aliovaa, ikiwa hayafiki maji chini ya pete inapasa aivue ili maji yaweze kufika chini ya pete. Anapotia udhu, akikosha uso aanzie kwa kukosha sehemu ya juu ya uso na ya kichwa, yaani kwenye kipaji cha uso; na wakati wa kukosha mikono na miguu aanzie kwenye ncha za vidole ikiwa anajitilia maji mwenyewe. Akiwa anatiliwa maji, na mtu, au anatia udhu kwa mfereji, aanzie kwenye vifundo, vya mikono au vya miguu.
Imependekezwa maji ya kutilia udhu yasipungue kibaba, wala asifanye israfu ya maji, wala asizidishe mara tatu tatu, wala asizungumze wakati anapotia udhu, wala asipige uso wake kwa maji. Na kama ilivyopokewa na Muslim kuwa akikamilisha kutia udhu asome du'a hii:
"Ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, hana mshirika, na ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba Muhammad ni Mtumwa na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, (mwenye kusoma du'a hii) hufunguliwa milango minane ya Pepo aingilie autakao". (Imehadithiwa na Muslim).
Akaongeza alivyopokea Al Tirmidhy r.a.:
  "Mwenyezi Mungu Mtukufu nijaalie niwe miongoni mwa wenye kutubia na nijaalie niwe miongoni mwa wenye ku'tahirika". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).
Na akaongeza alivyopokea Al Haakim:
  "Umetakasika Mola wangu Mlezi na kuhimidiwa ni Kwako, ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Wewe, ninakuomba maghfira na ninatubu Kwako". (Imehadithiwa na Al Haakim).
Vile vile inasuniwa baada ya kukamilisha kutia udhu kusali rakaá mbili za sunna, hivi ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
 "Hatii udhu mmoja wenu na akafanya vyema katika kutia udhu wake na akasali raka'a mbili za suna, akielekea kwa moyo wake na kwa uso wake, isipokuwa huwajibikia juu yake Pepo". (Imehadithiwa na Muslim).
Na tambua na ufahamu, lau akitia shaka wakati anatia udhu kuwa amekikosha kiungo maalumu cha udhu, au hakukikosha, haihisabiwi, kwani asili yake ni kuwa hakikukoshwa, yaani huchukuliwa kuwa hakukikosha. Ama akitia shaka baada ya kukamilisha kutia udhu, basi haichukuliwi hio shaka; hivyo ni kwa sababu lenye kutarajiwa ni kukamilia hivyo kutia udhu kwake, na kwa vile kuyumkinika kuendelea hio shaka.

0 Comments