Mambo 10 Yanayomtoa Mtu Katika Uislam

بسم الله الرحمن الرحيمJua ya kwamba mambo yanayomtoa Muislamu katika Uislamu ni mambo kumi:
Moja: Ni kumshirikisha Allaah Aliyetukuka katika ibada, Anasema Allaah:
“Hakika Allaah Haghufuri kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae.  Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali.” (An-Nisaa: 116)
Na Anasema Allaah:
“Hakika mwenye kumshirikisha Allaah bila shaka Allaah Atamharamishia Jannah, na makazi yake yatakuwa ni Motoni. Na madhalimu hawatopata mwenye kunusuru yeyote.” (Al-Maaidah: 72)
na miongoni mwa hizo shirki ni kuchinja kwa asiyekuwa Allaah kama anayechinja kwa ajili ya majini au makaburi.

Pili: Mwenye kufanya baina yake na Allaah viunganishi akawa anaviomba viunganishi hivyo na kuvitaka uombezi na kuvitegemea, basi hakika mtu huyo amekufuru  kwa makubaliano ya wanavyuoni.

Tatu: Asiyewakufurisha washirikina au akawa ana shaka katika ukafiri wao au akaupitisha (akausahihisha ) ukafiri wao amekufuru.

Nne: Mwenye kuamini kwamba muongozo wa asiyekuwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndio muongozo ulio kamili kuliko muongozo wa Mtume au ya kwamba hukmu ya mwengine ni bora kuliko hukmu yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama yule anayefadhilisha hukmu za Matwaghuut kuliko hukmu yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi mtu huyo ni kafiri.

Tano: Mwenye kuchukia chochote katika aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hata akatekeleza amekufuru.

Sita: Mwenye kufanyia mzaha (shere) kwa chochote katika dini ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) au akafanya utani katika thawabu au katika adhabu za Allaah amekufuru. Na dalili ni  neno Lake Allaah:
“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayaat Zake na Rasuli     Wake?” Msitoe udhuru. Mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (At-Tawbah: 65-66)

Saba: Uchawi; na miongoni mwa huo uchawi ni  uchawi  wa kutenganisha na kupendanisha basi yeyote mwenye kufanya huo uchawi au akauridhia amekufuru. Anasema Allaah:
“(hao Malaika wawili) hawamfundishi yeyote mpaka wamueleze: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru (kufanya sihiri).” (Al-Baqarah: 102)

Nane: Kusaidiana na kuwa pamoja na washirikina dhidi ya Waislamu, na dalili ni:
“Na yeyote atakayewafanya awliyaa wao; basi hakika yeye ni miongoni mwao. Hakika Allaah Haongoi watu madhalimu.” (Al-Maaidah: 51)

Tisa: Mwenye kuamini ya kwamba baadhi ya watu wanaweza kutoka katika shari’ah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama vile alivyoweza kutoka Al-Khidhr katika shari’ah ya Muwsaa basi mtu hiyo ni kafiri.

Kumi: Kuikataa na kuipa mgongo dini ya Allaah  Mtukufu na akawa hajifunzi chochote katika dini. Na dalili ni neno Lake  Allaah:
“Na nani dhalimu zaidi kuliko yule anayekumbushwa Aayaat za Rabb (Mola) wake, kisha akakengeuka nazo (kuzipuuza)? Hakika Sisi Tutawalipiza wahalifu.” (As-Sajdah: 22)
Na wala hakuna tofauti katika mambo haya yanayomtoa Muislamu katika Uislamu kwa yule anayefanya utani au anayefanya kwa kweli au anayeogopa ila anayetenzwa nguvu (kama kushikiwa silaha na akalizimishwa kufanya mambo hayo). Na yote hayo tuliyoyataja ni katika mambo makubwa yanayohatarisha na yanayotokea sana, kwa hivyo yapaswa kwa Muislamu kujihadhari nayo na ayaogope kwa nafsi yake.

Twajilinda kwa Allaah kwa yanayopelekea  hasira Zake na adhabu Zake kali na rahma na amani zimfikie kiumbe bora Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na jamaa zake na Maswahaba wake wote.

0 Comments