Watu Wananikejeli Kwa Sababu Ya Kuvaa Jilbaab, Je Nivue Kuwaridhisha?

SWALI:
Assalam aleykum warahmatullah wabarakat Natoa wingi wa shukurani za dhati kwa waanzishi wa web site hii na Mungu atawajaza kila la kheri naamini wazi si jambo la kawaida bali ni uwezo wake Allah S.A kuweza kuipa nguvu Uislam
Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 23 nimeolewa na nina mtoto mmoja swali langu kila siku mimi nilikuwa nikivutiwa sana nikiona watu wamejistiri kwa majilbab ingawa nilikuwa siendi kichwa wazi lakini nilikuwa nahisi kuwa ucha Mungu ulioje kuwa mtu kuvaa vazi la heshima kama hilo hadi huwa naota nikimuona mtu kavaa namuhusudu sana sasa na mie nimeanza kuvaa lakini wanakuja watu na maneno ya kila aina weye kijana mzuri unavaa hivyo mume wako ataenda kutafuta wengine huko nje wanovaa siyo weye na mishungi na maneno tele ya karaha na watu hao hao ndio ninao kwani wamo kwenye kazini kwangu sasa nifanyeje na ninataka kuwa karibu sana na Mungu na kuepukana na mambo ya kishetwan yaso faida wala heri.


JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kutaka nasiha zetu kuhusu suala la kuvaa jilbaab. Awali ya yote tunakuombea kwa Allaah Aliyetukuka Akupe msimamo wa kuweza kusimama imara katika hilo kwani wewe hufuati ya mtu na viumbe bali ya Muumba. Na hakuna jambo zuri kama kufanya hivyo.
Allaah Aliyetukuka Anasema:
"Na anachokupeni Mtume chukueni, na anachokukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuadhibu" (59: 7).
Kufuata watu hakumletei yeyote yule isipokuwa ni matatizo na mashaka. Ndio Allaah Aliyetukuka Akasema:
"Na ukiwatii wengi katika hawa waliomo duniani watakupoteza na Njia ya Allaah. Hawa hawafuati ila dhana tu, na hawakuwa ila ni wenye kusema uwongo tu" (6: 116).

Dada yetu wewe uko katika njia ya sawa wala usitazame wala kurudi nyuma kwani kufanya hivyo ni kuwafuata mashetani wa kibinaadamu ambao huwa hawawatakii wenzao mema na mazuri.
Kuvaa vazi la Kiislamu kwa msichana na mwanamke ni katika amri aliyoitoa Allaah Aliyetukuka kama Alivyosema:
"Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu" (33: 59).
Na katika surah hiyo hiyo, Allaah Aliyetukuka Akatuambia:
"Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allaah na Mtume Wake wanapokata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allaah na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi" (33: 36).
Uamuzi ni wako dada yetu, kufuata njia ya uongofu au ya upotevu kwa kuwafuata wanaadamu wasio na hamu ya Akhera. Nasiha yetu ya dhati ni kuwa tunakuomba ufuate ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na uache mengine yote.
Kufuata watu ikiwa ni rafiki, wazazi,  mume wako,  au yeyote mwenye mamlaka nawe katika maasi, utakuja kujuta siku ya Qiyaamah:
"Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto. Watasema: Laiti tungelimtii Allaah, na tungeli mt'ii Mtume!"   
"Na watasema: Mola wetu Mlezi! Hakika sisi tuliwatii bwana zetu na wakubwa wetu; nao ndio waliotupoteza njia"
"Mola wetu Mlezi! Wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana kubwa" [Al-Ahzaab: 66-68]
Tunakutakia kila la kheri na fanaka pamoja na kuwa na msimamo mwema katika dunia hii na Allaah Akuzidishie mapenzi yako makubwa katika Dini hii na Akuepushe na fitna za dunia na walimwengu.
Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments