Imaam Al-Albaaniy:
Je, kusherehekea Maulidi ya Nabiy ni khayr au shari?
Anayejadiliana na Imaam:
Ni khayr.
Imaam Al-Albaaniy:
Sawa. Lakini je,
kwani khayr hii Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) na Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) walikuwa hawaijui?
Anayejadiliana na Imaam:
Hapana!
Imaam Al-Albaaniy:
Sijaridhika na jibu
lako hilo la “hapana,” bali unawajibika kuendelea kusema: “Haiwezekani
kwamba ‘khayr’ hii (ya kusherehekea Maulidi), ikiwa ni khayr au
vinginevyo, kuwa ifichike na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum), na hali
sisi hatuujui Uislamu na Iymaan isipokuwa kutoka kwa Muhammad (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Basi vipi tuijue sisi hiyo ‘khayr’
ambayo yeye (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuijua! Haliwezekani hili!
Anayejadiliana na Imaam:
Kusimamisha Maulidi ni kuhuisha kumbukumbu zake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuheshimu.
Imaam Al-Albaaniy:
Falsafa hii
tunaijua sisi, tunaisikia kutoka kwa watu wengi na tumeisoma katika
vitabu vyao. Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) alipowalingania watu, je, aliwalingania katika Uislamu wote
au aliwalingania katika Tawhiyd? (kumpwekesha Allaah).
Anayejadiliana na Imaam:
At-Tawhiyd.
Imaam Al-Albaaniy:
Jambo la kwanza
alilowalingania ni Tawhiyd. Kisha ikafaridhishwa Swalaah. Kisha Swiyaam
(funga ya Ramadhwaan), kisha ikafaradhishwa Hajj, na hivyo ndivyo
ilivyokuwa. Basi nawe fuatia katika Sunnah hii ya Shariy’ah hatua kwa
hatua.
Tumekubaliana sasa
kuwa haiwezekani kwamba kuna ‘khayr’ ambayo hakuijua Rasuli wa Allaah
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kwani ‘khayr’ zote
tumezijua kupitia kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam) na uhakika huu hakuna wawili wanaoupinga wala hakuna kondoo
wawili watakaopigana kwa pembe zao juu ya hili, na naitakidi kwamba
yeyote atakayetilia shaka hili basi yeye si Muislamu. Na miongoni mwa
Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
inayounga mkono kauli hii ni kauli yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam):
مَا تَرَكْتُ شَيْئًا يُقَرِّبُكُم إلى اللهِ إلَّا وَأَمَرْتُكُم بِهِ
“Sikuacha jambo lolote linalokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni kwalo.” [Atw-Twabaraaniy Isnaad yake ni Swahiyh. Rejea Swiffatu-Swalatin-Nabiy (3/942) ya Imaam Al-Albaaniy]
Basi ingelikuwa
Maulidi ni ‘khayr’ na ingekuwa ni jambo linalotukurubisha kwa Allaah
basi ingebidi Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) atuelekeze nayo. Sawa au si sawa?
Mimi sitaki
ukubaliane nami bila ya kukinaika kila herufi ninayotamka. Una uhuru
kamili useme: “Tafadhali nukta hii sikukinaika nayo!”
Je, basi kuna lolote ambalo hukuridhika nalo nami au uko pamoja nami?
Anayejadiliana na Imaam:
Pamoja na wewe tamaam!
Imaam Al-Albaaniy:
Jazaaka Allaahu khayraa. Kwa hiyo ikiwa (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:
“Sikuacha jambo linalokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni kwalo.”
Sisi tunawaambia
wote wanaosema kuwa inafaa kusimamisha Maulidi: Maulidi haya ni ‘khayr’
kwa madai yenu. Basi ima Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) ametuelekeza kusherehekea Maulidi au hakutuelekeza
nayo.
Wakijibu kuwa “Ametuelekeza kusherehekea Maulidi,” tunawaambia:
هَاتُوا بُرْهَانَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٦٤﴾
“Leteni ushahidi wenu wa wazi mkiwa ni wakweli [An-Naml: 64]
Na wala hawatoweza kamwe kuipatia njia (dalili hiyo).
Nasi tumesoma
vitabu vya 'Alawiy na vinginevyo visivyokuwa vya 'Alawi kuhusu Maulidi,
na wala hawatumii dalili isipokuwa kusema tu kuwa “Maulidi ni bid’ah
hasanah, bid’ah hasanah! (uzushi mzuri!).”
