HIZI NI DALILI NA ISHARA 50 ZA MFADHAIKO/STRESS


Hali ya mfadhaiko inasemwa kutokea wakati ubongo unapokabiliana na tatizo la mvurugiko wa akili na kujikuta ukishindwa kuendana na hali zingine zinazohitaji umakini kwa wakati mmoja. Jambo hili linaweza kuuteka ubongo na kudhoofisha uwezo wake. Hatimaye hali hii ya ufadhaikaji katika ubongo inaweza kutengeneza dalili tofauti ambazo zimepachikwa majina mengi kwa mjibu wa sampuli tabia za nje anazozionesha mtu.
Idadi kubwa zaidi ya watu wanazidi kupatwa au wanategemewa kupatwa na aina fulani fulani za mifadhaiko. Baadhi ya aina za mifadhaiko ni hali za asili katika hatua za maendeleo na kukua kwa mtu.
Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu uwezo wao ni mdogo kushughurika na woga, wasiwasi na hamaki zinazohusiana na mifadhaiko. Kwa bahati mbaya tena wanapotafuta msaada wa kitaaluma, wanapewa aina fulani za madawa.
Mfadhaiko huongeza utiririkaji wa asidi ndani ya tumbo. Utafiti uliofanywa katika miaka ya hivi karibuni umeonyesha kuwa akili hutumia sehemu kubwa ya nguvu ya mwili. Baadhi ya madaktari wamesema mfadhaiko huchangia sana katika kutokea kwa magonjwa mengi mwilini zaidi ya 50. !

Inaelezwa na wataalamu kwamba karibu asilimia 50 ya wafanyabiashara wote duniani wanasumbuliwa na maradhi ya kutoridhika, kufunga choo, vidonda vya tumbo na maradhi ya moyo. Na wafanyabiashara ambao hawajui namna ya kupambana na wasiwasi au mashaka hufa wakiwa vijana.
Wasiwasi na hofu ya maisha humfanya yeyote kuwa mgonjwa. Mvurugiko wa hisia una matokeo hasi katika afya ya mwili, pia wasiwasi na hofu ya maisha huweza kuleta magonjwa yanayoweza kuuwa kabisa sawa sawa na inavyotokea pia kwa magonjwa yale yatokanayo na lishe dhaifu. Baridi yabisi, maradhi ya moyo, tezi, kisukari, vidonda vya tumbo, kansa, yote yanaweza kusababishwa na mvurugiko wa mawazo.

Utafiti wa kisayansi unasema hisia zetu na hali zetu na jinsi tunavyomudu kudhibiti mifadhaiko inaweza kutusaidia kuelewa ni kwa kiwango gani afya zetu zilivyo madhubuti au zilivyo dhaifu.
Ingawa utafiti katika uwanja huu ni mpya, lakini utendaji kazi wa mfumo wa kinga ya maradhi ya mwili unaweza kukandamizwa na mfadhaiko wa akili au mawazo yatokanayo na shida za maisha.

Majaribio yaliyofanywa kwa watu wenye mifadhaiko sana kama wajane, watu wanaosumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu, watu waliopewa talaka na wale wenye kupambana na adui yalionesha kuwa watu hao huweza kupata maradhi mara kwa mara kutokana na mfumo wao wa kinga ya maradhi kugandamizwa.
Mfano katika kukabiliana na adui, akili hutambua hofu na ubongo hupata taarifa; neva zenye kujiendesha zenyewe hupanda juu ili kukutana na adui. 

Hapo moyo huenda mbio, msukumo wa damu nao hupanda na damu huvimba kwenye misuli kwa ajili ya maandalizi ya mapigano au makabiliano na adui.
Oksijeni na virutubishi vingine hukimbilia kwenye ubongo vikimfanya mtu awe tayari zaidi kwa mapigano, na hapo mnyunyizo wa adrenalini, homoni inayohusika na uzalishwaji wa nguvu mwilini huongezeka.
Kadri mfadhaiko unavyokuwa ni wa muda mfupi, ndivyo pia athari zake zinavyokuwa ni fupi. Lakini pindi mfadhaiko unapodumu kwa muda mrefu kama vile kipindi cha ndoa isiyo na amani au katika hali ya matatizo mengi kila mara, athari zake nazo hudumu kwa muda mrefu.

Dalili na Ishara 50 za Mfadhaiko
Zifuatazo ni dalili na ishara 50 za kuongezeka kwa mfadhaiko au stress katika mwili wako;
1. Kuumwa kichwa kila mara
2. Kusagika meno
3. Kushikwa na kigugumizi
4. Kuhamanika, Kutetemeka kwa mdomo na mikono
5. Maumivu ya shingo, Maumivu nyuma ya mgongo, Misuli kujikaza
6. Kuwa na mashakamashaka , kizunguzungu na wasiwasi usioisha
7. Kusikia sauti au mvumo katika masikio
8. Fadhaa na hasira za mara kwa mara, kutokwa na jasho bila kazi
9. Homa au jasho katika mikono na miguu
10. Mdomo kuwa mkavu na kupata shida katika kumeza chakula
11. Homa za mara kwa mara na maambukizi,
12. Upele, muwasho wa ngozi na mabaka mabaka katika ngozi
13. Shambulio la mzio/aleji lisiloweza kuelezewa la mara kwa mara
14. Kiungulia, maumivu ya tumbo na kujisikia uvivu
15. Hasira kupita kiasi na gesi kujaa tumboni
16. Kufunga choo, kuharisha na kupoteza uwezo wa kujidhibiti
17. Kupata shida katika kupumua na kupiga miayo mara kwa mara
18. Kupaniki kwa ghafla
19. Maumivu katika kifua, na moyo kwenda mbio
20. Kukojoa mara kwa mara
21. Kupungua hamu ya tendo la ndoa na ufanisi hafifu
22.Wasiwasi uliozidi, mashaka, kujiona na hatia na kutokutulia kwa neva
23. Kuongezeka kwa hamaki au pupa na kuchanganyikiwa
24. Majonzi na huzuni kuu
25. Kuongezeka au kupungua kwa hamu ya kula
26. Kukosa usingizi, kuota ndoto za kutisha na kukosa utulivu katika usingizi
27. Kukosa utulivu katika mawazo na maamuzi
28. Mgumu au mzito katika kujifunza jambo jipya
29. Kupoteza kumbukumbu au kusahausahau, kukosa mpangilio katika mambo yako mengi na kujisikia umevulugwa
30. Kuwa mgumu katika kufanya maamuzi
31. Kujisikia umezidiwa na kazi au mawazo
32. Kulia mara kwa mara ikiwemo mawazo ya kutaka kujiuwa
33. Kujisikia mpweke na usiye na thamani
34. Kupungua kujipenda na kuwa mchelewaji
35. Kuongezeka kwa fadhaa na mahangaiko ya akili
36. Kuzidi kukata tamaa
37. Kuhamaki na kujibu kwa nguvu nyingi hata katika maudhi madogo madogo tu
38. Kuongezeka kwa idadi ya ajali ndogo ndogo katika shughuli zako za kila siku (bahati mbaya nyingi)
39. Kuwa na tabia ya hofu iliyozidi
40. Kupungua kwa ufanisi au uzarishaji katika kazi zako
41. Kuongopa au kuomba msamaha kufunika kazi zako duni
42. Kuongea haraka haraka au kumumunya maneno
43. Kujitetea au kujilinda binafsi kulikozidi
44. Matatizo katika mawasiliano au kushirikiana na wengine
45. Kujitenga na jamii na kukaa peke yako
46. Kuendelea kujisikia uchovu na udhaifu
47. Matumizi ya mara kwa mara ya dawa za kutuliza maumivu
48. Kuongezeka uzito au kupungua uzito bila kupunguza chakula i.e diet
49. Kuongezeka kwa uvutaji wa sigara, unywaji pombe au matumizi ya madawa ya kulevya
50. Kupenda vitu vya kubahatishabahatisha au kamari
Katika kujidhibiti au kujitibu na mfadhaiko au stress jambo la kwanza ni kutambua nini chanzo cha huo mfadhaiko wako, ukishapata kujuwa chanzo ni rahisi kupata suluhisho kwa haraka.
Tambuwa kuwa kila mtu ana matatizo na kila mtu hufeli katika mipango yake na kila mtu hupata hasara.

Tofauti ni kwamba wakati baadhi ya watu wanaweza kumudu kudhibiti mvurugiko wa mawazo, wengine hawajui kabisa nini cha kufanya na matokeo yake hupatwa na mfadhaiko ambao huweza kusababisha maradhi mengi mwilini bila idadi.
Kama utakubali kuyapokea maisha kama yanavyokuja, ukaacha kuyakopa maisha ya jana na ukaacha kuhofu maisha ya kesho, ni hakika kabisa utaweza kujidhibiti kupatwa na mfadhaiko.
Mengine unayoweza kuyafanya ni pamoja na kunywa maji ya kutosha kila siku, kuacha kabisa vilevi vya aina yote mara tu unapojihisi umefadhaishwa au una stress nyingi, usikae mpweke hata mara moja, fanya mazoezi kila siku, mazoezi ni dawa au tiba mhimu sana kwa mfadhaiko na mhimu kuliko yote ni kutokukaa kimya juu ya tatizo linalokusibu.
Kuna watu wakipatwa na matatizo huyaficha kimya na kuendelea kuumia ndani kwa ndani peke yao, hii ni tabia mbaya sana kiafya, unapopatwa na tatizo jaribu kutafuta mtu au watu unaowaamini na uwaeleze tatizo lako hata kama hawatakusaidia moja kwa moja lakini mawazo na ushauri wao tu vinaweza kuwa ni dawa tosha ya mfadhaiko au stress yako............."
Jifunze jambo hapo

0 Comments