FIQHI : HEDHI, NIFASI NA DAMU YA UGONJWA

Nini Hedhi?

Hedhi ni kutokwa na damu mwanamke katika sikuzake, bila ya ugonjwa; bali ni kwa maumbile ya kawaida. Hedhi pia huitwa nifasi, kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kuwa alimuuliza Sayyidah 'Aisha r.a.? "umepatwa na damu ya nifasi"? Hivi ni kwamba Sayyidah 'Aisha r.a. hakujaaliwa kupata mtoto, kwa hivyo hapa "nifasi" imekusudiwa "hedhi". Na asili ya hedhi imekuja kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
 "Na wanakuuliza juu ya hedhi,... .........". (Al Baqara : 222).
Na kuna Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
 "Kitu hiki kakiandika (kakijaalia) Mwenyezi Mungu kwa banati wa Adam".

Rangi ya Damu ya Hedhi

Damu ya hedhi huwa katika hali hizi:
Ya Kwanza, nyeusi, kwa qauli ya Fa'tima bint Abi Habiish r.a. kwamba alikuwa akipatwa na damu ya hedhi akaambiwa na Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kuwa:   "Ikiwa ni damu ya hedhi, basi hio inajuulikana kwa weusi wake". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Nissaai na Ibnu Hibbaan na Addarqu'tny).
Ya Pili, nyekundu; kwani hii ndio rangi ya asili ya damu.
Ya Tatu, manjano; nayo huwa kama rangi ya usaha.
Ya Nne, uchafu-uchafu; kama maji ya tope.

Muda wa Siku za Hedhi

Muda wa damu ya hedhi unatafautiana kwa kutafautiana na hali ya mwanamke mwenyewe, imebainika kuwa muda wa hedhi huwa hata kwa siku moja. Imepokewa kutoka kwa Sayyidna 'Ali r.a. na ndivyo alivyochukuwa Imam Shafi'ii r.a. na wengi wa Maimam r.a. kuwa ni siku sita au siku saba, hivi ni kutokana na qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kumwambia Hamna bint Jahsh r.a.:
" "Utapatwa na hedhi siku sita au siku saba - Mwenyezi Mungu Mtukufu ndie Mjuzi - kisha jiwoshe. Ukiona kuwa umesha'tahirika, (yaani damu imesita) na umeshajisafisha (yaani umekoga), basi sali siku (usiku na mchana wake) ishirini na nne au ishirini na tatu, na funga (muda huo huo) kwani muda huo hukutosheleza; na fanya hivyo hivyo katika kila mwezi". (Imehadidthiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy).
Imebainika damu ya hedhi wingi wa kuendelea kwake ni kwa muda wa siku (usiku na mchana wake) kumi na tano, hivi pia ndivyo ilivyoelezwa na Imam 'Ali r.a. Imam Shafi'ii amesema kuwa yeye aliwaona wanawake waliomthibitishia kuwa hawakuacha kupatwa na hedhi ya muda wa siku kumi na tano.

Ku'tahirikana na Hedhi

Katika njia za kuhakikisha kuwa damu ya hedhi imekwisha na anaweza kukoga na kufanya ibada zake kama kawaida ni kwa kutia pamba kwenye utupu, ikitoka safi hio pamba hapo ndio hakika kuwa damu ishasita. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Marjana r.a., kijakazi wa Sayyidah 'Aisha r.a. yenye maneno haya:
 "Walikuwa wanawake wakipeleka kwa Sayyidah 'Aisha r.a. chombo ndani yake imo pamba (waliotumia kutaka kujua kumalizika damu ya hedhi) yenye umanjano-manjano, Sayyidah 'Aisha r.a. huwambia, msifanye haraka, ngojeeni mpaka muione pamba inatoka safi, nyeupe". (Imehadithiwa na Malik)

Nini Nifasi?

Nifasi ni damu ya uzazi, damu inayotoka kwa kuzaa, ikiwa kilichozaliwa ni hai au kimekufa.

