FIQHI : NAJSI (UCHAFU)

Nini Najsi?

Kilugha ni kila uchafu, kisharia ni uchafu wenye kuzuia kusihi Sala; na imesemwa kuwa ni kila kitu anachokiona uchafu mtu wa dasturi na akajikinga nacho na akasafisha nguo yake au/na mwili wake kikimpata, kama vile choo kidogo au choo kikubwa.

Hukmu ya Kilichotoka Kwenye Tumbo la Mnyama

Vyenye kutoka kwenye tumbo la mnyama vinagawika mafungu mawili:
La Kwanza, vile ambavyo havikuwa kwa kutokana na kusagika tumboni, kama vile madenda na jasho na mfano wa haya; haya hukmu yake ni hukmu ya mnyama wenyewe, ikiwa mnyama wenyewe ni najsi, na haya ni najsi; ikiwa mnyama wenyewe ni 'taahir, na haya ni 'taahir.
La Pili, vile ambavyo vimekuwa kwa kutokana na kusagika tumboni, kama vile choo kidogo, choo kikubwa, damu, matapishi; hivi vyote ni najsi ikiwa vinatokana na mnyama asieliwa. Choo kidogo (mkojo), kuwa ni najsi kumetolewa hoja kwa yule Bedui aliekojowa msikitini; Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akaamrisha umwagiwe doo la maji huo mkojo. Na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kukhusu makaburi mawili, alipopita Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akaona wanavyo adhibiwa waliomo katika makaburi mawili hayo, akasema s.a.w.:   "Ama mmoja wao alikuwa hajikingi na mkojo wake". (Imehadithiwa na Muslim).
Ama amri ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. ya kunywa mkojo wa ngamia, hivyo ilikuwa ni kwa ajili ya dawa; na kujitibu kwa kitu najsi inajuzi iwapo kitakosekana kitu 'taahir ambacho kitakuwa mahala pa kile najsi. Ama qauli ya Mtume wetu Mmpenzi s.a.w.:  "Hajajaalia Mwenyezi Mungu Mtukufu dawa kwa umati wangu kwa kilicho haramishwa".
Imesemwa kuwa Hadithi hii imekusudiwa juu ya ulevi. Ama kukhusu najisi ya choo kikubwa imekuja hoja yake kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Hakika utakosha nguo yako ikiingia choo kidogo, choo kikubwa, madhii na matapishi". (Imehadithiwa na Ahmad na Darqu'tny na Al Bazzaar).
Hadithi hii ni dalili ya kwamba matapishi na madhii ni najsi. Madhii ni maji meupe mepesi yenye kuganda/kunata hutoka bila ya matamanio kwa kuchezeana na kwa kutazama. Ama unajsi wa mavi ya wanyama ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alipotaka kustanji akapelekewa mawe mawili na donge la mavi makavu ya mnyama, akachukuwa s.a.w. yale mawe mawili na akaacha kuchukuwa lile donge la mavi na akasema s.a.w.:  hili ni uchafu, na uchafu ni najsi.
Ama unajsi wa wa    wadii ni kwa qauli ya Sayyidah 'Aisha r.a.:
 "Ama wadii, hayo hutoka baada ya kukojoa, basi naaoshe utupu wake (wa kiume au wa kike), kisha atie udhu wala hakogi". (Imehadithiwa na Ibnu Al Mundhir).
Wadii,  ni maji meupe yenye uchafu na mazito hutoka baada ya kukojoa au kwa kuchukuwa kitu kizito.
Ama unajsi wa damu umethibiti kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
    " Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe ………". (Al Maida : 3).
Na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Jikoshe damu na usali".
Ama manii si najsi, sawa yakiwa ni manii ya mwanamume au ya mwanamke. Manii ya mnyama, inategemea, ikiwa ni ya mnyama ambae ni najsi, basi na manii yake ni najsi; ikiwa ni ya mnyama ambae si najsi, basi na manii yake si najsi.

