FIQHI : MLANGO WA KUKOGA

Nini Kukoga?

Kukoga kilugha ni kumwagia na kueneza maji kiwiliwili chote. Ama Kisharia ni kumwagia na kueneza maji kiwiliwili chote nje na ndani na kwa nia khaasa.

Yenye Kuwajibisha Kukoga
Yenye kuwajibisha kukoga ni mambo sita, matatu huwa kwa wanaume na wanawake:
Mosi, kukutana tupu mbili, yaani kuzama kichwa cha utupu au kadiri ya hivyo ndani ya utupu wa mbele au wa nyuma, wa binaadam au wa mnyama. Ikiwa ni pamoja na kutokwa na manii au bila ya kutokwa na manii. Asili ya haya ni qauli ya Sayyidah 'Aisha r.a. ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:
"Zikikutana tupu mbili au ukagusa utupu wa mwanamume utupu wa mwanamke, inawajibisha kukoga; nimefanya hivyo mimi na Mtume s.a.w., tukakoga". (Imehadithiwa na Muslim).
Pili, kutokwa na manii, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
 " "  "Hakika ya maji ni kwa maji". (Imehadithiwa na Muslim).
Kutokwa na manii, ni sawa ikiwa usingizini au nje ya usingizi, na sawa sawa ikiwa kwa matamanio au bila ya matamanio; ni kwa hali yoyote ile.
Hivi ni kutokana na hii Hadithi yenyewe ambayo haikuja na shuruti ndani yake.
Manii yana sifa tatu:
Ya Kwanza, yana harufu kama unga ulioumka au harufu ya kitale kibichi cha mtende (mnazi).
Ya Pili, yanatoka kwa kuchupa, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu
 " Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa ".       (A'ttaariq : 6).
Tatu, kuona raha yanapotoka na kufuatiliwa na kulegea dhakari (utupu wa mwanamume) na kukatika matamanio wakati huo.
Mwanamke ni tafauti na mwanamume, kwani maji ya mwanamke tafauti na maji ya mwanamume; wala maji ya mwanamke hayatoki kwa kuchupa. Na lau akiamka akaona ukavukavu mweupe kwenye nguo yake, haimlazim kukoga; kwani wadii pia nayo yana ukavukavu na weupe kama wa manii. Katika hali hii itakuwa ni khiyari yake kuchukulia kuwa hayo ni wadii wala si manii na akakosha dhakari yake bila ya kulazimika kukoga, au kuyajaalia kuwa ni manii; akakoga. Ikiwa atachukulia kuwa ni manii, akakoga, kisha yakatoka tena kwa sifa hio hio; basi itamuwajibikia kukoga tena.
La Tatu lenye kuwajibisha kwa mwanamume na kwa mwanamke kukoga, ni mauti. Hivi ni kutokana na qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kukhusu mtu aliekuwa kwenye ihraam akapigwa teke na ngamia wake akafa, akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Mwosheni kwa maji na (majani ya) mkunazi". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Ama mambo matatu ambayo yanawajibisha kukoga na yanawakhusu wanawake tu ni haya:
Mosi, hedhi, yaani damu ya siku zao wanawake; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
  "…… Wala msiwaingilie mpaka wat’ahirike. Wakisha t’ahirika basi waendeeni alivyo kuamrisheni Mwenyezi Mungu." (Al Baqarah : 222).
Na Hadithi ya Sayyidah 'Aisha r.a. ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema: "Ikikujia hedhi, usisali; ikiondoka kwa kiyasi cha muda wake; koga na usali". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Pili, damu ya uzazi, hii ni kama hedhi; Masahaba r.a. wamekubaliana ya kwamba nifasi ni sawa na hedhi.
Tatu, kuzaa; hata ikiwa ni kwa kutoka pande la damu tu, yaani kabla ya kuwa umbo la mtoto. Kuwajibika kukoga kwa hali hii kunatokana na sababu mbili, kwanza ni kwa ile dhana ya kutoka damu wakati wa kuzaa; na kwa hivyo hukmu imejengeka juu ya hii dhana, kama vile kudhaniwa kutokwa na udhu hali ya kuwa usingizini, pili ni vile kuwa binaadam ameumbika kutokana na manii ya mwanamume na manii ya mwanamke, na kutokwa na manii kunawajibisha kukoga.

