FIQHI : MLANGO WA KUTAYAMMAM

Nini Kutayammam?


Kutayammam kilugha ni kukusudia, inasemwa: "Anakukusudia fulani kwa kheri". Na amesema mshairi:    "Nilikujieni nilipokosa wenye busara na asiepata maji huukusudia mchanga ".

Na kisharia ni kufikisha mchanga ulio 'taahir kwenye uso na mikono miwili (pamoja na viganja vyake) kwa nia na shuruti zake. Asili ya kujuzu kutayammam kunatokana na Qur'ani Tukufu na Sunna za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na kwa hivyo wakakubaliana wanazuoni. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

 "…….. .na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi, mpake nyuso zenu na mikono yenu. ……….”. (Annissaai : 43).

Yaani mkiwa wagonjwa, au mmo safarini na msipate maji; basi tayammamuni kwa mchanga ulio ‘taahir.

Amesema Ibnu 'Abbas r.a., na akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

    "Imejaaliwa kwangu ardhi ni mskiti (pahala pa kusujudu) na mchanga wake ni wenye ku'tahirisha". (Imehadithiwa na Muslim).

Mambo Yenye Kujuzisha Kutayammam


Yenye kujuzisha kutayammam ni kushindwa kutumia maji kwa hisia au kwa sharia. Na kushindwa kutumia maji huwa katika hali nne, nazo ni:

1. Katika Hali ya Kuwa Safarini


Msafiri ana hali nne:

Kwanza, awe na hakika hakuna maji karibu na alipo; katika hali hii haitahitajia kutafuta maji, kwani hivyo kutafuta kwake hakutaleta natija.

Pili, kumkinika kuwepo maji karibu na alipo; katika hali hii itamlazim ayatafute, kwani kutayammam ni 'tahara ya dharura, na hapana dharura pamoja na kumkinika kuwepo (chenye kuondoa hio dharura) nacho ni kupatikana maji.

Tatu, kahakikisha kuwepo maji karibu na alipo. Ikiwa maji yapo kwenye masafa ya kadiri ya wanapofika wachungaji na wenye kutafuta kuni, itamlazim ayatafute maji wala haitajuzu kwake kutayammam. Ama ikiwa maji yako masafa ya mbali na ikiwa atayafuatia wakati wa Sala utampita, katika hali hio atatayammam kwa kuwa ni mwenye kukosa maji wakati ule, na lau kama ingaliwajibika kungoja apate maji hata ukitoka wakati wa Sala, isingaliekwa kutayammam.

Nne, maji yapo; lakini zahma za wasafiri inazuilia kufika yalipo hayo maji. Katika hali hii qauli ya wanazuoni wengi ni kwamba inamjuzia kutayammam kwa kushindwa kuyafikia maji; wala haitamlazim kuzilipa Sala atazozisali katika hali hii.

2. Katika Hali ya Ugonjwa


Hali ya ugonjwa imo katika hali tatu:

Ya Kwanza, akikhofia kuwa akitia udhu kwa kutumia maji, huenda akapoteza maisha yake, au akapoteza kiungo chake cha mwili, au ikasababisha kiungo chake kisifanyekazi kama inavyofaa; katika hali hii atatayammam.

Ya Pili, akikhofia akitia udhu kwa kutumia maji, maradhi yatamzidi, au kuzidi maumivu, au akakhofu kupata athari mbaya, kama vile kufanya baka usoni au sehemu yoyote ya mwili yenye kudhihiri; katika hali hii atatayammam kwa qauli ya wanazuoni wengi.

Ya Tatu, akikhofia athari ndogo kama vile alama ya tetekuwanga, au baka dogo, au akakhofia kupata athari mbaya lakini si kwenye sehemu ya mwili yenye kudhihiri, katika hali hii haitamjuzia kutayammam.

Ni juu ya mgonjwa mwenyewe kutumia ujuzi wake kukhusu hali ya

maradhi yake, ikiwa ano ujuzi au uzoevu wa hivyo; au ategemee maarifa na shauri ya daktari Muislam mwenye ujuzi wa hali ya maradhi yake na mwenye kuaminika uadilifu wake. Hivi kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu amewajibisha udhu, kwa hivyo haiwi kuuwacha isipokuwa kwa qauli ya mwenye kukubalika qauli yake; Mwenyezi Mungu Mtukufu hakubali qauli ya kafiri na mtu muovu (faasiq). Inakubaliwa hata kama ni qauli ya mtu mmoja, au qauli ya mwanamke.

