Fataawa Za Wanachuoni Mbalimbali Kuhusu Ramadhwaan

Nasaha Muhimu Ya Ramadhaan Kwa Waislamu


Fatwa Kutoka: ‘Allaamah Swaalih Ibn Fawzaan Al-Fawzaan

Swali:
Tunataka uwape vijana Nasaha kuhusiana na kuchunga wakati wao katika Ramadhaan?

Jibu:
Waislamu wote sawa Vijana na wengine wote wanatakiwa kutumia wakati wao katika kumtii Allaaah – wala Ramadhaan isiwajie kwa ghafla, au ikawakuta wako katika michezo na upuuzi, au ikawakuta wanajishughulisha na maigizo (sinema za mfululizo), filamu, muziki – kwa kuwa mambo haya imekuwa ni hasara (katika jamii yetu ya Kiislamu). Waislamu wachunge wakati wao siku zote na si katika Ramadhaan tu – katika yale ambayo yatayowafaa ima katika Dini yao au dunia yao. Wala wasipoteze mda wao katika upuuzi, michezo, kufuatilia maigizo (series) na filamu chafu na mfano wake.  


Mwanamke Mwenye Hedhi Aliyetwaharika Baada Tu Ya Alfajiri

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn´Uthaymiyn
Chanzo:  Su-alaat ‘An Ahkaamil-Haydhw, uk. 9-10]

Swali:
Je, mwanamke ambaye anayetwaharika baada tu ya alfajiri atafunga siku inayobaki, au ni juu take kulipa siku hiyo?
Jibu: 
Ikiwa mwanamke atatwaharika baada tu ya alfajiri, Wanachuoni wana kauli mbili kuhusiana na Swawm yake:
Maoni ya kwanza: Anapaswa kufunga siku iliyobaki bila ya kupewa thawabu ya siku hiyo. Kisha baadaye ni waajib kwake kulipa siku hiyo. Hii ni kauli maarufu katika madhehebu ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah).
Maoni ya pili: Hana haja ya kufunga siku iliyobaki. Swawm yake ni batili (ikiwa atafunga) siku hiyo  kwa kuwa alianza siku hali ya kuwa ni mwenye hedhi na si kama mwenye Swawm. Kwa hiyo hali kama hii Swawm yake sio sahihi, hakuna faida yoyote ya yeye kufunga.
Wakati huo hauna faida kwake. Kaamrishwa kujiepusha na kufunga katika siku za mwanzo ya siku hiyo. Kwa  kuwa amekatazwa kufunga wakati huo (wa hedhi). Msingi wa Shari’ah kuhusiana na Swawm kama tujuavyo sote ni kuacha chakula na kunywa kuanzia alfajiri mpaka jioni tukiwa na niyyah ya kumuabudu Allaah kwa hilo.
Tunaamini kuwa mtazamo huu ni wenye nguvu zaidi kuliko mtazamo unaosema afunge siku nzima iliyobaki. Hata hivyo maoni zote mbili ni waajib kwake kulipa siku hiyo.


Mtu Ambaye Anafunga Na Kuswali Tu Ramadhaan

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn 'Uthaymiyn
Chanzo: Fiqhul-'Ibaadat, uk. 248
Madar-ul-Watan, 1424
Swali: 
Unasemaje kwa yule mtu ambaye anaswali na kufunga wakati wa Ramadhaan tu? Wakati Ramadhaan inakwisha, anaacha kuswali na kufunga?
Jibu:
Kilicho dhahiri kwangu kutokana na dalili, ni kwamba mtu kama huyo anachukuliwa kama ni Kafiri kama haswali kabisa. Ama kuhusu yule ambaye anaswali wakati fulani na wakati mwingine haswali, sidhani kuwa dalili yaonesha kuwa mtu huyo ni Kafiri [moja kwa moja].
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"Mkataba baina yetu sisi na wao [makafiri] ni Swalah. Yule atakayeiacha huyo amekufuru.”
"Baina ya mtu na Mshirikina na Shriki ni mtu kuacha Swalah.”
Ndiyo maana nina mashaka ya imani ya mtu ikiwa anaswali na kufunga wakati tu ni Ramadhaan. Kama kweli ni Muumini wa kweli, anapaswa kuswali wakati wote sawa Ramadhaan na baada ya Ramadhaan.

