Nini 'Tahara?
Kilugha ni unadhifu, kama
kusema nimei'tahirisha nguo, yaani nimeinadhifisha. Kisharia, ni hali ya
kuondosha hadath kubwa (janaba, hedhi au nifasi), na ni hali ya kuondosha
hadath ndogo (kutokua na udhu), na ni hali ya kuondosha najsi (uchafu), kama
vile, mkojo, kinyesi, damu, usaha - mwilini, nguoni au pahala.
Vitu vyenye Ku'tahirisha
Vyenye ku'tahirisha ni vitu
vinne, maji, mchanga, “kudibaghi”* na kuchachuka. Maji hutumika kwa kuondoshea
hadath kubwa na/au ndogo na kuondoshea najsi (uchafu). Mchanga hutumika kwa
kutayamam na kwa kuondoshea najsi ya mbwa na nguruwe. Kudibaghi ni kwa
kuondoshea unajsi wa ngozi ya nyamafu. Kuchachuka huwa kwa tembo kugeuka
(wenyewe) ikawa siki.
Maji yanayojuzu Ku'tahirishia
Maji yenye kufaa ku'tahirishia
ni namna saba:
Ya Kwanza, maji ya
mvua; kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Ya Pili, maji ya
bahari; kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alipoulizwa kukhusu maji ya
bahari - akasema s.a.w.:
“Hayo
ni yenye ku'tahirisha maji yake, halali maiti yake”.
(Imehadithiwa na Al Sheikhan,
Al Tirmidhy na Ibnu Hibbaan).
Ya Tatu, maji ya
kisima, kwa Hadithi ya Suhail; kuwa baadhi ya Masahaba r.a. walisema: “Ewe
Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika yako unatia udhu kutoka kisima cha Bidha’a na
humo wanajisafisha wenye uchafu na wenye hedhi, na wenye janaba"? Akasema
Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
Ya Nne, Tano, Sita
na ya Saba; maji ya mto, , maji ya falaj; na hivyo inamaanisha pia maji
ya barafu na maji baridi. Haya ni kutokana na Hadithi ya Abu Hureira r.a.
aliposema kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w alikuwa akisha kabbiri, takbiir ya
kuingia kwenye Sala, husita kidogo kabla ya kusoma Alhamdu (Surat Al Fat-ha).
Akasema - Abu Hureira - kumuuliza s.a.w. - “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu
Mtukufu unasema nini"? Akasema Abu Huraira, akasema Mtume wetu Mpenzi
s.a.w:
"Nnasema: Mwenyezi Mungu
niweke mbali baina yangu na baina ya makosa yangu kama ulivyoweka mbali baina
ya urejua na uchejua, Mwenyezi Mungu nitakase kutokana na makosa yangu kama
inavyotakaswa nguo nyeupe kutokana na uchafu, Mwenyezi Mungu nikoshe kutokana
na makosa yangu kwa maji na barafu na maji baridi”. (Imehadithiwa na Al
Sheikhan).
Namna za Maji
Maji yanagawika namna tano:
Ya Kwanza, maji yenye
kujuulikana kuwa ni maji, hayakuongezewa kitu ndani yake; haya ni miongoni mwa
aina saba za maji yenye ku'tahirisha tuliozitaja hapo juu. Haya ni 'taahir kwa
nafsi yake na ni yenye ku'tahirisha, yanafaa kutumika kwa kuondoa hadath kubwa
na/au ndogo na kuondoa najsi, si karaha kuyatumia.
Ya Pili, maji
yaliopigwa sana na jua, haya vilevile ni miongoni mwa maji tulioyataja hapo
juu; lakini huwa yamepigwa sana na jua. Haya vilevile ni 'taahir kwa nafsi yake
na ni yenye ku'tahiarisha, yanafaa kutumika kwa kuondoa hadath kubwa na/au
ndogo na kuondoa najsi, ni karaha kuyatumia kwa vile kupigwa sana na jua.