Shuruti za Kusihi Tayammam


Kusihi kutayamma kuna shuruti, nazo ni:

Ya Kwanza, kuingia wakati wa Sala anayotaka kuisali, hivi ni kwa qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya ya sita ya Surat-l-Maida:

   

"Enyi mlio amini! Mnapo simama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, .......". (Al Maida : 6 ).

Na kuendelea mpaka kwenye Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:   "......... basi tayamamuni vumbi lilio safi,…………". (Al Maida : 6).

Kusimama kwa ajili ya Sala hakuwi isipokuwa kwa kuingia wakati wa hio Sala. Ama kutia udhu kunasihi hata kabla ya kuingia wakati wa Sala, hivi ni kama alivyofanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. Ama kutayammam, kama ilivyo kwenye hii Aya, na kwa qauli ya Mtume wetu mpenzi s.a.w. ni baada ya kuingia wakati wa hio Sala:

 "Imejaaliwa kwangu ardhi ni mskiti (pahala pa kusujudu) na mchanga wake ni wenye ku'tahirisha, popote inaponifikia Sala natayammam na nikasali". (Imehadithiwa na Muslim).

Qauli yake hii Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:  "inaponifikia Sala (wakati wa Sala) natayammam", ni dalili ya kwamba usipomfikia wakati wa Sala hatatayammam. Hivi ni kwa vile kuwa tayammamu ni 'tahara ya dharura, na haiwi kujuzu la dharura mpaka iwepo dharura; katika hukmu hii ni kuingia wakati wa Sala.

Ya Pili, kutafuta maji; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "…… na msipate maji…". (Annissaai : 43).

Mwenyezi Mungu Mtukufu ametuamrisha kutayammam wakati wa kukosekana maji, na haiwezikani kujuulikana huko kukosekana mpaka baada ya kutafutwa. Kwahivyo basi, mwenye kutaka kutayammam ni juu yake yeye mwenyewe kutafuta maji, hutosheleza kumwambia mtu mwenye kuaminika kuwa amtafutie maji. Katika kutafuta maji, atapekua kwenye mizigo yake ya safari; huenda ikawa yamo humo maji nae hajui au amesahau. Asipopata maji kwenye hio mizigo yake atatizama kila upande, khasa sehemu zenye miti na kijani-jani, na sehemu wanazo onekana ndege wakiruka-ruka; kwani humo huyumkinika kuwemo maji.

Ikiwa atakhofia nafsi yake au mali yake kwa kwenda huku na huku kutafuta maji, haitamlazim kufanya hivyo; na atatayammam.

Imejuzishwa kutayammam katika hali ya khofu kama hivi, juu ya hakika ya kuwepo maji; kwahivyo basi, katika hali ya tuhuma tu juu ya uwezekano wa kuwepo maji, ndio zaidi imejuzishwa kutayammam. Ikiwa hapana khofu ya nafsi yake au mali yake, itamuwajibikia kuyatafuta maji.

Ikiwa yuko kwenye msafara na wenziwe atawauliza kama wanayo maji. Ikilazim itamuwajibikia anunue maji ya kutilia udhu au/na ya kukogea kuondoa hadath kubwa, hatawajibika kununua maji ikiwa atachelea kupungukiwa na matumizi ya safarini; kwenda na kurejea. Vilevile haitamuwajibikia kununua maji ikiwa atauziwa kwa bei ya zaidi ya dasturi.

Ya Tatu, anasameheka kutumia maji na kujuzu kutayammam ikiwa atachelea kudhurika kwa kutumia maji; au atachelea wenziwe katika msafara wao wataondoka na kusababika kutaabika. Vilevile anasameheka kutumia maji na kujuzu kutayammam ikiwa maji alionayo yatahitajika kwa kunywa, yeye mwenyewe, au wenziwe kwenye msafara wao; au wanyama wao au wanyama wengine wasio dhuru; kwa wakati wa karibuni au baadae katika safari yao. Lau akifa mmoja miongoni mwao katika safari, nae anayo maji, basi itajuzu kwao kuyanywa hayo maji na yeye watamtayamamisha; thamani ya maji yake itatiwa kwenye mirathi yake. Ikiwa miongoni mwao anayo maji na hayahitajii, na wenziwe wameshikwa na kiu na yeye akakataa kuwapa wenziwe maji hayo kwa kunywa; basi inawajuzia wao kuyachukuwa hayo maji kwa nguvu ili wanywe na kumlipa thamani ya maji yake. Ama ikiwa yeye mwenyewe anayahitajia hayo maji, basi haitawajuzia wao kuyachukuwa maji hayo kwa nguvu; hivi ni kwa vile kuwa yeye mwenyewe ni mwenye kustahiki zaidi kwa hayo maji kuliko wengine.