Basi wote
wanaosherehekea Maulidi au wanaopinga sherehe hii wanakubaliana kwamba
Maulidi haya hayakuweko katika zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) wala zama za Maswahaba watukufu wala zama
za Maimaam Wanachuoni.
Lakini
wanaojuzisha sherehe hii ya Maulidi husema: “Kwani kuna nini Maulidi na
hali anatajwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) na kumswalia na kadhaalika.”
Sisi tunasema: Ingelikuwa ni ‘khayr’ wangetutangulia kwa hayo (Maulidi).
Wewe unaijua Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
خَيْرُ النَّاسِ قَرْنِي، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ
“Watu bora kabisa ni karne yangu, kisha wanaowafuatia kisha wanawafuatia.”
nayo imo katika Asw-Swahihayn [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na
karne ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
ndio ambayo wameishi humo Maswahaba, kisha waliowafuatia ambao ni
At-Taabi’uwna, kisha ambao wamewafuatia nao ni Atbaa’ut-Taabi’iyna. Na
hili pia hakuna kukhitilafiana kwalo.
Je, basi mnadhani kuwa kuna ‘khayr’ yoyote ambayo imewapita, katika yote mawili; elimu na ‘amali? Inawezekana hilo?
Anayejadiliana na Imaam:
Ama
kuhusu elimu, ingelikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) amemwambia yeyote katika zama zake kwamba “dunia
inazunguka…”
Imaam Al-Albaaniy:
Samahani!
Nakuomba usipindishe maneno. Kwa vile nimekuuliza kuhusu mambo mawili;
elimu na ‘amali. Na kwa hakika kupindisha kwako kumeninufaisha kwani
mimi ninavyokusudia elimu, huwa nakusudia elimu ya Dini (shariy’ah) si
ya utabibu. Mfano naweza kusema kuwa: “Daktari huyu ana ujuzi zaidi kuliko Ibn Siynaa katika zama zake kwa sababu (daktari huyu) ametokea
katika karne za baadaye, na amefanya majaribio mengi mno ya uzoefu.”
Lakini hii haina maana kuwa anasifika mbele ya Allaah wala haimtangulizi
mbele ya karne zilizoshuhudiwa (katika Hadiyth ya juu kuhusu watu bora
kabisa). Lakini anasifika katika elimu aliyoisomea na sisi tunazungumzia
kuhusu elimu ya shariy’ah, baaraka Allaah fiyka. Basi unapaswa
utanabahi kwa haya. Kwa hiyo ninapokuambia: “Je, unadhania kuwa tunaweza
kuwa ni wajuzi zaidi?” Nikimaanisha ni elimu ya shariy’ah na si elimu
ya majaribio kama jiografia au falaki au kemia au fizikia. Na
chukulia mfano zama hizi; mtu amemkufuru Allaah na Rasuli Wake (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) lakini yeye ni mjuzi kabisa katika
watu kwa elimu yake katika sayansi hii, je basi hiyo elimu yake
itampelekea kuwa karibu na Allaah?
Anayejadiliana na Imaam:
Hapana.
Imaam Al-Albaaniy:
Kwa hiyo sisi
hatuzungumzii elimu katika fani hizo, bali tunazungumiza elimu
inayotukurubisha kwa Allaah (Tabaaraka wa Ta’aalaa). Na hapo nyuma
kidogo tumezungumza kuhusu kusherehekea Maulidi. Basi swali linarudi
sasa na nataraji kuwa nitapata jibu la wazi bila ya kupindisha tena.
Basi nauliza: “Je unaitakidi kwa akili na fahamu uliyopewa kwamba
inawezekana sisi katika zama hizi tuwe wajuzi zaidi kuliko Maswahaba na
At-Taabi’iyna (Waliofuatia) na Maimaam waliofanya
juhudi katika elimu ya shariy-‘ah, na kwamba sisi tuwe ndio wepesi
zaidi katika kufanya ya khayr ya kujikuribisha kwa Allaah kuliko hao
Salafus-Swaalih (wema waliotangulia)?
Anayejadiliana na Imaam:
Unaposema “elimu ya shariy’ah” je, unakusudia elimu ya kufasiri Qur-aan?
Imaam Al-Albaaniy:
Wao wana elimu
zaidi kuliko sisi katika kufasiri Qur-aan, na wana elimu zaidi kuliko
sisi katika kufafanua Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam), na mwisho wana elimu zaidi kuliko sisi
katika Shariy’ah nzima ya Kiislamu.
Anayejadiliana na Imaam:
Kuhusu Tafsiyr ya
Qur-aan, labda kwa sasa ni zaidi kuliko zama za Rasuli wa Allaah (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mfano Aayah katika Qur-aan:
وَتَرَى
الْجِبَالَ تَحْسَبُهَا جَامِدَةً وَهِيَ تَمُرُّ مَرَّ السَّحَابِ ۚ
صُنْعَ اللَّـهِ الَّذِي أَتْقَنَ كُلَّ شَيْءٍ ۚ إِنَّهُ خَبِيرٌ بِمَا
تَفْعَلُونَ ﴿٨٨﴾
Na
utaona majabali ukiyadhania yametulia thabiti nayo yanapita mpito wa
mawingu. Utengenezaji wa Allaah Ambaye Ametengeneza kwa umahiri kila
kitu. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliyodhahiri na yaliyofichikana kwa yale myafanyayo. [An-Naml: 88]
Basi ingelikuwa
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema
katika zama zake kwamba “ardhi inazunguka”, je, hivi ataamini yeyote?
Hakuna ambaye angeamini!
Imaam Al-Albaaniy:
Hivyo wewe
unatutaka sisi – na nasema haya bila ya kukulaumu – kurekodi dhidi yako
kupindisha kwako tena maneno? Ee ndugu yangu! Mimi nauliza kwa ujumla na
si sehemu tu ya swali! Sisi tunauliza swali la ujumla. Nani wenye ujuzi zaidi kuhusu Uislamu kwa ujumla?
Anayejadiliana na Imaam:
Bila shaka ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake.
Imaam Al-Albaaniy:
Hivi ndivyo tunavyotaka kwako baaraka Allaahu fiyka.
Ama kuhusu Tafsiyr
unayoihojia, haina uhusiano na ‘amali, bali ina uhusiano na kutafakari
na kufahamu. Kisha tulishazungumza nawe kuhusu Aayah iliyopitia na na
tumekuthibitishia kwamba wale wanaonukuu Aayah hii kuwa ni dalili kwamba
dunia inazunguka wamekosea kwa sababu Aayaah inakusudia Siku ya
Qiyaamah:
يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ ﴿٤٨﴾
48.
Siku ardhi itakapobadilishwa kuwa ardhi nyingine na mbingu pia na
(viumbe wote) watahudhuria kwa Allaah Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na
kudhalilisha, Asiyepingika.” [Ibraahiym: 48]
Hata hivyo, sisi hatuko katika maudhui haya.
Nami kwa
kukubaliana nawe kimjadala, basi huenda akaweko mtu katika wale
waliokuja mwishoni ambaye ana utaalamu wa sayansi au utaalamu wa
ki-ulimwengu kuliko Swahaba au Taabi’iy (mwanafunzi wa Swahaba) na
kuendelea. Lakini haya hayana uhusiano na ‘amali njema. Kwa sababu mfano
leo, makafiri wana utaalamu zaidi ya falaki na aina zake, lakini je,
wananufaika nini kwayo? (kuhusiana na Allaah?) Si lolote! Basi sisi
hatutaki sasa kutumbukia katika haya. Tunataka kuzungumzia kila jambo
litakalotukurubisha kwa Allaah. Basi sisi sasa tunataka tuzungumzie
kuhusu Maulidi ya Nabiy Mtukufu.
Na tumeshakubaliana
kwamba kama ingelikuwa ni ‘khayr’, basi bila shaka Salafus-Swaalih
(wema waliotangulia) na kiongozi wao ni Rasuli wa Allaah (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wangekuwa na ujuzi nao zaidi kuliko
sisi na wepesi zaidi kuyatenda kuliko sisi. Je, una shaka na hili?
Anayejadiliana na Imaam:
Hapana, hapana hakuna shaka kwa hilo!
Imaam Al-Albaaniy:
Basi usivuke mipaka
ukachanganya haya na mambo ya elimu ya majaribio, kwani hayana uhusiano
nayo katika kukurubisha kwa Allaah kwa ‘amali njema.
Maulidi hayakuweko
zama za Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa
kukubaliana sote. Kwa maana ‘khayr’ hii haikuweko zama za Rasuli wa
Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba na
At-Taabi’iyn na Maimaam Mujtahidiyn. Vipi basi imefichika ‘khayr’ hii
kwao?
Hakuna budi ila tuseme mojawapo kati ya mawili:
Waliijua ‘khayr’ hii kama tunavyoijua sisi; nao ni wajuzi zaidi yetu. Au hawakuijua. Sasa vipi basi sisi tumeijua?
Tukisema: Waliijua
‘khayr’ hii, na hii ni kauli iliyo karibu zaidi na bora zaidi kwa wale
wanaosema Maulidi yanajuzu kusherehekewa, basi kwanini hawakuyafanyia
kazi? Je, sisi tuko karibu zaidi kwa Allaah (kuliko wao)?
Kwanini asikosee
mmoja wao hata mara moja; Swahaba au Taabi’iy au Mwanachuoni miongoni
mwao au mfanya ‘ibaadah mno miongoni mwao (kwanini wasikosee)
wakaifanyia kazi ‘khayr’ hii?
Je, inaingia akilini mwako kwamba ‘khayr’ hii haikufanywa kamwe na yeyote yule? Nao walikuwa ni mamilioni na ni wajuzi zaidi kuliko sisi na wema zaidi kuliko sisi na wako karibu zaidi na Allaah?
Hivyo wewe unajua kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
لاَ تَسُبُّوا أَصْحَابِي؛ فَإِنَّ أَحَدَكُمْ لَوْ أَنْفَقَ مِثْلَ أُحُدٍ ذَهَبًا مَا أَدْرَكَ مُدَّ أَحَدِهِمْ وَلاَ نَصِيفَهُ
“Msiwatukane
Swahaaba wangu. Ninaapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake,
hata mmoja wenu atajitolea katika njia ya Allaah kugawa dhahabu ukubwa
wake mfano wa jabali Uhud, basi hatofikia gao lao wala hata nusu ya gao
lao.“ [Al-Bukhaariy, Muslim]
Je, unaona upeo wa tofauti baina yetu na wao?
Kwa sababu wao
wamefanya Jihaad katika njia ya Allaah (Ta’aalaa) pamoja na Rasuli wa
Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wakapokea elimu
ikiwa mbichi safi mpya kutoka kwake moja kwa moja, bila ya kuwa kiungo
kirefu baina yetu na baina yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
Kama alivyoashiria (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) maana hiyo katika Hadiyth Swahiyh:
((مَنْ أَحَبَّ أنْ يَقْرَأَ القرآنَ غَضًّا طَرِيًّا؛ فَلْيَقْرَأْهُ على قراءةِ ابنِ أمِّ عَبْدٍ)) يعني عبد الله بن مسعود
“Anayependa kuisoma Qur-aan mbichi safi mpya basi asome kwa Qiraa cha Ibn Ummi ‘Abd” (Yaani ‘Abdullaah bin Mas’uwd) [As-Silsilah Asw-Swahiyhah (5/379)].
Hawa
Salafus-Swaalih (wema waliotangulia) na viongozi wao Maswahaba (Radhwiya
Allaahu ‘anhum), haiwezekani sisi tuwadhanie kuwa hawakujua ‘khayr’
iliyowakurubisha kwa Allaah, na kwamba sisi ndio tuliyoijua ‘khayr’
hiyo! Na kama tukisema kuwa waliijua kama tunavyoijua basi ni mustahili kwetu kufikiria kuwa wameipuuza ‘khayr’ hiyo.
Huenda haya yamekuwekea wazi nukta ninayoizungumzia In Shaa Allaah?
Anayejadiliana na Imaam:
AlhamduliLLaah.
Imaam Al-Albaaniy:
Jazaaka Allaahu khayraa.
Kuna jambo jengine.
Kuna Aayah na Hadiyth nyingi zinazobainisha kuwa Uislamu umekamilika.
Na nadhani kuwa ukweli huu wewe unautambua na unaamini na hakuna tofauti
baina ya ‘Aalim na Twaalibul-‘Ilm (mwanafunzi) na mtu wa kawaida asiye
msomi kuhusu kujua uhakika huu. Nao ni, Uislamu umekamilika na si kama
dini ya ki-Yahudi au ki-Naswara kila siku kuna mageuzo na mabadiliko.
Na nakukumbusha mfano kauli ya Allaah (Ta'aalaa):
الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الْإِسْلَامَ دِينًا
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu na Nimekutimzieni Neema Zangu kwenu na Nimekuridhieni Uislamu kuwa ni Dini yenu)) [Al-Maaidah 5: 3]
Na
sasa linakuja swali, nalo ni njia nyingine ya kubainisha kwamba
kusherehekea Maulidi si jambo la khayr, hii mbali na yaliyotangulia
kwamba ingelikuwa ni ‘khayr’ basi wangelitutangulia wao yaani:
Salafus-Swaalih; walio na elimu zaidi yetu na wenye kufanya ‘ibaadah zaidi yetu.
Maulidi haya ya
Nabiy ingelikuwa ni ‘khayr’ basi ni katika Uislamu. Tunasema: Je, hivi
sisi sote tunaopinga kusimamisha Maulidi na wenye kuyajuzisha, je, sote
tunakubaliana kama tulivyokubaliana nukta iliyotangulia kwamba sherehe
hii haikuweko zama za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam)? Je, tuko bado katika kukubaliana huku (nukta hii ya pili?)
kwamba sherehe hii, kama ni ‘khayr’ basi imo katika Uislamu na ikiwa si
‘khayr’ basi haimo katika Uislamu? Na siku ambayo Aayah hii imeteremshwa:
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu…
Siku iliyoteremshwa hakukuwa na sherehe ya Maulidi ya Nabiy. Kwa hiyo je, imo katika Dini katika uoni wako?
Tafadhali uwe mkweli nami. Wala usidhani kuwa mimi ni miongoni mwa Mashaykh wanaonyamazisha wanafunzi, bali hata watu wa kawaida kwa kuwaambia: “Nyamaza! Hujui! Huna elimu!” Hapana wewe uko na uhuru kamili kama kwamba unaongea na mtu kama wewe au chini yako kwa umri na elimu. Ikiwa hukukinaika sema: “Sikukinaika.”
Hivyo
sasa, ikiwa Maulidi ni ‘khayr’ basi hayo ni katika Uislamu, na ikiwa si
ya khayr basi sio katika Uislamu. Na tukikubalilana kwamba kusherehekea
Maulidi hayakuweko pindi ilipoteremshwa Ayaah iliyotangulia, basi ni mantiki kusema kuwa si katika Uislamu.
Na nitathibitisha nnayoyasema kwa aliyoyasema Imaam wa makazi ya hijrah (Madiynah) Imaam Maalik bin Anas ambaye amesema:
“Atakayezusha bid’ah katika Uislamu…” (Tanabahi amesema: “bid’ah moja” wala hakusema bid’ah nyingi!) “…kisha
akaiona kuwa ni nzuri basi amedai kuwa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) amekhini risaalah (ujumbe).”
Na hili ni jambo khatari mno! Nini dalili ee Imaam (Maalik)?
Akasema Imaam Maalik: “Someni mkipenda kauli ya Allaah (Ta’aalaa):
لْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمْ الْإِسْلَامَ دِينًا
Leo Nimekukamilishieni Dini yenu na Nimekutimzieni Neema Zangu kwenu na Nimekuridhieni Uislamu kuwa ni Diyn yenu)) [Al-Maaidah (5: 3]
"فمالم يكن يومئذٍ ديناً ؛ فلا يكون اليوم ديناً".
“Basi ambayo hayakuwa ni Dini siku hizo, hayawezi kuwa ni Dini leo.” (mwisho wa maneno yake Imaam Maalik)
Je,
alisema lini haya Imaam Maalik? (Alisema) Katika karne ya pili baada ya
hijrah ambayo ni mojawapo wa karne zilizoshuhudiwa kuwa ni karne bora.
Sasa itakuwaje basi ikiwa ni karne ya kumi na nne (tuliyonayo sasa?)
Maneno
haya (ya Imaam Maalik) yanapasa kuandikwa kwa dhahabu, lakini sisi
tumeghafilika na kitabu cha Allaah (Ta’aalaa) na Hadiyth za Rasuli wa
Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kauli za Maimaam
ambao tunadai kuwa tunawafuata. Mbali kabisa mbali kabisa! Na tofauti
baina yetu na wao katika kufuata ni kama tofauti ya Mashariki na
Magharibi.
Huyo
(Imaam Maalik) ni Imaam wa mji wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) alipohajiri (Madiynah). Anasema kwa lugha
safi sahihi kabisa ya Kiarabu: “Basi ambayo hayakuwa ni Dini siku hizo, hayawezi kuwa ni Dini leo.”
Leo
kusherehekea mazazi ya Nabiy ni ya Dini na ingekuwa si hivyo, basi
mjadala huu usingejiri baina ya ‘Ulamaa wanaoshikamana na Sunnah na
kuihami (Dini) dhidi ya bid’ah. Itakuwaje yawe (Maulidi) katika Dini
wakati hayakuweko wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) wala zama za Maswahaba wala zama za Taabi’iyna
(waliofuatia Maswahaba) wala Taabi’iy Taabi’iyna (Waliofuatia baada ya
Taabi’iyn)?
Imaam Maalik ni katika Atbaa’ut-Taabi’iyn na ni miongoni mwa waliotajwa katika Hadiyth:
((خَيْرُ النَّاسِ قَرْنِي ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ)) متفق عليه
((Watu bora kabisa ni wa karne yangu, kisha ambao wanafuatia kisha ambao wanafuatia)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Imaam Maalik amesema: “Basi ambayo hayakuwa ni Dini siku hizo, hayawezi kuwa ni Dini leo, na ummah wa mwisho hautatengemaa isipokuwa kwa kile kilichofanya ummah wa kwanza kutengamaa.”
Je,
ummah wa mwanzo kabisa ulitengamaa (ulikaa sawa) kwa nini? Kwa kuzusha
mapya katika Dini kwa kujikurubisha kwa Allaah (Ta’aalaa) mambo ambayo
hakujikurubisha nayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam)?
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe ndiye aliyesema:
ما تَرَكْتُ شيئاً يُقَرِّبُكُمْ إِلَى اللهِ إلى وأَمَرْتُكُمْ به
“Sijaacha lolote litakalokukurubisheni kwa Allaah isipokuwa nimekuamrisheni kwalo.”
Kwanini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakutuamrisha tusherehekee Maulidi yake? Swali hili lina jawabu:
Kuna sherehe ya kusherehekea Maulidi ya Nabiy yaliyowekewa shariy’ah kinyume
na hizi sherehe za Maulidi haya (mnayoyafanya) ambayo hayakuamrishwa.
Sherehe hii iliyoamrishwa ilikuweko zama za Rasuli wa Allaah (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), kinyume na yaliyokuwa
hayakuamrishwa yakiwa na tofauti kubwa kabisa iliyoko baina ya sherehe
mbili (hizi).
Tofauti ya kwanza: Ni kwamba sherehe iliyoamrishwa (tutaitaja) ni ‘ibaadah ambayo wamekubaliana Waislamu wote.
Tofauti
ya pili: Sherehe iliyoamrishwa inakariri kila wiki mara moja, lakini
hiyo yao ambayo haikuamrishwa inatokea mara moja tu kwa mwaka.
Hizi
ni tofauti mbili baina ya sherehe mbili hizo. Kwamba ya kwanza ni
‘ibaadah, na inakariri kila wiki mara moja, kinyume na ya pili ambayo si
ya kishariy'ah na si ‘ibaadah na wala haikariri kila wiki!
Na
mimi sizungumzi kwa matamanio yangu ambayo Allaah Hakuteremshia dalili,
bali nakutoleeni dalili kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo imehadithiwa katika Swahiyh Muslim
(Rahimahu Allaah):
عنْ
أَبِي قَتَادَةَ الْأَنْصَارِيِّ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ
اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ سُئِلَ عَنْ صَوْمِ
الِاثْنَيْنِ فَقَالَ: ((فِيهِ وُلِدْتُ وَفِيهِ أُنْزِلَ عَلَيَّ)).
Kutoka
kwa Abuu Qataadah Al-Answaariyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli
wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu
Swawm ya Jumatatu akasema: “Nimezaliwa siku hiyo na siku hiyo
nimeteremshiwa (Qur-aan).” [Muslim]
Yanamaanisha nini maneno hayo?
Ni kama vile anasema (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
Utaniulizaje hivyo na hali Allaah Amenitoa siku hiyo kuwa na uhai na nikateremshiwa wahyi humo?
Yaani
inawapasa mfunge Swawm siku ya Jumatatu kumshukuru Allaah (Ta’aalaa)
kuniumba mimi siku hiyo na kuteremsha Wahyi kwangu siku hiyo.
Na
hivyo ni sawa na Swawm ya Mayahudi siku ya ‘Aashuraa. Na huenda ukajua
kuwa kabla ya kufaridhishwa Swawm ya Ramadhwaan, Swawm ya siku ya
‘Aashuraa ndio ilikuwa fardhi kwa Waislamu. Na
kuna kauli nyengine za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) kwamba alipohamia Madiynah aliwakuta Mayahudi
wanafunga Swawm siku ya ‘Ashuraa. Akawauliza sababu yake wakamjibu: “Ni
siku ambayo Allaah Alimuokoa Muwsaa kutokana na watu wa Fir’awn, hivyo
tunafunga Swawm kumshukuru Allaah.” Hapo yeye (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) akasema:
“Sisi tuna haki zaidi juu ya Muwsaa kuliko nyinyi.”
Basi akafunga Swawm siku hiyo na akaamrisha watu, pia siku hiyo ikawa ni fardhi mpaka Allaah Alipoteremsha kauli Yake:
شَهْرُ
رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ
وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ
الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ ﴿١٨٥﴾
Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na upambanuo wa haki na batili. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu (mwandamo wa) mwezi na afunge Swiyaam. [Al-Baqarah: 185]
Hapo ikawa Swawm ya ‘Aashuraa ni Sunnah ,na kukafutwa kuwajibika kwake.
Ushahidi
wa haya ni kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) aliungana na Mayahudi kufunga Swawm siku ya ‘Aashuraa kama ni
shukurani kwa Allaah (Ta’aalaa) kumuokoa Muwsaa ('Alayhis-Salaam)
kutokana na Fir’awn. Hivyo mlango wa shukurani umefunguliwa kwetu kwa
kufunga Swawm siku ya Jumatatu kwa sababu ni siku ambayo Rasuli wa
Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amezaliwa na ni siku
ambayo ameteremshiwa Wahyi.
Sasa
nakuuliza: Je, hawa watu wanaosherehekea mazazi (yasiyokuweko katika
shariy’ah) ambayo tunajua kuwa hayana khayr ndani yake - najua kuwa
wengi ya watu hao hufunga Swawm Jumatatu kama wanavyofunga Swawm siku ya
Alkhamiys - lakini je, Waislamu wengi wanafunga Swawm ya Jumatatu
pekee?
Hapana! Hawafungi Swawm Jumatatu, lakini Waislamu wengi wanasherehekea mazazi ya Nabiy mara moja kwa mwaka. Je, hivi si kinyume na usahihi?
Hawa inawathubutikia kauli ya Allaah (Ta’aalaa) kwa Mayahudi:
أَتَسْتَبْدِلُونَ الَّذِي هُوَ أَدْنَىٰ بِالَّذِي هُوَ خَيْرٌ ۚ
“Je mnataka kubadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora? [Al-Baqarah: 61] (Kuchagua yaliyo duni na kuacha yaliyo bora)
Hiyo ndio khayr.
Kufunga Swawm iliyokubalika kwa Waislamu wote; nayo ni Swawm ya
Jumatatu, na juu ya hivyo Waislamu wengi hawafungi Swawm hiyo!
Kisha kwa ambao wanaifunga Swawm nao ni wachache. Je, wanajua siri ya Swawm hiyo?
Hapana hawajui!
Basi wako wapi Wanachuoni wanaotetea Maulidi?!
Kwanini
hawawabainishii watu kuwa Swawm ya Jumatatu ni kusherehekea
kulikoamrishwa kuwa ni Maulidi na wakahimiza kuifunga Swawm badala ya
kutetea ambayo hayakuamrishwa? Na Amesadikisha Allaah (Ta’aalaa)
Anaposema:
“Je mnataka kubadilisha yaliyo duni kwa yaliyo bora?
Na Amesadikisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
لَتَتَّبِعُنَّ سَنَنَ مَنْ قَبْلَكُمْ؛ شِبْرًا بِشِبْرٍ، وذِرَاعًا بِذِرَاعٍ؛ حَتَّى لَو دَخَلُوا جُحْرَ ضَبٍّ لَدَخَلْتُمُوهُ
“Mtafuata
nyendo za wale waliokuja kabla yenu hatua kwa hatua mpaka itafika hadi
wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na katika riwaayah nyingine iliyo khatari:
حتى لو كان فيهم مَنْ يَأْتِي أُمَّهُ على قارعةِ الطريقِ لَكَانَ فيكم مَنْ يَفْعَلُ ذلك
“...hadi
kwamba hata ingekuwa mmoja wao angejamiiana na mama yake katikati ya
barabara, angekuweko mtu miongonii mwenu ambaye angefanya hivyo pia” [Al-Haakim ikiwa ni Hasan kama alivyoisahihisha Al-Bazzaar na Al-Albaaniy ameikubali katika Silsilah Asw-Swahiyhah (1348)]
Basi
sisi (tunaosherehekea Maulidi) tunafuata mwendo wa Mayahudi,
tukabadilisha ambayo ni ya (kuchagua yaliyo) duni kwa (kuacha) yaliyo
khayr kama tulivyobadilisha (tukachagua) Maulidi ya Nabiy ambayo
yanatokea mwaka mara na hayana dalili kwa (kuacha) ambayo yaliyo khayr
nayo ni kusherehekea kila
Jumatatu ambayo ni kusherehekea kulikoamrishwa kwa kuifunga Swawm,
pamoja na kutanabahi siri yake humo kuwa unafunga Swawm kwa ajili ya
kumshukuru Allaah (Ta’aalaa) kwa kumuumba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) na Akateremsha wahyi humo (siku hiyo).
Na nahitimisha maneno yangu kwa kutaja kauli ya (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
أَبَى اللهُ أنْ يَقْبَلَ توبةَ مبتدعٍ
“Allaah Amekataa kabisa kupokea tawbah ya mwenye kufanya bid’ah.” [Ibn
Maajah na Imaam [Imaam Al-Albaaniy amesema ina udhaifu, lakini kuna
Hadiyth ambayo ameisahihisha yenye maana kama hiyo iliyokusanywa na Abuu
Imaam katika Taariykh Asbahaan (Uk. 259), Atw-Twabaraaniy katika Al-Awsatw (4360) na wengineo].
Na Allaah (Ta’aalaa) Anasema:
يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ وَإِن لَّمْ تَفْعَلْ فَمَا بَلَّغْتَ رِسَالَتَهُ ۚ وَاللَّـهُ يَعْصِمُكَ مِنَ النَّ
Ee
Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako. Na
usipofanya, basi utakuwa hukubalighisha ujumbe Wake. Na Allaah
Atakuhifadhi dhidi ya watu. [Al-Maaidah: 67]
Anayejadiliana na Imaam:
Je, kusoma Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) si takrima kwake?
Imaam Al-Albaaniy:
Naam (endelea).
Anayejadiliana na Imaam:
Si mna thawabu ya khayr kutoka kwa Allaah?
Imaam Al-Albaaniy:
Yote ni khayr! Lakini hutofaidika chochote kutokana na swali hili. Kwa hiyo nakukatisha kwa swali: Je ,kuna yeyote aliyekuzuia kusoma Siyrah yake?
Kisha
sasa nakuuliza swali: Ikiwa ni aina ya ‘ibaadah iliyoamrishwa lakini
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuiwekea
muda makhsusi wala hakuiwekea jinsi ya kuitekeleza; je, inajuzu kwetu
kuiwekea wakati makhsusi au namna ya kuitekeleza? Je, unalo jibu?
Anayejadiliana na Imaam:
Hapana sina jibu.
Imaam Al-Albaaniy:
Allaah (Ta’aalaa) Anasema:
أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ ۚ
Je, wanao washirika waliowaamuru Dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea idhini? [Ash-Shuwraa: 21]
Na Anasema pia Allaah (Ta’aalaa):
اتَّخَذُوا
أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ
وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا
وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٣١﴾
Wamewafanya
Wanavyuoni wao mafuqahaa wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miungu badala
ya Allaah, na (pia wamemfanya) Al-Masiyh mwana wa Maryam (kuwa ni
mungu); na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Ilaah (Allaah) Mmoja
(Pekee). Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Utakasifu ni Wake! kutokana
na yale yote wanayomshirkisha nayo. [At-Tawbah: 31]
‘Adiyy
bin Haatim (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliposikia Aayah hii na alikuwa
kabla ya kusilimu kwake, alipokuwa Mnaswara, ilikuwa ngumu kwake
akasema: “Hatukuwa tukiwaabudu.” Hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
أَلْيَسَ يُحَرِّمُونَ مَا أَحَلَّ اللهُ فَتُحَرِّمُونَهُ وَيُحِلُّونَ مَا حَرَّمَ اللهُ فَتُحِلُّونَهُ؟
“Je,
kwani hawakuwa wakiharamisha Aliyoyahalalisha Allalah nanyi
mkayaharamisha, na wakahalalisha Aliyoyaharamisha Allaah nanyi
mkayahalalisha?”
Akasema: Ndio.
Akasema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Basi hiyo ndio kuwaabudu kwao.” [At-Tirmidhiy (3095) na ameipa daraja ya Hasan Imaam Al-Albaaniy]
Na hii inabainisha khatari ya kufanya bid’ah katika Dini ya Allaah (Ta’aalaa):
Mwisho wa Mjadala
************************
Imetolewa kutoka katika moja ya kanda za Imaam Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika Silsilat Al-Hudaa wan-Nuwr Kanda namba (1//94)
Post a Comment