Imekuja hivi kuwa karaha kutumia maji yaliopigwa sana na jua kutokana na
Hadithi ya Imam Shafi’ii r.a. kwamba amesema Sayyidna Omar r.a. kuwa maji
yanayopigwa sana na jua yanasababisha ukoma. Imeshuritishwa hivi kuwa karaha
kuyatumia maji yaliopigwa sana na jua kwa sharti mbili:
Sharti ya Kwanza, Iwe
Yamo Katika Chombo Chenye Kuhunzika; Kama Vile chombo cha shaba, au cha chuma
au cha risasi; kwa sababu maji katika vyombo hivi yakipigwa sana na jua hutoa
madda yenye kusababisha maradhi ya ukoma.
Sharti ya Pili, iwe
hali hii kwenye nchi za joto sana; yaani jua lake ni kali sana..
Ya Tatu, maji yaliotumiwa kwa kuondoshea hadathi kubwa au hadath ndogo au
kuondoshea najsi, ikiwa hayakubadilika rangi, ladha au harufu; wala hayakuzidi
kiwango chake cha asli. Hivi ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi
s.a.w.:
“Mwenyezi Mungu Mtukufu
ameyaumba maji hali ya kuwa ni 'taahir na yenye ku'tahirisha, hayanajisiki
isipokuwa kwa kubadilika ladha yake au harufu yake" Na kwa Hadithi
iliopokewa na Ibn Maajah: "Au rangi yake".
Kukhusu kufaa ku'tahirishia
maji yaliotumika kuna tafauti ya rai za madhehebu, kwa kuwa juu ya kwamba
Masahaba r.a. walikuwa ni mno kushikamana na dini; lakini hawakuwa
wakiyakusanya maji yaliotumika na kutawadhia; na lau kama ingalifaa hivyo,
wangalifanya. Na wamesema baadhi ya wanazuoni ya kwamba hakika maji hayatoki
kuwa ni yenye kufaa ku'tahirishia basi kwa vile kutumika kwa ku'tahirisha, ila
ikiwa yatabadilika harufu yake, au rangi yake au ladha yake. Wakasema kuwa
Masahaba r.a. walikuwa hukaribia kugombania kutaka wapate maji yanayochururika
kutoka viungoni mwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. wakati anapo tia udhu ili wapate
barka zake s.a.w., na kutabaaruk ni kwa kutilia udhu baadhi ya viungo vya udhu
au kwa njia nyengine. Kufaa ku'tahirishia maji yaliotumika kunatiliwa hoja kuwa
asili ya maji ni 'taahir na ni yenye ku'tahirisha.
Ya Nne, maji
yaliobadilika kwa kuchanganyika au kuchanganywa na kitu 'taahir; hivi ikiwa
huku kubadilika haya maji kwa huu mchanganyiko kutaondoa jina asili la maji na
ikiwa huku kuchanganyika ni kwenye kuepukika, kama vile sharubati au marashi;
basi maji haya hubakia kuwa ni 'taahir, lakini hayafai ku'tahirishia. Ama ikiwa
kule kubadilika ni kwa sababu ya mchanganyiko ambao yale maji hayangaliweza
kuepukana nako, kama vile kwa sababu ya udongo, au mwani au jasi, au vitu kama
hivyo ambavyo vimo kwenye machimbuko au mapitio ya hayo maji, au ikiwa
kubadilika ni kwa sababu ya kuwemo maji kwa muda mrefu, kama vile katika hodhi;
haya hubakia kuwa ni 'taahir na yanafaa ku'tahirishia, hivi ni kutokana na
uzito na shida ya kuepukana na vitu hivyo na kwa vile kubakia jina la asli la
maji. Ni hivyo hivyo ikiwa maji yatabadilika (ladha yake) kwa kuongezwa chumvi
- ya maji au ya mawe - yatabakia kuwa ni 'taahir na yanafaa ku'tahirishia; kwa
sababu asili ya chumvi ni maji ya chumvi. Katika hali hizi hapana tafauti ikiwa
kubadilika huku ni kwa kuhisi au kwa maana ya neno, kama vile kubadilika na
kuondoka asili yake; kwa mfano maji ya mawaridi yakawa hayana harufu; haya
hukadiriwa kama yale yenye harufu.