Ya Nne, kutayammam iwe kwa mchanga ulio 'taahir na wenye vumbi lenye kuganda kwenye viungo vya tayammam, yaani uso na mikono mpaka vifundo vyake; hivi ni kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "........ basi tayamamuni vumbi lilio safi,…………". (Al Maida : 6).

Qauli hii inafahamisha kuwa mchanga wa kutayamamia ni wenye vumbi. Na Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amebainisha zaidi kwa qauli yake:  "…. Mchanga unakutosheleza….".

Vilevile ni kwa qauli yake Mtume wetu Mpenzi s.a.w. aliposema:

 "Imejaaliwa kwangu ardhi ni mskiti (pahala pa kusujudu) na mchanga wake ni wenye ku'tahirisha, popote inaponifikia Sala natayammam na nikasali". (Imehadithiwa na Muslim).

Imeshurutishwa mchanga uwe 'taahir kwa Qauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ﭽ  "… vumbi lilio safi,……".

Safi hapa imekusudiwa 'taahir, kwa sababu haijuzu kutilia udhu maji yasiokuwa 'taahir; na kwa vile hii tayammam ni badala ya udhu; kwa hivyo haijuzu isipokuwa kwa kutumia kitu 'taahir, nacho ni mchanga ulio 'taahir.

Fardhi za Kutayammam


Fardhi za kutayammam ni nne, nazo ni:

Ya Kwanza, nia; hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:   "Hakika ya kitendo (ibada) chochote ni kulingana na nia".

Na namna ya kutia nia ni kunuwia kuwa anatayammam   ili imsihie kusali kwa hio tayammam. Wala haimtoshelezi yeye kutia nia ya kuondoa hadath; kwani tayammam haiondoi hadath, lazima nia yake abainishe kumsihia kusali kwa hio tayammam. Hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa 'Amir bin l'Aas r.a.: "Umewasalisha wenzako nawe una janaba?"

Lau kama kutayammam kunaondoa hadath basi Mtume wetu Mpenzi s.a.w. asingalisema:  "nawe una janaba". Ilivyo tayammam ni kujuzisha kusali kwa hio tayammam, wala si kuondoa hadath kwa huko kutayammam. Hivi kunuwia   yaani kusihi kusali kwa tayammam kuna hali nne:

Hali ya Kwanza, anuwie yaani "kumsihia kusali Sala ya fardhi na ya sunna pamoja" kwa hii tayammam yake moja. Kwa nia hii itamsihia kusali Sala ya fardhi na ya sunna ya qabla na sunna ya baada, ndani ya wakati wa hio Sala ya fardhi au nje ya wakati wa hio Sala anayotaka kuisali.

Hali ya Pili, anuwie yaani "kumsihia kusali Sala ya fardhi", kwa nia hii itamsihia kusali Sala ya fardhi na sunna ya qabla na ya baada.

Hali ya Tatu, anuwie basi kusalia Sala ya sunna; katika hali hii haitamsihia kusalia Sala ya fardhi.

Hali ya Nne, anuwie basi kusali; katika hali hii huwa ni kama alienuwia kusalia Sala ya sunna.

Fardhi ya Pili Na Tatu, kupangusa uso na mikono miwili mpaka vifundoni, hivi ni kutokana na Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:

   "…… na mpake nyuso zenu na mikono yenu …". (Al Maida : 6).

Kwa vile kutayammam ni badala ya kutia udhu (kwa kutumia maji), basi hupewa hukmu ya kutia udhu kukhusu viungo vyenye kutiliwa udhu.

Katika kutia udhu ni kuosha mikono miwili mpaka kwenye vifundo vyake, kwa hivyo na katika kutayammam inakuwa ni hivyo hivyo, yaani utapaka mchanga mikono miwili mpaka kwenye vifundo vyake. Na hivi ndivyo alivyofanya Mtume wetu Mpenzi s.a.w., kama ilivyoelezwa na Ibnu 'Umar r.a. kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema: "Kutayammam ni mapigo mawili, pigo moja ni kwa (kupangusia) uso, na pigo la pili ni kwa (kupangusia) mikono miwili mpaka vifundo vyake". (Imehadithiwa na Al Haakim).

Imetiliwa nguvu hivi na kuchukuliwa kwa kiasi cha kutia udhu kwa vile kuwa kutayammam ni badala ya kutia udhu.

Ama kukhusu qauli ya kwamba kutayammam inatosha kwa pigo moja, yaani kupangusia uso na mikono mpaka vifundo vyake kwa hili pigo moja, hivi ni kutokana na Hadithi ya 'Ammar ya kwamba aliambiwa na Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

"Hakika inakutosheleza kama hivi, akapiga s.a.w. kwa mikono yake ardhi, akapuliza kwenye viganja vyake, kisha akapangusia uso wake na mikono yake". (Imehadithiwa na Al Sheikhan).

Amesema Imam Shafi'ii r.a., ikiwa Hadithi hii ni sahihi, basi ifuateni, na juweni kuwa hayo ndio madhehebu yangu (ndivyo ninavyo fanya), na Hadithi hii ni sahihi.

Amesema Imam Al Nawawi r.a. kwamba hivi ndivyo inavyo nguvu zaidi na karibu mno na sunna.

Ya Nne, kupangiliza; hivyo inapasa kutanguliza uso kisha mikono miwili mpaka vifundo vyake, hivi ni kwa vile tayammam ni kutia 'tahara kwa njia ya viungo viwili, yaani uso na mikono miwili mpaka vifundo vyake; kama ilivyo kwenye kutia udhu kwa kutumia maji. Kwa kutayammam lazima uvue pete (ikiwa unavaa pete) kwani mchanga haupiti chini ya pete, tafauti na maji. (Ukitia udhu kwa maji si lazima kuvua pete ikiwa maji yatapita chini ya pate - tizama kwenye hukumu za kutia udhu).

Sunna za Kutayammam


Miongoni mwa sunna hizo ni kusoma Bismillah , na kutanguliza kulia kabla ya kushoto, kupangiliza na kufululiza wakati wa kupangusa; hivi kama ilivyokuja kwa kuchukulia hukmu ya kutia udhu kwa maji. Miongoni mwa sunna pia ni kuanzia kupangusa sehemu ya juu ya uso, kupunguza vumbi/mchanga wa kutayammamia uliomo viganjani, na kuchanua vidole wakati wa pigo la mwanzo, na kupitisha baina ya vidole baada ya kupangusa mikono mpaka vifundo vyake.

Miongoni mwa sunna pia ni kutoinua mkono kutoka kwenye kiungo kinacho panguswa, hivi ili kuepuka khitilaf za qauli za wanazuoni kuwa ni waajibu kutoinua mkono mpaka kumaliza kupangusa kiungo.

Yenye Kuba'tilisha Tayammam


Tayammam huba'tilika kwa mambo matatu:

La Kwanza, kwa yale yenye kuba'tilisha udhu.

La Pili, kwa kuyaona (kuweza kuyapata na kufaa kuyatumia) maji kabla ya kuingia wakati wa Sala. Lau atatayammam, kisha akayapata maji kabla ya kuingia wakati wa Sala; itaba'tilika tayammam yake. Hivi ni kutokana na qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:

  "Mchanga safi ni cha kuji'tahirishia Muislam hata kama hatapata maji kwa muda wa miaka kumi; akipata maji ataosha (pangusa) mwili wake". (Imehadithiwa na Ahmad na Al Tirmidhy).

Ikiwa kayaona maji, lakini baina yake na hayo maji kipo kitu chenye kuzuilia yeye kuyapata na kuyatumia hayo maji; kama vile kuwa anayahitajia hayo maji kwa kiu aliyonayo, au ikawa kuna mnyama mwitu au kuna adui na kukhofia nafsi yake, ahli yake au mali yake au mfano wa hayo ambayo yatamzuilia kuyafikia na kuyatumia hayo maji; katika hali hizi tayammam yake haitaba'tilika, kwa sababu hali hazikua zenye kuba'tilisha kusihi tayammam, kwa hivyo ni ndivyo zaidi kutoba'tilisha tayammam yenyewe. Ama akiyaona maji naye yumo katika Sala, basi haitaba'tilika tayammam yake wala Sala yake.

