KUPANGUSA JUU YA KHUFFU MBILI

Nini Khuffu mbili?

Khaufi ni mfano wa soksi ambazo huvaliwa bila ya viatu na huweza kwendea masafa kwa miguu. Aghlabu hufanywa kutokana na ngozi ya wanyama-howa, kama vile kondoo, mbuzi au ngamia. Matumizi yake aghalabu ni kuvaliwa katika safari za jangwani.

Kujuzu Kupangusa Juu Ya Khuffu Mbili

Inajuzu kupangusa juu ya khuffu mbili kwa alioyapokea Imam Muslim r.a. kutoka kwa Jarir r.a. aliesema kuwa:
   "Nimemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu Mtukufu s.a.w. amekwenda haja ndogo kisha akatia udhu na akapangusa juu ya khuffu mbili zake". (Imekubaliwa na wapokezi wote wa Hadithi).

Shuruti za Kujuzu Kupangusa Juu ya Khuffu mbili

Kujuzu kupangusa juu ya khuffu mbili kuna shuruti mbili:
Kwanza, iwe khuffu mbili zote mbili zimevaliwa hali ya kuwa ana 'tahara kaamili. Lau kama ataosha mguu mmoja kisha akavaa khaufa moja, kisha akaosha mguu wa pili na akavaa khaufa ya pili; haitajuzu kupangusa juu ya khuffu mbili hizo. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Al Mughaira r.a. aliposema kuwa alimtilia maji Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa kutia udhu, alipofika kukosha miguu alitaka kuzivua khuffu mbili zake; Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akamwambia asizivue kwa qauli yake s.a.w.:
  "Ziwache (yaani usizivue) kwani nimezivaa na miguu yangu ni 'taahir". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Na ameeleza Imam Shafi'ii r.a. kutoka kwa Al Mughaira ya kwamba alisema: "Nikasema: "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nipanguse juu ya khuffu mbili"? Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "Naam, ikiwa utazivaa na miguu yako ni 'taahir".
Pili, iwe hizo khuffu mbili zinafaa kupangusika. Ili kufaa kupangusa juu ya khuffu mbili kuna mambo kadhaa.
La Kwanza, iwe hizo khuffu mbili zinafunika sehemu yote ya mguu yenye kulazim katika kutia udhu. Ikiwa sehemu yoyote ya mguu yenye kulazim katika kutia udhu haikufunikika kwa hio/hizo khuffu mbili basi haitajuzu kupangusa juu ya khaufani. Hivi kwa sababu ile sehemu ambayo haikufunikika kwa khuffu mbili - moja au zote mbili - itakuwa inalazim kuoshwa kwa kutia udhu, na ile sehemu iliofunikika itakuwa waajibu ni kupanguswa. Kwa vile hakuna hukmu ya kukosha na kupangusa wakati mmoja, itabidi kukosha miguu yote miwili kwa kutia udhu kaamil, kwani kukosha ndio asili katika kutia udhu.
La Pili, iwe hizo khuffu mbili madhubuti za kumuwezesha msafiri kuziendea kwa mujib wa haja yake, tangu kuondoka kwake mpaka kurejea kutoka safari yake; kwa sababu hii ruhusa ya kupangusa juu ya khufaini ni kwa ajili ya haja ya kuzivaa na kumuwezesha kuziendea. Na uchache wa masafa yenye kukubalika umadhubuti wa khuffu mbili ni kuweza kuendewa si chini ya meli tatu, hivi ndivyo alivyosema Imam Al Ghazali r.a., na amekadiria Sheikh Abu Muhamed kwa masafa yenye kuruhusiwa Sala ya safari; hivi ndivyo ilivyokubaliwa na kutegemewa na Maimam wengi. Ama ikiwa hizo khuffu mbili hazifai kutumika kwa kwendea kama hivi ilivyoelezwa hapa, ima kwa kuwa si madhubuti, kama vile kuwa zimefanywa kwa kitambaa; kama vile soksi ambazo hazizuii kuingia maji, au kwa ugumu wake, kama vile kuwa zimefanywa kwa chuma au kitu cha mfano wa chuma; katika hali hizi haitajuzu hukmu ya kupangusa juu yake.
La Tatu, ziwe zinazuia kuingia maji; ikiwa hazizuii kuingia maji basi haitajuzu hukmu ya kupangusa juu yake; hivi ndivyo walivyokubaliana Maimam wengi.
La Nne, ziwe hizo khuffu mbili ni 'taahir, kwani Sala haisihi kwenye najsi; kwa hivyo haitajuzu hukmu ya kupangusa ikiwa hizo khuffu mbili si 'taahir, kwa kupatwa na najsi au kwa kuwa zimefanywa kutokana na kitu ambacho ni najsi.

Muda wa Kuendelea Kujuzu Kupangusa

Mtu aliokuwa hayumo safarini anaruhisiwa kupangusa juu ya khuffu mbili muda wa siku moja (mchana na usiku wake), yaani saa 24. Kwa aliemo safarini anaruhusiwa kupangusa juu ya khuffu mbili muda wa siku (mchana na usiku wake) tatu, yaani saa 72. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Sayyidna Abu Bakar r.a. kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
 "Ameruhusu (Mtume wetu Mpenzi s.a.w.) kwa msafiri kupangusa juu ya khuffu mbili siku tatu, na kwa muqim (asiekuwa msafiri) siku moja; atapotia udhu kisha akazivaa". (Imehadithiwa na Ibnu Khuzaima na Ibnu Hibbaan).
Na kutoka kwa 'Safwani bin 'Assal r.a. kuwa kasema:
"Alikuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. tukiwa kwenye safari anatuamrisha tusivue khaufi zetu kwa muda wa siku tatu, isipokuwa kwa kupatwa na janaba; lakini kwa haja ndogo au haja kubwa au kwa kulala tusivue". (Imehadithiwa na Al Nissaai na Al Tirmidhy).
Haya yote imeshurutishwa ya kwamba safari yenyewe isiwe katika maasi, ikiwa si hivyo, yaani ikiwa safari ya katika maasi; basi ataruhusiwa kupangusa kwa hukmu ya muqim (asiekuwa msafirini), yaani siku moja.

Kuanza Muda wa Kupangusa

Unaanza muda wa kupangusa tangu pale kupatwa na hadathi - ndogo au kubwa - baada ya kuzivaa hizo khuffu mbili, sio tangu pale kuzivaa hizo khufaini, hivi ni kwa sababu huku kupangusa juu ya khufaini ni ibada ya wakati maalum (kama vile ilivyo Sala), na wakati wake ni pale inapojuzu kufanya hivyo, yaani kupangusa. Na amesema mwanazuoni, Daud Al Dhaahiry r.a. kwamba muda unaanza tangu pale kuzivaa hizo khuffu mbili, sio tangu pale kupatwa na hadathi.
Imam Al Nawawy r.a. yeye amesema kuwa ni kuchagua baina ya rai mbili hizi zilizotajwa hapo juu, hivi ni kwa vile kuwa Hadithi zote zilizokuja juu ya suala hili ni sahihi; na rai mbili hizi zimejengeka juu ya Hadithi hizo za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Ikiwa atapangusa juu ya khuffu mbili wakati ni msafiri, kisha akawa muqim, au akapangusa wakati ni muqim, kisha akasafiri; atatimiza kwa muda wa muqim. Hivi ni kwa vile kukusanyika hali mbili, yaani hali ya kuwa ni msafiri na hali ya kuwa ni muqim; basi hukmu ya muqim ndio yenye kutumika, kwa vile kuwa ndio asli ya hukmu.
Hivi ni sawa lau kuwa kaanza Sala zake wakati ni muqim, kisha akasafiri, basi haitajuzu kwake kusali safari (kupunguza Sala) zile Sala ambazo ilikuwa azisali wakati ni muqim; hivi ni kwa sababu hukmu ya muqim ndio asli ya hukmu. Ikiwa msafiri atatia shaka kuwa ameanza kupangusa juu ya khuffu mbili hali ya kuwa ni muqim au msafari; basi atachukuwa hukmu ya muqim, kwani ndio asli ya hukmu.

Namna ya Kupangusa Juu ya Khuffu Mbili

Uchache wa kupangusa juu ya khuffu mbili ni vile kupangusa kunakojuulika kwa dasturi kuwa ni kupangusa, na huwa kwa kuanzia sehemu ya juu ya kila ya moja ya hizo khuffu mbili. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Al Mughaira r.a. alivyosema:
   "Nimemuona Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akipangusa juu ya mgongo wa khuffu mbili (alizovaa)". (Imehadithiwa na Ahmad na Abu Daud na Al Tirmidhy).
Na ukamilifu wa kupangusa ni kupangusa juu ya hizo khuffu mbili na chini yake, hivi ni kutokana na Hadithi ya Al Mughaira bin Sha'abat r.a.:
   "Ya kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amepangusa juu na chini ya khuffu mbili".
Kupangusa huwa kwa kuweka mkono wa kushoto chini ya sehemu ya kisigino na mkono wa kulia juu ya sehemu ya vidole, kisha aupitishe mkono wa kulia mpaka mwisho wa sehemu ya kisigino na mkono wa kushoto aupitishe mpaka sehemu ya juu ya vidole vyake huku amechawanya vidole vyake vya mkono.

Yenye Kutenguwa Kupangusa Juu ya Khuffu Mbili

Inatenguka kupangusa juu ya khuffu mbili kwa mambo matatu:
La Kwanza, kuivua moja ya khuffu mbili au zote mbili, au zikawa khuffu mbili au moja yao haifai tena kutumika, ama kwa kutoboka, au kuwa dhaifu. Katika hali hii itamlazim kukosha miguu tu, ikiwa bado anao udhu, ikiwa atakuwa hana udhu basi itamlazim atie udhu kaamili.
La Pili, kumalizika muda ulio ruhusiwa kupangusa, yaani kwa msafiri ikipita siku tatu; na kwa muqim siku moja. Ukimalizika muda itabidi atie udhu na kuzivaa upya.
La Tatu, ikimlazim kukoga. Vilevile ikiwa mguu wake utaingia najsi na ikawa hawezi kuindoa hio najsi mpaka kwa kuivua khauf yake, itamlazim aivue na kwa hivyo itaba'tilika kufaa utumizi wa khuffu mbili. Ama ikiwa ataweza kuinadhifisha hio khauf kutokana na najsi bila ya kuivua, atafanya hivyo na itaendelea kujuzu utumiaji wa khuffu mbili kwa muda wake.

0 Comments