صَبْرٌ جَمِيلٌ Subira Njema - Yapasayo Na Yasiyopasa Wakati Wa Mitihani

Kwa vile subira ni kuzuia ulimi usinene yasiyopasa wala kumshtakia yeyote isipokuwa kumshtakia Allaah (سبحانه وتعالى), na moyo uvumilie asimahanike mtu na kukata tamaa, na viungo visitende yaliyoharamishwa kama kujipigia mashavu na kuchana nguo n.k., basi hana budi Muumini kuvumilia.

Yafuatayo anapaswa kuzingatia na kutekeleza au kujiepusha nayo:

1-Kuridhika Na Majaaliwa Na Kusalimu Amri

Muumini atambue kwamba kila linalomfika ni majaaliwa yaliyokwishakadiriwa katika Lawhum-Mahfuudhw (Ubao Uliohifadhiwa), kwa hiyo hana budi nayo, bali aridhike nayo apate radhi za Mola wake na ujira wa kuvumilia. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

((مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الأَرْضِ وَلا فِي أَنفُسِكُمْ إِلاَّ فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا إِنَّ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ)) ((لِكَيْلاَ تَأْسَوْا عَلَى مَا فَاتَكُمْ وَلاَ تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ وَاللَّهُ لاَ يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ))  

((Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwishaandikwa katika Kitabu kabla Hatujauumba. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi)) ((Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa Alichokupeni. Na Allaah Hampendi kila anayejivuna akajifakhirisha))[1]

Bali Muumini anapaswa kuwa na tawakuli na Allaah (سبحانه وتعالى):

((قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلاَّ مَا كَتَبَ اللّهُ لَنَا هُوَ مَوْلاَنَا وَعَلَى اللّهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ))

((Sema: Halitusibu ila alilotuandikia Allaah. Yeye Ndiye Mola wetu Mlinzi, na Waumini watawakali kwa Allaah))[2] 

Na huko ndiko kuthitibisha imani yake Muumini kwa  kuridhika na majaaliwa:    

((مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلاَّ بِإِذْنِ اللَّهِ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّهِ يَهْدِ قَلْبَهُ وَاللَّهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ))

((Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Allaah. Na mwenye kumuamini Allaah Huongoa moyo wake. Na Allaah ni Mjuzi wa kila kitu))[3]


2- Kutokumshtakia Kiumbe (Kutokulalamika Kwa Mtu)

Kulalamika au kushtaki kwa watu kunaharibu subira na kumkosesha mtu fadhila zake, kwani anayeshtaki mitihani ya Mola wake kwa kiumbe huwa amemshtakia ambaye hawezi kumnufaisha au kumuokoa katika mitihani yake. Bali amshtakie Mola wake Ambaye ni Pekee Mwenye uwezo wa kumteremshia Rehma Yake na kumpa faraja. Mmoja miongoni mwa Salafus-Swaalih alipomuona mtu anamshtakia mwenziwe alimwambia:
“Vipi unamshtaki Anayekurehemu kwa asiyekuwa na uwezo wa kukurehemu?”

Nabii Ayyuub (عليه السلام)  ametupa mfano bora pale alipojazwa na huzuni kwa kumkumbuka mwanawe mpenzi Yuusuf na kisha kupotelewa na mwanawe wa pili bin Yamiyn akasema:

((إِنَّما أشكُوا بَثِي وَحُزنِي إلى اللّهِ)) 

((Hakika mimi namshitakia Allaah sikitiko langu na huzuni yangu))[4]

Lakini inafaa kumshtakia mtu pale anapofikwa na hali ya kuhitaji msaada wa mtu aliojaaliwa na Allaah (سبحانه وتعالى), na si msaada ambao Allaah (سبحانه وتعالى) Pekee Ndiye Mwenye uwezo nao. Mfano, kulalamika dhulma anayotendewa na mwenzake inayoendelea ikiwa anayeshtakiwa ana mamlaka ya kumwepusha na anayemdhulumu, au anapotafuta msaada wa gharama za matibabu ya maradhi yake, au kuomba msaada wa kutatua jambo fulani gumu n.k. kwa kuitikadi kwamba uwezo huo unatokana na Nguvu na Uwezo wa Allaah (سبحانه وتعالى) Aliomjaalia huyo msaidizi.   


3- Kuomba Maghfira Na Toba

Huenda ikawa mitihani inayomsibu mtu ni kutokana na madhambi aliyoyatenda hivyo ni vyema arudi kwa Mola wake kuomba maghfira na toba. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى):

((ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ))

((Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyoyafanya mikono ya watu, ili Allaah Awaonyeshe baadhi ya waliyoyatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu))[5]


((وَمَا أَصَابَكُم مِّن مُّصِيبَةٍ فَبِمَا كَسَبَتْ أَيْدِيكُمْ وَيَعْفُو عَن كَثِيرٍ))


((Na misiba inayokusibuni ni kwa sababu ya iliyotenda mikono yenu. Naye Anasamehe mengi))[6]


4-Kumdhukuru Na Kumshukuru Sana Allaah

Kila unapomdhukuru Allaah (سبحانه وتعالى) Naye Hukukumbuka. Kauli nzuri iliyoje Yake Allaah (سبحانه وتعالى) Anaposema:

((فَاذْكُرُونِي أَذْكُرْكُمْ وَاشْكُرُوا لِي وَلا تَكْفُرُونِ))

((Basi nidhukuruni, Nikukumbukeni, na Nishukuruni wala msinikufuru))[7]

Tunajua kwamba kila kheri na shari ni mtihani kwetu, na katika hali zote inatupasa kumshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) ili kudhihirisha yakini ya kuamini Qadhwaa na Qadar[8]. Na hivo ndivyo ilivyo sifa ya Muumini bali huwa ni jambo la kuwastaajibsha wengineo kwa sifa yake hiyo ya ukamilifu wa imani:

((عَجَبًا لإَمْرِ الْمُؤْمِنِ إِنَّ أَمْرَهُ كُلَّهُ خَيْرٌ, وَلَيْسَ ذَاكَ لإَحَدٍ إلاَّ لِلْمُؤْمِنِ. إِنْ أَصَابَتْهُ سَرَّاءُ شَكَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ, وَإِنْ أَصَابَتْهُ ضَرَّاءُ صَبَرَ فَكَانَ خَيْرًا لَهُ))مسلم

((Ajabu ya jambo la Muumin kwamba kila jambo lake ni kheri. Na halipatikani hili isipokuwa kwa Muumin. Anapofikwa na jambo zuri hushukuru nayo ni kheri kwake na anapofikwa na jambo lenye madhara husubiri nayo ni kheri kwake))[9]  

Allaah (سبحانه وتعالى) Ameahidi kwamba kila mara mja Wake anapomshukuru, Humzidishia neema, na anapokanusha basi ametoa onyo la adhabu kali.


((وَإِذْ تَأَذّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لأَزِيدَنَّكُمْ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيد))

((Na Alipotangaza Mola wenu: Mkishukuru Nitakuzidishieni; na mkikufuru, basi adhabu Yangu ni kali))[10]

Na kutokuridhika na majaaliwa ya mja, ni aina mojawapo ya kukanusha au kukufuru makadirio ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwani hakuna mtihani au msiba unaomsibu mtu isipokuwa kwa amri Yake. Lililo la muhimu kwa mja ni kusalimu amri, kuridhika na kutegemea malipo mema ya duniani na Akhera. Anasema Allaah (سبحانه وتعالى) baada ya kauli Yake kuhusu kifo cha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wakati walipofadhaika Maswahaba hata wakafikia kutokuamini kuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) amefariki:

 ((وَمَا مُحَمَّدٌ إِلاَّ رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ أَفَإِن مَّاتَ أَوْ قُتِلَ انقَلَبْتُمْ عَلَى أَعْقَابِكُمْ وَمَن يَنقَلِبْ عَلَىَ عَقِبَيْهِ فَلَن يَضُرَّ اللّهَ شَيْئًا وَسَيَجْزِي اللّهُ الشَّاكِرِينَ)) ((وَمَا كَانَ لِنَفْسٍ أَنْ تَمُوتَ إِلاَّ بِإِذْنِ اللَّهِ كِتَابًا مُؤَجَّلاَ وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الدُّنْيَا نُؤْتِهِ مِنْهَا وَمَنْ يُرِدْ ثَوَابَ الآخِرَةِ نُؤْتِهِ مِنْهَا وَسَنَجْزِي الشَّاكِرِينَ)) 

((Na Muhammad si yeyote ila ni Mtume tu. Wameshapita kabla yake Mitume. Je akifa au akiuawa mtageuka nyuma ya visigino vyenu [mtarudi katika ukafiri]? Na atakayegeuka nyuma kwa visigino vyake basi hatamdhuru Allaah lolote. Na Allaah Atawalipa wenye kushukuru)) ((Na nafsi yeyote [haiwezi] haifi ila kwa idhini ya Allaah, yameandikwa muda wake maalumu. Na anayetaka thawabu za dunia Tutampa. Na anayetaka thawabu za Akhera Tutampa na Tutawalipa wanaoshukuru))[11] 


5- Kutokuombeleza Nje Ya Mipaka Ya Shari’ah

Kuombeleza kwa kujipiga mashavuni na kuchana nguo au kulaani wakati, au kupandisha sauti ya kilio na kusema maneno tele na kuojiombea maangamizi n.k. ni miongoni mwa mambo yaliyoharamishwa katika misiba.   

عَنْ عَبْدُ الله ابْن مَسْعُودٍ (رضي الله عنه) عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ:  ((لَيْسَ مِنَّا مَنْ ضَرَبَ الْخُدُودَ وَشَقَّ الْجُيُوبَ وَدَعَا بِدَعْوَى الْجَاهِلِيَّةِ)) متفق عليه

Imepokelewa toka kwa ‘Abdullahi bin Mas’uud (رضي الله عنه) amesema: Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم ) amesema: ((Si miongoni mwetu anayejipiga mashavu, akachana nguo na akaomba maombi ya kijahiliya))[12] 

Muislamu ana haki ya kubakia katika huzuni isiyozidi siku tatu. Baada ya hapo inampasa kujirudisha katika hali yake ya kawaida ya kimaisha na si kujiwekea masiku ya kuombeleza. Imekatazwa hayo katika masimulizi yafuatayo:


عَنْ زَيْنَبَ بِنْتِ أَبِي سَلَمَةَ (رضي الله عنهما) قَالَتْ: دَخَلْتُ عَلَى أُمِّ حَبِيبَةَ (رضي الله عنها) زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ حِينَ تُوُفِّيَ أَبُوهَا أَبُو سُفْيَانَ بْنُ حَرْبٍ ، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فِيهِ صُفْرَةُ خَلُوقٍ، أَوْ غَيْرِهِ،  فَدَهَنَتْ مِنْهُ جَارِيَةً، ثُمَّ مَسَّتْ بِعَارِضَيْهَا . ثُمَّ قَالَتْ: وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ، إِلا عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) قَالَتْ زَيْنَبُ: فَدَخَلْتُ عَلَى زَيْنَبَ بِنْتِ جَحْشٍ (رضي الله عنها) حِينَ تُوُفِّيَ أَخُوهَا، فَدَعَتْ بِطِيبٍ فَمَسَّتْ مِنْهُ ثُمَّ قَالَتْ: أَمَا وَاللَّهِ مَا لِي بِالطِّيبِ مِنْ حَاجَةٍ غَيْرَ أَنِّي سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ عَلَى الْمِنْبَرِ: ((لا يَحِلُّ لامْرَأَةٍ تُؤْمِنُ بِاللَّهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ أَنْ تُحِدَّ عَلَى مَيِّتٍ فَوْقَ ثَلاثِ لَيَالٍ إِلاَّ عَلَى زَوْجٍ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْرًا)) متفق عليه

Imepokelewa toka kwa Zaynab bint Abi Salamah (رضي الله عنهما) amesema: “Niliingia kwa Ummu Habiybah (رضي الله عنها)mkewe Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alipofiliwa na baba yake Abu Sufyaan bin Harb. Akaitisha manukato manjano na manukato ya aina nyingine. Akampaka mjakazi wake na akajipaka mashavuni. Kisha akasema: “WaLlaahi sikuwa nina haja ya kujipaka manukato isipokuwa nimemsikia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema juu ya mimbar: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho kumkalia maiti matanga zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe miezi minne na siku kumi)). Zaynab akasema: Kisha nikamwendea Zaynab bint Jahsh(رضي الله عنها) alipofiliwa na ndugu yake. Akaitisha manukato, akajipaka kisha akasema: “WaLlaahi sikuwa nina haja ya manukato, isipokuwa nilimsikia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akisema: ((Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya mwisho kumkalia maiti matanga zaidi ya siku tatu, isipokuwa amkalie mumewe miezi mine na siku kumi))[13]


Hayo ni mafunzo bora ya kufuata na tuchukue mfano wa Nabii Ya’quub
 (عليه السلام)  ilipomzidi huzuni yake baada ya kupotelewa na mwanawe Yuusuf miaka mingi:

((وَتَوَلَّى عَنْهُمْ وَقَالَ يَا أَسَفَى عَلَى يُوسُفَ وَابْيَضَّتْ عَيْنَاهُ مِنَ الْحُزْنِ فَهُوَ كَظِيمٌ))

((Na akajitenga nao akasema: “ee majonzi yangu juu ya Yuusuf”. Na macho yake yakageuka meupe kwa huzuni naye huku akiwa amezuia uchungu [wa huzuni]))[14].
[1]  Al-Hadiyd 57: 22-23
[2]  At-Tawbah 9: 51
[3]  At-Taghaabun 64: 11
[4]  Yuusuf 12:86
[5]  Ar-Ruum 30:41
[6]  Ash-Shuuraa 42:30
[7]  Al-Baqarah 2: 152
[8]  Rejea Mlango Wa ‘Maana Na Aina Za Subira’
[9]  Muslim
[10] Ibraahiym 14: 7
[11]  Aal-‘Imraan 3: 144-145
[12]  Al-Bukhaariy na Muslim
[13] Al-Bukhaariy na Muslim
[14]  Yuusuf 12: 84

0 Comments