FIQHI: Twahara | Mlango wa kwanza | Hukumu za Twahara pamoja na MajiUTANGULIZI:
Miongoni mwa masomo muhimu ambayo
Muumini hanabudi kuyajua,ni somo la Fiqihi.
Kwani somo hili lina ayazunguka maisha yetu ya kila siku.
Kuanzia upande wa ibada,upande wa miamala na uhalali wa vitu na uharamu wake.
Maana ya neno Fiqihi:
Neno Fiqihi,ni neno la kiarabu lenye maana ya Ufahamu.
Imekuja aya katika Qur ani kwa maana hii pindi watu wa nabii Shuibu-alayhi salaamu-walipo mwambia nabii wao:
(قَالُوا يَا شُعَيْبُ مَا نَفْقَهُ كَثِيرًا مِّمَّا تَقُولُ)
)Wakasema: Ewe Shua'ibu! Mengi katika hayo unayo yasema hatuyafahamu(Surat Hudi:91{Qur ani 11:91}
Ama maana ya Fiqihi katika istilahi ya wanazuoni,ina maana ya :
Elimu juu ya hukumu za kisheria,zinazo husiana na matendo,zilizo chumwa toka katika dalili zake za wazi.
Machimbuko ya Fiqihi:
Tunakusudia machimbuko ya Fiqihi yaani vyanzo vyake,
Pindi tunapo sema suala fulani ni halali au ni haramu,
tegemezi lake au chanzo chake kinakuwa ni nini?
Machimbuko hayo ni:
1}Qur ani Tukufu
2}Hadithi za Mtume{swala Allahu alayhi wasallam}
3}Makubaliano ya wanazuoni
4}Upimaji,ulinganishaji.
Maudhui ya somo hili:
Somo hili lahusiana na matendo ya waja mukalafiina{wenye akili ,walio balenge}
kwa sura ya kiujumla.
Kwa hiyo somo hili lina angalia mahusiano kati ya mja na Mola wake,mja na nafsi yake pamoja na mja na jamii yake.
Hukumu hizi za kimatendo zina husiana na yale yanayo toka kwa mwanaadamu miongoni mwa kauli na vitendo ,makubaliano na miamala mbali mbali.
Somo hili lina gawanyika sehemu mbili:
1}Ibadati:
Kwa kuangalia masuala yanayo husiana na ibada,
mfano swala na hija.
2}Muamalaati: 
Kwa kuangalia masuala yanayo husiana na miamala{mahusiano},mfano wa ndoa na biashara.


FAIDA YA ELIMU YA FIQIHI:
Kuitambua elimu ya Fiqihi na kuifanyia kazi kunapelekea kuboreka kwa mwanaadamu,kusihi kwa ibada zake na kutengamaa kwa mwenendo wake.Na mtu mmoja mmoja katika jamii akitengemaa ndiyo kutengemaa kwa jamii yote.Matokeo yake ni kuishi maisha mazuri hapa duniani na kesho akhera kujipatia ridhaa ya Allah na pepo yake.

FADHILA ZA FIQIHI{Ufahamu} JUU YA DINI NA MAHIMIZO JUU YA KUISOMA:
Kujipatia ufahamu juu ya dini ni miongoni mwa mambo bora kabisa.Aya za Qur ani na hadithi za mtume zimezungumzia fadhila zake na kuwahimiza watu katika kuisoma Fiqhi na kujipatia ufahamu.
Allah mtukufu anatueleza ndani ya Qur ani:
(Wala haifai kwa waumini kutoka wote na kwenda kupambana na maadui. Lakini kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapo warejea, ili wapate kujihadharisha?)Surat Attawba: 122
Pia kipenzi chetu mtume Muhamad-rehema na amani za Allah zimshukie-anatueleza:
(Yule ambaye Allah anamtakia kheri,basi anampatia ufahamu juu ya dini) Hadithi imepokelewa na imamu Bukhari na imamu Muslim.
Mtume kasema…yule ambaye Allah atamtakia kheri,neno kheri katika lugha ya kiarabu limekuja likiwa ni nakra na wala si maarifa, kumaanisha kuwa kheri zinazo kusudiwa ni kheri za aina yote.
Kutokana na hivyo Ufahamu katika dini ni jambo muhimu sana na lenye kuchukuliwa uzito katika dini yetu.Kwani muislamu akiitambua na kuifahamu dini yake ,na kufahamu mambo yaliyo wajibu kwake na kutambua haki zake,basi atamuabudu Mola wake kwa ujuzi na wala si kwa kubahatisha,na kuwafiqishwa katika kheri duniani na akhera.

MLANGO WA KWANZA:
TWAHARA:
Somo la kwanza:Hukumu za twahara pamoja na maji:
1)Umuhimu wa Twahara:
Twahara ni ufunguo wa swala na katika masharti yake lililo muhimu sana.
Twahara imegawanyika sehemu mbili:
a)Twahara ya kimaana:Nayo ni kuutwaharisha moyo dhidi ya shirki na maasi na kutu zote katika moyo.Nayo ni muhimu sana kuliko twahara ya mwili.
Na haiwezekani ikatimia twahara ya mwili iwapo kama mja atakuwa ni mshirikina.Allah anatueleza ndani ya 
Qur ani tukufu:
(Hakika washirikina ni najsi)Surat Attawba:28
b)Twahara hissy:Aina hii ya twahara tutaizungumzia baada ya mistari michache.
2:Maana ya twahara:
a)Kilugha:Twahara ni neno la kiarabu lenye maana ya usafi na kuepukana na uchafu.
b)Katika istilahi ya wanazuoni wa fiqihi:Ni kuondosha Hadathi na kuepukana na Khabathi.
Ufafanuzi:
Kuondosha Hadathi,ni kuondosha wasifu unaomzuia mja kuswali kwa kutumia maji kuoga mwili wote,iwapo kama hadathi hiyo ni kubwa,na iwapo kama hadathi yenyewe ni ndogo,basi kuiondosha kwake itakuwa ni kwa kutawadha,na uondoshaji wote huo wahitaji nia.
Na ikitokea mja kakosa maji au kashindwa kutumia maji kutokana na maradhi,basi mja huyo atatumia mchanga katika kutayammamu kama tutakavyokuja kufafanua hapo baadae.
Kwa hiyo Hadathi ni wasifu unaokuwepo katika mwili wa mja,wasifu huo wamzuia mja kuswali na ibada nyingine zinazohitaji twahara.
Na hadathi imegawanyika sehemu mbili:
{1}Hadathi ndogo:Nayo ni ile inayohusiana na viungo vya udhu.Mfano  ni kutokwa haja ndogo au kubwa au upepo (ushuzi).Kujitoharisha kwake kwa mtu atakayekuwa na hadathi ndogo ni kutawadha kama tutakavyokuja kufafanua hapo baadae.
{2}Hadathi kubwa: Hii ni hadathi inayohusiana na mwili mzima.Mfano  Janaba.Namna ya kujitoharisha na hadathi hii ni kuoga mwili mzima au kutayamamu kwa yule atakayekosa maji au atakayeshindwa kutumia maji.
Ama khabathi ni: Najisi mbali mbali nazo tutakuja kuzifafanua in shaa Allah.
Kwa hiyo kuondosha hadathi ni kuondosha wasifu unaomzuia mja kuswali au ibada mbali mbali zinazohitaji twahara.Uondoshaji huu unakuwa kwa kutumia maji au mchanga.Hadathi ikiwa ni ndogo mja atatawadha.Na ikiwa ni kubwa mja ataoga.
Ama kuondosha khabathi ni kuondosha najisi mwilini,katika nguo na sehemu ya ibada.