Kukosha Najsi

Kukosha kuiondoa najsi ni waajibu kama ilivyokuja katika amri kama tulivyo tangulia kueleza. Ama namna ya kukosha najsi kuna khitalifiana kwa kukhitalifiana najsi yenyewe. Ikiwa najsi yenye kuonekana kwa macho, ni lazima katika kuikosha iondoke kwa dhati yake, na rangi yake na ladha yake na harufu yake. Ikibakia ladha basi pahala ilipoingia hio najsi hapatakuwa pame'tahirika. Ikibakia rangi ya najsi yenyewe na hali ya kuwa si taabu kuondosheka, basi pahala ilipoingia hio najsi hapatakuwa pame'tahirika. Ikiwa ni taabu kuondosheka, kama vile nguo kuingia damu ya hedhi, basi hu'tahirika kwa vile kuwa ni taabu kuondosheka hio rangi ya damu. Na ikiwa najsi itabakia harufu yake, kama vile harufu ya ulevi basi hu'tahirika kwa vile ni taabu kuondosheka harufu ya ulevi. Ama najsi isio onekana kwa macho, kama vile najsi ya maji-maji ambayo haina rangi; hii inapasa kukoshwa kwa kusuguwa kwa nguvu mpaka iondoke, isipokuwa mkojo wa mtoto mchanga mwanamume ambae hajala wala hajanywa isipokuwa maziwa ya mama yake, huu utakoshwa kwa kurushiwa maji mpaka maji yazidi mkojo na kuenea sehemu yote ilioingia mkojo, si lazima maji yachururike. Ama mkojo wa mtoto mchanga mwanamke inapasa ukoshwe sawa na mkojo  wa mtumzima. Dalili ya tafauti hii, baina ya mkojo wa mtoto mchanga mwanamume na mkojo wa mtoto mchanga mwanamke ni Hadithi ya Sayyidah 'Aisha r.a. kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
"Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alipelekewa mtoto mchanga mwanamume, akakojoa kwenye pahala pake anapokaa s.a.w., akataka aletewe maji, akamwagia kwenye hapo pahala wala hakupakosha, na katika riwaya nyengine ni kuwa alinyunyizia maji juu yake; na katika riwaya nyengine alirashia juu yake maji wala hakupakosha".
Muhimu ni kwamba riwaya zote hizi zina maana moja, yaani Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alimwagia maji kwenye mkoja wa matoto mchanga mwanamume na wala hakukosha hapo pahala alipokojolea huyo mtoto. Na kwa alivyo hadithia Imam Al Tirmidhy r.a. kuwa:
  "Hurashiwa maji juu ya mkojo wa matoto mchanga mwanamume, na hukoshwa kwenye mkojo wa mtoto mchanga mwanamke".
Na kutokana na Sayyidna 'Ali r.a. kuwa amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kukhusu mkojo wa mtoto mchanga mwanamume na mkojo wa mtoto mchanga mwanamke:  "(Mkojo wa mtoto mchanga mwanamume) hurashiwa maji juu yake, na mkojo wa mtoto mchanga mwanamke hukoshwa". (Imehadithiwa na Ahmad).
Ama mtoto mchanga mwanamume akila chakula basi itabidi kukoshwa mkojo wake, sawa na mkojo wa mtoto mchanga mwanamke. Mtoto mchanga mwanamke yeye mkojo wake unakoshwa, ikiwa analishwa au hajalishwa.
Hii tafauti ya hukmu baina ya mkojo wa mtoto mchanga mwanamke na mkojo wa mtoto mchanga mwanamume imechukuliwa kwa kutizama ya kwamba mara nyingi watu huwa zaidi na watoto wanaume kuliko watoto wanawake. Hivyo huwa mara nyingi wanawachukua na kuwabeba, hivyo kuwepo uwezekano wa kupatwa na mkojo wao mara nyingi, kwa hivyo ikajaaliwa wepesi katika ku'tahirisha mkojo wa watoto wachanga wanaume.

Hukmu ya Mnyama Anaekufa Kwenye Kitu Cha Maji-Maji

Mnyama akifa kwenye kitu cha maji-maji, ikiwa ni maji, au mafuta, au samli au chakula, ikiwa huyo mnyama ni mwenye damu ya kuchururika basi hunajsika hicho alichokufia ndani yake; hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alipoulizwa kuhusu panya akifa kwenye samli, akasema s.a.w.:
"Ikiwa hio samli imeganda, basi mtoweni huyo panya na mtengue mtupe pale alipokufia na pembezoni mwake, ikiwa hio samli imeyayuka, majimaji; basi imwageni". Na kwa riwaya nyengine: "Mtoeni mumtupe, na iliopo pembezoni mwake imwageni na mle samli yenu (inayobaki)". (Imehadithiwa na Al Bukhary).
Amri ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. ya kuimwaga hio samli ni dalili ya kuwa imenajisika hio samli. Ama ikiwa huyo mnyama si mwenye damu ya kuchururika, kama vile nzi, mbu, nge, mende, sisimizi na wa mfano wao; hawa wakifa kwenye maji au kitu cha maji-maji hakinajsiki. Hivi ni kwa qauli yake Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
 "Akiingia nzi kwenye kinywaji cha mmoja wenu, basi na amzamishe wote kisha amtoe, kwani kati ya mmoja wa mbawa zake mna maradhi na wa pili mna dawa". (Imehadithiwa na Al Bukhary na Abu Daud na Ibnu Khuzaima na Ibnu Hibbaan).
Amri ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kumzamisha nzi ambae huenda akafa katika hicho kinywaji chetu ni dalili ya kutokuwa najsi huyo nzi, na kama ni najsi basi Mtume wetu Mpenzi s.a.w. asingaliamrisha kuzamishwa ndani ya kinywaji chetu. Vilevile kulinda vyombo vyetu visiingiliwe na wadudu hawa ni taabu, hivyo ikasamehewa kuwa ni najsi.
Hukmu hii ni kwa sharti ya kwamba hicho kilichoingiliwa na wadudu hawa hakijabadilika ladha, rangi au/na harufu kwa vile kuingiliwa na wadudu hawa, kikibadilika, rangi, ladha au harufu; basi hunajisika. Najsi isio onekana kwa macho, kwa uchache wake; kama vile cheche za mkojo au uchafu wenye kuganda kwenye miguu ya nzi, hukmu yake ni kutokuwa najsi kama ilivyo hukmu ya mnyama asiekuwa na damu yenye kuchururika, hivi ni kwa vile ni taabu kujilinda navyo.

Hukumu ya Mnyama Wakati Yuhai

Asili ya wanyama ni 'taahir, kwani wao wameumbwa kwa manufaa ya binaadam, kupatikana manufaa yao vyema ni kwa wao kuwa ni 'taahir. Imetolewa hoja juu ya hili kwa Hadithi kukhusu paka, kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Hakika yao (paka) si najsi, kwani wao ni wenye kupita baina yenu". (Imehadithiwa na Maimam watano wa Hadithi).
Wametolewa katika hukmu hii, mbwa na nguruwe kwani wao ni najsi. Unajsi wa mbwa umetolewa hoja kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
 "Ku'tahirika chombo cha mmoja wenu akitia ndani yake mbwa mdomo wake (au akiramba) ni kukoshwa mara saba, mara ya mwanzo (ya hizo mara saba) kukoshwa kwa mchanga". (Imehadithiwa na Ahmad na Muslim).
Qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.   ku'tahirika. Kuhitaji ku'tahirika hakuwi isipokuwa baada ya kunajisika, hivi ikathibiti unajsi wa mdomo wa mbwa. Ikiwa mdomo wake ni najsi na ndio sehemu safi mno katika mwili wake kwa vile kuuramba mdomo wake kila mara, basi kuwa najsi mbwa wenyewe ni ndivyo zaidi. Ama unajsi wa nguruwe ni kwa kuwa nguruwe ni mchafu zaidi ya mbwa. Vile vile Al Mawridy ametolea hoja juu ya unajsi wa nguruwe kwa qauli ya Mwnyezi Mungu Mtukufu: "………, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; ……". (Al An'aam : 145).

Hukmu ya Nyamafu

Nyamafu wote ni najsi kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
  "Mmeharimishiwa nyamafu, ........". (Al Maida : 3).
Na kuharimishwa kitu ambacho hakina karama, wala madhara ni dalili ya unajsi wake, kwani kitu huharimishwa ama kwa karama yake, kama vile kula maiti ya binaadam, au kwa madhara yake, au kwa unajsi wake. Na nyamafu hana karama wala madhara kumla, kwani kwa dharura  imeruhusiwa kula nyamafu, kama ilivyokuja kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  “…… Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu”. (Al An'aam : 145).
Kwa hivyo basi, imebakia unajsi kuwa ndio sababu ya kuharimishwa nyamafu. Nyamafu ni yule ulie muondoka uhai wake bila ya kuchinjwa Kisharia. Huingia katika hukmu hii mnyama asiejuzu kuliwa hata kama atachinjwa, vilevile na mnyama anae chinjwa na mtu ambae si Muislam wala si miongoni mwa (Watu wa Kitabu)  Hutolewa katika kundi la nyamafu, samaki, panzi, nyembure na wa mfano wao, vile vile kumbikumbi; na binaadam, wote hawa hawamo kwenye kundi la nyamafu.
Kutolewa samaki kwenye kundi na nyamafu ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kukhusu bahari:  "Hio (bahari) ni 'taahir maji yake, halali maiti wake". (Imehadithiwa na Maimam watano wa Hadithi).
Ama uhalali wa panzi na kutolewa katika kundi la nyamafu ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:     Tumehalalishiwa nyamafu (maiti) wawili: samaki na panzi". (Imehadithiwa na Ibnu Maajah na Al Bayhaqy).
Ama binaadam kutolewa katika kundi la nyamafu ni kwa qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na kwa hakika tumewatukuza wanaadamu.........". (Al Israai : 70).
Na huku kutukuzwa binaadam ndio kumemuondolea kuwa miongoni mwa nyamafu, najsi; hukmu hii ni kwa maiti wote wa binaadam, ikiwa ni Islam au Kafiri. Ama qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  "…… Hakika washirikina ni najsi, ……". (Tawba : 28).
Unajsi unaokusudiwa hapa ni unajsi wa itikadi au kujiepusha nao kama tunavyo jiepusha na najsi, wala si unajsi ya kiwiliwili, kwani ingalikuwa ni unajsi wa kiwiliwili ingaliwajibishwa kukikosha anachokigusa au kujikosha tukigusana nao.
Ikiwa atachinjwa mnyama (mwenye kuliwa) akakutikana tumboni mwake mtoto, basi inafaa kuliwa mtoto huyo wala haihitaji kuchinjwa, kwani huku kuchinjwa mama kumetosheleza.