Kumjua Mola wake wakati tu wa Ramadhaan, ninaingiwa na shaka kutokana na imani yake. Hata hivyo sisemi kuwa ni Kafiri moja kwa moja, badala yake ninamdhania vizuri na kumuachia suala lake kwa Allaah (‘Azza wa Jalla).


Je, Dawa Ya Mswaki Inabatilisha Swawm?

Fatwa Kutoka: ’Allaamah 'Abdul-'Aziyz Ibn 'Abdillaah Ibn Baaz
Chanzo: http://binbaz.org.sa/mat/18672
Swali: 
Je, dawa ya mswaki inabatilisha Swawm?
Jibu: 
Dawa ya mswaki haibatilishi Swawm ikiwa atasafisha meno yake kisha ateme bila ya kuimeza. Ikiwa atameza kwa kukusudia, Swawm yake imebatilika.


Mawaidha Baina Ya Rak’ah Katika Taarawiyh

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Muhammad Naaswiyrud-Diyn Al-Albaaniy
Chanzo: Silsilatul-Hudaa wan-Nuur (656)
Swali: 
Je, inajuzu kwa Imaam wa Msikiti ambaye anaongoza watu katika Taarawiyh kuwakumbusha watu wakati wa mapumziko na kuzungumzia juu ya Swalah na juu ya kumfuata Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwaonya baadhi ya watu wa Bid’ah na Washirkina?
Jibu:
Yote ni sawa.
Ikiwa kama ni tukio limetokea, ni waajib kufanya hivyo.
Ikiwa ni ada (Imaam) kuonya watu kila baada Rak’ah na mfano wake, hii ni kinyume na Manhaj ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).


Anayekula Mchana Wa Ramadhaan

Fatwa Kutoka: ’Allaamah 'Abdul-'Azizy Ibn 'Abdillaah Ibn Baaz
Swali: 
Je, nimkumbushe mtu ambaye anakula na kunywa (Ramadhaan) bila ya kusahau?

Jibu:
Ndiyo, anatakiwa kumkumbusha ikiwa anamuona mtu huyo anakula au kunywa na amwambie afunge. Bila shaka kitendo hichi ni dhambi ya wazi. Hata kama mtu ni mwenye kusamehewa kwa sababu ya kusahau kwake, si katika wakati ule. Anatakiwa kukumbusha mtu kama huyo.


Kusafiri Kwa Niyyah Ya Kukwepa Kufunga Ramadhaan

Fatwa Kutoka:  ‘Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn 'Uthaymiyn
Chanzo: Fath Dhiyl-Jalaal wal-Ikram (7/257)
Tuchukulie  mtu anasema:
"Kama inajuzu mtu kusafiri katika Ramadhaan - na inajuzu kutofunga kwa msafiri - ina maana kwamba mnajuzisha kuepuka waajib wa kufunga."

Kama niyyah (lengo) la safari ni kwa ajili ya kuepuka kufunga, hivyo safari imekatazwa. Safari haijuzu kwa kuwa mtu amenuia kuepuka kitu ambacho ni Waajib kwake. Hali kadhalika haijuzu kukata Swawm katika hali kama hii.  


Tofauti Kati Ya Taaraawiyh, Qiyaamul-Layl Na Tahajjud

Fatwa Kutoka: ’Allaamah 'Abdul-'Aziyz  Ibn ‘Abdillah Ibn Baaz
Chanzo: Majmuu’ Fataawa wa Maqaalaat Mutanawwi’ah (11/317)
Swali: 
Ipi tofauti kati ya Taaraawiyh, Qiyamul-Layl naTahajjud?
Jibu: 
Swalah ya usiku huitwa Tahajjud ‘Qiyamul-Layl’. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
“Na amka usiku kwa ‘ibaadah; ni ziada ya Sunnah khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Akakunyanyua cheo kinachosifika.” (17: 79)
“Ewe uliyejifunika! Kesha usiku kucha, ila kidogo tu!.” (73: 1-2)
Ama kuhusiana na Taaraawiyh, Wanachuoni wanaiita Qiyamul-Layl katika ile sehemu ya kwanza ya usiku katika Ramadhaan kwa ajili yake. [kwa kuwa] Swalah hii haiswaliwi kwa muda mrefu tena. Mtu pia anaweza kuiita Swalah hii Tahajjud na Qiyamul-Layl.

