TAHARA


Nini 'Tahara?

Kilugha ni unadhifu, kama kusema nimei'tahirisha nguo, yaani nimeinadhifisha. Kisharia, ni hali ya kuondosha hadath kubwa (janaba, hedhi au nifasi), na ni hali ya kuondosha hadath ndogo (kutokua na udhu), na ni hali ya kuondosha najsi (uchafu), kama vile, mkojo, kinyesi, damu, usaha - mwilini, nguoni au pahala.
Vitu vyenye Ku'tahirisha
Vyenye ku'tahirisha ni vitu vinne, maji, mchanga, “kudibaghi”* na kuchachuka. Maji hutumika kwa kuondoshea hadath kubwa na/au ndogo na kuondoshea najsi (uchafu). Mchanga hutumika kwa kutayamam na kwa kuondoshea najsi ya mbwa na nguruwe. Kudibaghi ni kwa kuondoshea unajsi wa ngozi ya nyamafu. Kuchachuka huwa kwa tembo kugeuka (wenyewe) ikawa siki.
Maji yanayojuzu Ku'tahirishia
Maji yenye kufaa ku'tahirishia ni namna saba:
Ya Kwanza, maji ya mvua; kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
   “…, na akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo…”. (Al Anfaal : 11).
Ya Pili, maji ya bahari; kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alipoulizwa kukhusu maji ya bahari - akasema s.a.w.:    “Hayo ni yenye ku'tahirisha maji yake, halali maiti yake”.
(Imehadithiwa na Al Sheikhan, Al Tirmidhy na Ibnu Hibbaan).
Ya Tatu, maji ya kisima, kwa Hadithi ya Suhail; kuwa baadhi ya Masahaba r.a. walisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika yako unatia udhu kutoka kisima cha Bidha’a na humo wanajisafisha wenye uchafu na wenye hedhi, na wenye janaba"? Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  “Ni maji yenye ku'tahirisha, hayanajisiki kwa chochote”. (Imehadithiwa na Al Tirmidhy na Ahmad akaipa darja ya Hadithi sahihi).
Ya NneTanoSita na ya Saba; maji ya mto, , maji ya falaj; na hivyo inamaanisha pia maji ya barafu na maji baridi. Haya ni kutokana na Hadithi ya Abu Hureira r.a. aliposema kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w alikuwa akisha kabbiri, takbiir ya kuingia kwenye Sala, husita kidogo kabla ya kusoma Alhamdu (Surat Al Fat-ha). Akasema - Abu Hureira - kumuuliza s.a.w. - “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu unasema nini"? Akasema Abu Huraira, akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w:
"Nnasema: Mwenyezi Mungu niweke mbali baina yangu na baina ya makosa yangu kama ulivyoweka mbali baina ya urejua na uchejua, Mwenyezi Mungu nitakase kutokana na makosa yangu kama inavyotakaswa nguo nyeupe kutokana na uchafu, Mwenyezi Mungu nikoshe kutokana na makosa yangu kwa maji na barafu na maji baridi”. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Namna za Maji

Maji yanagawika namna tano:
Ya Kwanza, maji yenye kujuulikana kuwa ni maji, hayakuongezewa kitu ndani yake; haya ni miongoni mwa aina saba za maji yenye ku'tahirisha tuliozitaja hapo juu. Haya ni 'taahir kwa nafsi yake na ni yenye ku'tahirisha, yanafaa kutumika kwa kuondoa hadath kubwa na/au ndogo na kuondoa najsi, si karaha kuyatumia.
Ya Pili, maji yaliopigwa sana na jua, haya vilevile ni miongoni mwa maji tulioyataja hapo juu; lakini huwa yamepigwa sana na jua. Haya vilevile ni 'taahir kwa nafsi yake na ni yenye ku'tahiarisha, yanafaa kutumika kwa kuondoa hadath kubwa na/au ndogo na kuondoa najsi, ni karaha kuyatumia kwa vile kupigwa sana na jua. Imekuja hivi kuwa karaha kutumia maji yaliopigwa sana na jua kutokana na Hadithi ya Imam Shafi’ii r.a. kwamba amesema Sayyidna Omar r.a. kuwa maji yanayopigwa sana na jua yanasababisha ukoma. Imeshuritishwa hivi kuwa karaha kuyatumia maji yaliopigwa sana na jua kwa sharti mbili:
Sharti ya Kwanza, Iwe Yamo Katika Chombo Chenye Kuhunzika; Kama Vile chombo cha shaba, au cha chuma au cha risasi; kwa sababu maji katika vyombo hivi yakipigwa sana na jua hutoa madda yenye kusababisha maradhi ya ukoma.
Sharti ya Pili, iwe hali hii kwenye nchi za joto sana; yaani jua lake ni kali sana..
Ya Tatu, maji yaliotumiwa kwa kuondoshea hadathi kubwa au hadath ndogo au kuondoshea najsi, ikiwa hayakubadilika rangi, ladha au harufu; wala hayakuzidi kiwango chake cha asli. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
“Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyaumba maji hali ya kuwa ni 'taahir na yenye ku'tahirisha, hayanajisiki isipokuwa kwa kubadilika ladha yake au harufu yake" Na kwa Hadithi iliopokewa na Ibn Maajah: "Au rangi yake".
Kukhusu kufaa ku'tahirishia maji yaliotumika kuna tafauti ya rai za madhehebu, kwa kuwa juu ya kwamba Masahaba r.a. walikuwa ni mno kushikamana na dini; lakini hawakuwa wakiyakusanya maji yaliotumika na kutawadhia; na lau kama ingalifaa hivyo, wangalifanya. Na wamesema baadhi ya wanazuoni ya kwamba hakika maji hayatoki kuwa ni yenye kufaa ku'tahirishia basi kwa vile kutumika kwa ku'tahirisha, ila ikiwa yatabadilika harufu yake, au rangi yake au ladha yake. Wakasema kuwa Masahaba r.a. walikuwa hukaribia kugombania kutaka wapate maji yanayochururika kutoka viungoni mwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. wakati anapo tia udhu ili wapate barka zake s.a.w., na kutabaaruk ni kwa kutilia udhu baadhi ya viungo vya udhu au kwa njia nyengine. Kufaa ku'tahirishia maji yaliotumika kunatiliwa hoja kuwa asili ya maji ni 'taahir na ni yenye ku'tahirisha.
Ya Nne, maji yaliobadilika kwa kuchanganyika au kuchanganywa na kitu 'taahir; hivi ikiwa huku kubadilika haya maji kwa huu mchanganyiko kutaondoa jina asili la maji na ikiwa huku kuchanganyika ni kwenye kuepukika, kama vile sharubati au marashi; basi maji haya hubakia kuwa ni 'taahir, lakini hayafai ku'tahirishia. Ama ikiwa kule kubadilika ni kwa sababu ya mchanganyiko ambao yale maji hayangaliweza kuepukana nako, kama vile kwa sababu ya udongo, au mwani au jasi, au vitu kama hivyo ambavyo vimo kwenye machimbuko au mapitio ya hayo maji, au ikiwa kubadilika ni kwa sababu ya kuwemo maji kwa muda mrefu, kama vile katika hodhi; haya hubakia kuwa ni 'taahir na yanafaa ku'tahirishia, hivi ni kutokana na uzito na shida ya kuepukana na vitu hivyo na kwa vile kubakia jina la asli la maji. Ni hivyo hivyo ikiwa maji yatabadilika (ladha yake) kwa kuongezwa chumvi - ya maji au ya mawe - yatabakia kuwa ni 'taahir na yanafaa ku'tahirishia; kwa sababu asili ya chumvi ni maji ya chumvi. Katika hali hizi hapana tafauti ikiwa kubadilika huku ni kwa kuhisi au kwa maana ya neno, kama vile kubadilika na kuondoka asili yake; kwa mfano maji ya mawaridi yakawa hayana harufu; haya hukadiriwa kama yale yenye harufu.
Ya Tano, maji yalioingia najsi, haya huwa katika namna mbili; mengi na kidogo. Maji kidogo hunajsika kwa kuingia ndani yake najsi, sawa sawa ikiwa yatabadilika rangi, ladha au harufu au hayatabadilika. Haya ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w:    “Maji yakifika (kiwango cha) qulateini hayachukui (hayawi) najsi”. (Imehadithiwa na Ahmad na Ibnu Hibbaan).
Hivi imefahamika ya kwamba maji ya kiwango cha qulateini* hayanajsiki kwa kuingia najsi, na maji ya kiwango cha kasoro ya qulateini hunajsika kwa kuingia najsi.
Maji mengi yanayo kusudiwa hapa ni yale ya kiwango cha qulateini na zaidi, haya hunajisika iwapo huku kuingia najsi kwenyewe kutabadilisha rangi, ladha au harufu ya hayo maji
Baadhi ya wanazuoni, miongoni mwao ni Arawyaani, Al Ghazali na Al Baydhawy; wao wamesema ya kwamba maji kidogo ni sawa na maji mengi, hayanajsiki kwa kuingia najsi; bali yana najsika kwa kuingia najsi yakabadilika hayo maji rangi, ladha au harufu yake. Qauli hii ni yenye nguvu kwa dalili ya kuzingatia ya kwamba cha kuchukuliwa kipimo ni Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. iliotangulia kutajwa hapo juu yenye maana kama hii: “Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyaumba maji hali ya kuwa ni 'taahir na yenye ku'tahirisha, hayanajisiki isipokua kwa kubadilika ladha yake au harufu yake" Na kwa Hadithi iliopokewa na Ibn Maajah: "Au rangi yake".
*Qulateini imekadiriwa ni maji yaliomo kwenye chombo cha dhiraa na robo
urefu, upana na kwenda chini.
Hii ni dalili iliotamkwa, ambayo ina nguvu na uzito kuliko dalili ya kufahamika (mafhuum). Zaidi ya hivyo, hapana tafauti baina ya kubadilika kidogo na kubadilika sana; na ikiwa kubadilika huko ni kwa rangi, ladha au harufu, au kama hio najsi ilioifika maji ni kwa kuchanganyika au kwa kuwa karibu yake; au najsi hio ilikuwa ni yenye kuweza kuepukika na au haiwezi kuepukika. Muhim ni vile kuwa ni najsi, kinyume na kubadilika maji kwa sababu ya mchanganyiko na kitu 'taahir. Lau kama itaingia kwenye maji mengi najsi yenye sifa ya maji, kama vile mkojo uliokatika harufu, basi hukadiriwa kwa kupewa hukmu kama ilivyotangulia kuelezwa kukhusu vitu 'taahir. Ama kukhusu vitu vya maji-maji, ambavyo si maji; kama vile mafuta, hivyo hunajsika kwa kuingia najsi ya kiwango chochote kile, ikiwa vitabadilisha rangi, ladha au harufu au havitabadilisha.
Hii tafauti ya hukmu iliopo baina ya viwili hivi, yaani maji na vitu vya majimaji; ni kwamba vitu vya maji-maji si taabu kuhifadhika visipatwe na najsi, kinyume na maji.

