November 16, 2015

Kisa Cha Nabii Swaaalih عليه السلام Sehemu ya 2

MIUJIZA YA NGAMIA
Wafasiri wamesema kwamba siku moja watu wa Thamuud walikusanyika katika baraza yao akaja  Nabii Swaalih عليه السلام  kuwanasihi kwa kuwaita katika Tawhiiyd, na akawapa mawaidha na kuwaonya. Wakataka alama au uhakikisho kuwa huo ujumbe aliokuja nao, ulitoka kweli kwa Mungu.    
Wakamwambia,  "ewe Swaalih ikiwa utatutolea katika jabali lile (wakaashiria jabali lililokuwepo) ngamia wa kike, ambaye ana mimba ya miezi kumi, na wakataja sifa nyingine kadha na kadha.
Nabii Swaalih عليه السلام akawauliza; "je, mkiletewa hiyo miujiza mliyoomba na mliyotaka iwe vile vile, mtaniamini na kuamini  ujumbe niliotumwa nao kwenu?" Wakajibu: "Ndio tutakuamini na kukusadiki yote utakayotuambia"  Nabii Swaalih عليه السلام akachukua ahadi hiyo kwa watu wake  kisha  akamuelekea Allaah  سبحانه وتعالى   kumuomba awaletee miujiza hiyo waliyotaka.
Kama tunavyojua na kuamini kuwa  kwa Allaah سبحانه وتعالى   hakuna jambo lolote linalomshinda   kulifanya kama Anavyosema mwenyewe:
}}إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَنْ يَقُولَ لَهُ كُنْ فَيَكُونُ{{  
 {{Hakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa}} Yasiyn: 82
Basi watu wa Nabii Swaalih عليه السلام  wakakusanyika mbele ya jabali hilo na wakaona muujiza huo wa ngamia mbele ya macho yao.  Allaah سبحانه وتعالى   Aliamrisha jabali lipasuke na akatoka ngamia mwenye sifa zile zile walizozitaka; ngamia mwanamke, mwenye mimba ya miezi kumi, mweupe na sifa zote walizozitaka.  Akatokeza huyo ngamia kutoka kwenye hilo jabali akipita mbele yao.
Ni jambo tukufu, miujiza mikubwa, ya pekee, ya kustaajabisha kabisa, yenye dalili za dhahiri ya uwezo mkubwa wa Allaah سبحانه وتعالى na bila ya shaka msomaji atawaza hapa  "Je, waliamini?"  mwengine atawaza  "bila ya shaka wataamini".  Lakini jambo la kushangaza ni kwamba juu ya kwamba wameoneshwa muujiza mkubwa mbele ya macho yao, si wote walioamini. Wako walioamini lakini wengi wao hawakuamini! Subhanah Allaah!
Hii inatuonyesha jinsi watu wa zamani walivyokuwa wakaidi sana katika kufuata haki. Hata makafikiri wa ki-Quraysh pia walikuwa hivyo hivyo, wakaidi. Miujiza mingapi imewafikia mbele ya macho yao na hawakukubali?.  AlhamduliLLaah sisi Umma Wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم tumepewa Rahma na Allaah سبحانه وتعالىya kuamini haki, kuamini Qur'aan ingawa wakati zilipokuwa zinateremshwa aya hatukuwepo, lakini tumeziamini aya hizo na zaidi kumpenda Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  bila ya kumuona.    Hivyo tunapaswa kushukuru neema hii tuliyojaaliwa na Allaah سبحانه وتعالى kuwa ni umma bora kabisa kuliko umma zote zilizopita.
Na tunaona katika aya zinazofuata kuwa wale wasioamini ambao zaidi ni wakubwa kwa cheo wakawa wanawashawishi walio dhaifu kutuokumuamini Nabii Swaalih عليه السلام  
}}قَالَ الْمَلأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُواْ مِن قَوْمِهِ لِلَّذِينَ اسْتُضْعِفُواْ لِمَنْ آمَنَ مِنْهُمْ أَتَعْلَمُونَ أَنَّ صَالِحًا مُّرْسَلٌ مِّن رَّبِّهِ قَالُواْ إِنَّا بِمَا أُرْسِلَ بِهِ مُؤْمِنُونَ{{
{{Waheshimiwa wa kaumu yake wanao jivuna waliwaambia wanao onewa wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Saleh ametumwa na Mola Mlezi wake? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyo tumwa}} Al-A'araaf :75
}}  قَالَ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُواْ إِنَّا بِالَّذِيَ آمَنتُمْ بِهِ كَافِرُونَ  {{  
{{ Wakasema wale wanao jivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayo yaamini}} Al-A'araaf: 76
Ngamia huyo wa Allaah سبحانه وتعالى aliletwa na shuruti zake walizoombwa wazitimize kama vile  wamwache huru wasimdhuru, wala wasimuuwe.
}}وَإِلَى ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُواْ اللّهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَهٍ غَيْرُهُ قَدْ جَاءتْكُم بَيِّنَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ هَذِهِ نَاقَةُ اللّهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللّهِ وَلاَ تَمَسُّوهَا بِسُوَءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ  {{
{{Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Saleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha kukufikieni Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye ni Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu}}. Al-A'araaf:73
Pia katika Suratul-Qamar  Allaah سبحانه وتعالى Kamuamrisha Nabii Swaalih عليه السلام asubiri na kuwatazama watafanya nini juu ya mtihani huu watakaopewa wa muujiza walioutaka, je wataamini kweli? Au wataendelea na kufru yao?
}}إِنَّا مُرْسِلُو النَّاقَةِ فِتْنَةً لَّهُمْ فَارْتَقِبْهُمْ وَاصْطَبِرْ  {{
{{Hakika Sisi tutawapelekea ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame tu na ustahamili}} Al Qamar: 27
Shuruti nyingine ni kwamba ilikuwa waweke zamu ya kunywa maji katika mji huo, siku moja wamwachie anywe ngamia huyo na siku nyingine wanywe wao kina Thaamuud.   
 }} وَنَبِّئْهُمْ أَنَّ الْمَاء قِسْمَةٌ بَيْنَهُمْ كُلُّ شِرْبٍ مُّحْتَضَرٌ  {{
{{Na waambie kwamba maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliye khusika}}
Al-Qamar:   28
Basi mwanzo wakawafikiana kwamba abakie huyo ngamia kwani alikuwa ni ngamia mwenye baraka nyingi, maziwa yake yaliyokamuliwa siku moja yaliwatosheleza watu wa mji mzima. Alikuwa akilala mahali ambapo wanyama wengine walikuwa hawapakaribii pahali hapo kulala naye, kwa hiyo walijua kuwa huyu hakuwa ngamia wa kawaida bali ni dalili na ishara kutoka kwa Allaah سبحانه وتعالى.  Kwa hivyo wakamwacha atembee anapotaka katika mji huo, ale  anavyotaka, na zamu iwe siku moja anywe maji yeye na siku ya pili wanywe wao. Na siku ya zamu yao kunywa maji walijichotea maji ya kutosha na kuyaweka ili kuyatumia kwa haja zao ya siku ya pili. Na ile siku ya kunywa ngamia maji, wao Wathamudu walikuwa wakinywa maziwa yake huyo ngamia.    
Na hii ndio kauli ya Allaah سبحانه وتعالى  
}}قَالَ هَذِهِ نَاقَةٌ لَّهَا شِرْبٌ وَلَكُمْ شِرْبُ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ{{  
{{ Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu}}
Ash-Shu'araa :155
Tena wakaonywa kuwa wasimdhuru wasije kupata adhabu.
}}وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ {{
{{Wala msimguse kwa uwovu, isije ikakushikeni adhabu ya Siku Kubwa}} Ash-Shua'raa :   156
Lakini wapi!  Hawakutaka kufuata amri ya mwanzo ya kuacha ibada yao ya masanamu wala amri hii ya kumtunza huyo ngamia kama walivyoambiwa, bali walimuua na kutaka kumuua pia Nabii Swaalih عليه السلام
Kasema Allaah سبحانه وتعالى  
   }}وَآتَيْنَا ثَمُودَ النَّاقَةَ مُبْصِرَةً فَظَلَمُواْ بِها{{    
{{Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye}}  Israa: 59
Maana yake ni kwamba walikanusha na wakamdhuru.  
Basi haukupita muda, wakaona hawawezi  kustahmili hali hiyo ya ngamia na masharti waliyopewa. Na chuki  zao walizokuwa nazo kwa Swaalih عليه السلام wakazigeuza kumchukia ngamia, wakakutana wakubwa wao Wathamudi wakapanga kumuua ngamia ili wapate uhuru wa maji yao, na shetani akawapambia njama zao hizo kama alivyosema Allaah سبحانه وتعالى : 
}} فَعَقَرُواْ النَّاقَةَ وَعَتَوْاْ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالُواْ يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ{{   
{{ Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe Swaalih! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume}} A'araaf :77
Juu ya hivyo wakamhimiza Nabii Swaalih عليه السلام  awaletee hiyo adhabu aliyowaonya nayo mwanzo ikiwa hawatofuata masharti ya kumhifadhi ngamia wa Allaah سبحانه وتعالى.  Kwa usemi wao huo yakajumuika maasi haya yafuatayo:
·                  Wamekhalifu amri ya Allaah سبحانه وتعالى na Mtume wake  kwa kumuua ngamia huyo.
·                  Kufanya istihizai na kuhimiza adhabu ya Allaah سبحانه وتعالى  iwateremkie.
Wakastahiki adhabu ya Allaah سبحانه وتعالى   kama alivyowaonya kabla:
}}وَلاَ تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ{{
{{wala msimguse kwa ubaya, isije ikakuangamizeni adhabu iliyo karibu}} Huud: 64
Katika aya nyingine Allaah سبحانه وتعالى  Ametaja aina za adhabu hizo:   
}}وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ{{
{{wala msimdhuru adhabu ya Siku Kubwa}}
Ash-Shu'araa :156
}}وَلاَ تَمَسُّوهَا بِسُوَءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ{{
{{wala msimdhuru isije kukushukieni adhabu chungu}}.
Al-A'araaf: 73
MPANGO WA KUMUUA NGAMIA
Wakapanga kumuua  ngamia na wakatafuta usaidizi kutoka kwa  mwanamke kutoka kabila la heshima na aliye tajiri kabisa  akiitwa  Saduq Bint   Mahya.  Akajitolea kujiuza kwa kijana aliyeitwa Masra'i ibn Mahraj kwa sharti amkate miguu ngamia. Mwanamke mwengine mtu mzima akiitwa Aniza, alijitolea kumuuza mtoto wake wa kike kwa kijana aliyeitwa Qudaar ibn Saluf kwa sharti amuue ngamia. Vijana hao wawili walipata tamaa na  hayo waliyoahidiwa ya kupata wasichana, wakatoka kutafuta watu wengine saba  kuwasaidia kufanya kazi hiyo. Vijana hao wawili wakaungana na wengine saba wakawa ni jumla ya watu tisa.   
Amesema Allaah سبحانه وتعالى   kuhusu hao watu tisa na mipango yao ya kumuua ngamia katika Suratun-Naml:
}}وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ {{
{{Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha}} An-Naml: 48
Wakawa wanamfuatilia ngamia na kumvizia, wakitazama nyendo zake zote. Alipokuja ngamia kunywa maji katika kisima, Masra'i akamdunga katika mguu wake kwa mshale. Ngamia aljaribu kukimbia lakini alishindwa kwani mshale ulishamwingia katika mguu na kumjeruhi. Qudaar akamfuata ngamia na kumdunga mshale katika mguu mwengine. Ngamia akaanguka chini, na kisha akamchoma na upanga.
}} فَنَادَوْا صَاحِبَهُمْ فَتَعَاطَى فَعَقَرَ}}       {{ فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ  {{
29. {{Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja}}
30. {{Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!}}
Al-Qamar:  29-30   
Maelezo zaidi yaliyopo katika Suratus-Shams yanaeleza:
}}كَذَّبَتْ ثَمُودُ بِطَغْوَاهَا{{   }} إِذِ انبَعَثَ أَشْقَاهَا{{    
 }}  فَقَالَ لَهُمْ رَسُولُ اللَّهِ نَاقَةَ اللَّهِ وَسُقْيَاهَا {{
 }}فَكَذَّبُوهُ فَعَقَرُوهَا فَدَمْدَمَ عَلَيْهِمْ رَبُّهُم بِذَنبِهِمْ فَسَوَّاهَا }}    {{ وَلَا يَخَافُ عُقْبَاهَا  {{
11. {{Kina Thamudi walikadhibisha kwa sababu ya upotofu wao}}
12. {{Alipo simama mwovu wao mkubwa,}}
13. {{Hapo Mtume wa Mwenyezi Mungu alipo waambia: Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu, mwacheni anywe maji fungu lake}}
14. {{Lakini walimkadhibisha na wakamchinja ngamia, kwa hivyo Mola wao Mlezi aliwaangamiza kwa sababu ya dhambi zao na akawafuta kabisa}}
15. {{Wala Yeye haogopi matokeo yake.}} 
Ash-Shams 11-15
Na hii ni hadithi ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kuhusu mtu muovu kabisa:
((عن عمار بن ياسر، قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم لعلي: "ألا أحدثك بأشقى الناس"؟ قال: بلى، قال: "رجلان: أحدهما أحيمر ثمود الذي عقر الناقة، والذي يضربك يا علي على هذا ـ يعني قرنه ـ حتى تبتل منه هذه ـ يعني لحيته((   رواه ابن أبي حاتم
((Kutoka kwa 'Ammaar bin Yaasir ambaye kasema: Alisema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  kumwambia 'Aliy, "Je, nikujulishe ni yupi mtu muovu kabisa?"  Akasema ndio; kasema, "watu wawili; mmoja ni mpiga chuku wa Thamuud aliyemuua ngamia na mwengine ni yule atakayekupiga ewe 'Aliy hapa juu (yaani kichwani kwake) mpaka hizi (ndevu) zirowe damu"))     Imesimuliwa na ibn Haatim
Aya nyingine katika suratul A'araaf inazidi kutuelezea tukio la uovu wao kwa ngamia:
}}فَعَقَرُواْ النَّاقَةَ وَعَتَوْاْ عَنْ أَمْرِ رَبِّهِمْ وَقَالُواْ يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ{{
{{Na wakamuuwa yule ngamia, na wakaasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe Swaalih! Tuletee unayo tuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume}} Al-A'araaf: 77
Wauaji hao wakashangiliwa na kupongezwa kwa uhodari wao huo, walifurahikiwa kwa nyimbo na mashairi ya kuwasifu uhodari wao.   Na kwa ujeuri wao wakamkejeli Swaalih عليه السلام   
Nabii Swaalih عليه السلام akawapa onyo kuwa waendelee kustarehe kwa muda wa siku tatu tu na wataona.
}}فَعَقَرُوهَا فَقَالَ تَمَتَّعُواْ فِي دَارِكُمْ ثَلاَثَةَ أَيَّامٍ ذَلِكَ وَعْدٌ غَيْرُ مَكْذُوبٍ   {{
{{ Wakamchinja. Basi (Saleh) akasema: Stareheni katika mji wenu muda wa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyo kuwa ya uwongo}} Huud:65
Wapi!  Hawakumuamini tena Swaalih عليه السلام kwa onyo hilo alilowapa, wakamuuliza Swalih عليه السلام    na kuihimiza kwa istihzai adhabu  "kwa nini siku tatu?"  Naye akawajibu kwa masikitiko  na huku kuwanasihi  kuwa ni bora kwao watubie kuliko kuhimiza hiyo adhabu.    
}}قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلُونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ لَوْلَا تَسْتَغْفِرُونَ اللَّهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ}}   
{{Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnauhimiza uwovu kabla ya wema? Kwa nini hamuombi msamaha kwa Mwenyezi Mungu ili mrehemewe?}} An-Naml: 46
Walimjibu tena kwa ujeuri:
}}قَالُوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَ قَالَ طَائِرُكُمْ عِندَ اللَّهِ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تُفْتَنُونَ {{

{{Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Yeye akasema: Uaguzi wa ukorofi wenu uko kwa Mwenyezi Mungu; lakini nyinyi ni watu mnao jaribiwa}}.
An-Naml: 47
Walisema "Swaalih anasema kuwa atatumaliza baada ya siku tatu, lakini sisi tutammaliza yeye na aila yake kabla ya hizo siku tatu hazikufika."    


Kinaendelea …./3

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only