Kisa Cha Nabii Swaaalih عليه السلام Sehemu ya 3

NJAMA ZA KUMUUA NABII SWAALIH عليه السلام

Kisha wakafanya njama za kumuua   Nabii Swaalih عليه السلام kama inavyoelezwa katika Suratun-Naml
Allaah سبحانه وتعالى  katika aya hizo Ametuelezea  kuhusu watu hao waovu  ambo ni viongozi wa  wa Thaamuud waliokua wakiwapotoa watu wao kutokumuamini Nabii Swaalih عليه السلام  na kumkanusha na ujumbe aliokuja nao.  Na baada ya kumuua ngamia sasa wamepanga kumuua Swaalih عليه السلام.  
}}وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ   {{
{{Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha}}. An-Naml: 48
                   
}}يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ{{ 
{{wakifanya ufisadi katika nchi wala hawafanyi la maslaha}}
Ni kwamba walikuwa wakilazimishia watu wa Thamuud rai zao kwa sababu wao walikuwa ni viongozi na vigogo. 
Al-Awfi kasema kwamba Ibn 'Abbaas رضي الله عنهما   kasema "hawa ni watu waliomuuwa  ngamia" (At-Twabariy 19:477)
Wamepanga njama kuwa Nabii Swaalih عليه السلام atakapolala  usiku na aila yake waende kumuua  kisha wawaambie jamaa zake Swaalih عليه السلام kuwa  wao hawajui lolote kuhusu kuuliwa kwake na yaliyotokea usiku huo na kwamba wao wanasema kweli kwa sababu hakuna wala mmoja wao aliyeona kitu.
Kila mmoja wao kaapa na kuchukua ahadi kwamba usiku ule yeyote atakayeonana na Swaalih عليه السلام  amuue. Lakini Allaah سبحانه وتعالى Alimuokoa Nabii Swaalih عليه السلام na aila yake pamoja na walioamini kutokana na njama za ukatili wa jamaa hao kwa kuwaondosha kwenda sehemu nyingine usiku ule. 
}}قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ {{
{{Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu tutamshambulia usiku yeye na ahali zake; kisha tutamwambia mrithi wake: Sisi hatukuona maangamizo ya watu wake, na sisi bila ya shaka tunasema kweli}} An-Naml :  49  
Lakini Allaah سبحانه وتعالى akapanga mipango yake adhimu  na kuifanya mipango yao iwarudie wenyewe. Mujaahid kasema: "Wameapa kiapo na kuchukua ahadi ya kumuua lakini kabla ya hawajamfikia, wao na watu wao wakaangamizwa". 

KUANGAMIA KWA WATU WA THAMUUD
Nabii Swaalih عليه السلام alikuwa ana sehemu ya kufanya ibada yake katika bonde lenye mawe.  Wakasema "akija kuswali tutamuua  kisha tutarudi, na tukimmaliza tutakwenda kwa aila yake  na kuwamaliza nao pia, "Allaah سبحانه وتعالى akawateremshia jiwe kubwa kutoka mlimani, wakaogopa kuwa jiwe lile litawasaga, wakakimbia  katika pango na lile jiwe likaziba upenyo wa pango lile na hali wakiwa ndani. Watu wao hawakujua wenzao wamekwenda wapi wala hawakujua yaliyowafika! Kwa hiyo Allaah سبحانه وتعالى   Kawaadhibu baadhi yao hivyo na wengineo kawaadhibu kwa adhabu ya aina nyingine kama tutakavyoona katika maelezo yajayo. Allaah سبحانه وتعالى Akamuokoa Mtume wake Swaalih عليه السلام na wale walioamini, ndipo Aliposema katika aya hii:
}} وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ{{  
{{Basi wakapanga mipango yao, na Sisi tukapanga mipango yetu, na wao hawatambui}} An-Naml:50
}}فَلَمَّا جَاء أَمْرُنَا نَجَّيْنَا صَالِحًا وَالَّذِينَ آمَنُواْ مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَمِنْ خِزْيِ يَوْمِئِذٍ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ {{
{{Basi ilipo kuja amri yetu tulimwokoa Swaalih na wale walio amini pamoja naye kwa rehema yetu kutokana na hizaya ya siku ile. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwenye kushinda}}Huud:66
Baada ya siku tatu ikaanza adhabu sasa kuwadhihirikia kama walivyoonywa na Nabii Swaalih عليه السلام, nayo ilianza siku ya Alkhamisi, nyuso zao zikaanza kubadilika rangi kuwa manjano.  Kisha siku ya Ijumaa zikawa nyekundu. Kisha siku ya Jumamosi nyuso zao zikageuka kuwa nyeusi kabisa.    
Baada ya kuchomoza jua siku ya Jumapili wakakaa kusubiri na kutaka kujua adhabu gani hiyo aliyosema Swalih عليه السلام. Mara kukanza mvua ya umeme iliyokuja kwa nguvu kisha ikafuatia mtetemeko wa ardhi mkali ambao uliharibu mji mzima na kuwaangamiza watu wake. Mji ulitingishwa na viumbe vyote vilivyokuwemo humo vilikufa.
}}فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُواْ فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ {{
{{Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipo kucha wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa}}
Al-A'araaf: 78
Athari za Adhabu za Allaah سبحانه وتعالى  zipo bado duniani sehemu mbali mbali kwa mfano 'bahari iliyokufa' (the dead sea) katika kisa cha Luut   عليه السلام  ndio maana Allaah سبحانه وتعالى   anasema katika Qur'aan katika aya mbali mbali:
}}قُلْ سِيرُواْ فِي الأَرْضِ ثُمَّ انظُرُواْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِين{{
{{Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha}} Al-An'aam:11
Hivyo kuhusu athari za Wathamudu, Allaah سبحانه وتعالى Anasema:
}}فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهُمْ وَقَوْمَهُمْ أَجْمَعِينَ{{
{{Basi angalia ulivyo kuwa mwisho wa mipango yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao pamoja na watu wao wote}}
An-Naml:  51
}}فَتِلْكَ بُيُوتُهُمْ خَاوِيَةً بِمَا ظَلَمُوا إِنَّ فِي ذَلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ{{
{{Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyo dhulumu. Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara kwa watu wanao jua}}An-Naml: 52
Na alama hizo za adhabu ya watu Wathamudu zipo kama tutakavyoelezea mwisho wa kisa hiki alipopita Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  katika mji wa Wathamudu.   
Vile vile Allaah سبحانه وتعالى Kataja adhabu yao nyingine ya ukelele mkali ambao kabla ya kumalizika kwake ukelele huo, makafiri wote wa Thamuud  walikufa pamoja wote kwa wakati mmoja.  Hakuna chochote kilichoweza kuwahifadhi, wala majumba yao ya fahari ya mawe hayakuweza kuwalinda na adhabu hizo.
}}وَأَخَذَ الَّذِينَ ظَلَمُواْ الصَّيْحَةُ فَأَصْبَحُواْ فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ {{
{{Na ukelele uliwaangamiza wale walio dhulumu, wakapambazukiwa nao ni maiti majumbani mwao}} Huud:  67
}}كَأَن لَّمْ يَغْنَوْاْ فِيهَا أَلاَ إِنَّ ثَمُودَ كَفرُواْ رَبَّهُمْ أَلاَ بُعْدًا لِّثَمُودَ {{
{{Kama kwamba hawakuwako huko. Hebu zingatieni! Hakika kina Thamud walimkufuru Mola wao Mlezi. Hebu zingatieni! Thamud wamepotelea mbali}} Huud:  68
Maelezo zaidi kuhusu adhabu hiyo:
}}فَكَيْفَ كَانَ عَذَابِي وَنُذُرِ{{
}}        إِنَّا أَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ صَيْحَةً وَاحِدَةً فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِرِ  {{
30. {{Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu}}
31. {{Hakika Sisi tuliwapelekea ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa}}  Al-Qamar:  30-31
As-Sudi kasema walikuwa kama  nyasi kavu za kichaka katika jangwa zinapoungua na kupeperushwa na upepo.  
Ibn Zayd kasema "Waarabu walikuwa wakisimamisha 'Hizar' (kutokana na neno 'almuhtazir') ambayo ni kichaka kikavu, (walichowazungushia) wakiwawekea ngamia na ngo'mbe. Ndipo Allaah سبحانه وتعالى   Aliposema:
}} فَكَانُوا كَهَشِيمِ الْمُحْتَظِر{{
{{wakawa kama mabuwa ya kujengea uwa}}  Al-Qamar: 31

MTUME صلى الله عليه وآله وسلم   ALIPOPITA MJI WA THAMUUD

Ibn 'Umar amesimulia kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa akipita nyumba za watu wa Thamuud  wakati akielekea na jeshi lake la Maswahaba kwenda  katika vita vya Taabuuk  alisimama hapo na Maswahaba wakachota maji katika visima ambavyo watu wa Thamuud walikuwa wakichota maji ya kunywa.   Wakatumia maji kukandia unga wao wa kupikia mikate, na wakajaza maji ya kunywa katika mifuko yao ya ngozi (viriba), lakini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliwaamrisha  wayamwage maji  na unga waliokanda walishe ngamia wao. Kisha akaondoka nao mpaka wakafika katika kisima ambacho ngamia wa Thamuud alikuwa akinywa maji, akawaonya wasiingie kwa watu walioangamizwa  kwa kuwaambia: "Nakhofu  msije kupatwa  yale yaliyowapata wao, kwa hiyo msiingie kwao"
Riwaya nyingine imesema hivi:
عن عبد الله بن عمر قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم وهو بالحجر: ((لا تدخلوا على هؤلاء المعذبين، إلا أن تكونوا باكين، فإن لم تكونوا باكين فلا تدخلوا عليهم، أن يصيبكم مثل ما أصابهم)). أخرجاه في (الصحيحين) من غير وجه.
 ((Imetoka kwa Abdullah Bin 'Amr ambaye alisema:  Kasema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa Hijr  "Msiingie kwao hawa walioadhibiwa, isipokuwa muingie na huku mnalia, na kama hamlii basi msiingie kwao msije kufikwa na masaibu kama yaliyowafikia wao)) Al-Bukhari Na Muslim
Wa Allaahu A'alam

لَقَدْ كَانَ فِي قَصَصِهِمْ عِبْرَةٌ ِلأُوْلِي الأَلْبَابِ مَا كَانَ حَدِيثًا يُفْتَرَى وَلَكِن تَصْدِيقَ الَّذِي بَيْنَ يَدَيْهِ وَتَفْصِيلَ كُلَّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ
Kwa hakika katika visa vyao yamo mazingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyo zuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.
[Yuusuf: 111]
 

0 Comments