Fardhi za Kukoga

Fardhi za kukoga ni mbili.
Kwanza, kutia nia; hivi ni kutokana na qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "Hakika ya kusihi ibada (kitendo) ni kulingana na nia". Na hii nia mahala pake ni moyoni, yaani si lazima kutamka; na hutiwa nia wakati wa kuosha sehemu ya kwanza ya kiwiliwili. Nia yake ni kunuia mwenye janaba kuwa kukoga kwake ni kwa ajili ya kuondoa janaba au kuondoa hadathi kubwa mwili mzima. Na mwenye hedhi atanuia kuondoa hadathi ya hedhi na mwenye nifasi atanuia kuondoa hadathi ya nifasi. Na inashurutishwa kusihi kuondoa hadathi kubwa kuwa kwanza kuondoa najsi yoyote iliomo mwilini, kama vile damu na kadhaalika; hivi ni kutokana na qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "Basi jioshe damu na usali".
Pili, kufikisha maji kwenye maoteo yote ya nywele na kwenye ngozi; hivi ni kutokana na qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  "Chini ya kila unywele pana janaba, basi zitieni maji vyema nywele zenu na ngozi zenu".
Pia imepokewa kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:
   "Hakika chini ya kila unywele pana janaba, basi osheni nywele zenu na osheni vyema ngozi zenu (miili yenu)". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhii na Ibnu Maajah).
Na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
   "Mwenye janaba akiwacha sehemu ya unywele bila ya kuuwosha basi atafanyiwa hivi na hivi huko Motoni".
Na ikiwa ni mwenye kucha ndefu zenye kuzuia maji kufika kwenye ngozi ya vidole, itamlazim azikate ili maji yaweze kufika kwenye ngozi. Hivi ni kutokana na qauli za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. zilizotangulia kutajwa hapo juu kukhusu dharura ya kukoshwa kila ugozi na unywele wa mwenye janaba, hedhi au nifasi.
Imepokewa kutoka kwa Ummu Ssalamah r.a. ya kwamba alimwambia Mtume wetu Mpenzi s.a.w. ya kuwa yeye (Ummu Ssalamah) ana nywele nyingi, jee azikate kwa ajili ya kukoga janaba? Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akamwambia:
 "Laa, (usizikate) inakutosheleza kusuguwa sana kichwa chako kwa maji mara tatu kisha ujimiminie maji, kwa kufanya hivyo uta'taharika na janaba". (Imehadithiwa na Muslim katika kitabu chake - 'Sahih Muslim).
Na kwa Hadithi nyengine kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alisema:
  "Kisha utajimiminia maji sehemu ya mwili iliobaki". (Imehadithiwa na Ahmad kutoka kwa Ummu Ssalamah).
Ama ngozi ya mwili inalazim kuiosha kwa kufikisha maji kila sehemu ya mwili hata sehemu yenye kuonekana ya masikio. Pia ni lazima kuosha mipasuko na mipindo na mikunjano yote ya mwili, pia ikiwa haja'tahiriwa (haja katwa govi) basi itabidi alifidue ili apate kukikosha kichwa cha dhakari yake. Vile vile mwanamke inampasa aoshe sehemu ya uchi wake inayodhihiri akichutama. Na inampasa aondoe (asafishe) kila chenye kuzuia maji kufika kwenye mwili wake na kucha zake, kama vile rangi ya kucha.Hina si lazima kuiondoa, kwani hina haizui kufika maji juu ya sehemu ya kucha yenye kupasa kukoshwa kuwa ni sehemu ya kukoga janaba; hivi ni kwa vile kuwa hina haina rangi ya kuganda.

Sunna za Kukoga Kuondoa Janaba, Hedhi au Nifasi

Sunna za kukoga kwa ajili ya kuondoa hadath kubwa ni nyingi, miongoni mwa sunna hizo ni kusoma  ,(Bismi Llahi Rrahmani Rrahim) kukosha viganja kabla ya kuvichovya ndani ya chombo chenye maji ya kukogea; hili limeelezwa pia kwenye mlango wa udhu. Vilevile miongoni mwa sunna za kukoga kwa kuondoa hadath kubwa ni kutanguliza kutia udhu kaamili, hivi ni kutokana na qauli ya Sayyidah 'Aisha r.a.:
 
"Alikuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. anapotaka kukoga kuondoa janaba hutia udhu kaamili kama anapotaka kusali". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Na amesimulia Imam Al Bukhari r.a. kuwa amepokea kutoka kwa Maimunah r.a.:  "Ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alikuwa ana akhirisha kuosha miguu yake."
Amesema Al Qadhi Hussain: "Akikhiarisha baina ya kutia udhu kaamili na baina ya kuakhirisha (kuosha) miguu mpaka anapo kamilisha kukoga, hivi ni kwa vile imepokewa kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amefanya hali zote mbili. Pia miongoni mwa sunna za kukoga ni kusugua kila sehemu ya mwili kama inavyo yumkinika, kufanya, hivi ni kuepuka khitilafu za qauli za wanazuoni kuwa ni waajibu kujisugua au si waajibu. Pia ajitahidi kuosha sehemu za mwili zilizofichika, kama vile kwapa, kitovu, masikio na mipindo ya tumbo. Miongoni mwa sunna ni kufululiza, yaani kukosha kiungo kabla ya kukauka kiungo. Pia miongoni mwa sunna za kukoga ni kutanguliza kulia kabla ya kushoto, hivyo ataanza kwa kukosha kichwa kisha atakosha upande wake wa kulia kisha ataosha upande wake ya kushoto. Hivi ni kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alikuwa akipenda kutanguliza kuanzia kulia katika kuji'tahirisha.
Kwa hakika Waislam kutanguliza kulia ni sunna katika mambo yao, hata wanaitwa "watu wa mkono wa kulia". Miongoni mwa sunna pia ni kukosha mara tatu tatu, hivyo ataosha kichwa mara tatu, kisha ataosha sehemu yake ya mwili yote mara tatu tatu, hivi pia ni katika sunna za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Na inapendekezwa maji ya kukogea yasipungue pishi na mji ya kutilia udhu yasipungue kibaba. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Safinah r.a.: "Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alikuwa akikoga maji ya pishi na akitia udhu kwa kibaba cha maji."
Wala si sunna kujadidi kukoga, kwani haijaja Hadithi juu ya hivyo; pia ni mashaka, tafauti na kutia udhu, kutia udhu tena baada ya kuusalia Sala moja ni sunna. Hivi ndivyo ilivyopokewa kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema: "Mwenye kujadidi udhu (yaani kutia udhu na anao udhu) Mwenyezi Mungu Mtukufu humuandikia hasanati (thawabu) kumi." Hivi ni kwamba awali ya Uislam ilikuwa ni waajibu kutia udhu kwa kila Sala, ikaondoshwa kuwajibika ikabaki asili ya hali bila ya kuwa ni waajibu, ikawa ni sunna. Pia inapendekezwa asinyowe wala asikate kucha hali ya kuwa yumo katika janaba (au hedhi au nifasi), ili akikoga iwe kila sehemu ya kiwiliwili chake kipate 'tahara. Akimaliza kukoga aseme:
 
"Ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba hapana Mola anaejuzu kuabudiwa kwa haqi isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Pekee, na ninashuhudia kwa qauli na kuqiri moyoni ya kwamba Muhammad s.a.w. ni Mtumwa na Mjumbe wa Mwenyezi Mungu Mtukufu".
Hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. baada ya kukamilisha kukoga.
Ni haraam mtu kukoga mbele za watu bila ya nguo, mwenye kufanya hivyo huaziriwa kwa kiasi cha hali ya hishima yake. Na ni haraam kwa wanaomuona akifanya hivyo mbele yao kumuacha kufanya hivyo, ni waajibu juu yao kumkanya kufanya hivyo. Wao wakinyamaza bila ya kumkanya hivyo kukoga uchi mbele yao, basi nao watapata dhambi na  watastahiki nao kuaziriwa vilevile. Hivi ni kutokana na qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:   "Mwenyezi Mungu Mtukufu amemlaani mwenye kutizama na mwenye kutizamwa".
Ama akikoga katika stara mbali na watu inajuzu kukoga uchi. Lakini kujisitiri wakati wa kukoga ni afadhali, hivi ni kwa vile Utukufu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kustahiki staha zaidi.
Na mtu akiingia mahala wanapokoga watu basi ainamishe macho yake asitizame watu wanaokoga na vilevile ajistiri anapokoga kuepusha kuonekana hali ya kuwa hana nguo. Ameeleza Imam Al Qur'tubii r.a. kukhusu tafsiri yake juu ya Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
  "Waandishi wenye hishima, Wanayajua mnayo yatenda". (Al Infint'ar : 11-12).
Ameeleza Imam Al Qur'tubii r.a. ya kwamba mtu akiingia "hamamni", (mahala pakukogea watu) hali ya kuwa uchi basi Malaika wake wawili humlaani. Amepokea kutoka kwa Jabir r.a. ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema: "Haraam kwa mwanamume kuingia mahala pakukogea (hamamni) bila ya (kuvaa) seruni/kikoi/suruali".
Ikiwa imeharimishwa kitendo hicho kwa wanaume, basi ni zaidi kwa wanawake, kwani wanawake ni wenye kuwajibika zaidi na stara.

Majosho ya Sunna

Imesuniwa kukoga katika siku/hali nyingi, miongoni mwa siku/hali zilizo suniwa kukoga ni siku ya Ijumaa. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  “Mwenye kutia udhu siku ya Ijumaa ndivyo inavyofaa na ni neema juu yake, na mwenye kukoga; basi kukoga ni afadhali". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy).
Amesema Imam Al Nawawi r.a. kuwa hii ni Hadithi sahihi, na maimam wengine wamewajibisha kukoga siku ya Ijumaa wakichukulia hoja kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. pale aliposema: "Mwenye kwenda kusali Sala ya Ijumaa, basi naakoge". (Imehadithiwa na Muslim).
Kwa Hadithi hii inadhihiri kuwajibika kukoga kwa mwenye kwenda kusali Sala ya Ijumaa. Imezidi kudhihiri kuwajibika huku kwa Hadithi hii nyengine ifuatayo ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Kukoga siku ya Ijumaa ni waajibu kwa kila baalegh". (Imehadithiwa na Al Sheikhan na wengineo).
Zimekuja hoja kuwa kukoga siku ya Ijumaa si waajibu (si lazima), bali ni sunna iliotiliwa nguvu. Imejengwa hoja ya kutowajibika kukoga kwa kuhudhuria Sala ya Ijumaa ya kwamba siku moja wakati Sayyidna Omar bin Alkha'taab r.a. anakhutubu katika Sala ya Ijumaa aliingia Sayyidna Othman bin 'Affan r.a. kachelewa, Sayyidna Omar r.a. akampigia ukelele kumuuliza: "Saa ngapi hivi sasa"? Sayyidna Othman r.a. akajibu kwa kusema: "Nilizongwa na shughuli sikufika nyumbani kwangu ila baada ya kusikia muadhini, hapo sikuwahi isipokua kutia udhu na kukimbilia Sala". Hapa Sayyidna Omar r.a. hakumuamrisha Sayyidna Othman r.a. kuwa akakoge, hivi ikaonesha kuwa kukoga kwa kuhudhuria Sala ya Ijumaa si waajibu, kwani lau kama ni waajibu basi Sayyidna Omar r.a. angalimuamrisha Sayyidna Othman r.a. kwenda kukoga na yeye Sayyidna Othaman r.a. asingaliwacha kukoga.

Kuingia Wakati wa Kukoga Kwa Kuhudhuria Sala ya Ijumaa

Unaingia wakati wa kukoga kwa kuhudhuria Sala ya Ijumaa inapoingia alfajiri ya siku ya Ijumaa. Kuakhirisha mpaka karibu na kwenda msikitini ni bora, kwani madhumuni ya huku kukoga ni kutokana na harufu mbaya inayosabishwa na zahma na mashughuli. Lau akichelea kumpita Sala ikiwa ataingia kukoga, basi atakimbilia Sala bila ya kukoga; kwani Sala ni fardhi na kukoga ni sunna.
Pia katika hali zinazosuniwa kukoga ni kwa kuhudhuria Sala ya Idi mbili, Idi-l-fi'tri na Idi-l-Adh-ha; hivi ni kwa qauli ya Ibni 'Abbas r.a. kwamba:
   "Alikuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. anakoga siku ya Idi-l-fi'tri na Idi-l- Aldh-ha".
Pia Sayyidna Omar r.a. na Ibnu Omar r.a. na Sayyidna 'Ali r.a. wakifanya hivyo. Hivi ni kwa vile siku ya Idi ni siku wanayo kusanyika watu kwenye Sala. Kukoga kwa kuhudhuria Sala ya Idi inafaa tangu baada ya Sala ya Alfajiri. Pia ni sunna kukoga kwa kuhudhuria Sala ya kuomba mvua, Sala ya kupatwa mwezi na Sala ya kupatwa juwa. Hivi ni kwa vile mote humu ni kukusanyika watu, kwa hivyo ni sunna kukoga kama vile ilivyo sunna kukoga kwa kuhudhuria Sala ya Ijumaa. Haya Inshaallah tutayaeleza kwa uwazi katika mlango wake huko mbele. Pia ni sunna kukoga kwa alieosha maiti, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
   "Aliekosha maiti naakoge, na aliechukua maiti naatie udhu".
Na amri hii iliokuja kwenye Hadithi hii haimaanishi kuwa ni waajibu (lazima) kukoga baada ya kuosha maiti, hivi ni kwa hizi Hadithi zifuatazo:
  "Hakika ya maiti wenu wanakufa hali yakuwa 'taahir, basi inakutoshelezeni kukosha mikono yenu". (Imehadithiwa na Al Bayhaqy).
Na imepokewa vilevile:  "Tulikuwa tunawaosha maiti wetu, wako kati yetu tuliokuwa tukikoga; na wako kati yetu tuliokuwa hatukogi". (Imehadithiwa na Alkha'tib).
Pia imepokewa:  "Si lazima juu yenu kukoga baada ya kuosha maiti wenu". (Imehadithiwa Al Haakim).
Na miongoni mwa hali zinazosuniwa kukoga ni kwa kafiri pale anaposilimu. Hivi ni kwa ilivyopokewa ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. aliwaamrisha Qais bin 'Aa'sim na Thumamah bin Athal wakoge pale waliposilim, lakini hakulazimisha juu yao kukoga, hivi ni kwa vile walisilim jamaa na wala Mtume wetu Mpenzi s.a.w. hakuwalazimisha kukoga. Haya ni kwa sababu kusilim ni kutubia kutokana na maasi ya kuwa si Islam, na kutubia kokote kule hakuwajibishi kukoga. Hivi ni kwa yule ambaye hakupatwa na janaba, hedhi au nifasi wakati bado hajasilim; lakini ikiwa amepatwa na janaba, hedhi au nifasi wakati bado hajasilim, itamuwajibikia akoge mara tu anaposilim ili awe 'taahir, ili zipate kusihi ibada zake, kama vile kusali, kusoma Qur'ani, na ibada zote zile ambazo hazisihi bila ya 'tahara, haya mbali na kuwajibika juu yake kutia udhu kama inavyo hitajika.
Pia miongoni mwa hali zenye kusuniwa kukoga ni pale anapopata fahamu/kurejea akili yake mtu aliepatwa na wazimu, pia mtu aliezimia pale anapozindukana. Imesuniwa kukoga katika hali hizi kwa vile kutokea kutokwa na manii wakati wa hali ya wazimu na/au kuzimia.
Amesema Imam Shafi'ii r.a. ya kwamba:
 "Hatokwi na akili, au hazimii mtu ila hutokwa na manii".
Pia katika hali zenye kusuniwa kukoga ni kwa ajili ya kuhirimia kutekeleza ibada ya 'Umra au/na ya Hija. Imepokewa kutoka kwa Zaid bin Thaabit r.a.:  "Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alijitayarisha kuingia kwenye ihraam na akakoga". (Imehadithiwa na Al Tirmidhy). Kufanya hivi ni sawa ikiwa kwa mwanamume, au mwanamke, mtumzima au mtoto. Kufanya hivi pia ni kwa yule aliomo kwenye hedhi au kwenye nifasi au kwa mwenye janaba. Hoja ya haya ni kwamba Asma bint 'Umais r.a., mke wa Sayyidna Abu Bakar r.a. alipatwa na nifasi wakati yuko Dhi-l-hulaifah; Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akamuamrisha akoge kwa ajili ya kuhirimia.  (Imehadithiwa na Muslim).
Wamesema Al Baghwy na Al Muhamily: "Wala hapana tafauti baina ya mwenye akili na asiekuwa na akili, na wala baina ya mtoto baalegh na asiekuwa baalegh". Ikiwa mtu wakati wa kuhirimia hakupata maji ya kukoga, basi atatayamam, ikiwa atapata maji ambayo hayatoshi kukoga, basi atatia udhu kwa maji hayo; na sunna ya kukoga itakuwa iko bado juu yake; atatayamam kwa kutekeleza sunna ya kukoga.
Pia katika hali zenye kusuniwa kukoga ni kwa kuingia Makka. Ibnu 'Umar r.a. alikuwa haingii Makka isipokua hulala Bidhi'tawi ili kumpambazukie hapo, akoge kisha ndio aingie Makka mchana wake.
Na inasemwa kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. hivi ndivyo alivyokuwa akifanya. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Hii sunna ya kukoga kwa kuingia Makka si sharti iwe kwa kuhiji au kufanya 'Umra au kwa lolote kati ya mawili haya, bali basi kwa kutaka kuingia Makka ni sunna kukoga. Amesema Imam Shafi'ii r.a. kwenye kitabu chake "Al-Umm", ya kwamba hata asietia ihraam basi pia nae ni sunna kukoga kwa kuingia Makka, haya yametolewa hoja kwa kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Mwaka wa Ufunguzi wa Makka, alikoga kwa kuingia Makka na hali hakuwa mwenye kuhirimia; akitia manukato. Na katika hali zenye kusuniwa kukoga ni siku ya kusimama 'Arafa, hivi ni kwa vile Ibnu 'Umar r.a. alikuwa akifanya hivyo. Yameelezwa haya na Imam Malik r.a. na akaeleza Ibnu-l-khal r.a. kutokana na Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Sunna hii ni kwa vile siku ya kusimama 'Arafa ni siku ya mkusanyiko mkubwa wa waumini, na kwa kila mkusanyiko wa waumini wa kidini imesuniwa kukoga, kama vile kuhudhuria Sala ya Ijumaa, Idi mbili, Sala ya kupatwa juwa au kupatwa mwezi, au Sala ya kuomba mvua; mote humu imesuniwa kwa mwenye kuhudhuria kukoga. Vilevile imesuniwa kukoga kwa mwenye kwenda kupiga (kulembea) jamrat, isipokuwa wakati wa kupiga jamrat-l-aqaba; kwa vile kuwa karibu na wakati wa kisimamo.   Tafauti na wakati wa kulembea kwenye zile jamaraat nyengine, na ni kwa vile kuwa ni kati ya mchana, yaani mara tu baada ya juwa kupindukia, na hivi pia ni kwa kuwa ni wakati wa watu kukusanyika; kwa hali hii ndio ikasuniwa kukoga kwa mwenye kwenda kulembea jamrat (isipokuwa jamraat-l-aqaba).
Pia imesuniwa kukoga kabla ya ku'tufu, sunna hii ni kwa 'tawaaf zote tatu; sunna hii nayo ni kwa vile 'tawaaf kuwa ni mkusanyiko wa waumini. Imam Shafi'ii r..a. nae ametilia nguvu juu ya hii sunna ya kukoga kwa ajili ya 'tawaaf, zote tatu.
Na imesuniwa kukoga kwa ajili ya kukaa 'itikaaf (msikitini). Imam Shafi'ii r.a. nae ametilia nguvu juu ya sunna hii. Pia imesuniwa kukoga kwa kuingia Madina - mji wa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Kama ilivyosuniwa kukoga katika kila usiku wa mwezi wa Ramadhani. Pia katika hali zilizosuniwa kukoga ni kwa mwenye kunyowa nywele za chini (nywele za kinena). Imehadithiwa ya kwamba Imam Shafi'ii r.a. amesema kuwa yeye anapenda kukoga baada ya kuumika, na kuingia hamamni, na katika kila hali ambayo hubadilisha hali ya kiwiliwili au hukidhoofisha; hivyo kwa sababu kukoga kuna changamsha mwili na kuna tia nguvu upya. Haya ya kiwiliwili kupata uchangamfu kwa kukoga, ni ndivyo kabisa; kwani maji ni yenye kuhuwisha.
Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia kwa maji uhai wa kila kitu:
  “……Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? ….”. (Al Anbiyaai : 30).

0 Comments