Mwanamke Mwenye Mimba Na Mnyonyeshaji Katika Ramadhaan

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah Swaalih Ibn Fawzaan al-Fawzaan
Chanzo: Al-Muntaqaa (3/147)
Swali:
Lini inajuzu kwa mwanamke mjamzito au mwenye kunyonyesha kuacha kufunga?
Jibu:
Inajuzu kwa mwanamke mjamzito au mwenye kunyonyesha kutofunga ikiwa kama ana hofu ya mtoto wake kudhurika ikiwa atafunga, kwa kuwa Swawm inaweza kupunguza kiasi cha virutubisho kwa mtoto aliye tumboni mwa mama yake. Ikiwa hali ni kama hii, anatakiwakutofunga kisha baadaye alipe siku hizo alizokula na alipe pia Kafara. Lakini ikiwa kama atahofia  afya yake mwenyewe kwa kufunga – ima kwa kutoweza kufunga wakati yeye ni mjamzito au kutoweza kufunga wakati yeye ananyonyesha – inajuzu kwake kutofunga na kisha baadaye alipe siku alizokula bila ya kutoa chakula (Kafara). Hili linahusiana na yule (mwanamke) mwenye mimba na mwenye kunyonyesha.


Maumivu Ya Hedhi Kabla Ya Jua Kuzama

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn 'Uthaymiyn
Chanzo: Su-alaat ‘an Ahkaamil-Haydh uk11
Swali: 
Je, Swawm ya mwanamke ni Sahihi, au ni waajib kwake kulipa siku hiyo, ikiwa anadhani (anahisi) atapata hedhi au yuko na maumivu ya hedhi lakini bila ya yeye kupata chochote kabla ya jua kuzama?
Jibu:
Ikiwa mwanamke aliye msafi anahisi kwamba damu iko njiani au ana maumivu ya hedhi wakati yeye ni mwenye kufunga bila ya yeye kutokwa na kitu kabla ya jua kuzama, Swawm yake ni sahihi. Hana haja ya kulipa siku hiyo ikiwa kama ni Swawm ya waajib, na hatokosa ujira wake wake ikiwa ni Swawm ya Sunnah.


Watoto Waamrishwe Kufunga Wanapofikisha Miaka Saba

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah Abdul-‘Aziyz Ibn ‘Abdillaah Ibn Baaz

Swali:
Je, mvulana ambaye kakomaa anapaswa kuamrishwa kufunga?
Je, Swawm yake ni sahihi ikiwa atabaleghe wakati wa Swawm (katika Ramadhaan)?
Jibu:
Ikiwa wavulana na wasichana wanafikisha umri wa miaka saba wanapaswa kuamrishwa kuanza kufunga ili wajizoeze. Wazazi wao ni juu yao kuwaamrisha Swawm hali kadhalika kama wanavyopasa kuwaamrisha Swalah. Wanapobaleghe, Swawm imewawajibikia. Ikiwa watakomaa wakati wa Swawm, siku zao (wanazofunga) ni sahihi. Ikiwa mvulana atafikisha miaka kumi na tano mchana wakati yuko na Swawm, siku yake ni sahihi. Mwanzo wa siku hiyo (Swawm kwake) ilikuwa ni Sunnah na mwisho wake itakuwa ni waajib ikiwa tayari kishatokwa na nywele za sehemu za siri au kishaanza kutokwa na manii. Hali kadhalika inawahusu wanawake ambao wanabaleghe kwa kutokwa na damu ya hedhi.


Mwanaume Ambaye kalazimishwa Jimai Katika Ramadhaan

Fatwa Kutoka: Imaam Ibn Qudaamah Al-Maqdisiy
Chanzo: Al-Mughniy (4/377)
Dar 'Alam lil-kutub, 1419/1999
Ikiwa mwanaume atalazimishwa Jimai, Swawm yake inabatilika. Kama Swawm ya mwanamke inavunjinka kwa sababu ya jimai, Swawm ya mwanaume ni aula zaidi kubatilika kwa sababu hiyo hiyo.
Kuhusiana na kafara, anasema al-Qaadhiy:
"Ni waajib kwake kulipa Kafara, kwa sababu haiwezekani [kwa mwanaume] akalazimishwa jimai. Mwanaume hawezi kufanya jimai bila kwanza ya duburi yake kusimama, na duburi kusimama inasababishwa na matamanio [ya mwanaume]. Kwa hali hiyo haonelei kabisa kuwa [mwanaume] alilazimishwa.
Abuul-Khattaab anasema:
"Kuna mapokezi mawili. Moja inasema kuwa si lazima kwake kulipa Kafara.” wao wanasema yeye si juu yake upatanisho. "
Hii pia ni kauli ya ash-Shaafi'iy. Suala zima la kafara ni ili imtakase mtu kwa madhambi yake. Kwa hivyo haihusiani na mtu kulazimishwa, kwa kuwa mtu anakuwa hana makosa. Hata hivyo anasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam):
"Ummah wangu umesamehewa makosa ya mtu kusahau na kulazimishwa."
Vile vile Shari'ah haijataja kuwa analazimika kutoa Kafara.
Ibn ‘Aqiyl kasema mwanaume ambaye amelala (huku) duburi yake imesimama, mke wake akaiingiza tupu wake kwake [kwa mumewe aliyelala]:
"Hatalazimika kulipa siku hiyo wala kulipa Kafara.”


Mwanamke Anayebakwa Wakati Wa Ramadhaan

Fatwa Kutoka: Imaam Ibn Qudaamah Al-Maqdisiy
Chanzo: Al-Mughniy (4/376)
Daar 'Alaam-il-kutub, 1419/1999
Ikiwa mwanamke atalazimishwa jimai, halazimiki kulipa Kafara. Analazimika tu kulipa siku hiyo.
 Muhannaa kasema:
"Nilimuuliza Ahmad kama wanamke aliyebakwa analazimika kulipa siku hiyo. Akasema:"Ndiyo." Pia nikamuuliza kama analazimika kulipa Kafara. Akasema: "Hapana!"
Maoni haya anakubaliana nayo pia al-Hasan, ath-Thawriy, al-Awza'iy na Hanafiyyah. 
Kulingana na swali hili, inamuhusu pia mwanamke ambaye kaingiliwa wakati amelala. Maalik kasema kuhusiana na mwanamke aliyelala:
"Ni juu yake kulipa siku hiyo, ila hatolipa Kafara. Ama kuhusiana na mwanamke ambaye kabakwa, analazimika kulipa siku hiyo na kutoa Kafara.”
ash-Shaafi'iy, Abu Thawr na Ibnul-Mundhir wanasema ikiwa atabakwa kwa matisho, basi wana maoni sawa na sisi.


Mwenye Kufunga Akisukutuwa Maji Kinywani Au Puani

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn 'Uthaymiyn
Chanzo: Fiqhul-'Ibaadat, uk. 253
Swali: 
Je, Swawm ya mfungaji inabatilika ikiwa atasukutua kinywa au pua na kwa bahati mbaya akameza maji?

Jibu: 
Ikiwa mfungaji anasukutua kinywa au pua na akaingiwa na maji, Swawm yake haibatiliki, kwa kuwa hakukusudia hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
ولكن ما تعمدت قلوبكم
”Lakini ipo lawama katika yale ziliyofanya nyoyo zenu kwa makusudi. (33: 5)


Je, Inajuzu Kutafuna Chingamu Kwa Aliyefunga?

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah ’Abdullaah Ibn Mani'
Chanzo: Majmuw’ Al-Fataawa wal-Buhuwth (1/313)
Swali: 
Je, (kutafuna) pipi ubani ’chingamu’ (chewing gum) kunabatilisha Swawm? Ambayo huchukuliwa kama mswaki?
Jibu:
Inajulikana wazi kama pipi ubani ’chingamu’ inakuwa na vitu (viungo) vya utamu. Viungo hivi vinachanganyika na mate ambavyo mfungaji humeza. Hii ina maana kuwa mfungaji amepata kitu ambacho kinavunja Swawm yake. Kwa hiyo chingamu hii inavunja Swawm ya mtu.
Chingamu si kama mswaki, kwa kuwa Mtume (Swalla Allaahu'alayhi wa ’aalihi wa sallam) kamuacha yule aliyefunga kutumia mswaki.Hii imeripotiwa na Abu Dawuud na at-Tirmidhiy. Mswaki si kama chingamu. Kwenye mswaki kuna kuwa hakuna viungo vitamu ambavyo mwenye kufunga anaburudika navyo pindi anautumia. Maji maji yanayokuwa kwenye mswaki yakachanganyika na mate huchukuliwa kama ni mate, hata kama yule mwenye kuswaki wakati fulani huyatema kutoka kinywani – na Allaah Anajua Zaidi.


Harufu Ya Kukithiri Ya Petroli Na Mfano Wake Kwa Aliyefunga

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Ahmad Ibn Yahyaa an-Najmiy
Chanzo: Fat-h-Ar-Rabb Al-Waduwd (1/326)
Swali: 
Je, harufu iliyokithiri kama ya petroli na mfano wake inabatilisha Swawm?
Jibu: 
Hapana, havibatilishi Swawm ikiwa mtu hatonusa kwa kukusudia.


Israfu Ya Chakula Wakati Wa Futari

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn 'Uthaymiyn
Chanzo: Fiqhu Al-'Ibaadah, uk. 252
Swali: 
Je, mtu hupata thawabu ndogo (ya Swawm) ikiwa atakithirisha kukata Swawm (Futari) kwa masahani ya vyakula mbali mbali?

Jibu:
Hapana, hupati thawabu ndogo ya Swawm. Mtu kufanya kitendo cha haramu baada ya kumaliza Swawm, (kitendo kile) hakiathiri thawabu (za Swawm). Bali inaingia katika neno Lake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):
 وكُلُواْ وَاشْرَبُواْ وَلاَ تُسْرِفُواْ إِنَّهُ لاَ يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ 
”na kuleni, na kunyweni na walamsifanye ubadhirifu. Kwa hakika Yeye hapendi wanaofanya israfu.” (7: 31)

Huku kufanya israfu ndiyo haramu. Kuwa mwana-uchumi na punguza ugavi (chakula) kwa nusu. Ikiwa kwa bahati mbaya kutabaki chakula, ni afadhali kitolewe swadaqah.

Ni Bora Kwa Msafiri Afunge Au Asifunge?

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Abdul-’Aziyz Ibn Baaz
Chanzo: Tuhfatu Al-Ikhwaan, uk. 161-162
Swali: 
Je, ni bora zaidi kwa msafiri afunge au asifunge hasa ukizingatia kwa kuwa usafiri wa leo imekuwa ni rahisi kama usafiri wa ndege  na vyombo vingine vya usafiri?
Jibu: 
Ni bora kwa msafiri asifunge. Hata hivyo, hakuna ubaya ikiwa atafunga, kwa kuwa hali zote mbili zimewahi kuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum). Ikiwa kwa mfano joto limekuwa kali na uzito ukaongezeka (katika safari), kuna sababu moja zaidi ya mtu kutokufunga, na Swawm inakuwa yenye kuchukiza [makruuh]. Wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliona msafiri kazidiwa na uzito kwa sababu ya kufunga kwake joto lilikuwa kali, alisema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
"Si katika wema kufunga katika safari."
Hakuna tofauti kusafiri kwa gari, ngamia, boti au ndege nk,  kwa kuwa vyote vinahusiana na kusafiri. Allaah kateremsha hukmu hiyo kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) wakati wa zama yake kwa wasafiri wote na wasiosafirina hukmu hiyo inaendelea mpaka siku ya Qiyaamah. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajua hali ya usafiri inavyobadilika. Ikiwa (mtu atadai) hukmu ingelifaa kubadilika kwa ajili ya usafiri, basi Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Angetueleza hili. Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:
Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.” (16: 89)
”Na [ameumba] farasi, na nyumbu, na punda ili muwapande, nakuwa ni pambo. Na ataumba msivyovijua.” (16: 8)


Maswali Matatu Kuhusu Ramadhaan Anayajibu Imaam an-Nawawiy

Fatwa Kutoka: Imaam Abu Zakariyyah an-Nawawiy
Chanzo: Fataawa Al-Imaam An-Nawawiy, uk. 55
Swali La Kwanza:
Ni miaka mingapi Mtume (Swala Allaahu ’alayhi wa sallam) alifunga mwezi wa Ramadhaan?
Jibu: 
Alifunga (Ramadhaan) miaka tisa. Swawm ilifaradhishwa mwezi wa Sha’abaan mwaka wa 2 baada ya Hijrah.

Swali La Pili:
Je, mwenye kufunga Swawm yake imebabidlika ikiwa:
Ataonja chakula bila kumeza? Kukata mkate kipande bila ya kumeza? Mtu Kukusanya mate mdomoni kisha baadaye akayameza? Kufungua kinywa ili nzi (mdudu) arukie ndani? Kutengeneza ngano (na mfano wake kama mpunga) bila kujali mtu kafungua mdomo na vumbi ikangia ndani? Kuingiwa na maji mdomoni au puani wakati wa kusukutua?
Jibu: Hakuna hata hata moja kati ya vitu hivi kinachobatilisha Swawm.

Swali La Tatu: 
Je, mtu ambaye anakula kwa kukusudia mchana wa Ramadhaan ni waajib kwake kulipa Kafara? Je, mtu ambaye kwa kusudi anamuingilia mke wake mchana wa Ramadhaan alipe KafaraNa kama alimuingilia mara kadhaa wakati wa Ramadhaan, anapaswa kulipa Kafara mara kadhaa?
Jibu: 
Kuhusiana na Kafara, halazimiki kulipa kafara. Hata hivyo anapata madhambi na analazimika kulipa siku iliyobaki. Hali kadhalika anapaswa kulipa siku alizofanya hivyo na kufanya Tawbah.
Ama kuhusiana masuala ya kumuingilia mke, analazimika pia kulipa Kafara kwa ile mara ya kwanza ya kumuingia mke na si lazima kwa kila siku moja – Na Allaah Anajua Zaidi.
Kutoa Manii Kwa Makusudi, Je Mtu Atalipa Kafara?
Fatwa Kutoka:  ‘Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn 'Uthaymiyn
Chanzo: Fataawa Arkaanil-Islaam, uk. 478
Swali:
Je, kutoa manii kunabatilisha Swawm? Mtu anapaswa kulipa Kafara?
Jibu: 
Mtu akitoa manii Swawm yake inabatilika, inabatilika na mtu analazimika kulipa siku hiyo na kufanya tawbah [kwa kuwa ni haramu]. Kulipa kafara ni pindi mtu anapofanya jimai wakati wa Swawm.


Swawm Ya Watoto

Fatwa Kutoka: ’Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Ibn 'Uthaymiyn
Chanzo: Fataawa fiy Ahkaami-Swiyaam, uk. 84

Swali:
Ipi hukmu ya Swawm kwa watoto?
Jibu: 
Swawm ya watoto kama tulivyosema imependekezwa na si waajib. Mtoto akifunga, anapewa thawabu; na kama akiacha, hapati dhambi. Hata hivyo inatakiwa kwa wazazi wao wawaamrishe kufunga ili wajizoeze.