Ku'tahirisha Najsi ya Mbwa Na Nguruwe

Hu'tahirishwa chombo alichotia mdomo au kikiramba mbwa au nguruwe kwa kukoshwa mara saba, moja ya mara saba hizo ni kwa mchanga.
Kukhusu mbwa imetolewa dalili kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "   "Mbwa akichovya mdomo katika chombo cha mmoja wenu, kikosheni mara saba, mara ya mwanzo kati ya hizo saba iwe kwa mchanga". (Imehadithiwa na Muslim).
Na kwa ilivyo hadithiwa na Al Tirmidhy r.a.:
 
"Ya mwanzo ya mara hizo, au moja ya mara hizo (iwe) kwa mchanga".
Ikiwa imethibiti kulazimika kukosha najsi ya mbwa kwa kuchovya mdomo wake, au kukiramba chombo, yaani kutokana na madenda yake; basi kulazimika kukosha najsi ya mbwa kama vile choo, au matapishi, jasho na kadhaalika ni kulazimika zaidi. Hadithi hizi ni dalili ya unajsi wa mbwa na kunajisika kile alichochovya mdomo wake ndani yake au kukiramba, kwani lau kama si najsi; isingekuwa kuvimwaga viliomo kwenye vyombo walivyochovya midomo yao. Kuvimwaga viliomo kwenye vyombo ni kupoteza mali, na Uislam unakataza kupoteza mali, na kama si najsi basi Mtume wetu Mpenzi s.a.w. asingalituamrisha kuvimwaga. Unajsi wa nguruwe umechukuliwa dalili kwa kiasi cha mbwa, na kwa vile kuwa nguruwe ni mchafu zaidi kuliko mbwa, kutokana na huu uchafu wake ndio tunakatazwa kuweka/kufuga nguruwe kwa hali yoyote ile, tafauti na mbwa. Najsi ya nguruwe hu'tahirishwa kwa kuoshwa sawa na najsi nyengine. Kuwajibishwa kukosha najsi ya mbwa mara saba - moja kwa mchanga kumekuja kwa makusudio ya kuondoa ile tabia ya Waarabu hapo zamani ya kuchanganinyika sana na mbwa wao.

