Urwah Bin Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhu)

Khushuu YA Ajabu Katika Swalah 

Ni mtoto wa Asmaa bint Abubakar ambaye pia ni dada yake bibi 'Aishah mke wa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Baba yake ni Zubayr ambaye ndiye mume wa Asmaa bint Abubakar (Radhiya Allahu 'anha).


Alipatwa na maradhi ya saratani (cancer) katika mguu wake, akaambiwa na madaktari kuwa lazima akatwe mguu wake ili maradhi yasienee mwilini mwake. Kwa hivyo hana budi ila anywe pombe ili asihisi maumivu. (Zama hizo kulikuwa hakuna sindano au dawa za kisasa za kuondosha fahamu ya mtu anapofanyiwa operesheni). Alipoambiwa hivyo 'Urwah alijibu: "Moyo wangu na ulimi wangu upotee katika kumkumbuka Allaah? WaLlahi sitoingia katika maasi kwa ajili hiyo". Wakamwambia: "Tutakupa kileweshacho (kuondosha fahamu) kama vile unusukaputi". Akasema: "Sipendi kuchomolewa kipande katika mwili wangu nikiwa katika hali ya kulala". Wakamwambia: "Tumlete mtu akukamate". Akasema: "Niachilieni mwenyewe hivi hivi" (yaani mnikate huu mguu hivi hivi bila ya kunipa chochote). Wakamwambia: "Hutoweza kuvumilia". Akasema: "Niacheni niswali.  Mtakakaponiona sitingishiki nikiwa nimetuliza misuli yangu nikiwa niko imara nisubirini hadi nitakapokwenda kusujudu. Kisha nitakaposujudu hapo huwa sifikirii dunia. (Maana kwamba huwa sioni wala sisikii lolote, wa kuhisi chochote wala sina habari ya lolote isipokuwa niko na Mola wangu katika khushuu). Hapo tena fanyeni mnavyotaka kunifanya".
Akaja daktari akasubiri. Aliposujudu 'Urwah, daktari akaleta msumeno akamkata mguu wake. Hakuwa anasema kitu 'Urwah isipokuwa:

لا إلهَ إلاّ اللّهرَضيـتُ بِاللهِ رَبَّـاً وَبِالإسْلامِ ديـناً وَبِمُحَـمَّدٍ  صََلى الله عليه وسلم  نَبِيّـاً وَرَسُولاً .  
 Laa Ilaa Illah Allaah, Radhwiytu BiLlaahi Rabba, wa bil-Islaami  Diyna, wa bi Muhammadin Swalla Allahu 'alayhi wa  wa aalihi wa sallam Nabiyyaw-wa Rasuula".
“Nimeridhika kuwa Allaah Ndiye Mola wangu, na Uislamu ndio dini yangu, na Muhammad Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam  kuwa ni Mtume na Mjumbe wangu”.
Akaendelea hivyo hadi akamaliza daktari kazi yake ya kumkata mguu, damu ikiwa inamchirizika. Hakupiga kelele 'Urwah wala kuugua kwa maumivu!
Alipozindukana 'Urwah, akaletewa mguu wake akautazama, huku akiuambia: "Naapa kwa Allaah! Sijapata kukupeleka (kutembea nao mguu huu) katika mambo ya haram, na Allaah Anajua. Mara ngapi nimesimama nawe usiku kwa ajili ya Allaah!".  Mmoja wao akamuambia: "Ee 'Urwah! Bishara! (Au pongezi!) Kipande cha mwili wako kimetangulia Peponi!". Akasema: WaLlahi hajapata mtu kuniliwaza maliwazo bora kama haya!

0 Comments