Somo la pili:Maji ya kujitwaharishia:
Ili kupata twahara kinahitajika kitu cha kujitwaharishia,kitu ambacho kitaondosha najisi na hadathi,kitu hicho ni Maji.
Maji ambayo kwayo yapatikana twahara ni Maji yaliyo twahara,na maji hayo ni maji ambayo ni Twahara katika dhati yake na yenye kutwaharisha kingine. Nayo ni maji yaliyo katika asili yake:Yaani katika asili yake ya kuumbwa.
Maji haya sawa yawe ni kutoka mawinguni:Kama vile Maji ya mvua na theluji.
Au kutoka ardhini,kama vile:
Maji ya mito,maji ya chemchem,visima,maziwa na bahari.
Kwa ibara nyingine,huelezwa ya kuwa maji ambayo yajuzu kujitwaharishia yapo saba:
1)Maji ya mbinguni 2)Maji ya baharini 3)Maji ya mto
4)Maji ya kisima 5)Maji ya chemchem 6)Maji ya theluji
7)Maji ya mvua ya mawe{Baada ya mawe hayo kuyeyuka}
Mwenyezi Mungu Mtukufu anatueleza:
(وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ)
(Na anakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili akutwaharisheni kwayo) Surat Al anfaal:11
Na anatueleza tena:
(وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً طَهُورًا)
(Na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi{twahara})
Surat Alfurqaani:48
Na kipenzi chetu mtume Muhamadi-rehema na amani za Allah zimshukie-anasema katika dua yake:
(Ewe Allah ninakuomba unisafishe na madhambi kwa maji na theluji na maji ya mvua ya mawe)Bukhari:744
Katika kutumia maji ya baridi{Maji ya mvua ya mawe}ndani yake kuna hekima na muujiza wa kisayansi.
Pia katika hadithi nyingine mtume-swala Allahu alayhi wasallam-anasema katika kujibu swali,pindi maswahaba walipomuuliza kuhusiana na utwahara wa maji ya baharini.Anasema:
(Ni twahara maji yake na halali maiti yake)Hadithi imepokelewa na Abu Daudi:83
Kutokana na hivyo mja hawezi kupata twahara kwa kutumia kimiminika chochote kama vile soda,juisi,mafuta na mfano wake. Kutokana na kauli yake Allah mtukufu:
(يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ فَاغْسِلُوا وُجُوهَكُمْ وَأَيْدِيَكُمْ إِلَى الْمَرَافِقِ وَامْسَحُوا بِرُءُوسِكُمْ وَأَرْجُلَكُمْ إِلَى الْكَعْبَيْنِ ۚ وَإِن كُنتُمْ جُنُبًا فَاطَّهَّرُوا ۚ وَإِن كُنتُم مَّرْضَىٰ أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ أَوْ جَاءَ أَحَدٌ مِّنكُم مِّنَ الْغَائِطِ أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ فَلَمْ تَجِدُوا مَاءً فَتَيَمَّمُوا صَعِيدًا طَيِّبًا فَامْسَحُوا بِوُجُوهِكُمْ وَأَيْدِيكُم مِّنْهُ ۚ مَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيَجْعَلَ عَلَيْكُم مِّنْ حَرَجٍ وَلَـٰكِن يُرِيدُ لِيُطَهِّرَكُمْ وَلِيُتِمَّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ)
(Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Swala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru)
Surat Al maaida:6
Laiti kama kungekuwa na kimiminika kingine tofauti na maji,ambacho mja akikitumia anapatwa twahara,basi Mwenyezi Mungu angetujulisha na wala asingetupeleka kwenye kutayamamu,lakini pindi alipotueleza ya kuwa tukikosa maji,basi tutayamamu,hali hii ikamaanisha ya kuwa twahara haipatikani isipokuwa kwa maji na mja akikosa au akishindwa kutumia twahara basi atatayamamu.

Somo la tatu:Maji yakichanganyika na najisi:
Maji yakichanganyika na najisi,kisha najisi hiyo ikabadili moja ya sifa tatu za maji,nazo ni:Harufu,ladha na rangi,basi maji hayo yanazingatiwa kuwa ni najisi kwa makubaliano ya wanazuoni wote,haifai kuyatumia maji hayo,kwani hayaondoi hadathi wala khabathi,sawa maji hayo yawe ni mengi au ni machache. 
Ama iwapo kama maji yatachanganyika na najisi,kisha najisi hiyo ikawa haijabadili moja ya sifa zake tatu,iwapo kama maji hayo yatakuwa ni mengi,basi hayato najisika,na yajuzu kujitwaharishia. Ama iwapo kama maji hayo yatakuwa ni machache,basi yananajisika,na wala haijuzu kujitwaharisha kwa maji hayo.
Kiwango cha wingi na uchache wa maji:
Tumeeleza ya kuwa maji yakiwa mengi kisha ikaingia au ikadondokea najisi ndani yake,na najisi hiyo ikawa haijabadili moja ya sifa tatu za maji,ambazo ni harufu,ladha na rangi,basi maji hayo yanakuwa ni twahara na yajuzu kujitwaharishia,ama najisi ikibadili moja ya sifa hizo tatu ndani ya maji,basi maji hayo yananajisika,na haifai kujitwaharishia.
Ama maji yakiwa ni machache,kisha ikaingia au kudondokea najisi ndani yake,basi moja kwa moja maji hayo yananajisika na wala haijuzu kujitwaharishia.
Je kiwango cha wingi wa maji na uchache wake ni kipi?
Wingi wa maji unaozungumziwa hapa,ni maji kufikia Kulateni,na maji machache ni kuwa kiwango cha chini ya kulateni. Na kulateni ni kiasi cha lita 160.5.
Na dalili juu ya hayo ni kuwa,mtume-swala Allahu alayhi wasallam-anatueleza katika hadithi iliyosimuliwa na Abi Saidi Al-khudry-radhi za Allah zimshukie-amesema,kasema mtume-rehema na amani za Allah zimshukie-:
(Hakika ya maji ni twahara,hayanajisiwi na chochote)Imepokelewa na imamu Ahmadi 10/3.
Yaani maji yakiwa mengi kuanzia kulateni,basi ni twahara na wala hayanajisiki,muda wa kuwa najisi hiyo haijabadili moja ya sifa tatu za maji.
Na katika hadithi iliyosimuliwa na Ibun Omara-radhiya Allahu anhumaa-hakika ya mtume-swala Allahu alayhi wasallam-amesema:
(Maji yakifikia kulateni,basi hayabebi najisi)
Hadithi imepokelewa na Tirmidhy ndani ya mlango wa twahara 67.
Ufahamu wa hadithi hii wajulisha ya kuwa maji yakiwa chini ya kiwango cha kulateni basi yanabeba najisi.

