MUISLAMU NA MALEZI : JINSI YA KUMLEA MTOTO WA MIAKA 0 MPAKA 5 KATIKA MISINGI MEMA

As salaam aleykum warahamatullah wabarakatuh ndugu zangu katika Iymaan tunaendelea na kipengele hiki cha familia leo tuangazie kuhusu Muislamu na malezi, siku zote Maisha ya kifamilia na kidunia yanapitia mambo mengi. Ni jukumu letu sisi wazazi, walezi, madada, makaka na waalimu kumtayarisha mtoto ili aweze kukabiliana nayo. Mambo hayo yanaweza kuwa wazazi kuachana, kifo cha mzazi mmojawapo au wote, kuzaliwa kwa mtoto mwingine, tabia ya nyumbani kukiwa na wageni na kadhalika. Mtoto anastahili matayarisho ya kisaikolojia kuhusu mambo hayo. Pia jua tabia mbalimbali za mtoto kwa jinsi anavyokua hadi kufikia ujana.

Kumfunza mwanao/mtoto nidhamu

Utafanyaje kumuepusha mwanao asiangalie video kwa muda mrefu kama ameshazoea? Je, mwanao akiwa shuleni kama mwanafunzi mwenzake akianzisha fujo mfano amempiga ngumi, afanyeje? na ufanyeje ili mwanao aheshimu mamlaka yako kama mzazi? Haya ni baadhi tu ya masuala ya msingi ambayo wazazi wengi tumeshindwa kuelewa madhara yake katika kujenge nidhamu ya mtoto.

Ni vyema mzazi uwe na msimamo ambao uko wazi kwa mwanao. Ukiongelea masuala ya mzaha iwe ni mzaha kweli kwani kufanya mzaha na mwanao kutamjengea yeye kujiamini na kutokukuogopa, linapokuja suala la nidhamu uonyeshe unamaanisha nidhamu kweli. Kama maamuzi unayofanya yanakinzana kila mara hata mwanao ni vigumu kuyafuata.
Katika sehemu hii tunaeleza jinsi unavyoweza kuweka nidhamu ya watoto wako ndani ya familia. Nidhamu unayotakiwa kuijenga hutofautiana kati ya mtoto na mtoto kulingana na umri.

Mwaka 0 hadi miaka 2

Watoto wa umri huu mara nyingi hutaka kushika kila kitu, kumbuka ni umri huu ambapo mtoto anatambaa, anaanza kutembea, anaanza kuongea na anaanza kula vyakula mbalimbali ni vyema kuweke mbali vitu vinavyowapeleka kwenye majaribu ya kutaka kufanya jambo fulani mfano kuwasha TV, redio, kugusa vitu vya thamani, kula vitu anavyookota, dawa nk. Vitu hivi ni muhimu viwekwe sehemu ambayo watoto hawawezi kufikia.

Mzoeshe mwanao anayetambaa kumkataza, mwambie “ACHA” au “HAPANA” anapotaka kushika vitu hatari au vitu ambavyo unawasiwasi anaweza kuviharibu au vinaweza kumletea madhara na mtoe eneo hilo.

Tusiadhibu watoto wetu wa umri wa umri wowote kwa kuwapiga au kuwachapa viboko, mtoto hawezi kuhusisha viboko na kosa alilotenda zaidi ya kuhisi tu maumivu ya fimbo.

Watoto wetu wanajifunza kutokana na yale tunayoyafanya kama wazazi, ni jukumu la mzazi kujaribu kuwa mfano wa kuigwa. Watoto ambao wamezoea kuona mama na baba daima ndani ni ugomvi, kupigana na matusi, watoto hao hawana amani na mara nyingi huishia kuiga tabia mbaya kutoka kwa wazazi hawa, ni vema wazazi au walezi mnapokuwa na kutokuelewana msionyeshe dhahiri mbele ya watoto wenu.

Miaka 3 hadi 5

Mtoto wa umri huu anaanza kujifunza na kuelewa mema na mabaya kutokana na matendo yake. Kuanzia umri huu anza kumfundisha mt oto kuhusu dini yake sheria na taratibu za familia yako. Mfano kumsalimia baba na mama kila anapoamka asubuhi kumshukuru muumba wake, kusema asante baada ya chakula au anapowewa kitu, kusalimia watu wanaomzidi umri nk.

Unapowapa watoto wa umri huu onyo au karipio waeleze kwanini kosa alilofanya ni kosa au kwanini alivyofanya si sahihi. Mfano mtoto amechora ukuta kwa rangi, mwambie rangi za kuchorea ni kwa ajili ya karatasi si kwa ajili ya ukuta na mwambie ukichora ukuta unaharibu mwonekano mzuri wa ukuta, hivyo asirudie.

Wakati unawajengea watoto ufahamu wa kipi ni kibaya ambacho wakifanya wataadhibiwa, ni vyema pia uwajengee nidhamu ya kuelewa kuwa ni mambo gani ambayo wakiyafanya vizuri watapata zawadi au wewe kama mzazi unayafurahia. Mfano, wazoeshe watoto umuhimu wa kufanya vizuri madrasa au shuleni. Waambie umuhimu wa kusoma dini yao na sekula, wajengee hamu ya kutaka kuhifadhi qurani , hadiyth na kufika Chuo Kikuu n.k na uwaeleze faida zake.

Watoto wa umri huu wanapokosa unaweza kuwapa adhabu kama vile kumtenganisha na vitu fulani fulani ili kumjengea mtoto wa umri huu tabia nzuri. Mtenganisshe kwa muda ni vitu kama vile, kumzuia mtoto kungalia TV, kusikiliza redio, kucheza na wenzake kwa muda fulani nk.


Alhamdulillah leo tuishie hapa ila insha allaah mola wetu mlezi akitujaalia tutaendelea kukuletea mfululizo wa makala mbalimbali za kijamii kipindi hiki tupo katika mchakato wa kuandaa makala kuhusu benki za kiislamu jinsi zinavyoendesha huduma zake n.k 

0 Comments