Hukmu ya Maji Makombo

Maji makombo ni yale yaliobakia kwenye chombo baada ya kunywiwa na binaadam au mnyama, haya huwa katika hali kama hizi:
Kwanza, makombo ya binaadam, haya ni 'taahir kwa Qauli ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu:  “Na hakika tumewatukuza wanaadamu, ...”. (Al Israai : 70).
Na katika kutukuzwa binaadam ni hivi kuwa yeye ni 'taahir - hai au maiti.
Ama kukhusu unajsi uliotajwa kwenye Qauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu:   “…… Hakika ya washirikina ni najsi……". (Tawba : 28).
Unajsi unaokusudiwa ni unajsi wa itikadi kwa uovu wanaouficha nyoyoni mwao, si unajsi wa kiwiliwili. Hawa mushrikina siku za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. walikuwa wakichanganyika na Waislam, na tume zao zikija kwa Mtume wetu Mpenzi s.aw., na wakiingia msikitini kwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na wala hakuamrisha s.a.w. kukoshwa chochote kilichogusa miili yao.
Pili, makombo ya mnyama; mnyama wakati yuhai ni 'taahir, ikiwa ni mnyama anaeliwa au asieliwa; isipokua mbwa na nguruwe, hawa ni najsi. Haya ni kutokana na Hadithi ya Jabir r.a. alipoulizwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kuwa: “Tutawadhie makombo ya maji yalionywiwa na punda”? Mtume wetu mpenzi s.a.w. akajibu:   “Na'am, na waliobakisha wanyama mwitu”. (Imehadithiwa na Shafi’ii na Darqu’tny na Al Bayhaqy).
Na kutokana na Yahya bin Said ya kwamba Omar bin Khatab r.a. alikuwa kwenye msafara pamoja na Amri bin Al‘A'si r.a. mpaka wakafika kwenye hodhi, Amri bin Al‘A'si akamuuliza mwenye hodhi kama wanyama mwitu hunywa maji kutoka hodhi hilo. Sayyidna Omar r.a. akasema, usitwambie, kwani sisi tunawazunguka wanyama mwitu na wanyama mwitu wanatuzunguka sisi. (Ameipokea Malik). Na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kukhusu paka, alipoulizwa s.a.w. kukhusu kunywa paka katika chombo, kama kinanajisika au hakinajisiki; akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  “Hakika ya paka si najsi, wao ni wenye kupita baina (kuishi nanyi) yenu”. (Imehadithiwa na Maimam wa tano wa Hadithi).
Ama makombo ya maji yaliyonywiwa na mbwa au nguruwe, hayo ni najsi; inapasa kuyaepuka, hivi ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  “Ku'tahirisha mmoja wenu chombo alicho ramba au alichochovya mbwa mdomo wake ndani yake ni kwa kukoshwa mara saba, mara ya mwanzo ni kwa mchanga.” (Imehadithiwa na Ahmed na Muslim).
Ama makombo ya maji yaliyonywiwa na nguruwe ni najsi, kwani nguruwe ni akhasi kuliko mbwa, na imejengwa hoja ya unajsi wa nguruwe kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  “….. au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu;.....”. (Al An’aam :145).
Na uchafu ni najsi.

Ngozi za Nyamafu

Hu'tahirishwa ngozi ya nyamafu (mnyama aliokufa) kwa kudibaghiwa, sawa ikiwa wanyama hao ni wenye kuliwa au wasioliwa, hivi ni kwa Hadithi ya Maimuna alivyosema kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w alisema:
 
“Lau mungalichukuwa ngozi yake”. Wakasema: “Hakika yake hiyo ni ya nyamafu”. Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: “Inai'tahirisha maji na (qaradhi) matunda yenye ukali”. (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Nissaai).
Na kutokana na Abi 'Abbas r.a. kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:  “Ikidibaghiwa ngozi, huwa ime'tahirika”. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Hudibaghiwa ngozi ya nyamafu kwa kutumia vitu vikali kama vile shabu, siki, maganda ya makomamanga, chumvi, chokaa, na mfano wake. Na hupatikana huko kudibaghi kwa kuondoka uchafu unaokuwemo kwenye ngozi, kwa kusafishwa uzuri ikawa hata kama itarowekwa ndani ya maji basi haitatoa harufu mbaya. Ikiwa hivi kudibaghi kumefanyika kwa kutumia kitu ambacho ni najsi, basi italazim baada ya kudabighiwa ikoshwe hio ngozi ili kuondoa unajsi uliosababishwa kwa kile kitu najsi kilichotumiwa katika kudabighi. Bali pia hata kama imedabighiwa kwa kitu ambacho si najsi; basi inapendekezwa ikoshwe baada ya kudabighiwa. Ama ngozi ya mbwa na nguruwe, na vizaliwa vyao, hai'tahiriki hata kwa kudabighiwa. Hivi kwa sababu wao ni najsi asli yao tangu wahai, na kudabighi ni ku'tahirisha ngozi ambayo imenajsika kwa kufa yule mnyama ambae asili yake ni 'taahir. Mbwa na nguruwe na vizaliwa vyao ni najsi tangu wahai, basi ni ndivyo zaidi mizoga yao kuwa ni najsi, wala hai'tahiriki.

Mifupa na Nywele za Nyamafu

Nyamafu ni maiti ya mnyama ulieondoka uhai wake bila kuchinjwa kisharia. Hivi huwa pia maiti ya mnyama asieliwa, hata ikiwa atachinjwa, na mnyama anaeliwa ikiwa hakuchinjwa kwa mujibu wa sharia, huwa sawa na nyamafu. Kwa hivyo basi, nyamafu ni najsi kila kitu chake; tangu nyama, ngozi, mifupa na manyoya yake, haya ni kutokana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema: Mmeharimishiwa nyamafu ………”. (Al Maidah : 3).
Kuharimishwa kitu ambacho asili yake si najsi wala si haram, wala hakina madhara kukila* ni dalili ya kuwa ni najsi. Hivi ni kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufua:
 “Sema: Sioni katika yale nilio funuliwa mimi kitu kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayo mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hio ni uchafu, au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu" . (Al-An-'aam : 145).
"Rijsi" ni uchafu, na uchafu ni najsi. Ni ndivyo kwamba manyoya, sufi, nywele na mifupa ni sehemu ya mwili, kwa hivyo hivi vinachukua hukmu ya mwili wenyewe, yaani nyamafu; kwa hivyo navyo ni najsi. Kuna qauli kuwa manyoya ya nyamafu* si najsi kwa hoja kuwa manyoya hayana uhai, kwani yakikatwa hali ya kuwa huyo mnyama yuhai hahisi maumivu, na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.::
    "Haidhuru kukhusu ngozi ya nyamafu ikiwa itadabighiwa na manyoya yake na sufi yake ikiwa vitaoshwa". (Imehadithiwa na Darqu’tnii).
Na sehemu iliotengeka ya mnyama hai ni sawa na nyamafu ya mnyama huyo, ikiwa asili yake ni 'taahir basi nacho huwa 'taahir, na ikiwa ni najsi, basi nacho huwa ni najsi.
*Nyamafu imeruhusiwa kuliwa wakati wa haja, lau kama anadhara kuliwa; isingali ruhusiwa kuliwa.
Hivi ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
   “Kilichokatwa kutokana na kiumbe hai, (hukmu yake) ni sawa na maiti yake". (Imehadithiwa na Al Haakim).
Kilichokatwa kutokana na binadam, au samaki, au panzi, au nyembure; basi hivyo ni 'taahir, kwani asili yao ni 'taahir, na kwa hivyo maiti/nyamafu yao ni 'taahir. Mbali na hivi basi ni najsi, kwani nyamafu yao ni najsi. Ama nywele na sufi na manyoya ya mnyama mwenye kuliwa ni 'taahir kwa kukubaliana wanazuoni.
Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
  “ ……. Na kutokana na sufi zao na manyoya yao na nywele zao mnafanya matandiko na mapambo ya kutumia kwa muda". (Annahl : 80).
Maneno haya ya Mwenyezi Mungu Mtukufua yamechukuliwa kufahamika ikiwa vitu hivi vimechukuliwa kutokana na mnyama baada ya kuchinjwa au hali yuhai, kama inavyofanywa daima. Ikiwa itaingia shaka, kuwa vitu hivi vinatokana na najsi au 'taahir; basi tutachukua kuwa vinatokana na 'taahiri, kwani hio ndio asili, na sisi tumetia shaka juu ya najsi na asili ni kutokua najsi, yaani 'taahir.
Ama nywele za binaadam ni 'taahir, ikiwa zimekatwa hali yuhai au maiti, hivi ni kutokana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kukirimiwa binaadam:  “ Na hakika tumewatukuza wanaadamu............ “. (Al Israai : 70).
Na suala hili la kukirimiwa binaadam ndio hoja ya kutokua najsi binaadam, akiwa yuhai au maiti, ni Muislam au si Muislam.
Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:   “…… Hakika ya washirikina ni najsi…….”. (Tawba : 28).
Makusudio katika Aya hii ni unajsi wa itikadi, si unajsi wa kiwiliwili. (Imetangulia kuelezwa haya kwenye mas-ala ya "Makombo Ya
Binaadam".