Muda wa Damu ya Nifasi

Imebainika kwamba uchache wa muda wa damu ya nifasi ni muda ule ule wa kumaliza kuzaa, na wingi wa muda ni siku sitini. Amesema Al Auza'i: "Tunae mwanamke aliona damu ya uzazi katika muda wa miezi miwili". Na amesema Rabi'at Sheikh wa Malik: "Nimewahi kuwasikia watu wakisema kuwa kipindi kikubwa cha mwanamke kuwa na damu ya uzazi ni siku sitini".
Aghlab ya muda wa damu ya uzazi ni siku arubaini, kama ilivyopokewa kutoka kwa Sayyidah 'Aisha r.a.:
"Walikuwa wazazi zama za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. wanakaa siku arubaini baada ya kuzaa". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy na imepewa darja ya Hadithi sahih na Al Haakim).

Uchache wa Muda wa 'Tahara

Baada ya hedhi, yaani muda baina ya hedhi na hedhi ni siku kumi na tano. Hisabu hii imechukuliwa kwa kufanyiwa utafiti na kwamba madhali wingi wa muda wa hedhi ni siku kumi na tano, basi na uchache wa 'tahara baina ya hedhi na hedhi ni siku kumi na tano. Hakuna wingi wa muda wa 'tahara, kwani wanawake wengine hawapati hedhi kabisa na wala si ugonjwa, ni maumbile.

Damu ya Ugonjwa

Damu ya ugonjwa ni ile damu anayotoka mwanamke mbali na muda wa hedhi na muda wa nifasi. Mwanamke akipatwa kutokwa na damu mbali na muda wa hedhi na muda wa nifasi huwa amepatwa na damu ya ugonjwa.

Hali za Kupatwa na Damu ya Ugonjwa

Hali ya damu ya ugonjwa ni hizi:
Ya Kwanza, yenye kuanza na yenye kupambanulika; nayo ni vile mwanzo wake kuona baadhi ya siku anatokwa na damu kwa wingi na baadhi ya siku anatokwa na damu kidogo, basi hivyo kutokwa na damu kidogo-kidogo hio huwa ni damu ya ugonjwa, na ile yenye kutoka kwa nguvu ndio damu ya hedhi. Hivyo basi, kwa sharti, ile damu ya hedhi; yaani ile yenye kutoka kwa wingi isipungue muda wa uchache wa damu ya hedhi, na wala isizidi muda wa wingi wa muda wa damu ya hedhi.
Ya Pili, yenye kuanza lakini haipambanuliki; nayo ni vile kuona damu mara moja tu, na akaingia kwenye 'tahara kwa muda wa siku ishirini na tisa zilizobaki katika mwezi.
Ya Tatu, yenye kujuulikana na yenye kupambanulika, nayo ni vile kupata hedhi, kisha akaingia kwenye 'tahara, na akawa anajua aghlab ya muda anaokuwa katika damu ya hedhi na kiwango cha damu ya hedhi inayotoka; itapoendelea baada ya hapo huwa ni damu ya ugonjwa.
Ya Nne, yenye kujuulikana, lakini si yenye kupambanulika; nayo ni vile kuona damu mara moja tu, na asiweze kupambanua kama ni damu ya hedhi au damu ya ugonjwa, katika hali hii huchukua ada yake, yaani aghlab ya hali inavyomtokea. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Ummu Salamah kwamba mwanamke alikuwa akitokwa na damu katika zama za Mtume wetu Mpenzi s.a.w., Mtume wetu Mpenzi akamtolea fatwa kwa kusema:
 
"Naakae muda wa usiku na siku ambazo akipata damu ya hedhi katika mwezi kabla hajafikwa na haya yaliyomfika, kisha naawache Sala katika muda huo katika kila mwezi". (Imehadithiwa na Malik na Al Nissaai na Abu Daud na Al Bayhaqy na kutiliwa nguvu na Al Tirmidhy).

Uchache wa Miaka Mwanamke Kupata Hedhi

Kwa vile hakuna kilichotajwa katika Sharia wala lugha uchache wa miaka ya kupata hedhi, utafiti umehakikisha kuwa miaka tisa ni uchache wa umri wa kupata hedhi. Amesema Imam Shafi'ii r.a. kuwa wanawake aliosikia wanapata hedhi mapema ni wanawake wa Tihama, wao hupata hedhi katika umri wa miaka tisa. Na Hadithi alioipokea Al Baihaqy kutoka kwa Sayyidah 'Aisha r.a. kwamba hakuna wingi wa miaka mwanamke anaweza kukaa bila ya kupata hedhi, bali huenda hata asipate hedhi katika umri wake wote.

Uchache na Wingi Wa Muda Wa Ujauzito

Uchache wa muda wa ujauzito ni miezi sita na vipindi viwili vidogo, kipindi cha kuingiliana mke na mume na kipindi cha kujifungua. Sayyidna 'Uthman r.a. alifikiwa na mwanamke aliejifungua mimba ya miezi sita, akawashauri watu kuwa apigwe mawe huyu mwanamke, akasema Ibnu 'Abbas r.a. akateremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu:
 "………Na kuchukuwa mimba kwake hata kumwachisha ziwa ni miezi thalathini………". (Al Ahqaaf : 15).
Na akateremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu:  "……, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili……". (Luqman : 14).
Kuwachisha ziwa kwa miaka miwili na mimba miezi sita, kwa kuteremka Qauli hizi za Mwenyezi Mungu Mtukufu wakafuta hukmu ya kumpiga mawe yule mwanamke na ikawa ni dalili ya kufuatwa. Ama muda mrefu wa kuendelea ujauzito ni miaka minne, hivi imethibiti kwa utafiti.
Amesema Imam Malik r.a.:
 "Huyu jirani yetu mke wa Muhamad bin 'Ajlaan, ni mwanamke mkweli na mumewake ni mtu mkweli; amechukuwa mimba tatu katika muda wa miaka kumi na mbili, kila mimba imechukuwa miaka minne". (Imehadithiwa na Mujaahid).
Alikwenda mtu kwa Malik bin Dinar akamwambia: "Ewe Ba Yahya! Muombee du'a mwanamke mjamzito wa tangu miaka minne yumo katika shida kubwa, akamuombea du'a. Akamtokea mtu akamwambia: "muwahi mke wako", akenda; baada ya muda akarejea amebeba shingoni mwake mtoto wa miaka minne, amejaa meno kinywa tele.

Yenye Kuharimishwa kwa Mwenye Hedhi na Nifasi

Inaharamishwa kwa aliomo kwenye hedhi na aliomo kwenye damu ya uzazi mambo manane:
La Kwanza, Sala, vilevile sujudi iliobainishwa katika Qur'ani (mumo mwahala katika Qur'ani ukifika katika kusoma hutakiwa usujudu) vilevile sujudi ya kushukuru, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: " إذا  "Ukipatwa na hedhi wacha kusali". Na kwa Hadithi zifuatazo Sala zilizowachwa wakati wa hedhi hazilipwi, imepokewa kutoka kwa Sayyidah 'Aisha r.a.:
"Tulikuwa zama za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. tukipata hedhi tukisha 'tahirika tunaamrishwa kulipa Saumu zetu, hatukuwa tukiamrishwa kulipa Sala". Na katika Hadithi nyengine:
 "Ilikuwa yakitupata hayo - yaani hedhi - tukawa huamrishwa kulipa Saumu, wala hatukuamrishwa kulipa Sala". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
La Pili, Saumu, yaani kufunga; hivi ni kutokana na hizi Hadithi ambazo zinaeleza kuwa "wakiamrishwa kulipa Saumu zao". Na kwa Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi:  "Kwani sio hivyo kuwa akipatwa na hedhi hasali wala hafungi"? (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Na hivi kusamehewa kulipa Sala ni kwa vile Sala zinakuwa nyingi, kinyume na Saumu; kwa kuepusha mashaka na uzito ndio ikasamehewa kulipa Sala. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
  "..........Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini.......". (Al Hajj : 78).
La Tatu, kusoma Qur'ani hata kama ni kidogo, hivi ni kwa vile Utukufu wa Qur'ani na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  "Asisome chochote katika Qur'ani mwenye janaba wala mwenye hedhi". (Imehadithiwa na Abu Daud na Al Tirmidhy).
Ama nyiradi za Qur'ani na nyenginezo za mawaidha na Hadithi na hukmu za kusoma Qur'ani, tajwiid; na kama vile du'a ya kipando:
  "……, Ametakasika aliye mfanya huyu atutumikie, na tusingaliweza kufanya haya wenyewe". (Azzukhruf : 13).
Au du'a ambayo husomwa mtu anapofikwa na msiba:
  "........... Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea". (Al Baqara : 156).
Zote hizi asili yake ni Qur'ani, lakini zinapokusudiwa kuwa ni du'a, si kusomwa kuwa ni Qur'ani hujuzu kuzisoma hata mwenye janaba, hedhi au nifasi. Ama ikiwa zitakusudiwa Qur'ani pekee au Qur'ani na du'a; hapo itakua ni haram kwa mwenye janaba, hedhi au nifasi kuzisoma. Pia inajuzu kusema (si kusoma) Bismillah au kushukuru Mwenyezi Mungu, Alhamdulillah.
La Nne, kuugusa msahafu na kuuchukua, hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
   "Hapana akigusaye ila walio takaswa". (Al-Waqi'ah : 79).
Na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Hagusi Qur'ani isipokuwa mtu 'taahir". (Imehadithiwa na Al Darqu'tny).
Ikiwa kuugusa ni haram, basi kuuchukuwa ni haram zaidi, ila ikiwa unachukuliwa kwenye vitu vingine na haikusudiwi kuchukuwa hio Qur'ani tu; hivyo hujuzu.
La Tano, kuingia msikitini; hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: "  "Hauhalalishwi msikiti kwa mwenye hedhi wala janaba". (Imehadithiwa na Abu Daud).
Ama kuingia msikitini kwa kupita tu, inajuzu; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:  "……isipokuwa mmo safarini…..". (An-nisaai : 43).
Kupita msikitini kwa mwenye hedhi inajuzu, iwapo hatachelea kuuchafua msikiti kwa damu, pia haitajuzu kupita msikitini mwenye kisonono, au kikojozi au mwenye kijaraha chenye kuchururika damu; hivi ni kwa kuchelea kuja kuuchafua msikiti.
La Sita, kufanya 'tawafi (kwenye msikiti wa Makka) hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akimwambia Sayyidah 'Aisha r.a. alipopatwa na hedhi wakati yumo katika Hija:
  "Fanya anayofanya mwenye kuhiji isipokuwa usifanye 'tawaaf mpaka u'tahirike". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
La Saba, kumuingilia mwanamke; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "……. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wa'taharike……". (Al Baqara : 222).
La Nane, kuchezea sehemu (ya mke) iliopo baina ya kitovu na magoti. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akimjibu Ibna Masoud r.a. alipomuuliza Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kitu chenye kumhalalikia wakati mkewe (mkewe Ibni Masoud) yumo kwenye hedhi, Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akasema:  "Chako ni sehemu ya juu ya mwili". (Imehadithiwa na Abu Daud).
Imehadithiwa na Sayyidah 'Aisha r.a. kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
   "Alikuwa (Mtume wetu Mpenzi s.a.w.) anamuamrisha mmoja wetu akiwa kwenye hedhi avae wizari (nguo inayovaliwa kuanzia juu ya kitovu mpaka chini), na akajisaidia kwa juu ya wizari". (Imehadithiwa na Muslim na Muimunah nae amepokea kama hivi).
Na maana ya kuharimishwa ni kuharimishwa utupu, na amesema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
  "Mwenye kuchunga pembezoni mwa bustani hukhofiwa kujakuchunga ndani ya hio bustani". Na kwa qauli kongwe ya Imam Shafi'ii r.a. kwamba chenye kuharimishwa ni kuingilia katika utupu, na hoja yake Imam Shaafi'ii r.a. ni Hadithi ya Anas r.a. kwamba Mayahudi walikuwa akipatwa na hedhi mwanamke wao hawalinae wala hawakai nae nyumbani, akaulizwa Sahaba wa Mtume wetu Mpenzi s.a.w.; akateremsha Mwenyezi Mungu Mtukufu hii Aya:
                  "…….Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka wa'taharike……". (Al Baqara : 222).
Kwa kuteremshwa Aya hii, Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akasema:
  "Fanyeni kila kitu isipokuwa kuingilia". (Imehadithiwa na Muslim).
Hakika ya kumuingilia mwanamke wakati yumo katika hedhi au nifasi kumeharimishwa, mwenye kufanya hivyo atakuwa amefanya miongoni mwa madhambi makubwa  itamlazim atubie kwa haraka. Kwa mwenye kufanya kosa hili, pamoja na kutubia haraka; inapendekezwa atoe sadaka, ikiwa kamuingilia siku za mwanzo wa hedhi, atoe dinari moja, na ikiwa katika siku za kukaribia mwisho wa hedhi atoe nusu dinari. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
 
