KUVAA MKUFU MIGUUNI INAFAA?

SWALI:
asalam alaykum,
mie nilikuwa napenda kuuliza hivi jee inafaa kwa mwanamke kuvaa mkufu wa dhahabu au fedha katika mguu wake kwa ajili ya mume wake?
inshallah naomba jawabu,jazakallahul kheir.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakuna ubaya kwa mwanamke kuvaa mkufu miguuni ikiwa ni kwa ajili ya kujipamba kwa mumewe. Na wala asidhihirishe mapambo hayo nje kwa wasiomhusu, yaani wasio maharimu zake. Dalili tunapata katika Aaya ya hijaab inayomalizia kukataza wanawake wanaovaa mikufu miguuni mwao wasitembee kwa kupiga miguu yao hadi ijulikane kuwa wamevaa mapambo hayo miguuni mwao:
 ((وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ))
((Wala wasipige chini miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha)) [An-Nuur: 31]
Hii ni wazi pia kuwa hijaab ya sheria inampasa mwanamke ajifunike hadi miguuni mwake. Tunaona dada zetu wengi wanajifunika tokea juu lakini miguu yao iko wazi hata katika Swalah utawaona wanaswali na miguu, vidole vya miguu vinaonekana. Swalah zao hawa zinakuwa hazikukamilika kwani mwanamke anatakiwa ajifunike kote isipokuwa uso tu na viganja vya mikono.
Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments