Je, Inafaa Mume Kumlazimisha Mke Kuvaa Niqaab?

SWALI:
Asalam Aleykum Warahmatullah Wabarakat
Ninavyojua ni kwamba mwanamke anafaa kujistiri kila pahali isipokuwa uso na vitanga vya mikono. Sasa nataka kuuliza ni nini hukumu ya kuvaa hijab na niqab, na jee inafaa mume wako kukulazimisha kuvaa niqab?
Shukran.


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kuna ikhtilaaf za wanachuoni  kuhusu mas-ala haya, kuna waliosema kwamba kujifunika kwa mwanamke ni kujifunika kila sehemu ya mwili isipokuwa uso na viganja vya mikono. Lakini wengine wameona kwamba ni wajib mwanamke kujifunika kila kitu mpaka uso kutokana na dalili katika Qur-aan na Sunnah. Dalili kutoka katika Qur-aan ni kutokana na maneno ya Allaah سبحانه وتعالى  yafuatayo:

((Ee Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiweNa Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Al-Ahzaab:59]

Jilbaab ni nguo ambayo mwanamke anaivaa juu ya khimaar kutoka kichwani na inashuka kumfunika uso wake.

'Aliy bin Abi Twalhah amerepoti kwamba Ibn 'Abbaas amesema kwamba Allaah سبحانه وتعالى Amewaamrisha wanawake waumini wajifunike nyuso zao kutoka vichwani mwao wakiacha jicho moja tu, wanapotoka nje ya nyumba zao kwa ajili ya kutafuta mahitajio yao. [Ibn Kathiyr: 8: 45].

Kuna Hadiyth nyingi zinazoonyesha kwamba maana ya kujifunika kwa wanawake ni kujifunika kila kitu mpaka uso:
Mama wa Waumini 'Aaishah  رضي الله عنها   amesema ilipoteremeshwa Aayah:        
 ((...وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَى جُيُوبِهِنَّ...))
((….Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao….)) [An-Nuur 24.31]
Wanawake wa Ki-Muhaajirina walichana na kukata gauni zao pembeni ili kufunikia nyuso zao )) [Al-Bukhaariy]

Vile vile Hadiyth ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliyosema  ((Haifai mwanamke kujifunika uso wake katika Ihraam au kuvaa burqa))  Hii inaonyesha kwamba wanawake walipokuwa nje ya Ihraam walikuwa wakijifunika nyuso zao.

Hadiyth nyingine kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aaishah رضي الله عنها  kwamba ((Tulikuwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  katika Ihraam, na ilikuwa kila wakipita wanaume tulikuwa tukiteremsha khimaar zetu vichwani kufunika nyuso zetu na walipopita tukijifunua))

Kwanza mshukuru Allaah سبحانه وتعالى kwa kukujaalia mume ambaye anakutakia jambo la kheri na stara kwani wako wapi siku hizi wanaume kama hao waliokuwa na hima ya kutaka wake zao wabakie katika stara na heshima? Ni wachache sana, kwa sababu aghlabu ni kwamba utasikia mwanamke anataka kujifunika uso lakini mume wake hataki. Hivyo inakuwa ni mtihani kwake mwanamke. Na zaidi ya hao kuna wengine hata hijaab (kujifunika kila kitu ila uso na mikono)  tu hawataki wake zao wavae. Basi je, huoni kama ni neema kwako kuwa umebahatika kuwa miongoni mwa wachache wenye waume wema ambao wanajali  amri za Mola wao?

Kwa hiyo mche Allaah سبحانه وتعالى kwa kuitikia amri mbili; amri kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى na amri kutoka kwa mume wako. Bila shaka hii ni kheri kwako, kwani mumeo hakuamrishi jambo ovu bali ni jambo jema la stara zaidi na halali. Kwa hivyo,  ni bora kumtii na kumridhisha kuliko angekuwa anakulazimisha katika jambo la kumuasi Allaah.

Na kumtii mume wako bila shaka itampa furaha mumeo na azidi kuwa na mapenzi na wewe na uzidi kuijenga nyumba yako katika furaha na amani. Na pia utakapotekeleza amri hizo utakuja kutambua faida nyinginezo na kuridhika nafsi yako. Kuna wangapi waliokuwa hawajifuniki mwanzo uso, na baada ya kuanza kujifunika wanajuta kwanini wamechelewa muda wote huo kujifunika.

Vile vile hii ni njia mojawapo ya njia za kufunga milango ya shaytwaan  kwani itakupunguzia usumbufu na maudhi majiani kwa wale wahuni na wenye uchu wa haramu. Na wewe ndiye utakayekuwa ni sababu ya kuwazuia kutazama yaliyo haramu kwao hivyo utajiepusha na dhambi hizo.

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments