Swala ya safari na shuruti zake


Shuruti za Safari

Inashurutishwa kwa safari yenye kujuzu kufupisha Sala:

Kwanza, isiwe safari ya ma'asi; kwa hivyo hukubalika safari ya kutekeleza waajibu, kama vile kwenda kuhiji, kwenda kulipa deni, na ya mfano wake. Pia inaingia safari ya kwenda kutekeleza sunna, kama vile kwenda kufanya hija ya sunna, yaani kwa mtu aliekwisha hiji ya fardhi, au kwenda kufanya 'Umra. Pia inaingia safari ya kwenda kuwaona wazee, pia huingia safari ya kwenda kutekeleza jambo la mubah, kama vile kwenda kufanya biashara; pia huingia safari yenye sababu yenye kukirihishwa kisharia, kama vile kusafiri kwa kujitenga na rafiki. Ama safari yenye ma'asi ndani yake, kama vile safari ya ujambazi; biashara ya haraam, kama vile kuuza/kununua ulevi, madawa ya kulevya na ya mfano wake, katika hali hizi haijuzu Sala ya safari. Vilevile safari ya mwanamke bila ya ruhusa ya mumewe, safari ya mwenye kudaiwa na hali anao uwezo wa kulipa, akasafiri bila ya ruhusa ya anaemdai. Wote hawa na wa mfano wao kwa vile safari zao ni za ma'asi, basi hawaruhusiwi kufupisha Sala, vile vile hawaruhusiwi kuchanganya Sala, wala hawaruhusiwi kusali sunna juu ya kipando, wala hawaruhusiwi kupangusa juu ya khuffu mbili, wala hawaruhusiwi kula maiti (mzoga) kwa dharura; yote haya kwa sababu safari yao msingi wake ni haraam. Amesema Sufiyan Al Thauriy r.a. lau akikutikana dhaalim porini au jangwani (peke yake) hana maji wala chakula, basi hapewi maji wala chakula; kwani akifa itastarehe miji, na watastarehe binaadam na miti na wanyama pia watastarehe kwa kufa huyo dhaalim.

Pili, iwe ni safari ndefu; na safari ndefu nyenye kukubalika ni isiyopungua mwendo wa miguu wa siku mbili kwa mwendo wa kawaida, hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:
  "Haifupishwi Sala ikiwa ni safari ya chini ya burudi nne - baina ya Makka na 'Asfaan". 'Asfaan ni mwendo wa miguu wa siku mbili kutoka Makka, kwa kipimo cha kilomita (km) ni km 84. Na inampasa msafiri kubainisha sababu ya safari yake, haitoshi kutia nia ya kusafiri tu; bila ya kubainisha sababu ya safari; hata ikiwa safari yake ni ndefu.

Tatu, iwe Sala ya rakaá nne - adhuhuri, laasiri, au Sala ya ‘íshaa, iwe anaisali katika wakati wake; si Sala ya/za kulipa. Ikiwa ni Sala ya/za kulipa itakuwa katika hali nne kama hivi:

Ya Kwanza, ikiwa Sala itampita wakati yumo safarini, na ikawa anailipa nae bado yumo safarini; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya msafiri, yaani atafupisha.

Ya Pili, ikiwa Sala ilimpita wakati hayumo safarini, yaani muqim; kisha ikawa anailipa wakati yumo safarini, yaani msafiri; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya muqim, yaani hatafupisha; kwani hivyo ndivyo asili ya hukmu juu yake.

Ya Tatu, ikiwa Sala itampita wakati yumo safarini, kisha ikawa anailipa wakati hayumo safarini; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya muqim, yaani hatafupisha, kwani hivyo ndivyo asili ya hukmu juu yake.

Ya Nne, ikiwa itamjia shaka, kuwa Sala ilimpita wakati ni muqim au msafiri; katika hali hii atailipa kwa hukmu ya muqim, yaani hatafupisha; kwani hivyo ndivyo asili ya hukmu juu yake.

Shuruti za Kufupisha Sala
Shuruti za kufupisha Sala ni tano:

Kwanza, kutia nia kuwa anasali Sala ya safari na kubainisha sababu ya safari yake katika huku kutia nia, asipotia nia ya kusali Sala ya safari itafunganika takbiira yake ya kuingia kwenye Sala kuwa ni Sala ya kawaida, kwani hivyo ndivyo asili ya Sala.

Pili, iwe tangu awali ya Sala mpaka mwisho wa Sala inaendelea juu yake shuruti za kujuzu kusali Sala ya safari. Hivi ni kama ilivyokuja kwenye hii Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuainisha kuwemo kwenye safari  kwahivyo isiekuwemo kwenye safari hatofupisha Sala.

Tatu, kujua kujuzu msafiri kufupisha Sala, asiejuwa kujuzu msafiri kufupisha Sala haitajuzu kwake kufupisha. Hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:   "……. Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.". (Annahal : 43).

Nne, asimfuate mwenye kusali Sala kaamili, au kutimiza Sala yake; akiwafata hawa atatimiza Sala yake pamoja na Imam kwani haifai kumuwacha Imam na weye umo ndani ya Sala. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w. alipoulizwa na Ibnu 'Abbaas r.a.: "Nini inakuwa kwa msafiri anaposali raka'a mbili (yaani kafupisha Sala), anaposali peke yake; na akasali raka'a nne akimfuata mwenye kusali Sala ya muqim? Akasema s.a.w. kujibu:  ذلك السنة  hio ni sunna”. (Imehadithiwa na Ahmad).

Tano, iwe ni Sala ya raka'a nne, yaani iwe ni Sala ya adhuhuri au Sala ya laasiri au Sala ya 'ishaa; kwani hakuna kufupisha Sala kwa Sala ya alfajiri walaa Sala ya magharibi.

Lini Msafiri Anafupisha Sala
Msafiri hajuziwi kufupisha Sala mpaka atoke kwenye majengo ya mji alioondokea. Amesema Ibnu Al Mundhir: "Sijui kwamba Mtume  s.a.w. amepata kufupisha Sala katika safari zake ila baada ya kutoka nje ya mji. Na hufupisha Sala muda anaokuwa kwenye safari, akitua kwa kungojea kutekeleza haja yoyote ile, huendelea kufupisha Sala kwa muda wa siku nne, akiendelea kuwepo hapo baada hizo siku nne na ikiwa hio haja imekwisha au haijesha, husali Sala ya muqim, yaani Sala kaamili bila ya kufupisha. Imethibiti kwa ilivyopokewa kwamba Mtume s.a.w.:
"(Mtume s.a.w.) aliingia Makka taarikh nne ya mfunguo tatu, akakaa hapo hio taarikh nne, na taarikh tano, na taarikh sita na taarikh saba, na akasali alfajiri ya taarikh nane kisha akenda Mina". Mtume s.a.w. alipokaa hapo Makka siku nne alifupisha Sala, na hivi kuazimia kwake s.a.w. kukaa hapo Makka kwa muda maalum katika kutekeleza vitendo vya Hija, ni dalili kwamba mwenye kuazimia kukaa mahala kwa muda maalum (nje ya kwake) wakati yumo safarini, atafupisha Sala zake kwa siku nne, baada ya hapo atasali Sala ya muqim. Hivi ni kufuata alivyofanya Mtume s.a.w. Kwa qauli ya Imam Shafi'ii r.a. kwamba msafiri anaruhusiwa kufupisha Sala zake kwa muda wa siku kumi na tisa au siku kumi na nane, hivi ni kutokana na alivyopokea Imam Bukhary r.a. kutoka kwa Ibni 'Abbaas r.a.:
"Mtume s.a.w. amekaa kwenye baadhi ya safari zake muda wa siku kumi na tisa anasali raka'a mbili, yaani anafupisha Sala; na sisi tukikaa (nje ya kwetu) muda wa siku kumi na tisa tunasali raka'a mbili, yaani tunafupisha Sala; na tukikaa zaidi ya muda huo, tunasali Sala ya muqim".
Na imepokewa vilevile kwamba:
"Mtume s.a.w. alikaa Makka muda wa siku kumi na nane baada ya Ufunguzi wa Makka, kwani alitaka kuifungua Hunaina, lakini haikuwa; baada ya hapo akawa anasali Sala za muqim, yaani bila ya kufupisha".

Kuchanganya Sala Mbili
Inajuzu kwa msafiri kuchanganya Sala ya adhuhuri na laasiri na kuchanganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa kwa kutanguliza na kuzisali katika wakati wa Sala ya mwanzo. Kuchanganya namna hivi kunaitwa:
  (jam'u taqdiim), yaani kuchanganya kwa kutanguliza. Na inajuzu vilevile kuchanganya Sala ya adhuhuri na Sala ya laasiri na inajuzu vilevile kuchanganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa kwa kuakhirisha na  kuzisali katika wakati wa Sala ya pili. Kuchanganya namna hivi kunaitwa  (jam'u taakhiir), yaani kuchanganya kwa kuakhirisha.
Dalili ya kujuzu hivi ni vile alivyoeleza Mu'adh bin Jabal r.a.:
"Tulikuwa pamoja na Mtume s.a.w. kwenye vita vya Tabuk, akawa s.a.w. anachanganya kusali Sala ya adhuhuri pamoja na Sala ya laasiri, na anasali Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa, akapumzika; kisha akatusalisha Sala ya adhuhuri na Sala ya laasiri zote pamoja, akapumzika, kisha akatusalisha Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa zote pamoja".
Kwa ilivyoelezwa ni kwamba hivi vyote ilikuwa ni kusali  (jam'u taqdiim), yaani kuchanganya kwa kutanguliza. Hivi kusali jam'u taqdiim kuna shuruti tatu:

Ya Kwanza, kusali Sala ya mwanzo, kwa mfano kuchanganya Sala ya adhuhuri na Sala ya laasiri; ukifika wakati wa Sala ya adhuhuri, ataadhini, ataqim; atasali Sala ya adhuhuri raka'a mbili atatoa salam, atainuka kwa kusali Sala ya laasiri, ataqim (bila ya adhana), atasali Sala ya laasiri raka'a mbili; atatoa salam. Kuchanaganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa; ukifika wakati wa Sala ya magharibi, ataadhini, ataqim; atasali Sala ya magharibi bila kufupisha, yaani rakaa tatu, atatoa salam, atainuka kwa kusali Sala ya íshaa, ataqim (bila ya adhana), atasali Sala ya 'ishaa rakaa; mbili atatoa salam.

Ya Pili, kutia nia (moyoni) tangu awali ya kuingia kwenye Sala ya mwanzo (adhuhuri), kuwa anasali Sala ya adhuhuri pamoja na Sala ya laasiri. Atasali kila moja mbali mbali, yaani kila moja ataisali kwa iqama yake, nia yake na takbiir yake. Ataadhini mwanzo, mara moja tu; kuqim ndio ataqim kwa kila Sala.

Ya Tatu, mfululizo baina ya Sala ya mwanzo na Sala ya pili, yaani akishasali Sala ya adhuhuri hapo hapo atainuka kwa kusali Sala ya laasiri, ataqim (hatoadhini) atasali Sala ya laasiri. Na kwa kuchanganya Sala ya magharibi na Sala ya 'ishaa ni vile vile, akimaliza kusali Sala ya magharibi hapo hapo atainuka kwa kusali Sala ya íshaa, ataqim (bila ya adhana) atasali Sala ya 'ishaa. Imethibiti ya kwamba Mtume s.a.w. alipokuwa Namra alisali Sala ya safari, akachanganya baina ya adhuhuri na laasiri na akaamrisha iqama baina ya Sala mbili hizo, yaani imeqimiwa kwa Sala ya adhuhuri kumaliza kusali Sala ya adhuhuri, ikaqimiwa kwa Sala ya laasiri.
Vilevile kwa  (jam'u taakhiir), kuchanganya kwa kuakhirisha; anatakiwa atie nia ndani ya wakati wa Sala ya adhuhuri kuwa anaakhirisha kusali Sala ya adhuhuri na ataisali pamoja na Sala ya laasiri katika wakati wa Sala ya laasiri. Katika hali hii, inajuzu kusali kwanza Sala ya adhuhuri kisha akasali Sala ya laasiri, au akasali kwanza Sala ya laasiri kisha akasali Sala ya adhuhuri. Muhim ahakikishe kuwa wakati wa Sala ya laasiri haumpiti. Hivi hivi ndivyo atavyofanya kwa kuakhirisha Sala ya magharibi na kuisali pamoja na Sala ya 'ishaa, katika wakati wa Sala ya íshaa. Inajuzu kwa muqim, yaani si msafiri kwa sababu ya mvua kuchanganya Sala, kwa kusali Sala ya adhuhuri - raka'a nne na Sala ya laasiri - raka'a nne wakati wa Sala ya adhuhuri, na akachanganya kwa kusali Sala ya magharibi - raka'a tatu na Sala ya 'ishaa - raka'a nne wakati wa Sala ya magharibi. Hivi ni kwa alivyo hadithia Imam Al Bukhary na Muslim r.a. kutoka kwa Ibni ‘Abbaas r.a. kwamba Mtume s.a.w.:
"(Mtume s.a.w.) alisali nae yuko Madina raka'a nane na raka'a saba zote pamoja, yaani alisali Sala ya adhuhuri rakaá nne na akasali Sala ya laasiri raka'a nne, wakati wa Sala ya adhuhuri; na akasali Sala ya magharibi raka'a tatu na akasali Sala ya ‘ishaa raka'a nne, wakati wa Sala ya magharibi". Hivi kuchanganya Sala katika hali hizi, haiwi kuzisali kwa kufupisha Sala, kwa sababu si Sala ya safari, ni Sala ya muqim; lakini imeruhusiwa kuchanganya kwa sababu ya mashaka yaliopo kwa ile hali ya kuendelea kunyesha mvua katika wakati wa Sala hizi. Na katika upokezi wa Imam Muslim r.a. amesema:  yaani bila ya khofu wala safari. Hii ni dalili kuchanganya huku kunajuzu bila ya sababu ya khofu au safari. Miongoni mwa shuruti za kujuzu kuchanganya hivi ni kama vile zilivyo kwenye Sala ya  (jam'u taqdiim), yaani kuchanganya kwa kutanguliza. Vilevile miongoni mwa shuruti zake ni kuendelea kuwepo hio sababu - kunyesha mvua - tangu awali ya Sala ya mwanzo na awali ya Sala ya pili. Vilevile iwe hizi Sala zinasaliwa kwenye mahala ambapo mtu akienda kufuatia kusali atarowa kwa mvua inayonyesha.
Na wamesema wanazuoni miongoni mwao as-haabu Imam Shafi'ii r.a. na wengineo kujuzu kuchanganya Sala kwa sababu ya ugonjwa. Na imesemwa kwamba Mtume s.a.w. amefanya hivyo, yaani amechanganya Sala kwa sababu ya ugonjwa

0 Comments