La Tatu, kurtadi (Mwenyezi Mungu atunusuru), yaani kutoka katika Uislam. Kurtadi kunavunja ibada zote na kupoteza thawabu zote, na tayammam ni ibada; kwa hivyo huba'tilika kwa kurtadi.

Kupangusa Juu ya Jips (POP), Kitata na Bendeji


Ikiwa kimoja kati ya hivi, yaani jips (pop), kitata au bendeji kiko juu ya kiungo cha udhu, ikiwa ataweza kukifungua wakati wa kutia udhu, bila ya madhara yoyote juu yake atakifungua; atatia udhu kama dasturi. Akifika kwenye kiungo cha udhu chenye ugonjwa atakikosha, kama hatoweza kukikosha kwa sababu ya ugonjwa wa kiungo hicho basi atatayammam kwa sababu kiungo cha udhu hakuweza kukikosha kwa kuwa kina ugonjwa.

Ikiwa akikifungua kile kiungo kitadhurika, basi hatokifungua; atatia udhu kama dasturi kwa kukosha viungo vyote vya udhu vilivyo vizima pamoja na sehemu ambayo inaweza kukosheka ya kiungo chenye ugonjwa kisha atapaka maji juu ya jips/kitata/bendeji; na atatayammam, kwa sababu kiungo cha udhu haikuwezekana kukoshwa kwa sababu ya ugonjwa ulioko juu ya kiungo hicho. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Jabir r.a. kwamba mtu lilimpata jiwe likampasua kichwa, kisha akaota akatokwa na manii (akawa ana janaba); akawauliza wenziwe (Masahaba wenziwe) kama watampatia ruhusa ya kutayammam, (yaani kama kuna Hadithi inayoruhusu kutayammam katika hali kama iliyomfika yeye). Wakamwambia kuwa hawampatii ruhusa ya kutayammam madhali anaweza kukoga, akakoga; akafa. Walipofika kwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. wakamueleza yote yaliotokea, Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akasema:

"Wamemuuwa, (yaani wamekuwa sababu ya kufa); Mwenyezi Mungu awauwe. Kwani wasingaliuliza ikiwa kitu hawakijui, hakika dawa ya usilolijua ni kuuliza. Hakika ilikuwa inamtosheleza atayammam, na afunge kitamba - bandeji - juu ya jaraha au anyunyizie maji juu ya jaraha kisha apanguse juu yake na aoshe sehemu ya mwili iliobaki ambayo haina jaraha". (Imehadithiwa na Abu Daud na Ibnu Maajah na Darqu'tny).

Ikiwa mtu kafunga kitata akafikwa na janaba, basi anaweza kutanguliza kukoga kisha akapangusa juu ya kitata kisha akatayammam, au akapangusa juu ya kitata, akatayammam kisha akakoga; hali zote mbili zinajuzu. Ama kukhusu kutia udhu, hawezi kuchupa kiungo cha udhu na kwenda kingine, lazima afuatilize; akifika kwenye kiungo chenye ugonjwa atapangusa kama ilivyoelezwa hapo juu na kutayammam kisha ataendelea na kiungo cha udhu chenye kufuatilia. Hivi ni kwa sababu miongoni mwa shuruti za kutia udhu ni kufuatiliza na kufululiza. Ama ikiwa viungo vyote vinne vya udhu, yaani (1) uso, (2) mikono miwili na vifundo vyake, (3) kichwa na (4) miguu miwili na vifundo vyake. Ikiwa vyote vina ugonjwa na vimefungwa kitata, basi tayammuma moja itatosheleza kwa viungo vyote hivyo. Yote tulioleza hapo juu kukhusu kufunga jips/kitaka/bendeji, ni lazima hio jips/kitata/bendeji iwe imeekwa juu ya kiungo cha udhu hali ya kuwa ni 'taahir, yaani anao udhu kaamili.

Ikiwa imewekwa juu ya kiungo cha udhu nae hana udhu itabidi kuzilipa Sala zote baada ya kupowa*.

*Ina suniwa mtu awe ana udhu kila wakati, ikiwa mtu atakuwa na dasturi ya kuwa na udhu kila wakati, basi - Mwenyezi Mungu Mtukufu atunusuru - akipatwa na ajali yoyote ikabidi atiwe jips/kitata/bendeji itakuwa anatiwa nae ana udhu, hivyo hatolazimika kuzilipa Sala atazozisali katika hali hii atakuwa ameondoka duniani na deni la Sala; Mwenyezi Mungu Mtukufu atunusuru na hili.

