Qiyaamah Kitatufikia Tu Lakini Tumeghafilika Nacho

Anasema Allaah سبحانه وتعالى ,
((اقْتَرَبَ لِلنَّاسِ حِسَابُهُمْ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ مَّعْرِضُونَ))
 )) مَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مَّن رَّبِّهِم مُّحْدَثٍ إِلَّا اسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ))
((Imewakaribia watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza))   

 ((Hayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo)) [Al-Anbiyaa: 1-2]

Hili ni onyo kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى kwa watu kuhusu kukaribia kwa Qiyaamah lakini watu wameghafilika nacho, kwa maana kwamba hawajitahidi kuifanyia kazi au hawajitayarishi nacho.
An-Nasaaiy amehadithia kwamba Abu Sa'iyd amesikia kutoka kwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kuhusu,
((فِي غَفْلَةٍ مَّعْرِضُونَ))
 ((katika mghafala wanapuuza))
Kwamba ni 'katika dunia'
Mtu mmoja alimuuliza Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kwa sauti kubwa alipokuwa naye katika msafara
 " يا محمد" و فقال له النبي صلى الله عليه وسلم نحوا من صوته ((هاؤم)). فقال: " متى الساعة؟"  فقال له رسول الله صلى الله عليه وسلم: ((ويحك, إنها كائنة، فما أعددت لها؟)) فقال: "حُب الله ورسوله" . فقال: ((أنت مع من أحببت))
"Ewe Muhammad", Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akamjibu naye kwa sauti: ((Niko hapa)). Yule Mtu akasema: "Lini Saa (Qiyaamah) itafika"? Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Ole kwako, itafika tu. Je, umefanya nini kujitayarisha nacho?)) Akasema: "Mapenzi ya Allaah na Mtume Wake".Akasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  ((Wewe utakuwa pamoja na wale unaowapenda)) [Fath-AlBaari 10:573, Muslim 4:2033]

Na Anasema Allaah  سبحانه وتعالى :
((أَتَى أَمْرُ اللّهِ فَلاَ تَسْتَعْجِلُوهُ))
((Amri ya Mwenyezi Mungu itafika tu. Basi msiihimize)) [An-Nahl: 1]
Maana kwamba, kilichokuwa mbali sasa kiko karibu kwa hiyo msihimize.
Wasioamini hukiulizia kwa kejeli na kuhimiza kifike. Ama walioamini wao wanakhofu nacho kwani wanajua kwamba ni haki na kwamba kitatokea tu bila shaka:
((وَمَا يُدْرِيكَ لَعَلَّ السَّاعَةَ قَرِيبٌ))
 ((يَسْتَعْجِلُ بِهَا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِهَا وَالَّذِينَ آمَنُوا مُشْفِقُونَ مِنْهَا وَيَعْلَمُونَ أَنَّهَا الْحَقُّ أَلَا إِنَّ الَّذِينَ يُمَارُونَ فِي السَّاعَةِ لَفِي ضَلَالٍ بَعِيدٍ))
((Na nini kitakacho kujulisha ya kwamba pengine Saa ya Qiyaamah ipo karibu?))
((Wasioamini huihimiza hiyo Saa ifike upesi; lakini wanaoamini wanaiogopa, na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika hao wanaobishana katika khabari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa)) [Ash-Shuura:17-18]

Na wengine wanaona kuwa hiyo adhabu itakayowafikia siku ya Qiyaamah iko mbali lakini Allaah سبحانه وتعالى  Anasema kuwa iko karibu kabisa:
((إِنَّهُمْ يَرَوْنَهُ بَعِيدًا))    (( وَنَرَاهُ قَرِيبًا))
((Hakika wao wanaiona iko mbali))  
((Na Sisi tunaiona iko karibu)) [Al-Ma'aarij: 6-7]

Na Allaah سبحانه وتعالى Akitaka, ni Mwenye uwezo wa kukileta haraka zaidi kuliko upepeso wa macho:
((وَمَا أَمْرُ السَّاعَةِ إِلاَّ كَلَمْحِ الْبَصَرِ أَوْ هُوَ أَقْرَبُ إِنَّ اللّهَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ))
((Wala halikuwa jambo la Saa (ya Qiyaamah) ila kama kupepesa kwa jicho, au karibu zaidi ya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu)) [An-Nahl:77]

Hivyo inatupasa Waislamu tujitayarishe nacho Qiyaamah kwa kutenda mema mengi na kujiepusha na maovu ili Atulipe Pepo Allaah سبحانه وتعالى , maana Pepo haipati mtu kwa wepesi ila kwa kuifanyia kazi kama Anavyosema:
((وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ))
((Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka Tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni neema iliyoje huo ujira wa watendao)) [Al-'Ankabuut: 58]

0 Comments