Somo la nne:Maji yakichanganyika na kitu kisafi{twahara}:
Maji yakichanganyika na mada yoyote ambayo ni twahara,kama vile:
majani ya miti,sabuni,karafuu,mdalasini,sidiri na mfano wake miongoni mwa mada ambazo ni twahara,kisha mada hiyo ikawa haijazidi au kukolezwa katika maji hayo,kuzidi ambako kunapelekea maji hayo mpaka yakabadilika rangi yake,basi usahihi ni kuwa maji hayo ni twahara yajuzu kujitwaharishia kwa kuondoa hadathi na najisi.Kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema:
(Na mkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu) Surat Al maaida:6
Katika aya hii tunaona ya kuwa Allah Mtukufu kataja maji
(na hamkupata MAJI) neno hili maji lajumuisha maji yote,hakuna tofauti baina ya yale yaliyochanganyika na mada ambayo ni twahara au yale ambayo hayajachanganyika na mada yoyote.
Pia miongoni mwa dalili zinazo thibitisha utwahara wa maji haya na kujuzu kwake kujitwaharishia ni kauli yake mtume-swala Allahu alayhi wasallam-kwa wanawake ambao walimuosha binti yake pindi alipo fariki:
(Muosheni mara tatu au tano au zaidi mkiona yahitajika,kwa maji na sidiri na mwishoni wekeni-katika maji hayo-kafura au kiasi cha kafura)Hadithi imepokelewa na Bukhari{1253} na Muslim{939}.

Somo la tano:Hukumu ya maji yanayotumika katika twahara{kujitwaharisha}:
Maji yaliyotumika katika twahara,kama vile maji ambayo yamesafisha viungo katika udhu,au yale yaliyotumika katika kuoga,maji haya ni twahara na yajuzu kujitwaharishia,yanaondoa hadathi na najisi katika rai iliyokuwa sahihi baina ya wanazuoni,muda wa kuwa maji hayo hayajabadilika moja ya sifa zake tatu:Harufu,ladha na rangi.
Dalili ya utwahara wa maji haya:
Ni kuwa mtume-rehema na amani za Allah zimshukie-(Alikuwa akitawadha,basi maswahaba wakikaribia kupigana kwa kuyawahi maji yanayotoka katika viungo vyake mtume) Bukhari:189. 
Walikuwa wakifanya hivyo kutokana na baraka ya maji haya yaliyopita katika viungo vya mtume.Laiti kama maji ambayo yametumika katika twahara yangekuwa si twahara,basi mtume angewakataza maswahaba,na maswahaba wasingefanya hivyo.
(Pia mtume-swala Allahu alayhi wasallam-alimmwagia Jabiri-Allah amridhie-maji aliyo yatawadha,pindi Jabiri alipokuwa mgonjwa)Bukhari:5651,Muslim 1616.
Laiti kama ingelikuwa ni najisi,basi mtume asingefanya hivyo.
Pia mtume-swala Allahu alayhi wasallam- na maswahaba zake na wake zao-radhi za Allah ziwashukie wote-walikuwa wakitawadhia katika vyombo ambavyo vilikuwa wazi,pia walikuwa wakioga katika vyombo vinavyofanana na mabeseni,na mfano wa vifaa hivi ni vigumu baadhi ya matone ya maji yanayotoka katika viungo kudondokea ndani yake.
Vile vile miongoni mwa dalili zinazothibitisha ya kuwa maji yaliyotumika katika kuosha viungo ni twahara,muda wa kuwa hayajabadilika moja ya sifa zake tatu,ni kauli yake mtume-rehema na amani za Allah zimshukie-alipomueleza Abu Hurayra-radhiya Allahu anhu-nae alikuwa ni mwenye janaba:
(Hakika ya muumini hanajisiki)Muslim:371.
Kwa hiyo maji yakipita katika viungo vyake,yanabaki katika hali ya utwahara.
Kutokana na ushahidi huo maji hayanajisiki na kukosa utwahara wake kwa kutumika katika twahara muda wa kuwa hayajabadilika moja ya sifa zake tatu.

Somo la sita:Maji yaliyobaki baada ya kunywewa au binadamu na wanyama wanaoliwa na wale wasioliwa:
Maji yaliyobaki baada ya kunywewa na binadamu au mnyama anayeliwa nyama yake katika lugha ya kiarabu huitwa السّؤر Assu-uri.Binadamu ni twahara na maji yake anayoyaacha baada ya kunywa ni twahara pia,sawa awe ni muislamu au kafiri,pia mwenye janaba,hedhi na nifasi.
Katika hadithi iliyosimuliwa na mama wa waumini bi Aisha-radhi za Allah zimshukie- hakika yake alikuwa akinywa maji katika chombo hali ya kuwa yupo katika siku zake,basi mtume-swala Allahu alayhi wasallam- anachukua chombo kile na kuweka mdomo wake sehemu aliyokuwa kaweka bi Aisha mdomo wake na kunywa. Hadithi imepokelewa na Muslim.
Pia wanazuoni wamekubalia juu ya utwahara wa maji yanayobaki baada ya kunywewa na mnyama anayeliwa nyama yake .
Ama wale wanyama wasioliwa nyama zao-ambao si najisi- basi rai yenye nguvu zaidi ni kuwa maji wanayoyabakisha baada ya kunywa ni twahara pia,khususani maji hayo yakiwa mengi.
Na dalili juu ya utwahara wa maji haya ni
kauli yake Allah Mtukufu:
(وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ)
(Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini)Surat Al hajj:78
Bila shaka laiti kama ingelikuwa maji yakinywewa na wanyama mbali mbali yananajisika na kuwa si twahara,basi kungekuwa na uzito kwa watu,kwani kuna baadhi ya maeneo hakuna maji isipokuwa ya mito au visima na wanyama mbali mbali wanashiriki katika kuyanywa maji hayo.
Vile vile kipenzi chetu mtume Muhamadi-rehema na amani za Allah zimfikie-aliulizwa kuhusiana na maji ambayo yamekuwa yakinywewa pia na wanyama mbali mbali wakufungwa na wasiofungwa,akajibu:
(Pindi maji yakifikia kulateni,basi hayabebi najisi)
Hadithi imepokelewa na Tirmidhy ndani ya mlango wa twahara 67.
Pia mtume-swala Allahu alayhi wasallam-alieleza kuhusiana napaka aliyekunywa katika chombo:
(Hakika yake{paka} si najisi, bali ni miongoni mwa wanaowazunguka na kuwa nanyi)Hadithi imepokelewa na imamu Ahmad 5/296
Na laiti kama paka angekuwa ni najisi pia kungekuwa na ugumu mkubwa wa kuiepuka najisi yake kutokana na kuwa nasi na kutuzunguka katika majumba yetu.
Ama maji yaliyoachwa na Mbwa na Nguruwe ni najisi.
Ufafanuzi:
Mbwa:Katika hadithi iliyosimuliwa na Abuhurayra-radhiya Allahu anhu-hakika ya mtume-rehema na amni za Allah zimshukie-amesema:
(Utwaharishaji wa chombo cha mmoja wenu pindi mbwa atakapokunywa katika chombo hicho,ni kuoshwa mara saba,mara moja kati ya hizo ni kwa mchanga)Hadithi imepokelewa na imamu Bukhari:172,imamu Muslim:279.
Ama nguruwe ni kutokana na unajisi wake na uchafu wake. Allah ametueleza ndani ya Qur ani:
(…فَإِنَّهُ رِجْسٌ…)
(…kwani hiyo{nyama ya nguruwe} ni uchafu…)
Surat Al an-aam:145


In shaa Allah mpaka hapa tumekwisha fika mwisho wa mlango wa kwanza katika maswala ya twahara.
Katika somo letu linalokukuja in shaa Allah tutaingia katika mlango wa pili katika twahara nao ni mlango wa Vyombo.

0 Comments