Swali:
'Je hii hukmu ya kuuwawa kwa murtadi si katika kulazimishana katika dini?'
Jawabu:
Allaah Anasema:
"Hapana
kulazimisha katika Dini. Kwani Uongofu umekwisha pambanuka na upotofu.
Basi anaye mkataa Shaytwaan na akamuamini Allaah bila ya shaka amekamata
kishikio madhubuti, kisicho vunjika. Na Allaah ni Mwenye kusikia,
Mwenye kujua."
Al Baqarah – 256
Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Atakayebadilisha dini yake muuweni."
Bukhari
Na akasema:
"Si halali (kumwaga) damu ya Muislamu isipokuwa kwa matatu; Nafsi kwa nafsi (Aliyeua auwawe), na mzinzi 'thayyib' (aliyekwishaoa au kuolewa) na aliyeacha dini akafarikiana na kundi."
Bukhari na Muslim
Hapana
mgongano wowote baina ya hukmu mbili hizi. Ya mwanzo ni juu ya
asiyekuwa Muislamu. Huyu akitaka kubaki katika dini yake ya Ukristo au
Uyahudi au dini yoyote ile, anao uhuru kamili wa kubaki huko, na haijuzu
kumlazimsha kuiacha dini yake.
Ama
hukmu ya pili ni juu ya jambo jingine kabisa. Ni juu ya yule
uliyekwishambainikia ukweli, akamjua Allaah, akaikubali hidaya Yake,
kisha akaamua kwa hiari yake mwenyewe kuingia katika dini ya Kiislamu
bila kulazimishwa.
Atakayeamua
kusilimu kwa hiari yake mwenyewe, hatakiwi kufanya kufru tena.
Haiwezekani mtu leo aseme mimi ni Muislamu, kisha aanze kumtukana Allaah
kuwa amefanya makosa au dhulma n.k. Au amtukane Mtume wa Allaah (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au Sahaba zake (Radhiya Allaahu
anhum) au Wake zake (Radhiya Allaahu anhunna), au aseme mimi sioni kama
Swalah ina umuhimu wowote au aitie ila yoyote dini. Au afanye jambo
lolote litakaloingiza shaka ndani ya nafsi dhaifu. Huyu anakuwa
hajaingia katika dini isipokuwa kwa ajili ya kuwababisha watu. Huyu ni
mzizi mbaya unaotaka kuleta fitna katika dini na lazima ung'olewe.
Na hii ndiyo maana mtu atakayetoka katika dini, akinyamaza kimya asiseme kitu, hawezi kuhukumiwa kama
ni murtadi. Na hii ni kwa sababu Waislamu hawatakiwi kufuatilia na
kuchunguza aibu au matendo ya watu yaliyotendwa kwa kujisitiri au kwa
kujificha. Bali
wanahesabiwa kwa matendo yaliyofanywa kwa jahara tena pawe na ushahidi
usio na shaka kuwa mtu huyo anajuwa analotenda na alilikusudia.
Kwa
hivyo mwenye kurtadi kisha akatamka jahara mbele ya watu, anakuwa
keshatangaza vita dhidi ya Uislamu, na anakuwa keshainyanyua bendera ya
upotovu, na kwa ajili hiyo kisheria mtu huyo lazima apigwe vita kwa
sababu anahesabiwa kuwa ni mwenye kuipiga vita dini, na Uislamu
haukubali kugeuzwa mchezo, leo mtu anaingia na kesho anatoka.
Allaah Anasema:
"Na
kikundi katika Watu wa Kitabu walisema: Yaaminini yale waliyoteremshiwa
wenye kuamini mwanzo wa mchana, na yakataeni mwisho wake; huenda
wakarejea."
Aal Imran -72
Ufafanuzi wa Aayah hii:
"Miongoni
mwa vitimbi walivyokuwa wakifanya Mayahudi na Manasara ili kuwababaisha
watu na dini ya haki - ya Uislamu- ni kuwaamrisha baadhi yao kwenda
kusilimu kisha kurejea katika dini yao ili wawatie wasiwasi na wahka
wale Waislamu wa kweli waone 'labda si dini ya haki hii. Mbona wameingia mahodari wale kisha wakatoka?'
Nani Murtadi
Allaah Anasema:
"Wala hawataacha kupigana nanyi, mpaka wakutoeni katika dini yenu, kama wakiweza. Na watakaotoka dini yao
katika nyinyi, kisha wakafa hali ya kuwa makafiri, basi hao ndio ambao
amali zao zimeharibika katika dunia na Aakhirah. Nao ndio watu wa
Motoni. Humo watakaa milele."