Ya Tano, maji
yalioingia najsi, haya huwa katika namna mbili; mengi na kidogo. Maji kidogo
hunajsika kwa kuingia ndani yake najsi, sawa sawa ikiwa yatabadilika rangi,
ladha au harufu au hayatabadilika. Haya ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi
s.a.w:
“Maji
yakifika (kiwango cha) qulateini hayachukui (hayawi) najsi”. (Imehadithiwa na
Ahmad na Ibnu Hibbaan).
Hivi imefahamika ya kwamba
maji ya kiwango cha qulateini* hayanajsiki kwa kuingia najsi, na maji ya
kiwango cha kasoro ya qulateini hunajsika kwa kuingia najsi.
Maji mengi yanayo kusudiwa
hapa ni yale ya kiwango cha qulateini na zaidi, haya hunajisika iwapo huku
kuingia najsi kwenyewe kutabadilisha rangi, ladha au harufu ya hayo maji
Baadhi ya wanazuoni, miongoni
mwao ni Arawyaani, Al Ghazali na Al Baydhawy; wao wamesema ya kwamba maji
kidogo ni sawa na maji mengi, hayanajsiki kwa kuingia najsi; bali yana najsika
kwa kuingia najsi yakabadilika hayo maji rangi, ladha au harufu yake. Qauli hii
ni yenye nguvu kwa dalili ya kuzingatia ya kwamba cha kuchukuliwa kipimo ni
Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. iliotangulia kutajwa hapo juu yenye maana
kama hii: “Mwenyezi Mungu Mtukufu ameyaumba maji hali ya kuwa ni 'taahir na
yenye ku'tahirisha, hayanajisiki isipokua kwa kubadilika ladha yake au harufu
yake" Na kwa Hadithi iliopokewa na Ibn Maajah: "Au rangi yake".
*Qulateini imekadiriwa ni maji
yaliomo kwenye chombo cha dhiraa na robo
urefu, upana na kwenda chini.
Hii ni dalili iliotamkwa,
ambayo ina nguvu na uzito kuliko dalili ya kufahamika (mafhuum). Zaidi ya
hivyo, hapana tafauti baina ya kubadilika kidogo na kubadilika sana; na ikiwa
kubadilika huko ni kwa rangi, ladha au harufu, au kama hio najsi ilioifika maji
ni kwa kuchanganyika au kwa kuwa karibu yake; au najsi hio ilikuwa ni yenye
kuweza kuepukika na au haiwezi kuepukika. Muhim ni vile kuwa ni najsi, kinyume
na kubadilika maji kwa sababu ya mchanganyiko na kitu 'taahir. Lau kama
itaingia kwenye maji mengi najsi yenye sifa ya maji, kama vile mkojo uliokatika
harufu, basi hukadiriwa kwa kupewa hukmu kama ilivyotangulia kuelezwa kukhusu
vitu 'taahir. Ama kukhusu vitu vya maji-maji, ambavyo si maji; kama vile
mafuta, hivyo hunajsika kwa kuingia najsi ya kiwango chochote kile, ikiwa
vitabadilisha rangi, ladha au harufu au havitabadilisha.
Hii tafauti ya hukmu iliopo
baina ya viwili hivi, yaani maji na vitu vya majimaji; ni kwamba vitu vya
maji-maji si taabu kuhifadhika visipatwe na najsi, kinyume na maji.
Hukmu ya Maji Makombo
Maji makombo ni yale
yaliobakia kwenye chombo baada ya kunywiwa na binaadam au mnyama, haya huwa
katika hali kama hizi:
Kwanza, makombo ya
binaadam, haya ni 'taahir kwa Qauli ya Mwenyezi
Mungu Mtukufu:
“Na hakika tumewatukuza wanaadamu, ...”.