"Mwenye kumuingilia mkewe nae yumo katika hedhi, ikiwa damu nyekundu, basi atoe sadaqa dinari* moja; na ikiwa damu ya kimanjano, atoe sadaqa nusu dinari"
Na nifasi inapewa hukmu hii hii ya hedhi.

Yenye Kuharimishwa kwa Mwenye Janaba

Inaharimishwa kwa mwenye janaba mambo matano miongoni mwa yale mambo manane yenye kuharimishwa kwa mwenye hedhi au nifasi, nayo ni:
La Kwanza, Sala.
La Pili, kusoma Qur'ani.
*Kujua thamani ya dinari kwa pesa za mahala, ni kuuliza wanazuoni wajuzi wa hesabu za fedha.
La Tatu, kuchukuwa au kugusa mas-hafu.
La Nne, kufanya ‘tawafu (ndani ya Msikiti wa Makka).
La Tano, kukaa ítikafu msikitini
Hukmu ya mambo matano haya kwa mwenye janaba ni sawa na ilivyo kwa mwenye hedhi au nifasi, isipokuwa kukhusu Sala. Mwenye kupatwa na janaba itamlazim ailipe Sala ikiwa hakuweza kuisali katika wakati wake, tafauti na anaepatwa na hedhi au nifasi, wao haiwajibikii kulipa Sala zinazowapita nao wamo katika hedhi au nifasi.
Kuharimishwa kwa mwenye janaba kukaa msikitini  , iwapo kwa udhuru; kama vile amelala na kuota akapatwa na janaba nae yumo msikitini na hawezi kutoka, amesema Imam Al Nawawi r.a. kwamba katika hali hii itampasa atayammam. Ikiwa katika sehemu ya huo msikiti papo pahala pakukogea, basi atakoga, ikimkinika; kama sio hivyo atatayammam.
Ama kupita msikitini kwa mwenye janaba, ikiwa kwa kazi maalum basi haidhuru, yaani inajuzu kupita.
Hivi ni kutokana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
  ......      isipokuwa mmo safarini

Yenye Kuharimishwa kwa Asiekuwa na Udhu

Inaharimishwa kwa mwenye hadathi ndogo, yaani asiekua na udhu mambo matatu:
La Kwanza, Sala yenye kurukui na kusujudi, vile vile sijida ya kushukuru, na sijida ya kusoma Qur'ani, na Sala ya maiti. Hivi ni kwa Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "Mwenyezi Mungu Mtukufu hakubali Sala bila ya 'tahara, wala sadaqa kwa mali ya haram".
La Pili, kufanya 'tawaf kwenye Msikiti wa Makka. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu mpenzi s.a.w.:   "Ku'tufu kwenye Msikiti wa Makka ni Sala". (Imepokewa na Al Haakim).
La Tatu, kuugusa mas-hafu na/au kuuchukuwa.
Ama mwanafunzi wa chuoni na ambae anatambua jema na baya, si mtoto mdogo; yeye anaweza kuugusa na kuuchukuwa mas-hafu hata ikiwa hana udhu, hivi ni kwa vile ni taabu kuweza yeye kubaki na udhu kila wakati; lakini ni vyema kuzoweshwa kuwa na udhu kama inavyowezekana. Hivi hivi ndivyo ilivyo hukmu kwa mwalim wa Qur'ani.
Yote haya ni kuepusha mashaka na uzito, wakati ambapo Dini yetu tukufu inakataza uzito, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
   " ……. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini………". (Alhajj : 78).

0 Comments