Ku'tahirika Tembo (Ulevi) Kwa Kua Siki

Ku'tahirika vitu huwa ama kwa kukoshwa, kwa kudabighiwa au kwa mchanga; haya tumetangulia kuyaeleza; na huenda ikawa ku’tahirika kwa kugeuka, yaani kitu kutoka hali hii na kuwa katika hali nyengine; kama vile tembo kugeuka siki. Tembo likigeuka siki huwa si najsi, hivi ni kwa sababu unajsi wa tembo ni kwa vile kulevya (madhara), na kwa kugeuka ikawa siki huondoka kulevya, kwa kuondoka kulevya; kumeondosha unajsi. Wamekubaliana wanazuoni ya kwamba kugeuka kunako kusudiwa ni kugeuka wenyewe, bila kugeuzwa; kugeuka kwa hali hii ndivyo hio siki haiwi najsi, huwa ni 'taahir. Ama ikiwa ni kwa kugeuzwa (si kugeuka wenyewe) kwa kutiwa vitu vya kugeuzia, kama vile vitunguu au hamira, basi siki hio haiwi 'taahiri, bali huwa najsi. Haya yametolewa dalili pale alipoulizwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama tembo hufanywa siki, Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akasema, halifanywi: Maana ya Hadithi hii ni kama hivi:  "Ameulizwa (Mtume wetu Mpenzi s.a.w.) kama tembo linafanywa siki akasema: Laa, yaani halifanywi". (Imehadithiwa na Muslim).
Amekataza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. tembo kuligeuza siki kwa kutia ndani yake vitu vya kugeuzia, imetolewa dalili ya kuharamishwa kufanya hivyo; kwamba:
 "'Talha r.a. alisilimu nae analo tembo la mayatima, akamuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kama alifanye siki, Mtume s.a.w. akamwambai: Laa, (yaani asilifanye)".
Imekatazwa kulifanya tembo siki kwa kutia vitu ndani yake kwa sababu vile vitu vitakavyotiwa ndani ya tembo ambalo ni najsi, hunajsika kwa vile kuchanganyika na kitu najsi, yaani lile tembo; kwa hivyo basi, litapogeuka hili tembo kuwa siki ile najsi ya vile vitu vilivyotiwa kwenye tembo na kunajisika kwa kugusana na tembo, ambalo ni najsi, vitainajisisha hii siki yenyewe, kwa hivyo hii siki itakuwa ni siki ilio najsi; hivyo ndivyo ikaharimishwa tembo kuligeuza siki kwa kutia vitu ndani yake. Ama likigeuka siki wenyewe bila ya kutiwa vitu, hivyo hufaa na hutumiwa hio siki kuwa hali ya kuwa ni 'taahir, si najsi.

Kusamehewa Kutokana na Baadhi ya Najsi Kidogo

Zenye kusamehewa miongoni mwa najsi kidogo kwa sababu ya shida ya kujikinga nazo ni:
Kwanza, tope za njiani.
Pili, vile ambavyo ni taabu kuviona kwa jicho la kawaida; kama vile cheche za mkojo, tembo, vyenye kuganda miguuni mwa nzi, mende, wadudu wa kundi la sisimizi.
Tatu, damu ya vidudu, kama vile kunguni, chawa na viroboto; na mavi ya ndege au ya mijusi misikitini.
Nne, manyoya kidogo ya wanyama wasioliwa (asipokuwa mbwa na nguruwe) na manyoya ya wanyama wenye kupandwa kama punda, nyumbu, farasi.
Tano, moshi na vumbi la najsi vinavyo peperushwa na upepo.
Sita, mnyama najsi; kama vile mbwa akiingia kwenye maji yasiopita, kama vile kisimani au ndani ya kidimbwi; na akatolewa kabla hajafa.
Saba, damu inayobakia kwenye nyama au mifupa ya nyama inayojuzu kuliwa.
Nane, ikiwa mnyama 'taahir kama vile paka; akitia mdomo kwenye kitu najsi, kisha akapotea kwa muda na ikamkinika kuwa wakati alipopotea imewezakana kuwa katia mdomo wake kwenye maji mengi, kama vile mtoni au kwenye kidimbwi cha maji, kisha akarejea na akanywa maji kwenye chombo, basi hayo maji na hicho chombo havinajsiki.
Tisa, kamba ikiwa itaanikiwa nguwo yenye najsi; baada ya muda ikikauka hio kamba kwa jua au kwa upepo, basi inajuzu kuanikia nguo bila ya kukoshwa hio kamba wala haitanajisisha nguo zinazoanikwa juu yake.
Kumi, mtu akimwagikiwa na maji kutoka kwenye nyumba na hajui kama ni maji safi au si safi, haimlazim kuuliza; atachukulia kuwa ni maji safi, isipokuwa akiona uchafu kutokana na hayo maji. Hivi ni kwa hadithi iliotokea wakati wa Sayyidna 'Umar r.a. kuwa yeye na sahibu wake walipita chini ya nyumba wakamwagikiwa na maji kutoka mchirizini mwa nyumba hio. Sahibu yake Sayyidna 'Umar r.a. akamuuliza mwenye nyumba kama ni maji 'taahir (safi) au si safi; Sayyidna 'Umar r.a. akamwambia mwenye nyumba kuwa asiwambie, wakaendelea na safari yao.
Kumi na moja, maji/damu-damu za chunusi; ikiwa kidogo zinasamehewa; ama ikiwa nyingi basi huwa ni najsi na hunajisisha.
Kumi na mbili, ikiwa mnyama anaekula na kuchakuwa baadae, kama vile n'gombe au mbuzi; ikiwa wakati akichakuwa akanywa kwenye chombo hayanajisiki hayo maji wala hicho chombo yaliomo hayo maji.

0 Comments