(Al Israai : 70).
Na katika kutukuzwa binaadam
ni hivi kuwa yeye ni 'taahir - hai au maiti.
Ama kukhusu unajsi uliotajwa
kwenye Qauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu:
“…… Hakika ya washirikina ni najsi……".
(Tawba : 28).
Unajsi unaokusudiwa ni unajsi
wa itikadi kwa uovu wanaouficha nyoyoni mwao, si unajsi wa kiwiliwili. Hawa
mushrikina siku za Mtume wetu Mpenzi s.a.w. walikuwa wakichanganyika na
Waislam, na tume zao zikija kwa Mtume wetu Mpenzi s.aw., na wakiingia msikitini
kwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. na wala hakuamrisha s.a.w. kukoshwa chochote
kilichogusa miili yao.
Pili, makombo ya
mnyama; mnyama wakati yuhai ni 'taahir, ikiwa ni mnyama anaeliwa au asieliwa;
isipokua mbwa na nguruwe, hawa ni najsi. Haya ni kutokana na Hadithi ya Jabir
r.a. alipoulizwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kuwa: “Tutawadhie makombo ya maji
yalionywiwa na punda”? Mtume wetu mpenzi s.a.w. akajibu:
“Na'am,
na waliobakisha wanyama mwitu”. (Imehadithiwa na Shafi’ii na Darqu’tny na Al
Bayhaqy).
Na kutokana na Yahya bin Said
ya kwamba Omar bin Khatab r.a. alikuwa kwenye msafara pamoja na Amri bin Al‘A'si
r.a. mpaka wakafika kwenye hodhi, Amri bin Al‘A'si akamuuliza mwenye hodhi kama
wanyama mwitu hunywa maji kutoka hodhi hilo. Sayyidna Omar r.a. akasema,
usitwambie, kwani sisi tunawazunguka wanyama mwitu na wanyama mwitu
wanatuzunguka sisi. (Ameipokea Malik). Na kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.
kukhusu paka, alipoulizwa s.a.w. kukhusu kunywa paka katika chombo, kama
kinanajisika au hakinajisiki; akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
Ama makombo ya maji
yaliyonywiwa na mbwa au nguruwe, hayo ni najsi; inapasa kuyaepuka, hivi ni
kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
Ama makombo ya maji
yaliyonywiwa na nguruwe ni najsi, kwani nguruwe ni akhasi kuliko mbwa, na
imejengwa hoja ya unajsi wa nguruwe kwa Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: “….. au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni
uchafu;.....”. (Al An’aam :145).
Na uchafu ni najsi.
Ngozi za Nyamafu
Hu'tahirishwa ngozi ya nyamafu
(mnyama aliokufa) kwa kudibaghiwa, sawa ikiwa wanyama hao ni wenye kuliwa au
wasioliwa, hivi ni kwa Hadithi ya Maimuna alivyosema kuwa Mtume wetu Mpenzi
s.a.w alisema:
“Lau mungalichukuwa ngozi yake”.
Wakasema: “Hakika yake hiyo ni ya nyamafu”. Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w.: “Inai'tahirisha
maji na (qaradhi) matunda yenye ukali”. (Imehadithiwa na Abu Daud na Al
Nissaai).
Na kutokana na Abi 'Abbas r.a.
kwamba Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:
“Ikidibaghiwa ngozi, huwa
ime'tahirika”. (Imehadithiwa na Al Sheikhan).