Kafiri Ambaye Anasilimu Katika Ramadhaan

Fatwa Kutoka: Imaam Muwaffaqud-Diyn Ibn Qudaamah Al-Maqdisiy
Chanzo: Al-Mughniy (4/414-415)
Al-Khiraqiy kasema:
"Ikiwa Kafiri atasilimu wakati wa Ramadhaan, anatakiwa kufunga mwezi (masiku) yaliyobakia.
Ama kuhusu siku za mwezi huo zilizompita kabla hajakuwa Muislamu, sio waajib kwake kulipa siku hizo. Kauli hii ni ya ash-Sha'biy, Qataadah, Maalik, al-Awza'iy, ash-Shaafi'iy, Abu Thawr na Hanafiyyah.
'Atwaa kasema analazimika kulipa siku hizo.

Kutoka kwa al-Hassan [al-Baswriy] kumepokelewa kauli zote mbili.
Ama kuhusu sisi – Hanaabilah – hatuoni kama ni waajib kwake kulipa siku hizo ambazo zilipita hali ya kuwa alikuwa Kafiri. Hali kadhalika si waajib kwake kulipa Ramadhaan iliyopita.


Mke Anampikia Chakula Mume Wake Asiefunga Katika Ramadhaan
Fatwa Kutoka: ’Allaamah 'Abdul 'Aziyz Ibn ’Abdillaah Ibn Baaz
Swali: 
Mume wangu hataki kufunga zaidi ya miaka ishirini. Kipindi chote hicho nilikuwa nikimpikia chakula wakati mimi mwenyewe nimefunga. Je ninapata madhambi?
Jibu: 
Ndiyo, ni dhambi. Lazima utubu kwa Allaah kwa kitendo hicho. Wakati wewe unampikia chakula mchana wa Ramadhaanunamsaidia kumuasi Allaah (’Azza wa Jall). Allaah (Jalla wa 'Alaa) Anasema:
ولا تعاونوا على الإثم والعدوان
”Wala msisaidiane katika dhambi na uadui.” (5: 2)
Kumpikia chakula au kumtengea chakula na kumpa mchana wa Ramadhaan au kumpa sigara au pombe n.k. ni dhambi, na ni maovu juu ya maovu. Hupaswi kabisa kumsaidia kutofunga sawa ikiwa ni [kwa kumpa] chakula, kinywaji, sigara au pombe. Yote haya ni madhambi juu ya madhambi. Badala yake unatakiwa kumnasihi na kukataa kumtii na kumwambia huwezi kumsadia kwa hilo. (Ni juu yake) Achume mwenyewe na afanye madhambi mwenyewe.  


Kwa Aliyefunga Kumbusu Mke Wake

Swali:
Ikiwa kijana au mzee atambusu mke wake wakati amefunga, je atakuwa kafanya dhambi?
Jibu.
Mwenye kufunga atakuwa hakutenda dhambi kwa kumbusu mke wake, bila kujali akiwa ni kijana au mzee. Hii ni kutokana na kilichopokelewa kutoka kwenye Swahiyh ya Muslim kwamba ’Umar Ibn Abi Salamah alimuuliza Mtume (Swala Allaahu ’alayhi wa sallam):”Je, aliyefunga anaweza kubusu? Mtume (Swala Allaahu ’alayhi wa sallam) akasema: Muulize huyu mwanamke (akimaanishaUmm Salamah). Hivyo, akamwambia kuwa Mtume (Swala Allaahu ’alayhi wa sallam) angefanya hivyo. Kisha akasema (’Umar Ibn Salamah): ”Ee Mtume WaLlaahi! Lakini wewe Allaah Amekusamehe madhambi yako yaliyotangulia na yajayo. Kisha Mtume (Swala Allaahu ’alayhi wa sallam) akasema: ”Kwa haki, mimi ni mwema zaidi kwa Allaah (katika Shari’ah Zake) na ninamuogopa Allaah zaidi kuliko nyinyi nyote.” [Muslim namba 1108]


Miji Ambayo Masaa ya kufunga Ni Marefu Sana

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah Muhammad Ibn Swaalih `Uthaymiyn
Chanzo: Fataawa Islamiyah uk. 276, mj. 2
Swali.
Tuko katika Mji ambapo jua halizami mpaka saa 3:30 au 4:00 (saa tatu au saa nne) za usiku. Ni lini tunatakiwa tufungue Swawm?
Jibu:
Utafuturu Swawm wakati jua linapozama. Maadamu tu mko na mchana na usiku kwa masaa 24, unawajibika kufunga, hata kama masaa ni marefu kiasi gani.