(Al - Baqarah -217)
"Murtadi"
ni yule aliyeiacha dini ya Kiislamu akiwa na akili timamu, bila
kulazimishwa na mtu akaingia katika dini nyingine kama vile Ukristo au
dini ya Kiyahudi au kutokuwa na dini kama vile Ukoministi, au akakanusha
jambo lolote lijulikanalo kama ni la lazima katika dini kama vile
kuwajibika Kuswali, kutoa Zakaah au akafanya jambo dhidi ya Uislamu au
dhidi ya sheria zake zilizo dhahiri au akatamka kauli ambayo haina
tafsiri nyengine isipokuwa kukufuru.
Kurtadi kwa itikadi
Mwenye
kumshirikisha Allaah au kumpinga au akakanusha moja wapo katika sifa
Zake zilizothibiti. Ikijulikana wazi kuwa mtu huyo bila shaka anazielewa
vizuri sifa hizo. Au amsingizie Allaah jambo ambalo Yeye mwenyewe
amelikanusha; mfano; kuwa na mtoto, au kukanusha kuwepo kwa Malaika au
vitabu au Mitume au kuikanusha Siku ya Qiyaamah au Qadar kheri yake na
shari yake au akatae jambo lolote linalojulikana kuwa ni la lazima
katika dini, basi mtu huyu huwa ni Murtadi, aliyetoka katika dini.
Inajulikana
pia kuwa anahesabika Murtadi, Muislamu yeyote anayeipinga au kuikanusha
Qur-aan yote, au sehemu yoyote ya Qur-aan au hata aya moja katika aya
za Qur-aan.
Huhesabiwa
kuwa amertadi pia, mwenye itikadi kwamba Qur-aan inakhitalifiana
yenyewe kwa yenyewe au ina khitilafu ndani yake, au mwenye kuwa na shaka
katika miujiza yake au kujigamba kuwa ana uwezo wa kuleta mfano wake,
na pia mwenye kuivunjia heshima, au kuongeza au kupunguza ndani yake.
Anahesabiwa
kuwa amertadi mwenye kuitakidi kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema uongo katika baadhi ya aliyokuja
nayo, na pia yule anayeitakidi kuwa ni halali jambo lolote
liloharamishwa kama vile kuzini kunywa pombe n.k.
Kurtadi kwa matamshi
Kuapa kwa mila nyengine isiyokuwa ya Kiislamu.
Ameelezea Thabit bin Dhwahaak kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Atakaekula kiapo kwa mila isiyokuwa ya Kiislamu anakuwa kama alivyosema".
Abu Daud
(Mfano
wake ni baadhi ya watu wanaopenda kuwaiga wasio waislamu katika kula
kiapo akasema; ‘Yesu kristo’ au kwa lugha yoyote ile, viapo vya aina
hiyo).
Na
kutoka kwa Buraydah (Radhiya Allaahu anhu) ameeleza kuwa Mtume wa
Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Atakayesema;
‘Mimi si Muislamu’, ikiwa anasema uongo basi kama alivyosema, na ikiwa
anasema kweli basi hatorudi katika Uislamu akiwa amesalimika".
Abu Daawuud , Annasai na Ibn Maajah
Atakayemtukana
Allaah au Qur-aan au akamtukana Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) au moja wapo kati ya Mitume ya Allaah, anakuwa
amertadi hata kama ametamka hayo kwa mzaha au kweli au kwa istihizai.
Allaah Anasema:-
"Na kama
ukiwauliza (kwa nini wanaifanyia mzaha dini)? Wanasema; "Sisi tulikuwa
tukizungumza zungumza na kucheza tu." Sema; "Mlikuwa mkimfanyia mzaha
Allaah na Aayah zake na Mtume Wake?
"Msitoe udhuru (wa uongo) umekwisha kudhihiri ukafiri wenu (mlokuwa mkiuficha) baada ya kule kuamini kwenu (kwa uwongo)."
At - Tawba - 65 - 66
Maulamaa
wote wamekubaliana kuwa mwenye kumsingizia uongo Bibi Aisha (Radhiya
Allaahu anha) katika kile kisa cha uongo alichozuliwa (Tukio la
"Al-Ifki") na ilihali Allaah keshaukanusha uongo huo kisha akamtakasa,
basi anakuwa si Muislamu tena.
Allaah Anasema:-
"Hakika
wale walioleta uongo huo (wa kumsingizia bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu
anha) mkewe Mtume wa Allaah Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam
kuwa amezini)) Ni kundi miongoni mwenu (ni jamaa zenu) msifikiri ni
shari kwenu bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata
aliyoyachuma katika madhambi yao na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa (zaidi)
Kwa
nini mlipo sikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini
hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na ilivyo kuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Allaah ni waongo.
Na
lau kuwa si fadhila ya Allaah juu yenu na rehema yake katika dunia na
Aakhirah, bila ya shaka ingeli kupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale
mliyo jiingiza.
Mlipoupokea
(uwongo huo mkawa mnautangaza) kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa
vyenu msiyo yajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Allaah ni
kubwa.
Na kwa nini mlipo yasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhaanaka (Mola wetu) Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!?
Allaah anakuonyeni msirudi kabisa (msirejee tena) kufanya kama haya, ikiwa nyinyi ni Waumini! (Waislamu) kweli.”
(An Nur– 11-17)
Kwa hivyo atakaerudia kueneza uongo huo hatakuwa Muislamu tena.
Kuitukana dini
Yeyote
atakayeituhumu kuishambulia au kuitukana dini ya Allaah au kuwataka
watu wafuatae siasa ya kutoamini Mungu au kuwataka wakufuru basi anakuwa
Murtadi.
Allaah Anasema:-
"Na kama
wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu,
basi wapigeni vita viongozi wa ukafiri. Hakika viapo vyao havina maana
wauweni (piganeni nao) ili wapate kujizuia (na kufanya ubaya wao).”
(At - Tawba -12)
Kurtadi kwa matendo
Maulamaa
wote wa Kiislamu wamekubaliana kuwa; amefanya kitendo cha kurtadi
Muislamu yeyote atakayeutupa msahafu mahala panapotupwa taka, au
kuuchafua (kwa kukusudia) kwa kuumwagia taka, na pia kuvifanyia hivyo
vitabu vya Hadiyth za Al Qudsiy au vya Hadiyth za Mtume wa Allaah
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pia atakayeufanyia
dharau msahafu.
Allaah Anasema:-
"Na kama
ukiwauliza (kwa nini?) Wanasema; "Sisi tulikuwa tukizungumza zungumza
na kucheza tu, Sema; "Mlikuwa mkimfanyia mzaha Allaah na aya zake na
Mtume wake?".
At - Tawba -65
Wamekubaliana
Maulamaa kwamba Muislamu yeyote akilisujudia sanamu, jua au mwezi, au
akasema neno au kufanya kitendo kinachoonyesha wazi kuwa kaifanyia
istihizai dini, basi anakuwa ametoka katika dini ‘Amertadi’.
Muislamu
yeyote atakayekimbilia nchi ya makafiri wanaowapiga vita Waislamu na
akaungana nao katika kupigana vita hivyo dhidi ya Waislamu, basi kesha
kuwa kafiri, na hii ni kutokana na kauli ya Allaah isemayo:
"Na
miongoni mwenu atakayefanya urafiki huo nao, basi huyo atakuwa pamoja
nao. Hakika Allaah hawaongozi (njia ya kheri watu madhalimu)."
Al - Maidah -51
Muislamu
yeyote atakayeipiga vita sheria ya Kiislamu akaibadilisha kwa kanuni za
wanadamu kwa nia ya kuizuia sheria ya Kiislamu isitumike, basi amekuwa
kafiri.
Allaah Anasema:-
"Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah basi hao ndio makafiri".
Al - Maidah - 44
Hukmu ya mwenye kurtadi
Kutokana
na dalili zilizotangulia tunafahamu kuwa mwenye kurtadi akiwa na akili
timamu, damu yake inakuwa halali, na hukmu ya kuuliwa inatolewa na Imam
mwenye kuwahukumu Waislamu au msaidizi wake kama vile Qaadhi, na haoshwi, hasaliwi wala hazikwi katika makaburi ya Waislamu.
Hauliwi
hapo hapo, bali kwanza hutubishwa na kuonyeshwa dalili mbali mbali kuwa
kitendo chake hicho kinamtoa katika dini, hasa kwa vile huenda kitendo
chake hicho au kauli aliyotamka ilikuwa kwa kukisia tu au kwa jitihada
akidhani kuwa ndiyo haki inayofaa kufuatwa. Akaiendelea kuishikilia
kufru yake hiyo akakataa kuifuata haki, ndipo hukmu inapotendeka.
Anasema Ibn Qudaamah (Allaah amrehemu) katika Al Mughniy:
"Mwenye
kurtadi hauliwi mpaka Qadhi amtubishe muda wa siku tatu. Na hii ndiyo
kauli ya Maulamaa wengi akiwemo Umar na Ali na Atwaa na Al Nakhaiy na
Imaam Maalik na Ath-Thawry na Al-Awza'iy na Is-haaq na wengi kati ya
maulamaa wenye rai, kwa sababu kurtadi kwake huenda kukawa kwa dhana na
dhana kwa kawaida haiondoki mara moja. Kwa ajili hiyo inawajibika
kusubiri muda mrefu ili apate wakati wa kutosha kujirudi na kuitambua
haki."
Vipi aliyertadi anaweza kurudi katika Uislamu?
Aliyertadi
anaweza kurudi katika Uislamu kwa kutamka shahada mbili "Ash' hadu an
Laa ilaaha illa Llah wa Ash' hadu anna Muhammadan RasuwluLLaah." Ni
ikiwa kurtadi kwake kunatokana na kupinga jambo linalojulikana kuwa ni
la dharura katika dini, hakubaliwi mpaka kwanza akiri makosa yake na
alikubali jambo hilo."
Wa-Allaahu Ta'alaa A'lam
Post a Comment