Hudibaghiwa ngozi ya nyamafu
kwa kutumia vitu vikali kama vile shabu, siki, maganda ya makomamanga, chumvi,
chokaa, na mfano wake. Na hupatikana huko kudibaghi kwa kuondoka uchafu
unaokuwemo kwenye ngozi, kwa kusafishwa uzuri ikawa hata kama itarowekwa ndani
ya maji basi haitatoa harufu mbaya. Ikiwa hivi kudibaghi kumefanyika kwa
kutumia kitu ambacho ni najsi, basi italazim baada ya kudabighiwa ikoshwe hio
ngozi ili kuondoa unajsi uliosababishwa kwa kile kitu najsi kilichotumiwa
katika kudabighi. Bali pia hata kama imedabighiwa kwa kitu ambacho si najsi;
basi inapendekezwa ikoshwe baada ya kudabighiwa. Ama ngozi ya mbwa na nguruwe,
na vizaliwa vyao, hai'tahiriki hata kwa kudabighiwa. Hivi kwa sababu wao ni
najsi asli yao tangu wahai, na kudabighi ni ku'tahirisha ngozi ambayo
imenajsika kwa kufa yule mnyama ambae asili yake ni 'taahir. Mbwa na nguruwe na
vizaliwa vyao ni najsi tangu wahai, basi ni ndivyo zaidi mizoga yao kuwa ni
najsi, wala hai'tahiriki.
Mifupa na Nywele za Nyamafu
Nyamafu ni maiti ya mnyama
ulieondoka uhai wake bila kuchinjwa kisharia. Hivi huwa pia maiti ya mnyama
asieliwa, hata ikiwa atachinjwa, na mnyama anaeliwa ikiwa hakuchinjwa kwa
mujibu wa sharia, huwa sawa na nyamafu. Kwa hivyo basi, nyamafu ni najsi kila
kitu chake; tangu nyama, ngozi, mifupa na manyoya yake, haya ni kutokana na
Qauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu aliposema:
Mmeharimishiwa
nyamafu ………”. (Al Maidah : 3).
Kuharimishwa kitu ambacho
asili yake si najsi wala si haram, wala hakina madhara kukila* ni dalili ya
kuwa ni najsi. Hivi ni kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufua:
“Sema: Sioni katika yale nilio funuliwa mimi
kitu kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu
inayo mwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hio ni uchafu, au kwa upotofu
kimechinjwa kwa jina la asiye kuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na
dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni
Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu" . (Al-An-'aam : 145).
"Rijsi" ni uchafu, na uchafu ni najsi. Ni ndivyo
kwamba manyoya, sufi, nywele na mifupa ni sehemu ya mwili, kwa hivyo hivi
vinachukua hukmu ya mwili wenyewe, yaani nyamafu; kwa hivyo navyo ni najsi.
Kuna qauli kuwa manyoya ya nyamafu* si najsi kwa hoja kuwa manyoya hayana uhai,
kwani yakikatwa hali ya kuwa huyo mnyama yuhai hahisi maumivu, na kwa qauli ya
Mtume wetu Mpenzi s.a.w.::
Na sehemu iliotengeka ya
mnyama hai ni sawa na nyamafu ya mnyama huyo, ikiwa asili yake ni 'taahir basi
nacho huwa 'taahir, na ikiwa ni najsi, basi nacho huwa ni najsi.
*Nyamafu imeruhusiwa kuliwa
wakati wa haja, lau kama anadhara kuliwa; isingali ruhusiwa kuliwa.
Hivi ni kutokana na Hadithi ya
Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
Kilichokatwa kutokana na
binadam, au samaki, au panzi, au nyembure; basi hivyo ni 'taahir, kwani asili
yao ni 'taahir, na kwa hivyo maiti/nyamafu yao ni 'taahir. Mbali na hivi basi
ni najsi, kwani nyamafu yao ni najsi. Ama nywele na sufi na manyoya ya mnyama
mwenye kuliwa ni 'taahir kwa kukubaliana wanazuoni.
Amesema Mwenyezi Mungu
Mtukufu:
Maneno haya ya Mwenyezi Mungu
Mtukufua yamechukuliwa kufahamika ikiwa vitu hivi vimechukuliwa kutokana na
mnyama baada ya kuchinjwa au hali yuhai, kama inavyofanywa daima. Ikiwa
itaingia shaka, kuwa vitu hivi vinatokana na najsi au 'taahir; basi tutachukua
kuwa vinatokana na 'taahiri, kwani hio ndio asili, na sisi tumetia shaka juu ya
najsi na asili ni kutokua najsi, yaani 'taahir.
Ama nywele za binaadam ni
'taahir, ikiwa zimekatwa hali yuhai au maiti, hivi ni kutokana na Qauli ya
Mwenyezi Mungu Mtukufu ya kukirimiwa binaadam:
“ Na hakika tumewatukuza
wanaadamu............ “. (Al Israai : 70).
Na suala hili la kukirimiwa
binaadam ndio hoja ya kutokua najsi binaadam, akiwa yuhai au maiti, ni Muislam
au si Muislam.
Qauli ya Mwenyezi Mungu
Mtukufu:
“…… Hakika ya washirikina ni najsi…….”. (Tawba
: 28).
Makusudio katika Aya hii ni
unajsi wa itikadi, si unajsi wa kiwiliwili. (Imetangulia kuelezwa haya kwenye
mas-ala ya "Makombo Ya
Binaadam".
Kutumia Vyombo vya Dhahabu na Fedha
Imeharamishwa kwa wanaume na
kwa wanawake kutumia vyombo vya dhahabu na vya fedha kwa kulia, kunywiya; hivi
ni kutokana na Hadithi ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
Na katika Hadithi nyengine
imepokewa kuwa:"Hakika ya anaekula au kunywa”, mpaka mwisho wa Hadithi.
Kama inavyo haramishwa kutumia
vyombo vya dhahabu na fedha kwa kulia na kunywiya, vilevile ina haramishwa
katika matumizi mengine.
Amesema Imam Al Nawawi r.a.
katika sherhe Muslim: “Amesema jamaa zetu wamekubaliana wote juu ya
kuharamishwa kula na kunywa na matumizi mengine katika vyombo vya dhahabu na
fedha.
Akaendelea mpaka akasema: “Kuharamishwa
huku ni sawa kwa wanaume na kwa wanawake, bila ya khilafu, na hakika tafauti
baina ya mwanamume na mwanamke ni katika mapambo ya kike kwa kujipamba kwa
ajili ya mume wake.
Vilevile ina haramishwa
kupamba maduka, majumba na maseble kwa vyombo na vitu vya dhahabu na fedha.
Vilevile ina haramishwa kuwanavyo vyombo hivi, hata bila ya kuvitumia; kwani
chenye kuharamishwa kutumia, kina haramishwa (kumilikiwa) kuwanacho na kwa kuwa
ni kitu cha kujifurahishia na pambo. Hivi ni kwamba kila ambacho asili yake
haram, basi ni haram kukitizama. Na imeharamishwa kwa masonara kutengeneza vitu
hivi, wala haijuzu kulipwa kwa kazi hii; kwa sababu kazi yao hii ni maasi. Lau
kama mtu akavivunja na kuviponda-ponda vyombo hivi, basi hatalipishwa, wala si
halali mtu kutaka alipwe kwa vyombo hivyo vilivyo pondwa-pondwa au kuvunjwa,
wala haijuzu kushitaki ili kutaka alipwe.
Vyombo vilivyochovywa fedha
kwa ajili ya pambo, hivyo vimeharamishwa kuvitumia; sawa sawa ikiwa kuchovywa
huko ni kwa kiwango kikubwa au kidogo. Ama ikiwa kuchovywa ni kwa kiwango
kidogo kulingana na haja tu, haiharimishwi kutokana na huo udogo wake, wala
haiwi makruuh kwa sababu ya haja. Haya ni kutokana na alivyopokea Imam Al
Bukhari r.a. kutoka kwa ‘Asim Al Ahwal aliesema: “Nimeiona bilauli (chombo cha
kunywiya) ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa Anas bin Malik r.a. nayo imefanya
kutu, ikatiwa utepe (upapi) wa fedha, yaani ikazuiliwa kwa upapi wa fedha”.
Akasema Anas bin Malik r.a. kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amenyweya chombo hiki
mara kadhaa wa kadhaa. Ama vyombo vinavyochovywa kwa dhahabu vimeharamishwa
kabisa kuvitumia kwa hali yoyote ile.
Kusuwaki
Kusuwaki ni kusafisha kinywa -
meno, ulimi - pembezoni na baina yake kwa kutumia msuwaki; wa kijiti au
uliotengenezwa kisasa, ili kuondoa harufu mbaya na kuondoa masalio ya chakula
yaliomo kinywani. Kupiga msuwaki ni sunna iliotiliwa nguvu kwa qauli ya Mtume
wetu Mpenzi s.a.w.:
“Kusuwaki ni ku'tahirisha (kusafisha) kinywa
na ni kumridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu”. (Imehadithiwa Ibnu Khuzaimah, Ibnu
Hibbaan, Al Baihaqy na Al Nissaai).
Kusuwaki kunapendekezwa na
kunasisitizwa katika hali hizi:
Ya Kwanza,
kinapobadilika kinywa harufu yake kwa kula kitu chenye harufu mbaya, kama vile
kitunguu thom, kitunguu maji, doriani au chochote kile chenye harufu yenye
kukirihisha.
Ya Pili, baada ya
kuamka; haya ni kutokana na Hadithi mbili zilizo sahihi.
Hadithi ya kwanza:
Hadithi ya pili:
Ya Tatu, wakati wa
kutaka kusali, hivi ni kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
Na imepokewa kutoka kwa
Sayyidah 'Aisha r.a. kuwa Mtume wetu Mpenzi s.a.w. amesema:
Ya Nne, wakati wa kutia
udhu, kwa qauli ya Mtume wetu Mpenzi s.a.w.:
Ya Tano, wakati wa
kusoma Qur’ani, hivi ni kwa sababu kwa vile kutakiwa 'tahara ya kinywa wakati
wa Sala, ambayo miongoni mwa nguzo zake ni kusoma Qur’ani, basi ni bora zaidi
'tahara ya kinywa wakati wa kusoma Qur’ani pekee, yaani bila ya kuwa kwenye
Sala.
Kusuwaki huwa ni kwa kitu
chochote chenye kuondoa uchafu kinywani. Lakini kutumia msuwaki wa mti unaoitwa
“arak” ni afadhali, kwa sababu msuwaki wa "arak" una faida nyingi.
Miongoni mwa faida hizo ni, umadhubuti wa ufizi, kuondoa maradhi ya meno,
kusaidia uwezo wa kutafuna chakula, kusaidia mzunguko wa mkojo, kusafisha vyema
kinywa, bali zaidi humridhisha Mwenyezi Mungu Mtukufu. Msuwaki wa الأراك
) ) “arak” pia
unadumisha uwezo wa ujana, unasafisha koo, unasaidia uwezo wa akili, una ujira
zaidi, unasafisha kwa wepesi na una saidia kukumbusha kushahadia wakati wa
mauti.
Inapendezewa kuukosha msuwaki
kabla na baada ya kuutumia na iwe kusuwaki kwa kutumia mkono wa kulia. Vilevile
inapendekezwa kuanzia mkono wa kulia wa kinywa, na apitishe msuwaki sehemu ya
juu ya kinywa na kwenye maoteo ya meno - ufizi. Na inapendekezwa msuwaki uwe
wenye urefu wa kadiri ya shubiri kama ilivyothibiti kwa sunna. Asiekuwa na meno
(kibogoyo), yeye asuwaki kwa kutumia kidole chake.
Haya ni kutokana na Hadith ya
Mtume wetu Mpenzi s.a.w. alipoulizwa na Sayyidah 'Aisha r.a. kukhusu mtu
asiekuwa na maneno kuwa na yeye asuwaki? Akasema Mtume wetu Mpenzi s.a.w. kwa
maneno yenye maana kama hii: “Na'am, asuwaki kwa kutia kidole chake kinywani”.
(Imehadithiwa na Al ‘Tibraani).
Post a Comment