HISTORIA YA MUADH BIN JABAL (RADHWIYA ALLAAHU 'ANHUMAA) KWA UFUPI

Jina lake ni Muadh bin Jabal bin Amru bin Aws bin Aidh bin Uday bin Kaab bin Amru bin Adiy bin Saad Al Khazraji Al Ansari, na umaarufu wake ni Abu Abdul Rahman (Radhiya Llahu anhu). Alizaliwa mwaka wa ishirini kabla ya Hijra.

Katika mwaka wa kumi na tatu tokea kupewa utume Mtume wa Mwenyezi Mungu (), na baada ya washirikina wa Makka kukataa kumfuata, na badala yake wakawa wanawatesa na kuwaadhibu wale wachache waliomuamini, uliwasili Makka kutoka Madina ujumbe wa watu sabini na tano uliokuja kukutana na Mtume wa Mwenyezi Mungu () kwa siri kwa ajili ya kufungamana naye katika fungamano lililokuja kujulikana kwa jina la 'Fungamano la Aqaba la pili'.

Waliagana kukutana naye nyakati za usiku katika kijiji kimoja pale Mina karibu na Jamarat la mwanzo.

'Jamaraat la mwanzo' ni yule anayeitwa 'shetani mkubwa', anayepigwa mawe siku za Hija.

Kabla ya kufungamana naye, Mtume wa Mwenyezi Mungu () aliuhutubia ujumbe huo, akasema:

"Nafungamana nanyi kwa masharti yafuatayo; Mnipe himaya kama mnayowapa watu wenu, na mufuate amri na kutii na kutoa katika dhiki na faraji, na katika kuamrisha mema na kukataza mabaya, na musimamie kazi ya Mwenyezi Mungu bila ya kuogopa lawama za wenye kulaumu".

Wote kwa pamoja waliyakubali masharti hayo, wakafungamana naye () kwa kumpa mkono mmoja baada ya mwengine huku wakimuahidi Mtume wa Mwenyezi Mungu () kuwa watamlinda kwa hali na mali atakapohamia katika mji wao – Madina. Katika mikono iliyonyoshwa kufungamana naye siku hiyo ulikuwa mkono wa kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi na nane - Muadh bin Jabal (Radhiya Llahu anhu).
Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) anarudi Madina

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alisilimu mikononi mwa Masaab bin Umair (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) aliyepelekwa Madina na Mtume wa Mwenyezi Mungu () kwa ajili ya kuwafunza dini na kuwasomesha Qurani tukufu, na hii ilikuwa baada ya Fungamano la mwanzo lililofanyika mwaka mmoja kabla, mahali pale pale lilipofanyika Fungamano la pili.

Juu ya udogo wa umri wake, Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alikuwa aalim miongoni mwa maulamaa waliokuwa wakitamba kwa elimu yao katika Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (), na alikuwa mcha Mungu sana.

Alirudi Madina baada ya kuhudhuria fungamano hilo akiwa na nia pamoja na hamasa kubwa ya kuilingania dini ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuizamisha mizizi yake vizuri katika mji wa Madina kwa ajili ya kuutayarisha mji huo kuwa makao makuu ya dini ya Kiislamu na ngome imara itakayomlinda Mtume wa Mwenyezi Mungu () pale atakapohamia kwao, na ili pia pawe mahali itakapoanza daawa ya kuieneza dini hii pembe zote za dunia.
 
Kuvunja Masanamu

Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) akishirikiana na kijana mwenzake aitwae Thaalaba bin Athamah (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) pamoja na baadhi ya vijana waliosilimu wa kabila la Bani Salamah, walikuwa kila wanapopata fursa katika giza la usiku wakiyaendea masanamu ya washirikina na kuyavunjavunja au kuyatupilia mbali.

Katika masanamu waliyokuwa wakiyashambulia lilikuwa lile la Amru bin Jamouh mmojawapo wa wakuu wa kabila la Bani Salamah aliyekuwa na sanamu la mbao alolipa jina la Manaat.

Walikuwa wakiliiba sanamu hilo nyakati za usiku na kulitupa ndani ya mojawapo ya mashimo ya kijiji cha Bani Salamah yaliyokuwa na vinyesi vya watu ndani yake, na Amru anapoamka asilikute sanamu lake, huanza kutukana na kulaani huku akisema;

"Ole wenu! Muovu gani aliyemfanyia uadui mungu wetu usiku wa leo?" Kisha anatoka na kuanza kulitafuta, na anapolikuta limetupwa juu ya uchafu kichwa kimeangukia kinyesi, huliokota na kulichukuwa nyumbani, akalikosha na kulisafisha, kisha analipaka mafuta mazuri huku akiliambia:

"Wallahi ningelimjuwa aliyekufanyia hivi ningemdhalilisha."

Ikawa kila siku wakati wa usiku Amru anapokwenda kulala, vijana hao huliendeea sanamu lake na kufanya yale yale.

Siku moja baada ya kuchoshwa na kazi ya kulifuta na kulisafisha sanamu lake, akaamua kulifunga na upanga, kisha akaliambia;

"Wallahi mimi simjui anayekutendea haya, lakini ikiwa una kheri yoyote basi jilinde kwa upanga huu." Kisha akenda kulala.

Vijana wale wakaja na kulichukuwa sanamu hilo, wakalifunga na mzoga wa mbwa na kama kawaida yao wakalitupa ndani ya moja wapo ya mashimo ya kufanyia haja ya kijiji cha Bani Salamah, na Amru alipoamka asilione sanamu lake. Akatoka na kuanza kulitafuta, na kama kila siku akalikuta limetupwa ndani ya shimo, na safari hii likiwa limefungwa na mzoga wa mbwa.

Akalitizama muda kidogo kisha akalitungia shairi akiliambia;

"Wallahi ungekuwa Mungu wa kweli, usingekubali kuwa dhalili, ukatupiliwa mbali, pamoja na mzoga wa mbwa ndani ya shimo hili."

Amru alisilimu baadaye na akawa Muislamu mwema.


Anawalingania Mayahudi Katika Dini Ya Mwenyezi Mungu

Tokea Mtume wa Mwenyezi Mungu () alipohamia Madina, Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alikuwa daima yupo pamoja naye akiipokea Qurani moja kwa moja kutoka mdomoni mwake, huku akijifunza sheria za dini kutoka kwake (), jambo lililomfanya awe msitari wa mbele miongoni mwa maulamaa wa wakati wake, na pia katika kuwalingania watu wa mji wake.

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) hakuridhika na kuwalingania watu wa kabila lake na Waarabu peke yao pamoja na kuvunja masanamu yao, bali alikuwa pia akiwalingania Mayahudi wa pale Madina ambao hapo mwanzo walikuwa wakizungumza sana juu ya Mtume mpya atakayekuja. Kwani wasifu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu( ﷺ) umeandikwa ndani ya Taurati, lakini zilipowafikia habari za kuja kwake, walimkanusha na kumkataa, na kwa ajili hiyo Muadh akifuatana na Bishr bin Al Bara-a aliwaendea na kuwaambia:

"Enyi Mayahudi, muogopeni Mwenyezi Mungu na ingieni katika dini ya Kiislamu, kwani si nyinyi mliokuwa mkitubashiria juu ya kuja kwa Mtume huyu wakati ule tulipokuwa washirikina tukiabudu masanamu, kisha mkawa mnatupa wasifu wake? Na mlipokuwa mkipigana vita kabla ya kuja kwa Mtume huyu si mlikuwa mkiomba mpate ushindi kwa baraka zake?

Akasema Sallaam bin Mishkam mmoja katika Mayahudi wa kabila la Bani Nadhiyr:

"Hana wasifu wowote katika ule tunaoujuwa, na wala si huyu tuliyekuwa tukikubashirieni."

Ndipo Mwenyezi Mungu alipoteremsha kauli Yake;

"Na kilipo wajia Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kinacho thibitisha waliyo nayo - na wao walikuwa wakitafutia ushindi kuwashinda makafiri - yalipo wajia yale waliyo kuwa wakiyajua waliyakanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu juu ya wakanushao!"

Al Baqarah – 89
 
Jihadi Yake

Tokea siku ile alipounyosha mkono wake na kuuingiza ndani ya mkono wa Mtume wa Mwenyezi Mungu () huku akimuahidi kuilingania dini aliyokuja nayo, Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alisimama imara katika kulinyanyua neno la Mwenyezi Mungu ili liwe juu, na akaendelea juu ya njia hiyo maisha yake yote.

Alishiriki katika vita vya Badar, Uhud, Tabuk na vita vyote alivyoshiriki ndani yake Mtume wa Mwenyezi Mungu (). Alikuwa daima ubavuni mwake, na baada ya vita vya Tabuk, Mtume wa Mwenyezi Mungu () alimpeleka Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) Yemen kwa ajili ya kuwaongoza watu wa huko na kuwafundisha dini pamoja na kitabu cha Mwenyezi Mungu, na hakurudi tena Madina mpaka baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu () kufariki.

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) hakuacha kupigana jihadi hata baada ya kufariki kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, bali alishiriki katika vita vingi vilivyopiganwa katika nchi ya Sham na kwengineko.
 
Elimu Yake

Juu ya udogo wa umri wake, Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alikuwa aalim aliyezama katika bahari ya elimu, na siku ile Mtume wa Mwenyezi Mungu () alipokuwa akiwasifia Masahaba wake (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alisema:

"Mwenye huruma kupita wote katika umma wangu Abubakar, na mkali kupita wote katika dini ya Mwenyezi Mungu ni Omar, na mwenye kuona haya kupita wote Othman, na mwenye hekima kupita wote katika kutoa hukmu Ali, na mwenye elimu zaidi juu ya halali na haramu Muadh bin Jabal."

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alipata sifa zote hizo akiwa na umri mdogo sana, kwani wakati alipofariki alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitatu tu.Mtume wa Mwenyezi Mungu () aliwausia Masahaba (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) wajifunze Qurani kutoka kwa wanne, na Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alikuwa katika wanne hao. Alisema;

"Jifunzeni Qurani kutoka kwa wanne; Ibni Masaud, Salim mawla Abu Hudhaifa, Ubay na Muadh bin Jabal."

Bukhari 7/125 hadithi nambari 3806

Muslim 2464Abu Muslim Al Khoulaniy, na huyu ni katika wacha Mungu maarufu wa Taabi'ina (waliokuja baada ya Mtume wa Mwenzi Mungu () wakawaona Masahaba (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) anasema:

"Niliingia msikiti wa mji wa Hims nikawakuta Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu () watu wazima wapatao thelathini, na miongoni mwao akiwemo kijana mwenye macho meusi na mwanya unaong'ara aliyekuwa amekaa kimya. Na kila watu wanapokhitalifiana au wanapotatanishwa na jambo humwendea kijana huyo na kumuuliza. Nikamuuliza aliyekaa karibu nami: 'Nani huyu?' akaniambia; 'Muadh bin Jabal'.

Al Tabakaat al Kubra 3/590Omar bin Khattab (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alipozuru nchi ya Sham aliwahutubia watu wa huko na kuwaambia:

"Mwenye kutaka kuuliza juu ya fardhi amwendee Zeid bin Thabit, na mwenye kutaka kuuliza juu ya fiq'hi amwendee Muadh bin Jabal."Imepokelewa pia kuwa Omar bin Khattab (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) aliwahi kusema:

"Nikimpa uongozi Muadh na Mola wangu akiniuliza: 'Kwa nini umempa uongozi?' Nitasema: "Nilimsikia Mtume wako akisema; 'Hakika maulamaa watajapohudhurishwa mbele ya Mola wao Azza wa Jalla, Muadh atakuwa mbele yao."

Rijaal haula Rasuul –Khalid Muhammad KhaledImepokelewa pia kuwa Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu () wanapokuwa wanazungumza, na Muadh yuko pamoja nao, walikuwa kila mara wakimuangalia, na hii inatokana na haiba aliyokuwa nayo Sahaba huyu mtukufu (Radhwiya Allaahu 'anhumaa).

Juu ya kuwa alikuwa akipenda kukaa kimya, lakini anapoanza kuzungumza wote kwa pamoja hunyamaza na kumsikiliza.

Anasema mmoja katika sahibu zake:

"Anapozungumza Muadh, inakuwa kama kwamba vipande vya lulu vinadondoka kutoka mdomoni mwake".
 
Ibada yake

Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alikuwa mcha Mungu sana mwenye kupenda kusali. Alikuwa akishamaliza kusali msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu () akirudi kijijini kwake, kijiji cha Bani Salamah waliokuwa wakiishi nje ya mji wa Madina na kuwasalisha watu wa kabila lake msikitini kwao.

Alikuwa anaposali akiona kama kwamba Sala yake hiyo ni ya mwisho na kwamba hatopata tena fursa nyingine ya kusali.

Imepokelewa kuwa alikuwa akimuusia mwanawe kwa kumwambia: "Unaposali, sali Sala ya kuaga, kama kwamba hutopata tena fursa ya kusali Sala nyengine. Na elewa ewe mwanangu kuwa mtu anakufa baina ya mema mawili. Jema alilojitangulizia na jema aloliacha asilifanye."
 
Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) anapelekwa Yemen

Baada ya vita vya kuuteka mji wa Makkah 'Fat'hi Makkah' na vita vya Tabuk kumalizika, Mtume wa Mwenyezi Mungu () aliamua kuwaacha Makkah Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) na Utab bin Usayd (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ili wawe magavana wa mji huo na kuwafundisha watu wake Qurani pamoja na hukmu za dini. Na haukupita muda mrefu Mtume wa Mwenyezi Mungu () akaamua kumpeleka Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) Yemen kwa ajili ya jukumu hilo hilo.

Anasema Bukhari katika mlango wa kupelekwa Abu Musa Al Ash'ary Yemen ili awe gavana wa huko, na hii ilikuwa kabla ya Hija ya mwisho ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ():

"Ametuhadithia Musa, aliyehadithiwa na Abu Awanah aliyehadithiwa na Abdul Malik, kutoka kwa Abu Bardah kuwa; Mtume wa Mwenyezi Mungu () aliwapeleka Yemen Abu Musa na Muadh bin Jabal na kila mmoja alipewa sehemu yake, na Yemen ilikuwa sehemu mbili wakati huo, kisha akawaambia; "Yarahisisheni mambo wala msiyafanye magumu, na muwapendezeshe watu wala msiwachukize."

Imepokelewa pia kuwa alipokuwa akimsindikiza Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhumaa), Mtume wa Mwenyezi Mungu () alikuwa akitembea kwa miguu huku Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) akiwa amepanda mnyama, akawa anamwambia:

"Ewe Muadh! unakokwenda kuna watu wa kitabu (Mayahudi na Manasara), basi utakapokutana nao, jambo la mwanzo utakalofanya ni kuwalingania katika 'La ilaaha illa Llah' na kwamba Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu. Wakikutii katika hilo utawajulisha kuwa Mwenyezi Mungu amewafaradhishia Sala tano kila usiku na mchana. Na wakikutii katika hilo utawajulisha kuwa Mwenyezi Mungu amwewafaradhishia kutoa Zaka zitakazochukuliwa kutoka kwa matajiri wao na kupewa masikini wao. Na watakapokutii katika hilo usije ukawalazimisha tena kutoa katika mali zao wanazozipenda sana (muhimu watoe Zaka na kiwango kiwe kinachokubaliana na sheria), na uigope dua ya aliyedhulumiwa, kwani haina kizuwizi baina yake na baina ya Mwenyezi Mungu (hapana kitakachoweza kuizuwia dua ya aliyedhulumiwa isifike kwa Mwenyezi Mungu)."Imepokelewa pia siku hiyo alimuusia mambo mengi, kisha akamuambia:

"Ewe Muadh! Huenda usionane na mimi tena baada ya mwaka wangu huu. Na huenda ukaja msikitini kwangu hapa na kulipitia kaburi langu." Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alilia sana baada ya kujuwa kuwa anafarikiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu () kwa mara ya mwisho. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu () akamwambia:

"Usilie (sana) ewe Muadh, kwani kilio kinatokana na shetani."

Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu () akaugeuza uso wake kuelekea upande wa mji wa Madina, akasema:

"Wanaonistahiki zaidi ni wacha Mungu, wowote watakaokuwa na popote watakapokuwa."

Kisha akamwambia:

"Ewe Muadh! Nakupeleka kwa watu wenye nyoyo laini na wenye kuipigania haki mara mbili. Kwa hivyo pigana pamoja na atakayekupa Mwenyezi Mungu katika hao dhidi ya watakaokuasi."
Wallahi mimi nakupenda

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alibahatika kupata sifa ambayo kila Muislamu anatamani aipate, nayo ni mapenzi ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (). Imepokelewa kuwa siku aliyokuwa akimsindikiza kuelekea Yemen, Mtume wa Mwenyezi Mungu () aliuingiza mkono wake mtukufu ndani ya mkono wa Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kisha akamwambia:

"Ewe Muadh! Wallahi mimi nakupenda."

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) akasema:

"Na mimi Wallahi nakupenda ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu."

Ndipo Mtume wa Mwenyezi Mungu () alipomuambia;

"Ewe Muadh! Nakuusia Kila utakapomaliza kusali usiache kusema; 'Allahumma ainniy alaa dhikrika wa shukrika wa husnu ibaadatika.'

Niusie;

Imepokelewa pia kuwa Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu (): "Niusie."

Mtume wa Mwenyezi Mungu () akamwambia: "Mche Mwenyezi Mungu popote utakapokuwa."

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) akasema: "Niongeze."

Mtume wa Mwenyezi Mungu () akamwambia: "Ukitenda ovu, lifuatilie na jema litalifuta."

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) akasema: "Niongeze."

Mtume wa Mwenyezi Mungu () akamwambia: "Ishi na watu kwa mwenendo na tabia njema."

Al Bidaya wal Nihaya – juz. 5
 
Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) anarudi kutoka Yemen

Mtume wa Mwenyezi Mungu () alifariki dunia wakati Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) bado yupo Yemen, akarudi Madina wakati wa ukhalifa wa Abubakar al Siddique (Radhwiya Allaahu 'anhumaa)
Mwalimu kisha gavana wa Sham

Wakati wa ukhalifa wa Omar bin Khattab (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) ulikuja ujumbe kutoka Sham na kumwambia:

"Ewe Amiri wa Waislamu! Watu wa Sham ni wengi na wanahitajia waalimu wa kuwafundisha dini ya Mwenyezi Mungu."

Omar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) akawachaguwa Masahaba watatu akiwemo Muadh bin Jabal (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) na kuwapeleka huko, na alipofariki dunia Abu Ubaidah Amir bin al Jarrah aliyekuwa gavana wa nchi ya Sham, Omar (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alimchagua Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) kushika mahali pake, na Muadh akakubali, lakini hakuishi muda mrefu naye pia akafariki dunia.


Kufariki kwake

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alifariki dunia katika mji wa Amuwas uliopo baina ya Baytul Maqdis na Ramalah katika nchi ya Palastina, na alifariki kwa maradhi ya tauni yaliyopewa jina la mji huo wa Amuwas (Taaun Amwas). Maradhi haya yaliuwa zaidi ya watu elfu ishirini, na katika riwaya nyengine; zaidi ya watu elfu thelathini na tano.

Alipokuwa akiirudisha roho kwa Mola wake Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alikuwa akisema:

"Najikinga kwa Mola wangu na usiku ambayo asubuhi yake inaelekea motoni. Nayakaribisha mauti, nayakaribisha kwa mauwa. Mola wangu nilikuwa nikikuogopa, lakini leo nakuomba. Mola wangu unajuwa kuwa sikuwa nikiipenda dunia wala sikuwa nikipenda kubaki ndani yake muda mrefu, wala sikuwa nikiipenda kwa ajili ya kupandisha miti, bali nilikuwa nikiipenda kwa ajili ya kukaa pamoja na maulamaa na kukaa katika vikao vya kukutaja".

Muadh (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) alifariki dunia katika mwaka wa kumi na nane baada ya Hijra akiwa na umri wa miaka thelathini na mitatu.

0 Comments