Hayo tulioyaeleza yana khusu ikiwa mtu atahitaji kufunga jips/kitata/bendeji, ikiwa hatohitaji kufunga jips/kitata/bendeji; lakini anakhofia kuingia maji kijaraha chake, basi atakosha sehemu isio na ugonjwa kama anavyoweza, itamlazim kutayammam; wala haitamlazim kukosha sehemu nyenye ugonjwa.

Kuwajibika Kutayammamu kwa Kila Sala


Tumetangulia kueleza kukhusu muhimu wa nia, sasa Inshaallah tutaleta dalili na hoja juu ya hayo tulioyaeleza. Tumeeleza ya kwamba tayammamu moja inafaa kusalia Sala moja tu ya fardhi, ama Sala za sunna unaweza kusalia sunna unazotaka. Kusali Sala moja ya fardhi kwa tayammamu moja hoja kuu iliojengeka kwa hili ni qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Aya ya sita ya Suratu-l-maida ambayo imeshatangulia kutajwa. Kuwajibika kutia udhu au kutayammam kwa kila Sala kulikuwa ni lazima katika zama za awali ya Uislam, kisha ikatoka haja ya kutia udhu kwa kila Sala kwa kitendo cha Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kuwa "Siku ya Ufunguzi" Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alisali Sala tano kwa udhu mmoja. (Imehadithiwa na Ibnu 'Umar). Ikabakia kuwa kutayammam ni kwa kila Sala moja ya fardhi. Na amehadithia Al Baihaqy r.a. kutokana na Ibni 'Umar r.a. kuwa kasema: "Anatayammam kwa kila Sala hata ikiwa hakutengukwa na udhu". Ama Sala za sunna anaweza kusali idadi ya sunna anazozitaka.

Ikiwa mwenye janaba au hadathi ndogo - asiekuwa na udhu - hakupata maji ya kutosha kwa kukogea au kutilia udhu, itamlazim atumie hayo  maji alionayo na atayammam kwa palipobakia. Ikiwa atakuwa amepatwa na najsi akapata maji ya kukoshea hio najsi, lakini hayatoshi kukosha najsi yote; atakoshea itakavyokosheka. Ikiwa kapatwa na janaba au ikawa hana udhu na akapatwa na najsi na akawa na maji yasiotosha kuondolea najsi na kukogea/kutilia udhu, basi atatumi maji hayo kwa kuondolea najsi na atatayammam, hivi ni kwa sababu hakuna badili ya cha kuondolea najisi, lakini ipo badili ya udhu na kukoga nayo ni kutayammam. Ikiwa mtu atakosa maji, na akakosa mchanga wa kutayammamia; basi atasali hivyo hivyo kwa heshima ya wakati wa Sala, kisha atalipa hio/hizo Sala zake alizozisali katika hali hii.

Yafuatayo ni yalivyoelezwa kwenye kitabu: "Fiqhi Sunna" (Mwenye kukosa maji, na akakosa mchanga wa kutayammamia, atasali hivyo hivyo na haitamlazim kulipa Sala hio/hizo. Hivi ni kutokana na Hadithi hii: "Amehadithia Muslim r.a. kutokana na Sayyidah 'Aisha r.a. kuwa yeye (Sayyidah 'Aisha) aliazima kidani cha Asma, kikapotea. Mtume wetu Mpenzi s.a.w. akawapeleka baadhi ya Masahaba zake s.a.w. kukitafuta, ikawakuta Sala, wakasali bila ya udhu. Waliporejea kwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. wakamshtakia hali hio iliowakuta, ikateremka Aya juu ya kutayammam, akasema Asyad bin Hadhiir, Mwenyezi Mungu Mtukufu akujazi kheri, "Fawallahi" halikushuka juu yako jambo hata mara moja isipokuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hukujaalia njia, na akajaalia kwa Waislam barka; hawa Masahaba wamesali wakati walipokosa kile walichojaaliwa kuwa cha kuji'tahirishia na wakashtaki hali hio kwa Mtume s.a.w. na Mtume wetu Mpenzi s.a.w. hakuwakanya kwa kitendo chao hicho, wala hakuwaamrisha kulipa Sala. Amesema Imam Al Nawawy r.a.: "Na hii ni qauli yenye nguvu zaidi na kutolewa dalili".
Mwisho wa maelezo ya "Fiqhi Sunna.

0 Comments