UKUMBUSHO KWA NDUGU ZETU JUU YA HUKUMU YA SAWMU YA RAMADHANI

BISMILLAHI RAHMANI RAHEEM
Hivyo nasema nikitaka msaada kwa Allaah:

MAANA YA SAWMU
Na maana ya sawmu kisheria ni kujizuia kutokana na kula na kunywa na kukutana na mwanamke kimwili kwa nia ya kufanya ibada kwaajili ya Allaah kuanzia kuchomoza kwa alfajiri ya kweli mpaka kuzama kwa jua.

SAWMU NI WAJIBU KWA NANI?
Ni wajibu kufunga sawmu ya Ramadhani kwa kila muislamu ambaye ni Baleghe, mwenye akili timamu na mwenye uwezo wa kufunga na inapendeza kuamrishwa mtoto mdogo kufunga sawmu kama ataweza.

WANAORUHUSIWA KUTOKUFUNGA SAWMU YA RAMADHANI NI WATU WA AINA NNE
Wa kwanza: Ni mgonjwa amabaye anapata madhara kwaajili ya kufunga na msafiri kama sawmu itamletea madhara kwenye safari yake, na juu yao hao watu wawili kuilipa hiyo sawmu na kama watafunga katika hali hiyo sawmu hiyo inafaa.

wapili:  mwanamke mwenye hedhi atafungua na kuja kuilipa hiyo sawmu na kama atafunga katika hali hiyo sawmu yake haitofaa

Watatu: mwanamke mjamzito na yule anayenyonyesha kama watahofia juu ya nafsi zao kupata madhara au kudhurika mtoto wanaruhusiwa kufungua na kuja kulipa.

wanne: Ni yule asiyeweza kufunga kutokana na umri mkubwa (uzee) au maradhi yasiyopona, kwa hakika yeye atalisha chakula masikini mmoja kila siku hadi mwezi utakapoisha.

VITU VINAVYOHARIBU SAWMU
Inaharibika sawmu  kutokana na kula au kunywa au kukutana na mwanamke kwaajili ya Jimaa kwa makusudi na hali ya kuwa anakumbuka kuwa ana sawmu, na vilevile inaharibika sawmu kwa kupatikana hedhi kwa upande wa mwanamke na yeyote atakaefungua kwa kufanya jimaa yeye atawajibika kwa kulipa hiyo sawmu kwa kumuacha mtumwa huru, Kama akimkosa mtumwa basi atafunga miezi miwili inayofuatana (yaani atafunga siku sitini bila kuacha), na kama akishindwa kufunga basi atalisha masikini sitini na kama akiwakosa masikini basi hilo litakuwa si wajibu kwake.

NI WAKATI GANI ITAKUWA NI WAJIBU KUFUNGA SAWMU YA RAMADHANI?
Ni wajibu kufunga Ramadhani katika hali mbili: Hali ya kwanza wakati unapoonekana mwezi muandamo wa ramadhani baada ya kuzama kwa jua siku ya tarehe ishirini na tisa, na kama mwezi haukuonekana au pakawa na mawingu basi itakuja hali ya pili nayo ni kukamilisha siku thelathini za mwezi wa shaaban.

NI VITU GANI VINAVYOPENDEZWA KUFANYA KATIKA MWEZI WA RAMADHANI?
Fahamu ya kwamba Allaah hakuweka sheria ya kufunga sawmu ispokuwa kwaajili ya hekma ambayo ni kubwa, ambayo ni kumcha Allaah, kabla ya kutaja vitu vinavyopendezwa kufanya fahamu ya kuwa ni wajibu kuswali swala ya jamaa katika msikiti kwa wanaume ispokuwa kama utapata dharura ya kisheria, na ni wajibu kujiweka mbali na madhambi yaliyodhihiri na yaliyofichika, na vipi mtu atajizuia na vitu vya halali na akafunga kwa vitu vya haramu na ni juu yake kufanya haraka katika mambo ya kumtii Allaah kama kuunganisha undugu, kuwafanyia wema wazazi na mengineyo katika mambo ya kheyri kisha baada ya hilo inapendeza kwa muislamu kuanza sawmu yake kwa kula kama inavyopendekezwa kuchelewesha daku na kuwahi kufuturu utakapofika wakati wa kufuturu na ni bora kufuturu kwa tende au chochote ambacho kinapatikana kwa wepesi katika riziki, Kisha akithirishe kusoma Quran tukufu na kuzingatia katika aya zake na uzifanyia kazi hukumu zake,na kisha kuhifadhi kisimamo cha ramadhani (Tarawehe) Rakaa kumi na moja ni bora kuswali kwa jamaa pia si vibaya kuswali mwenyewe nyumbani kwako. Na inapendeza kukithirisha kuwasaidia wajane na wasiojiweza na inapendeza kwake kufanya itikafu msikitini katika kumi la mwisho wa Ramdhani ili kuitafuta LAYLATUL KADR. Ambayo inapatikana katika masiku ya witir kwenye kumi la mwisho katika mwezi mtukufu wa ramadhani, na inapendeza kwake kufanya UMRA sababu itachukuliwa kama amefanya Hijja pamoja na Mtume (J u u    y a k e   r e h m a  n a  a m a n i)
na inapendeza kwake kukithirisha dua katika mwezi mtukufu wa ramadhani, na kulingania watu katika njia ya Allaah mtukufu.


0 Comments