HUKUMU YA KUBADILI MAUMBILE AU KURUDISHA BIKRA

SWALI:
 KWA MWANAMKE; ANARUHUSIWA KUTUMIA DAWA ZA KURUDISHA BIKIRA? AMA KUYARUDISHA MATITI YAWEZE KUSIMAMA?  KWA MWANAUME; ANARUHUSIWA KUTUMIA DAWA ZA KUONGEZA NGUVU ZA KIUME? AMA KUUREFUSHA UUME? AMA KUUNENEPESHA UUME? NA JE NI KWELI KUWA DAWA HIZO ZIPO?
 JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.

Kila mmoja wetu anafaa ajiulize mwanamke anataka kuurudisha ubikira wake kwa sababu gani? Katika jamii zetu mwanamke hutaka kufanya hivyo kwa sababu alitembea nje na ubikira ukawa ni wenye kuondoka. Inapokuwa hivyo nawe unataka kumuonyesha yule anayetaka kukuoa kuwa wewe bado ni bikra utakuwa umedanganya na hivyo kufanya makosa makubwa sana katika Dini. Ikiwa umeolewa na ubikira ukaondolewa kwa kuingiwa na mumeo haina haja tena ya kurudisha ubikira. Hivyo, kwa hali yoyote wakati ubikira ukiondoka haifai kwa mwanamke kuurudisha kwa kutumia dawa. Kisha mara nyingi hizi dawa za kemikali huwa zina madhara makubwa kwa mwenye kutumia.

Mas-ala ya kurudisha matiti yawe yatasimama utakuwa unashindana na maumbile ya Alalah (Subhaanahu wa Ta'ala),
Ambaye Ameonya:

  (( ...وَقَالَ لَأَتَّخِذَنَّ مِنْ عِبَادِكَ نَصِيبًا مَّفْرُوضًا ))  ((وَلأُضِلَّنَّهُمْ وَلأُمَنِّيَنَّهُمْ وَلآمُرَنَّهُمْ فَلَيُبَتِّكُنَّ آذَانَ الأَنْعَامِ وَلآمُرَنَّهُمْ فَلَيُغَيِّرُنَّ خَلْقَ اللّهِ وَمَن يَتَّخِذِ الشَّيْطَانَ وَلِيًّا مِّن دُونِ اللّهِ فَقَدْ خَسِرَ خُسْرَانًا مُّبِينًا))  (( يَعِدُهُمْ وَيُمَنِّيهِمْ وَمَا يَعِدُهُمُ الشَّيْطَانُ إِلاَّ غُرُورًا ))   (( أُوْلَئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَلاَ يَجِدُونَ عَنْهَا مَحِيصًا)) 

((Naye Shaytwaan alisema: Kwa yakini nitawachukua sehemu maalumu katika waja wako))  ((Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili Aliyoumba Allaah. Na mwenye kumfanya Shaytwaan kuwa ni mlinzi wake badala ya Allaah basi huyo amekhasiri khasara ya dhaahiri)).   ((Anawaahidi na anawatia tamaa. Na Shaytwaan hawaahidi ila udanganyifu))   ((Hao makao yao ni Jahannamu, na wala hawapati makimbilio kutoka humo))  [An-Nisaa 4:118-121]


Ni hali ya kimaumbile kuwa kila umri ukizidi kuwa mkubwa matiti huwa yanaanguka. Na kurudisha matiti inabidi kufanyiwa upasuaji au kutumia dawa na hizo zinakuwa na madhara kwa mwanaadamu. Na katika Uislamu haifai kujidhuru au kumdhuru mwengine. Ikiwa unayo magonjwa ambayo dawa yake ni kufanya hivyo hayo yatakuwa ni mas-ala mengine, kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Allaah Hakuleta magonjwa isipokuwa Ameleta na dawa yake” (Ahmad, Muslim na an-Nasaaiy).

Mas-ala ya dawa nyingi ambazo zipo madukani kama viagra na kadhalika zina madhara makubwa kwa mwanamume hasa akiwa bado ni kijana au barobaro kwani huwa zikiua kabisa maume. Hizi zinaweza kutumiwa na wale ambao umri wao ni mkubwa, wazee ambao kwa sababu ya uzee wao utupu wao huwa hausimami au huwa wanamaliza mara moja haja zao wanapokutana na wake zao. Vijana wengi huathirika na kupoteza nguvu maume yao kwa sababu ya kuangalia filamu za ngono au picha au kuangalia wanawake barabarani kwa matamanio. Hivyo, ikiwa kila mara kijana atakuwa akitoa manii ule uume huwa unazorota mpaka unakuwa hauna nguvu tena. Kupiga punyeto ni sababu nyingine kubwa yenye kudhoofisha maume.

Ni nasaha zetu kuwa mwanamume akiwa angali kijana asiwe ni mwenye kutumia dawa hizi kwani angali ana nguvu na inabidi ajitahidi anapokutana na mkewe apandishe ashiki kwa kumbusu, kuzungumza maneno matamu, kumshika shika sehemu nyeti na vitangulizi vya mapenzi kabla ya kumuingilia mkewe ili kila mmoja apate raha. Ikiwa mtu hana budi atumie dawa basi atumie dawa za miti kama hawlinjaan ambayo inatiwa katika maziwa nusu saa kabla ya kitendo cha ngono. Hii dawa inasaidia na haina madhara kwa mwili.

Kila mmoja ana urefu na upana wa uume wake ambao unamtosha katika shughuli ambayo imeumbiwa kwayo. Kurefusha na kuunenepesha uume ni katika kubadilisha maumbile ya Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) jambo ambalo limekatazwa katika sheria ya Kiislamu kama tulivyotaja katika hiyo Aayah ya juu.

Ama kuhusu dawa hizo huwa zinapatikana kwa matabibu hawa katika miji yetu ya Afrika Mashariki na hasa mwambao wa Pwani.

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments