Mdhukuru Allaah Kwa Wingi Na Omba Maghfirah Baada Ya Kutenda Mema Katika Siku Kumi Bora Kabisa Za Allaah

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 ((وَاذْكُرُواْ اللّهَ فِي أَيَّامٍ مَّعْدُودَاتٍ))
((Na mtajeni Allah katika zile siku zinazohisabiwa)) [Al-Baqarah:203]
Ibn 'Abbaas (Radhiya Allahu 'anhumaa) kasema: "Siku zinazohisabiwa ni siku za Tashriyq" (11, 12, 13 Dhul-Hijjah) [Al-Qurtubiy: 3.3] Kwa maana ni siku ya piliya tatu na ya nne baada ya siku ya 'Iyd. Hivyo ndivyo Anavyotuamrisha Mola wetu Mtukufu kuwa tumdhukuru baada ya kusherehekea sikukuu yetu ya 'Iydul-Adhwhaa ('Iyd ya kuchinja). Na hivi ndivyo ilivyo desturi ya ibada zetu kuwa zinamalizika kwa kuambatana na mema na si kwa maasi.
Mahujaji wanapotekeleza ibada yao ya Hajj ipasavyo na wanapomaliza kisimamo cha 'Arafah, huwa wameghufuriwa madhambi yao yote kama ilivyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:
  عن عائشة رضي الله عنها_ عن النبي صلى الله عليه وسلم قال  :((ما من يوم أكثر من أن يعتق الله فيه عبدأ من النار من يوم عرفة، وإنه ليدنو ثم يباهي بهم الملائكة فيقول: ما أراد هؤلاء؟))   مسلم   

 Kutoka kwa Mama wa Waumini 'Aishah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Hakuna siku ambayo Allaah Huwaacha waja huru zaidi kutokana na moto kama siku ya 'Arafah, na siku hiyo Allaah Hukaribia (Huteremka katika mbingu ya dunia [kwa namna inayomstahiki Yeye]) kisha kwa fakhari Husema kwa Malaika Wake: Wanataka nini hawa (waja wangu?))?[Muslim]

Na katika usimulizi ufuatao pia imetajwa kufughuriwa kwao madhambi:

عن أبي هريرة رضي الله عنه ((إن الله تعالى يباهي بأهل عرفات ملائكة السماء ، يقول : انظروا إلى عبادي ، أتوني شعثا غبرا من كل فج عميق ، أشهدكم أني قد غفرت لهم))المصدرحلية الأولياء  خلاصة الدرجةصحيح  الشيخ األباني 


Kutoka kwa Abu Huraryah (Radhiya Allaahu 'anhu) ((Allaah Huwafakharisha watu (waliosimama) 'Arafah kwa Malaika wa mbinguni na Husema: Watazameni waja Wangu waliokuja wamejaa nywele, wana mavumbi, wamekuja kutoka kila pande (za dunia) Nakushuhudieni kuwa Nimewaghufuria)) [Hilyat al-Awliyaa – Shaykh Al-Albaaniy kaipa daraja ya swahiyh]


Lakini juu ya kwamba wameghufuriwa, Mola Mtukufu Anawaamrisha Mahujaji wamdhukuru kwa wingi na waombe maghfira Kwake baada ya kumaliza kutekeleza nguzo muhimu kabisa na ambayo ni kilele cha kutekeleza fardhi ya Hajj:


  (( ...فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُواْ اللّهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ وَاذْكُرُوهُ كَمَا هَدَاكُمْ وَإِن كُنتُم مِّن قَبْلِهِ لَمِنَ الضَّآلِّينَ)) (( ثُمَّ أَفِيضُواْ مِنْ حَيْثُ أَفَاضَ النَّاسُ وَاسْتَغْفِرُواْ اللّهَ إِنَّ اللّهَ غَفُورٌرَّحِيمٌ)) (( فَإِذَا قَضَيْتُم مَّنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُواْ اللّهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا ...))

((Na mtakapomiminika kutoka 'Arafaاh mtajeni Allaah penye Mash'aril Haraam. (Muzdalifah) Na mkumbukeni kama Alivyokuongoeni, ijapokuwa zamani mlikuwa miongoni mwa waliopotea)) ((Kisha miminikeni kutoka pale wanapomiminika watu, na muombeni Allaah msamaha: hakika Allaah ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu))  ((Na mkishatimiza ibada zenu basi mtajeni Allaah kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu au mtajeni zaidi))  [Al-Baqarah: 198-200]

Amri hii ya kuomba maghfira na kumdhukuru kwa wingi  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kila baada ya kutenda kitendo chema tunapata katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.  Haya ni mafunzo kwetu kujidhalilisha kwa Allaah (Subhaana wa Ta'ala) na kuishi daima katika hali ya matumaini na khofu (al-khawf war-rajaa). Na hivi ndivyo hali ya Waumini inavyopasa kuwa kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Alipoteremsha Aayah:


((وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَى رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ))  

(Na wale ambao wanatoa walichopewa, na hali nyoyo zao zinagopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao )) [Al-Muuminuun:60]  

Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anhaa), alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ilipoteremshwa Aayah hii: "Ewe Mjume wa Allaah, je, hawa ni wale wale ambao wanaiba, wanazini na kulewa huku wakimkhofu Allaah?" Akajibu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ((Sio ewe bint Abubakar, Bintis-Swiddiyq! Hao ni wanaoswali, wanafunga, wanatoa sadaka na huku wanamkhofu Allaah 'Azza waJalla (Mola Mtukufu)).  [Ahmad]


Tukiangaza katika Siyrah ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tokea kuanza da'awah yake ya Utume, tabu aliyopata, maudhi mbali mbali ya Makafiri wa Ki-Quraysh, watu wake kumtenga, kufukuzwa na kupigwa mawe na watu wa Twaaif, maafa mbali mbali yaliyomjaza huzuni kubwa, juhudi nzito za kupigana vita na Makafiri, na mengi mengineyo, hadi mwisho wa Fat-hu Makkah (Ufunguzi wa (kuitwaa) Makkah), makundi kwa makundi  ya watu waliingia  katika dini ya Kiislam. Mafanikio hayo yamechukua muda wa miaka 23 tokea alipopewa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Utume hadi kukaribia kufariki  kwake. Tujiulize, je, baada ya kufaulu huko, ni jambo gani Mola wake Alimfunza afanye? Jibu ni uteremsho wa Surah  tukufu ifuatayo:


 ﴿ بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾
((إِذَا جَاء نَصْرُ اللَّهِ وَالْفَتْحُ)) ((وَرَأَيْتَ النَّاسَ يَدْخُلُونَ فِي دِينِ اللَّهِ أَفْوَاجًا)) ((فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَاسْتَغْفِرْهُ إِنَّهُ كَانَ تَوَّابًا))

KWA JINA LA ALLAAH MWINGI WA REHMA MWENYE KUREHEMU
((Itakapo kuja nusura ya Allaah na ushindi))  ((Na ukaona watu wanaingia katika Dini ya Allaah kwa makundi))  ((Zitakase sifa za Mola wako  na umwombe msamaha; hakika Yeye Ndiye Anayepokea toba)) [An-Naswr: 1-3]


Ni Surah ya mwisho iliyoteremshwa kikamilifu [kauli ya ibn 'Abbaas katika Swahiyh Muslim]


Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe na hata Maswahaba walitambua kuwa hii ni alama ya kukaribia mauti yake.

Mfano mwengine mzuri tunao wa kipenzi cha Allaah na rafiki Yake (Khaliylul-AllahNabii 'Ibraahiym (alayhis-salaam) alipomaliza kujenga Ka'abah yeye na mwanawe Ismaa'iyl. Ka'abah hiyo inayozungukwa na mamilioni ya Waislamu kama ni ibada tukufu tokea siku hizo hadi siku ya Qiyaamah. Lakini hawakutegemea kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Atawapokelea amali hiyo moja kwa moja, bali kwanza wamemuomba Mola Awatakabalie kisha Awaghufurie:

 ((وَإِذْ يَرْفَعُ إِبْرَاهِيمُ الْقَوَاعِدَ مِنَ الْبَيْتِ وَإِسْمَاعِيلُ رَبَّنَا تَقَبَّلْ مِنَّا إِنَّكَ أَنتَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ)) (( رَبَّنَا وَاجْعَلْنَا مُسْلِمَيْنِ لَكَ وَمِن ذُرِّيَّتِنَا أُمَّةً مُّسْلِمَةً لَّكَ وَأَرِنَا مَنَاسِكَنَا وَتُبْ عَلَيْنَآ إِنَّكَ أَنتَ التَّوَّابُالرَّحِيمُ))
((Na kumbukeni Ibraahiym na Ismaa'iyl walipoinyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ee Mola wetu! Tutakabalie! Hakika Wewe Ndiye Msikizi Mjuzi)) ((Ewe Mola  wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu Kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe Ummah uliosilimu Kwako. Na Utuonyeshe njia za ibada yetu na Utusamehe. Bila shaka Wewe Ndiye Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu)) [Al-Baqarah: 127-128]


Vile vile Kipenzi chetu Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa kila tunapomaliza ibada ya fardhi  ya Swalah zetu tano, tuombe maghfira mara tatu kwa kusema:

أَسْـتَغْفِرُ الله   
AtastaghfiruLLah


“Naomba msamaha Allah” (mara tatu)  

Ikiwa hali ni kama hizo tulizozitaja zote, basi na sisi tutakapomaliza kutenda mema katika siku Kumi Bora Kabisa za Allah, za Dhul-Hijjah, inatupasa tuombe maghfira na tumdhukuru  kwa wingi  Allaah kwani hatujui kama vitendo vyetu vitakuwa vimetakabaliwa au la. Desturi hii tuwe tunaidumisha daima tunapotoka kumaliza kitendo chochote chema tukifanyacho kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).  


Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kuzidisha juhudi kufanya mema mengi tukiwa na matumaini na pia khofu ya kukubaliwa  amali zetu.  Aamiyn.

0 Comments