JE, YAFAA MWANAMKE KUCHINJA NA MWANAMUME KULA KUTOKAMANA NA KICHINJO CHAKE?

Kuchinja ni miongoni mwa Ibadah, kwani zipo Ibadah ambazo wanashirikiana wanaume na wanawake,vile vile kuna Ibadah zinazowahusu imma wanaume pekee au wanawake pekee.....Ila katika kuchinja hii ni miongoni mwa Ibadah inayowajumlisha wote (mume na mke),sio kama vile wengi wetu tunavyodhani kwamba mwanamke hapaswi kuchinja na anapochinja inakuwa haraam kwa mwanmume kukila kichinjo kile,la hasha!! lazima ifahamike kwamba kuchinja ni Ibadah ya wote kwa kuzingatia masharti na adabu zilizoekwa na shari'ah za uchinjaji.
Kwa ushahidi wa kuonesha kwamba Ibadah ya kuchinja haijabainisha jinsia kwa mchinjaji,Anasema Allah ('Azza Wa Jallah):
((Basi Swali na uchinje kwa ajili ya Mola wako)) [Al-Kawthar: 2]

((Sema: Hakika Swalah yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Allaah Mola wa viumbe vyote))

((Hana mshirika Wake. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu)) [Al-An'aam: 162-163].
Amma tukizirudia aya hizo inatudhihirikia kwamba hakuna ubainisho wowote wa jinsia unaotajwa
Na Hadiyth iliyopokelewa toka kwa Yahya,kutoka kwa Ka'ab Ibn Maalik,Kutoka kwa Naafi,Kutoka kwa mwanamume wa kianswaar,kutoka kwa Muadh Ibn Sa'ad kwamba kijakazi mmoja wa kike alikuwa malishoni na kondoo wake katika Sai (mlima uliopo Madiyna) alichinja kondoo kwa kutumia jiwe lenye makali. Hivyo mtume (swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza kuhusu hilo na akaamuru watu kula ile nyama. (Muslim: 24/2/4)
Kwa hivyo basi kutokana na hadiyth hiyo endapo kutapatikana vigezo hivi:
1) Mwanamke awe ni muislamu
2) Aanze kwa BismiLlaah (asome Basmala)
3) Apige Takbiyr (Allaahu Akbar) wakati wa kuchinja
Inakuwa halali hata wewe mwanamume kula. 

Allaahu A'alam

MNYAMA ALIYECHINJWA NA MWENYE JANABA AU HEDHI

Swali:


Mwanamume mwenye janaba amejichinjia mnyama mwenyewe,je,anapata dhambi juu ya hilo?

Jawabu:

Mnyama aliyechinjwa na mwenye janaba au hedhi ni halaal, na wala hana dhambi juu ya hilo.

Ibn Qudaamah amesema: Ikiwa ana janaba, inajuzu kwake yeye kusema Bismillaah na achinje.
Hili ni kwa sababu mwenye janaba anaruhusiwa kusema Bismillaah na hakuna sababu yeyote inayomzuia yeye kuchinja. Iinalo katazwa kwa mwenye janaba ni kusoma Qur-aan, Ila anaweza kuisoma moyoni. Vile vile inaruhusika kwake yeye kusema Bismillaah anapotaka kufanya ghusl. Mwenye Janaba sio zaidi ya kafiri kwamba atataja jina la Allah na achinje.

Miongoni mwa wale wanaosema kwamba yajuzu kwa mwenye janaba kuchinja ni:
Al-Hasan, Al-Hakam, Al-Layth, As-Shaafi'y Ishaaq, Abu Thawr and Ashaab al-ra’y.

Ibn Al-Mundhir Amesema: Simjui yeyote aliyekataza hilo. Halikadhalika inajuzu kwa mwenye hedhi kuchinja, kwa sababu analingana sababu sawa na mwenye janaba. Mwisho wa nukuu (Tazama:
"Al-Mughniy 11/61")

Imam An-Nawawiy (rahimahu Allaah) amesema katika "Al-Majmuu’" (9/74):
Ibn Al-Mundhir ameeleza kwamba wanazuoni wanaonelea kuwa yajuzu kwa mwenye janaba kuchinja. Akasema:
Kama Qur-aan inavyoonyesha kwamba mnyama aliyechinjwa na ahlul kitaab ni halaal ingawa wao ni najisi, hivyo basi itakuwa sawa kabisa mnyama kuchinjwa na yule ambae kwamba Sunnah haijamtaja yeye kuwa ni najisi,hivyo inajuzu.
Na akasema: Mwanamke mwenye hedhi ni kama mwenye janaba.

Wanazuoni wamenukuu ushahidi wa hili hadiyth iliyopokelewa na Al-Bukhaariy (5501) na Muslim iliyotangulia hapo juu ya yule kijakazi

Inaelezwa katika "Sharh Al-Muntaha" (3/417): Hii inaonesha kwamba ni halaal kula nyama iliyochinjwa na mwanamke, kijakazi,mwanamke mwenye hedhi na hata mwenye janaba,kwa sababu mtume (swalla Allaahu'alayhi wa sallam) alipofikishiwa habari za kijakazi yule hakuuliza lolote la zaidi kumhusu.

Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

0 Comments