Mwanaume Kuswali Tarawiyh Nyumbani Na Familia Yake

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah Muqbil
Chanzo: 'Fadaa'ih wa Naswaaih, Al-’Allaamah Al-Muhaddith Muqbil Ibn Haadiy Al-Waadi'iy, Daarul-Haramayn, Cairo. ukurasa 86

Swali:
Je, inajuzu kwa mwanaume kuswali Swalah ya Tarawiyh na familia yake nyumbani?
Jibu:
Hakuna ubaya kufanya hivyo, ni bora kama alivyofanya.


Kuvunja Swawm Kwa Ajili Ya Kazi Ngumu

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah Muhammad Ibn Swaalih Al-’Uthaymiyn
Chanzo: Hukumu ya Kiislamu juu ya Nguzo za Uislamu, mj. 2, uk. 630
Swali:
Yapi maoni yako kuhusu ugumu wa kazi ya mtu na ikawa vigumu kwake kufunga. Je inajuzu kwake kukata Swawm?

Jibu:
Maoni yangu ni yeye kuvunja Swawm yake kutokana kazi hii ni Haramu kwake kuvunja Swawm, haijuzu (kuacha kufunga). Haijuzu kwa mtu kulinganisha kazi yake na Swawm, anatakiwa kuchukua likizo kazini wakati wa Ramadhaan, ili iwe kwake rahisi kuweza kufunga.
Swawm ya Ramadhaan ni katika nguzo za Uislamu na haijuzu kwake kuacha kufunga (kwa sababu ya kazi).

Mwanamke Hakumbuki Siku Ngapi Zilizompita Alipokuwa Na Hedhi

Fatwa Kutoka: ‘Allaamah ’Abdul-’Aziyz Ibn Baaz
Chanzo: Fataawa Kiislamu Kuhusu Wanawake – Darussalam, uk. 145

Swali:
Sikuweza kulipa siku zilizonipita za mwezi wa Ramadhaan kutokana na kipindi changu cha hedhi na sikumbuki ni siku ngapi zilizobaki. Nifanye nini?  
Jibu:
Ukhtiy katika Uislamu, unatakiwa (kujitahidi) kuchunguza suala hili vizuri na ufunge (takriban) siku ambazo unafikiria zilikupita. Na muombe Allaah Akusaidie kwa hili. Mola wetu! Usituchukulie tukisahau au tukikosea.” (2: 286)
Jitahidi kuchunguza suala hilo na kuwa muangalifu kwa heshima yako mwenyewe mpaka ufunge kile unachoamini (unachofikiria) kilikupita. [baada ya hapo] unatakiwa kufanya tawbah kwa Allaah.

Swawm Imempiga Sana. Je anaweza kuoga au Kuweka Maji usoni?

‘Allaamah Swaalih Ibn Fawzaan

Swali:
Mwanamke anauliza, inajuzu nikipigwa na Swawm kuweka baadhi ya maji usoni?

Jibu:
Hakuna ubaya kufanya hivyo. Mtu anajipatia nguvu hali ya kuwa amefunga. Mtu anaweza hata kuoga, kuweka maji usoni. Walikuwa Maswahaba (Radhiya Allaahu ’anhum) wamefunga katika safari, wakiweka maji usoni. Hakuna ubaya kufanya hivyo.Kufuturu Kwa Tende Ni Sunnah – La Sivyo Mtu Anywe Maji

‘Allaamah Swaalih Ibn Fawzaan

“Dalili ya hadiyth zinaonesha kuwa ni Sunnah mtu anapofuturu afungue Swawm yake kwa tende tatu , nne, tano au zaidi. Mtu akikosa tende afuturu kwa maji kwani ndivyo Mtume (Swala Allaahu ’alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akifanya. Na mtu akifuturu kwa vyakula vingine haikatazwi – lakini ni kinyume na Sunnah.

0 Comments