Kutumia Vyombo vya Dhahabu na Fedha

Imeharamishwa kwa wanaume na kwa wanawake kutumia vyombo vya dhahabu na vya fedha kwa kulia, kunywiya; hivi ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  “Mwenye kunywa kwenye chombo cha dhahabu na cha fedha hakika unanguruma tumboni mwake Moto wa Jahannam”. (Imehadithiwa na Muslim).
Na katika Hadithi nyengine imepokewa kuwa:"Hakika ya anaekula au kunywa”, mpaka mwisho wa Hadithi.
Kama inavyo haramishwa kutumia vyombo vya dhahabu na fedha kwa kulia na kunywiya, vilevile ina haramishwa katika matumizi mengine.
Amesema Imam Al Nawawi r.a. katika sherhe Muslim: “Amesema jamaa zetu wamekubaliana wote juu ya kuharamishwa kula na kunywa na matumizi mengine katika vyombo vya dhahabu na fedha.
Akaendelea mpaka akasema: “Kuharamishwa huku ni sawa kwa wanaume na kwa wanawake, bila ya khilafu, na hakika tafauti baina ya mwanamume na mwanamke ni katika mapambo ya kike kwa kujipamba kwa ajili ya mume wake.
Vilevile ina haramishwa kupamba maduka, majumba na maseble kwa vyombo na vitu vya dhahabu na fedha. Vilevile ina haramishwa kuwanavyo vyombo hivi, hata bila ya kuvitumia; kwani chenye kuharamishwa kutumia, kina haramishwa (kumilikiwa) kuwanacho na kwa kuwa ni kitu cha kujifurahishia na pambo. Hivi ni kwamba kila ambacho asili yake haram, basi ni haram kukitizama. Na imeharamishwa kwa masonara kutengeneza vitu hivi, wala haijuzu kulipwa kwa kazi hii; kwa sababu kazi yao hii ni maasi. Lau kama mtu akavivunja na kuviponda-ponda vyombo hivi, basi hatalipishwa, wala si halali mtu kutaka alipwe kwa vyombo hivyo vilivyo pondwa-pondwa au kuvunjwa, wala haijuzu kushitaki ili kutaka alipwe.
Vyombo vilivyochovywa fedha kwa ajili ya pambo, hivyo vimeharamishwa kuvitumia; sawa sawa ikiwa kuchovywa huko ni kwa kiwango kikubwa au kidogo. Ama ikiwa kuchovywa ni kwa kiwango kidogo kulingana na haja tu, haiharimishwi kutokana na huo udogo wake, wala haiwi makruuh kwa sababu ya haja. Haya ni kutokana na alivyopokea Imam Al Bukhari r.a. kutoka kwa ‘Asim Al Ahwal aliesema: “Nimeiona bilauli (chombo cha kunywiya) ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa Anas bin Malik r.a. nayo imefanya kutu, ikatiwa utepe (upapi) wa fedha, yaani ikazuiliwa kwa upapi wa fedha”. Akasema Anas bin Malik r.a. kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amenyweya chombo hiki mara kadhaa wa kadhaa. Ama vyombo vinavyochovywa kwa dhahabu vimeharamishwa kabisa kuvitumia kwa hali yoyote ile.

Kusuwaki

Kusuwaki ni kusafisha kinywa - meno, ulimi - pembezoni na baina yake kwa kutumia msuwaki; wa kijiti au uliotengenezwa kisasa, ili kuondoa harufu mbaya na kuondoa masalio ya chakula yaliomo kinywani. Kupiga msuwaki ni sunna iliotiliwa nguvu kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  “Kusuwaki ni ku'tahirisha (kusafisha) kinywa na ni kumridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu”. (Imehadithiwa Ibnu Khuzaimah, Ibnu Hibbaan, Al Baihaqy na Al Nissaai).
Kusuwaki kunapendekezwa na kunasisitizwa katika hali hizi:
Ya Kwanza, kinapobadilika kinywa harufu yake kwa kula kitu chenye harufu mbaya, kama vile kitunguu thom, kitunguu maji, doriani au chochote kile chenye harufu yenye kukirihisha.
Ya Pili, baada ya kuamka; haya ni kutokana na Hadithi mbili zilizo sahihi.
Hadithi ya kwanza:
  “Alikuwa (Mtume wetu Mpenzi) s.a.w. akitoka usingizini husafisha kinywa chake, yaani husuwaki”.
Hadithi ya pili:
 "Alikuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. anapoamka husuwaki".
Ya Tatu, wakati wa kutaka kusali, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  “Kama si kuwaonea mashaka umma wangu ningaliwaamrisha kusuwaki kila wakisali”. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Na imepokewa kutoka kwa Sayyidah 'Aisha r.a. kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:
  “Raka'a mbili zinazosaliwa kwa kusuwaki (yaani baada ya kusuwaki) ni afadhali kuliko raka'a sabiini zinazosaliwa bila ya kusuwaki”. (Imehadithiwa na Abu Na’im na Darqu’tni na Dilmi).
Ya Nne, wakati wa kutia udhu, kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  “Kama si kuwaonea mashaka umma wangu ningaliwaamrisha kusuwaki kila wanapotia udhu”. (Imehadithiwa na Al Nissaai na Ibnu Maajah).
Ya Tano, wakati wa kusoma Qur’ani, hivi ni kwa sababu kwa vile kutakiwa 'tahara ya kinywa wakati wa Sala, ambayo miongoni mwa nguzo zake ni kusoma Qur’ani, basi ni bora zaidi 'tahara ya kinywa wakati wa kusoma Qur’ani pekee, yaani bila ya kuwa kwenye Sala.
Kusuwaki huwa ni kwa kitu chochote chenye kuondoa uchafu kinywani. Lakini kutumia msuwaki wa mti unaoitwa “arak” ni afadhali, kwa sababu msuwaki wa "arak" una faida nyingi. Miongoni mwa faida hizo ni, umadhubuti wa ufizi, kuondoa maradhi ya meno, kusaidia uwezo wa kutafuna chakula, kusaidia mzunguko wa mkojo, kusafisha vyema kinywa, bali zaidi humridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Msuwaki wa الأراك ))  “arak” pia unadumisha uwezo wa ujana, unasafisha koo, unasaidia uwezo wa akili, una ujira zaidi, unasafisha kwa wepesi na una saidia kukumbusha kushahadia wakati wa mauti.
Inapendezewa kuukosha msuwaki kabla na baada ya kuutumia na iwe kusuwaki kwa kutumia mkono wa kulia. Vilevile inapendekezwa kuanzia mkono wa kulia wa kinywa, na apitishe msuwaki sehemu ya juu ya kinywa na kwenye maoteo ya meno - ufizi. Na inapendekezwa msuwaki uwe wenye urefu wa kadiri ya shubiri kama ilivyothibiti kwa sunna. Asiekuwa na meno (kibogoyo), yeye asuwaki kwa kutumia kidole chake.

Haya ni kutokana na Hadith ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alipoulizwa na Sayyidah 'Aisha r.a. kukhusu mtu asiekuwa na maneno kuwa na yeye asuwaki? Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa maneno yenye maana kama hii: “Na'am, asuwaki kwa kutia kidole chake kinywani”. (Imehadithiwa na Al ‘Tibraani).

0 Comments