HUKMU YA KUWA NA RAFIKI MWANAMUME (BOYFRIEND)

SWALI:
Assalam alaikum warahmatullahi wabarakatuh, nataka kuuliza kama kuwa na boy frend inaitikiwa katika dini ya islam,na nataka niwe na dalili ayat ama hadith.
          
wahadha assalam alaikum,kazi njema
 
 

 
JIBU:
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
Tunamshukuru dada yetu kuuliza Swali muhimu kama hili ambalo linahitajika kujibiwa na kuelimisha ndugu zetu makatazo hayo ambayo sasa imekuwa kama ni jambo la kawaida katika jamii zetu na hali sio kutokana na mafunzo ya dini yetu.
 
Ayaah na dalili za kukataza jambo hili zipo nyingi zikiwa zinazoashiria makatazo moja kwa moja (directly) na nyinginezo zenye uhusiano na makatazo haya. Kuwa na boyfriend bila shaka kutasababisha yatendeke maasi baina ya mwanamke na mwanamume kwani shaytwaan huwa pamoja nao akiwachochea kuingia katika kumuasi Mola wao:
 
 
عن عمر رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم : ((ما خلا رجل بامرأة إلا كان الشيطان ثالثهما)) الترمذي
 
Kutoka kwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila shaytwaan huwa ni watatu wao)) [At-Tirmidhiy]
 
 
Ndio maana pia Mtume ((Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameonya kukaa faraagha mwanamke na mwanamume:
 
قال صلىالله عليه سلم : ((لا يخلوّنّ أحدكم بامرأةإلا مع ذى محرم)) متفق عليه
 
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hawi faraagha mmoja wenu pamoja na mwanamke ila awepo Mahram wake)) [Al-Bukhaariy Na Muslim]
 
 
Matokeo yake ni shaytwaan kuwafikisha kuingia katika maasi ya zinaa na ndio maana sheria ya Kiislamu haikuruhusu jambo hilo au kufunga uchumba inavyojulikana engagement. Bali inatakiwa kufunga ndoa moja kwa moja baada ya kuwafikiana pande zote. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
 
 
((وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الْمُؤْمِنَاتِ وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ الَّذِينَأُوتُواْ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّمُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ وَلاَ مُتَّخِذِي أَخْدَانٍ وَمَنيَكْفُرْ بِالإِيمَانِ فَقَدْ حَبِطَ عَمَلُهُ وَهُوَ فِي الآخِرَةِ مِنَالْخَاسِرِين))
 
((Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa waliopewa Kitabu kabla yenu, mtakapowapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uasharati wala kuwaweka kinyumba. Na anayekataa kuamini bila shaka amali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye khasara)) [Al-Maaidah: 5].
 
 
Hizo ni mila za kikafiri ambazo zinapasa tuepukano nazo na ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametuonya:
 
 ((وَلَن تَرْضَى عَنكَ الْيَهُودُ وَلاَ النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُم))
((Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao)) [Al-Baqarah: 120].
 
 
Msichana wa Kiislamu unapokabiliwa na mvulana kutaka kufanya urafiki ujiepushe kabisa bali umshauri kwanza awasiliane na wazazi wako na baada ya kumjua kuwa ni mtu mwenye dini na tabia nzuri basi wazazi wasichelewa kukuozesha nawe uridhike kwani hivyo ndivyo ipasavyo na tulivyopewa mafunzo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) :
 
((إِذَا خَطَبَ إِلَيْكُمْمَنْ تَرْضَوْنَ دِينَهُ وَخُلُقَهُ فَزَوِّجُوهُ إِلَّا تَفْعَلُوا تَكُنْ فِتْنَةٌفِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ عَرِيضٌ))   رواهالترمذي   وقال الألباني : حسن
 
((Atakapoposa kwenu yule mtakaeridhika na dini yake, na tabia yake, basi muozesheni, kwani kutokufanya hivyo itakuwa fitna katika ardhi (duniani) na ufisadi mpana (mkubwa) )) [At-Tirmidhiy kasimulia na Shaykh Albaaniy amesema ni Hadiyth Hasan].
 
 
Tunatumai dada yetu na wengine wote wataridhika na mafunzo ya dini yetu ili wabakie wote katika usalama, stara na Ridhaa ya Mola wetu. 
 
 
Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments