MATAYARISHO YA RAMADHAAN, JE WEWE UKO TAYARI?

Mkusanyaji: Abu FaattimahShukrani zote ni Zake Mfanya Alitakalo; Asiyeulizwa kwa Alifanyalo; Al-Waahidul Al-Ahadu Asw-Swamad; Ambaye hakuzaa na wala hakuzaliwa; Hapana kitu mfano Wake. Naye ni As-Samiy’ul Baswiyru.Ar-Rahmaan [Mwingi wa Rahmah] Ametutunukia Ramadhaan kuwa ni pahala na wakati wa kila mmoja wetu kuonyesha juhudi yake kwa kupania na kujipamba kwa kila aina ya amali nzuri na njema; na kujihakikishia kuwa kuna mabadiliko katika mitindo ya maisha yetu ya kila siku kama alivyotusunia na kutuwekea mwenendo huo Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili tupate kurehemewa, kufutiwa madhambi yetu na kuokolewa na Moto wa Jahannamu.Rehema na Amani za Allaah zimfikie Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliye ielewa na kuithamini Ramadhaan ndio akawa anaonekana na hali tofauti kabisa kila anapokutana na mwezi wa Ramadhaan; (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akionekana na jitihada zaidi akilinganishwa na hali aliyokuwa akionekana nayo kwenye miezi mingine isiyokuwa Ramadhaan kama ilivyothibiti katika hadiythi ya Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) aliposema kwamba:

“Alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ajwad (mkarimu) wa watu, na alikuwa ajwad zaidi katika Ramadhaan wakati anapokutana na Jibriyl (‘Alayhis Salaam), alikuwa -Jibriyl (‘Alayhis Salaam)- akimjia Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam kila usiku wa Ramadhaan akimdurusisha Qur-aan” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Swawm, mlango alikuwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mkarimu/mbora zaidi katika Ramadhaan, Hadiyth namba 1179].Ndugu zangu katika iymaan, napenda kujiusia nafsi yangu kwanza na kisha kuziusia nasfi zenu kuwa na Taqwah ya Allaah na kumtii Allaah na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kutekeleza kila Aliloliamrisha kadiri ya uwezo wetu, na kujikataza na kila Alichokikataza mara moja.Tunaukaribia mwezi wa Ramadhaan, mwezi wenye fadhila nyingi, mwezi ambao ndani yake tunasamehewa madhambi yetu, mwezi ambao hauna wenye kufanana naye katika miezi yote ya mwaka kwa mavuno na ujira, mwezi ambao hupatikana na kutekelezwa ndani yake nguzo moja katika nguzo tano za Uislam mwezi ambao ndani yake kuna usiku mmoja wenye cheo –Laylatul Qadr- ambao ni bora kuliko miezi elfu moja, mwezi ambao ndani yake milango yote ya Jannah huwekwa wazi na milango ya Moto hufungwa, mwezi ambao mashetani hufungwa minyororo, mwezi ambao katika kila usiku wake Allaah Huwatowa watu kwenye Moto wale waliostahiki kutupwa Motoni, mwezi wa Qur-aan, mwezi wa Rahmah, mwezi wa Maghfirah, mwezi wa Tawbah na mwezi wa Taraawiyh.Ndugu zangu katika iymaan, mwezi wa Ramadhaan ni mgeni mtukufu, mgeni aliyejenga uhusiano mzuri na wenye nguvu na Waumini wa kila zama, kwa njia ya kuwatembelea na kukaa nao kwa kipindi cha masiku anayojaaliwa.  Mgeni huyu ndiye yule yule aliyewahi kuwatembelea na kukutana na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na waislamu wote wa karne zilizopita, na ni mgeni huyu huyu atakaye tutembelea sisi na kuwatembelea in shaa Allaah Waislamu wa karne zitakazokuja baada yetu tutakapokuwa chini ya tani za udongo.

Ndugu zangu katika iymaan, ni vyema tuwe na kawaida ya kujitathmini iwe kwa kujiuliza maswali au kwa namna yoyote ile itayotusaidia kuweza kufikia kuelewa kama tunafaidika na yale yote tunayo soma, au sikia, au fanya.Ndugu yangu katika iymaan, suali lolote lile utalojiuliza nafsi yako litaweza kukusaidia katika kukufunua macho, moyo, na akili; kila suali likiwa zuri na la kweli basi akili na moyo vitakuja na jawabu zuri na la kweli ambalo litasaidia katika kuathiri namna unavyoona na kufasiri mambo na matukio; hivyo tunahitaji kujiuliza maswali mengo tu; kama haya na mengine yenye kufanana na haya; nini kizuri katika mwezi wa Ramadhaan? Nini naweza kujifunza kutokana na mwezi wa Ramadhaan? Vipi naweza kujichukulia au kujinyakulia mazuri na yaliyobora kutoka kwenye mwezi wa Ramadhaan?  Je, niko tayari kuukaribisha mwezi wa Ramadhaan? Au, je kweli nimejiandaa kwa Ramadhaan? Je, kweli mimi niko tayari kupitisha wakati wangu ninao uthamini kwa kumtumikia Allaah? Je, niko tayari kuchukua mapumziko -livu- kwa ajili ya Allaah?Ndugu yangu katika iymaan, ukweli ni kuwa kila kitu huwa tuna matayarisho na maandalizi yake, kwa mfano, tunapotarajia kuwa na shughuli huwa tunaanza kupanga na kujianda kwa wiki nyingi au wakati mwingine miezi mingi tu, na huwa makini na waangalifu sana, kwani hata huwa haitupigi chenga siku au tarehe, na wala hutusahau wakati wa hiyo shughuli, na hutughafiliki na pahala itakapokuwa wachilia mbali chakula kitachotengenezwa na nguo tutakazovaa au zinazo takiwa kuvaliwa.Hata hivyo, kwa mshangao mkubwa naweza kusema kuwa inapokuja jambo lenye kuhusiana na Dini ya Haki, Dini ya Muumba wa ulimwengu na vyote viliomo ndani yake, jambo lenye kuhitaji maandalizi na matayarisho, utaona watu hawana maandalizi yoyote yale au yenye kulingana na hilo jambo, na kama wataamua wajitayarishe au wajiandae, basi watakuwa na maandalizi au matayarisho madogo na machache yasiyodhihirisha utukufu wala nafasi ya hilo lenye kuja na kutakiwa watu wajitayarishe; au wakati mwingine hujitayarisha lakini kwa matayarisho na maandalizi yenye kila aina ya maasi na kila lenye kuchukiwa na Allaah na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hasa ikiwa lenye kuja ni  mwezi wa Ramadhaan.Ndugu yangu katika iymaan, huenda sababu kubwa ni kuwa wengi wetu hatuelewi utukufu, fadhila na nafasi ya mwezi wa Ramdhaan, au huenda wengi wetu wanadhania bali huwa na yakini kuwa tunaweza kubadilika na kuwa Swaalihiyna [wema] na Muttaqiyna [wenye kumuoga Allaah na wachaji Allaah] funga fungua, kama tuwashavo taa, ndio tunaweza kubadilika na kugeuka na kuwa tayari kutekeleza yenye kutakiwa kutekelezwa kwenye mwezi wa Ramadhaan.

Ndugu yangu katika iymaan, ukweli ni kuwa huenda tukabadilika funga fungua, lakini hii kama itakuwa, basi ni kwa muda mfupi tu, na katika muda mrefu -ambao ndio lengo- huenda mambo yakawa magumu na yasiyotarajiwa, kwani huenda tukarejea katika hali zetu tulizojing’oa na kujibadilisha, au huenda tukarejea katika hali mbaya zaidi ya zile tuzizokuwa nao kabla ya kuja Ramadhaan baada tu ya mgeni Ramadhaan kutuaga.Je, si kweli kuwa baada ya hayo matayarisho na maandalizi yetu tunayoyaanda yasiyokuwa na msingi wenye taqwah, je, si kweli kuwa inapokuwa kati kati ya mwezi wa Ramadhaa na wakati mwingine hata kabla ya hapo misikiti huwa imekwisha hamwa -hasa wakati wa Swalah ya Taraawiyh- na wale waliojidhania na kuwa na yakini kuwa wanaweza kujibadilisha bila ya matayarisho, wakisahau kuwa umuhimu, ubora na utamu wa mwezi wa Ramadhaan si katika masiku yake ya mwanzo bali ni kwenye kumi la mwisho wakati ambao wengi huwa wanajishughulisha na matayarisho ya ‘Iyd ambayo huwa muhimu zaidi kwao kuliko Ramadhaan yenyewe wachilia mbali hayo masiku yake kumi ya mwisho ambayo yalikuwa na uzito, umuhimu na nafasi ya aina yake mbele ya macho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nafasi iliyompelekea (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujifunga kibwebwe na kujidhatiti sawa sawa kwa kuhuisha nyakati za usiku za masiku hayo kumi ya mwisho kwa kujishughulisha yeye na ahli zake kwa ibadah kuliko siku zote zilizotangulia katika mwezi wa Ramadhaan kama ilivyothibiti katika hadiyth za mama wa Waumini bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) aliposema:

"Zilipokuwa zikiingia siku kumi za mwisho (za Ramadhaan), alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akikaza Izaar (shuka) yake, na akihuisha usiku wake (kwa kufanya ibadah), na akiamsha ahli zake”[Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Swalah ya Taraawiyh, mlango wa amali kwenye kumi la mwisho la Ramadhaan, hadiyth namba 1895].Pia kutoka kwake mama wa Waumini bibi 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) amesema kwamba:

"Alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akijitahidi katika kumi la mwisho asivyojitahidi katika siku nyingine (zisizokuwa hizo kumi za mwisho)"[Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Al I’tikaaf, mlango wa kujitahidi kwenye kumi la mwisho la Ramdhaan, hadiyth namba 2016].Ndugu zangu katika iymaan, hali hii ya kutojitayarisha ambayo tunakuwa nayo kila inapokuja Ramadhaan inatuthibitishia kuwa tunahitaji maandalizi na matayarisho ya kweli, ya uhakika, ya kidhati na ya msingi tena wenye taqwah; na ukweli ni kuwa kama hatukujianda vyema –tahadhari kuingia kwenye Ramadhaan bila ya matayarisho- kwa mambo ya Dini kama au kuliko tunavyojiandaa kwa mambo ya kidunia, basi ni vyema tuelewe kuwa hatutokuwa na uwezo wa kubakia kuwa thabiti wala kushikamana na wala kuendela kutekeleza amali yoyote ile tuliyoichukuwa na kuitekeleza kwenye mwezi wa Ramadhaan kwa lengo la kuwa nayo mpaka tutakapo kutana na Muumba wa Ramadhaan.Ndugu yangu katika iymaan, Ramadhaan itakuwa nasi baada ya siku chache tu kama ilivyo yenyewe ni masiku machache tu; Allaah Anasema:

“(Kufunga kwenyewe ni) Siku za kuhesabika. Basi atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu, au yuko safarini (akafunga baadhi ya siku); basi (akamilishe) idadi (ya siku anazotakiwa kufunga) katika siku nyinginezo.Na wale wasioiweza (Swawm) watoe fidia; kulisha masikini. Na atakayejitolea kwa jema lolote lile basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu mkiwa mnajua.” [Al Baqarah 2:184].Hivyo ni vyema kuwa na maandalizi na matayarisho, na katika matayarisho hayo ni vyema kila mmoja wetu awe na orodha ya amali, matendo na mambo atayopenda kushikamana nayo katika mwezi wa Ramadhaan na kujihakikishia kuwa atayaendeleza kuwa nayo na kuyatekeleza baada ya Ramadhaan kumuaga.

Ndugu yangu katika iymaan, tunashauriana kuhusu matayarisho na maandalizi ya kumpokea mgeni wetu kwa kuwa ni mgeni adhimu katika majumba yetu. Hivyo basi tunashauriwa kuhakikisha kuwa tunakaa na kuishi naye kwa wema na ihsaanna kujipamba kwa tabia njema na kujitahidi katika kutekeleza ibadah kwa uangalifi.Ndugu yangu katika iymaan, Ramadhaan ya mwaka huu kama kawaida za Ramadhaan za miaka mingi iliyopita na ijayo haitakuja na kipya, kwani kutakuwa na Swawm, Qiyaam, kufutarisha, kukaa itikafu na kadhalika; na kubwa linalotutakia Ramadhaan ni kuhakikisha kuwa tunajilea katika kuweza kufikia kuwa na taqwah, taqwah ambayo ndio kitu cha pekee kitachotuwezesha kwa uwezo wa Mola kuwa thabiti katika mapambano yetu na mitihani yote ya safari yetu ya dunia na kufikia kuwa wenye kufaulu huko Aakhirah.Ndugu yangu katika iymaan, ni jambo linalo eleweka kuwa wengi wetu katika maisha yao wamewahi kukutana na Ramadhaan nyingi tu, lakini nasubutu kusema kuwa ni jambo lisiloeleweka na kufahamika na wengi wetu kuwa japokuwa tumewahi kukaa na kuishi na Ramadhaan na kuielewa hiyo Ramdhaan, lakini ukweli –ambao wengi wetu hatuelewi- ni kuwa kila Ramadhaan inatakiwa iandaliwe, ihudumiwe na kutayarishwa kivyake, na kuchukuliwa kuwa ni fursa ya pekee katika uhai wetu kwani hakuna ajuaye kama atakutana na Ramadhaan nyingine baada ya kuondoka hii inayotukabili kama tutakutano nayo.

Hivyo ni vyema sote kwa pamoja tuwe na lengo kuu moja, nalo ni kumuomba Allaah Aijaaliye Ramadhaan hii kwetu kuwa ni bora zaidi kuliko zote katika zile tulizowahi kukutana nazo, Aijaaliye iwe yenye mavuno na matunda ya heri na mazuri.Ndugu yangu katika iymaan, hebu tuandae na tutayarishe chochote kile kwa ajili ya Ramadhaan, jambo ambalo kwa uwezo wa Mola litatusaidia kuweza kupata uchangamfu katika siku zote za mwezi wote wa Ramadhaan na sio kwenye siku zake za mwanzo pekee.  Moja katika maandalizi na matayarisho ni kujitathmini, kujiangalia hali zetu, hali za ibadah zetu, hali za amali zetu na kadhalika; je, kuna mabaya na yenye kumchukiza Allaah ambayo yanahitajika kuachwa na kila mmoja wetu kwa kujing’oa nayo kabisa na kuomba tawbah ya kweli? Je, kuna amali au matendo mema ambayo nafikiria na nitapenda kuanza kuyatekeleza na kuwa nayo katika masiku ya Ramadhaan na kuendelea kubakia nayo kwenye maisha yangu?Ndugu zangu katika iymaan, huenda katika kuacha jambo kukawa kugumu, lakini tukiazimia, Allaah Atatuwafikisha kama kunavyohitajia kuazimia katika kuanza jambo kwani kuna ugumu pia.Ndugu yangu katika iymaan, maandalizi au matayarisho ninayotaka kuyapendekeza sio Wahy [ufunuo], bali ni yenye kukubali maoni na mapendekezo, hivyo kuwa huru kuyapokea au kupendekeza na kushauri mengineyo, kinachotakiwa na ndio lengo la waraka huu ni kukushajiisha na kukusaidia uweze kufikia kuwa mwenye mawazo, fikira na mipango kwa kubuni matayarisho na maandalizi ya kuupokea mwezi wa Ramadhaan, hivyo uko huru kuchukuwa au kuchagua amali yoyote ile ambayo utapenda kushikamana nayo katika masiku ya Ramadhaan, kila mmoja wetu anaielewa nafsi yake vyema hata akileta nyudhuru gani; na pia kila mmoja wetu anaelewa vizuri na vyema kila kilicho na manufaa naye katika maisha yake; hivyo shikilia na shikamana kwa jitihada kubwa na kile unachohitajia kukitekeleza au kukirekebisha.Ndugu yangu katika iymaan, kwa ujumla mapendekezo ni kama hivi:Chagua amali –mfano: tabia fulani, utoaji wa sadaqa, ufungaji, kwenda msikitini, utiaji udhu na kadhalika- yoyote ile unayohisi kuwa huna tamkini nayo au bado hujafikia kwenye daraja inayotakiwa katika utekelezaji wake kama inavyotakiwa kutekelezwa kwa sababu moja au nyingine na kuiwekea mikakati ifuatayo itayokusaidia kuwa na tamkini wa hiyo amali kwenye mwezi huu wa Ramadhaan:* Fanya utafiti wa kina kuhusu hali yako ya sasa katika utekelezaji na mahusiano yako na hiyo amali (uzuri, uzoevu wako utekelezaji wako wa hiyo amali mara kwa mara, na kadhalika).* Fanya utafiti wa kina utaokusaidia kuweza kufikia kugundua udhaifu wako, na matatizo uliyonako katika utekeleza wako na kiini chake (elimu, khushui na kadhalika).* Fikiria njia au mbinu zitazokusaidia kuweza kuepukana na kujikombowa kutokana na huo mzizi unaosababisha uwe hivyo.* Weka mikakati ya kweli na uhakika na yenye kutekelezeka itakayo kusaidia kuweza kutatua hatua kwa hatua tatizo lako katika masiku haya kabla ya Ramadhaan na kisha kuwa na mwenendo mwepesi kwenye mwezi wa Ramadhaan.

Mfano SwalahKila mmoja wetu anaelewa nafasi ya Swalah katika Uislamu, kuwa ndio nguzo ya dini, na kwamba anaye isimamisha huwa ameisimamisha dini yenyewe, na asiye isimamisha huwa ameivunja dini yenyewe, na kuwa ndio kitu cha kwanza atakachokuja ulizwa kila mmoja wetu Siku ya Qiyamaah, na kwamba Swahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) hawakuona kitu kinachomtoa mtu katika Uislam kama mtu kuacha kuswali.

Ndugu yangu katika iymaan, ikiwa nasafi ya Swalah kama hiyo imo katika moyo na akili yako; maandalizi na matayarisho yako ya kwanza ya mwezi wa Ramadhaan yatahitaji yawe na mikakati ifuatayo:

Hali na mambo yalivyo na dalili zakeJitathmini kwa kujiuliza maswali:

Je, ni kweli naielewa na kuifahamu vyema nasafi ya Swalah kwenye huu uhai wangu na nitakapo kuwa chini ya tani za udongo na Aakhirah?  Je, ni kweli mimi naisimamisha Swalah itakiwavyo au ndio nimo katika wenye kupuuza Swalah zao? Je, Swalah zangu huwa za jamaa msikitini au pekee yangu nyumbani? Je, Swalah zangu naziswali kwa wakati wake uliowekwa au natoa kipa umbele kwa mambo mingine na kupelekea kuchelewa kutekeleza Swalah? Je, ni kweli ninafanya juhudi yoyote kuhakikisha kuwa naziswali jamaa? Je, nina unyenyekevu, khushui na utulivu kwenye Swalah, au wakati mwengine kuna mambo yenye kunishughulisha na kusababisha kutokuwa na unyenyekevu na khushui katika Swalah?Ndugu yangu katika iymaan, kuna mengi tunayoweza kuorodhesha na kuyatafakari kuhusiana na Swalah, lakini kwa sasa ni bora tuyazingatie na kuyaangalia hayo.Ndugu yangu katika iymaan, tafakari kwa undani kila suali, na jaribu kudhibiti majawabu yako; kuwa mkweli na mwaminifu wa nafsi yako, na fanya hayo ima ukiwa uko pweke bila ya kumshirikisha mtu – kama utaona kutakuwa na faida katika kutomshirikisha mtu-, au kwa kumshirikisha mwandani wako -lakini asiwe shaytwaan- ikiwa utaona kuwa kutaleta tija na manufaa zaidi.

Fanya utafiti wa kina utaokusaidia kuweza kufikia kugundua Mzizi wa matatizo yakoNdugu yangu katika iymaan, sasa kwa uangalifu wa hali ya juu na bila ya haraka zingatia na tafakari kwa undani kabisa kutakokupelekea kuweza kufikia kuelewa kiini au mzizi wa tatizo lako au udhaifu wako. Orodhesha kila tatizo pamoja na ishara zake unazoweza kuzigundua (mfano: kukosa unyenyekevu kwenye Swalah, moyo wangu au akili huwa vinatekwa na kuchukuliwa au kunyakuliwa na kitu gani?). Kisha jaribu kutafuta nini kiini cha tatizo hili kwa kudadisi kila ishara. Jiulize nafsi yako, “kwanini?”  Ishara hii inadumu na haibadiliki au haiondoki?. Na endelea kujiuliza tena na tena “Kwanini?” Kwa kila suali mpaka ufanikiwe kufikia kuweza kupata shina au mzizi wake.

UtatuziNdugu yangu katika iymaa, matatizo yako ushayagundua, alama au ishara zake ushazielewa na kuzitambua, na kiini au shina ushalifikia na kulipata; sasa fikiria njia na mbinu za uhakika na za kutekelezeka zitazokusaidia kuweza kutatua haya matatizo kutoka kwenye mzizi.

Kwa mfano, ikiwa akili yako au moyo wako unachotwa na mishughuliko yako ya kila siku kwenye Swalah; je, ni kwa kuwa wewe unapitisha wakati wako mwingi katika kufungamana na hizo shughuli, kisha bila ya matayarisho yanayotakiwa kwa haraka haraka na kwa muda mfupi tu na bila ya hata kiwili wili chako na akili na moyo wako kuwa tayari kuipokea hiyo Swalah unachupa na kujitupa kwenye kuitekeleza Swalah?

Ndugu yangu katika iymaan, ikiwa hali ndio kama hiyo, utatuzi mmoja ni kuipa nafsi yako maandalizi na matayarisho ya kutosha kabla ya kutekeleza kila Swalah, ipatie nafsi yako muda mfupi, muda ambao utajiweka mbali na kujitenga na hizo shughuli zako, kaa kimya na kwa utulivu na pweke na jaribu kuhakikisha kuwa fikira na mawazo yote yanatoweka na kuwa mbali huku kimoyo na kiakili unajitayarisha na kujiandaa kwa mkutano wako wa faragha na Allaah, na baada ya kumaliza hiyo Swalah jaribu kuchukuwa dakika fulani na kukaa kwenye hali yako hiyo uliyokuwa nayo kawenye Swalah kabla ya kurejea kwenye shughuli zako za maisha.

AzimioNdugu yangu katika iymaan, utatuzi ushaeleweka na kufahamika, sasa tafiti jaduweli yako na hali yako ya maisha kwa wakati huu, na uje na mpango au mkakati wa kweli utaokusaidia kuweza kutatua tatizo.  Kumbuka na elewe kuwa utatuzi uko mbali sana na kuathiri ikiwa utakwenda hatua kwa hatua, badala ya kutaka utatuzi wa haraka na mabadiliko makubwa na ya mara moja kwa muda mfupi kwani utajiumiza na kujiangamiza. Azimia kujitayarisha hatua kwa hatua kama za mtoto katika masiku haya ya mwezi wa Shaaban, ukijua na kuelewa fika kuwa kwa sasa unaanza kidogo kidogo na utaongeza hima na juhudi na hatua kuwa kubwa itakapowasili na kuingia Ramadhaan kwani utakuwa ushajiweza na kujimudu na kujimiliki.Wakati wowote ule ukigundua kuwa ulikwenda kombo katika kujikadiria uwezo wako wa kufuata mikakati na mipango uliyojipangia, kwa wepesi kabisa fanya marekebisho kama yatavyohitajika.  Lengo kuu la mwezi huu na miezi mingine inayofuatia ni kukusaidia kuweza kutekeleza hatua za uhakika kwa ajili yako, nini unachoweza kukifanya nasio kukuangamiza.

VisaidiziNdugu yangu katika iymaan, ili kuweza kukusaidia zaidi na kufikia kuvuna mavuno uyatakayo katika utekelezaji wako wa Swalah au amali yoyote ile nyengine uliyoichagua kwenye mwezi wa Ramadhaan na miezi mingine, ningependa kukuelekeza kwenye vitabu vya mafundisho sahihi; kwa mfano, ikiwa umechagua Swalah, basi kitabu chenye mafunzo sahihi kwa jina ni Sifa ya Swalaha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kitabu cha pekee kilichokusanya kila utalolihitaji kuhusiana na Swallaah. Ikiwa huna uwezo wa kukipata, basi unaweza kuingia katika mtandao na kuweza kukisoma.

Ndugu yangu katika iymaan, kisaidizi muhimu kabisa kuliko vyote ni kuwa na nia safi na sahihi, ikhlaasw na kumtegemea Allaah na  kumuomba kila siku na kila wakati Akuwafikishe na Akufanikishe katika yenye kumridhisha huku ukionyesha juhudi zako za dhati na za kweli na za kuendelea kadiri ya uwezo wako kwenye utekelezaji wako.Ndugu yangu katika iymaan, katika matayarisho ya mwezi wa Ramadhaan ni kujitayarisha vyema katika utekelezaji wa yote tunayofikiria kuyatekeleza kwa tawfiki Yake Mola; hivyo inatupasa tuwe na hadhari kubwa kabla ya kupanga na kupangua kuhusiana na cha kufanya na kukitekeleza kwa nguvu zetu na kwa hima, au cha kuacha kwenye Ramadhaan -na nje ya Ramadhaan-; ni muhimu tuelewe kuwa si kila amali au si kila lenye kufanywa ni sahihi au huwa sahihi au limethibiti na kupelekea kukubaliwa; ni kusema kuwa kama hatutakuwa na hadhari, tutarejeshewa bidhaa zetu mbovu; hivyo tusijichokeshe, wala tusijisimbuwe, na wala tusijitesa kwani Allaah Yuko wazi kuwa Hakutuamrishwa Aliyotuamrishwa kwa lengo la kututesa wala kutuadhibu:

“Allaah Anakutakieni mepesi, na wala Hakutakieni magumu.” [Al Baqarah 2:185].Ndugu yangu katika Iymaan, amali njema ni nyingi na wakati mwingine ni rahisi na wepesi kuzifanya au kuzitekeleza au kufikiria kutekeleza au kuona utekelezaji wake, lakini kukubaliwa kwake ambako ndio muhimu –na wengi wetu hatuelewi hilo- na huku ndiko kwenye uwanja wa kushindana kwa wenye kutaka kushindana ni mtihani mkubwa, kwani hawakubaliwi isipokuwa Muttaqiyna (wenye taqwah), je, tumo katika hao; Allaah Anasema,

“Hakika Allaah Anatakabalia Muttaqiyn.” [Al Maaidah 5:27].Ndugu yangu katika iymaan, inawezekana kuwa mtu anatenda matendo mengi, lakini hafaidiki na chochote isipokuwa kupata machofu kutokana na matendo hayo hapa duniani na kupata adhabu huko Aakhirah kwa kuwa yote au baadhi ya aliyoyatenda yamekosa roho ya utendeji.

Ndugu yangu katika iymaan, ni vyema tuelewe kuwa amali yoyote ile kuweza kufikia kukubaliwa na kutakabaliwa katika Uislamu inatakiwa iwe na mambo [masharti] mawili:

La kwanza: Ikhlaasw; kwamba hapakusudiwi katika utekelezaji wa hiyo amali chochote kile isipokuwa Wajhi wa Allaah.La Pili: Al Mutaaba’ah; kwamba hicho kinachotekelezwa kinaendana na Sunnah; kwa kufuata na kuuigiza mafundisho ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwamba katika utekelezaji wa hiyo amali kunafuatwa vile alivyotekeleza au amrisha, au findisha, au elekeza, au fafanua, au idhinisha Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).Ndugu yangu katika iymaan, ikiwa moja kati ya mambo mawili haya limekosekana, kitendo kinakuwa si chema na wala si sahihi hivyo huwa hakina njia ya kutazamwa wachilia mbali kukubalika.Ndugu yangu katika iymaan, je, tunayaelewa ni matendo yepi hayo ambayo yana Ikhlaasw na yako sahihi?  Suali hili na mengine kama hili ni muhimu kuyatafakari kwani amali huenda ikiwa sahihi lakini haina Ikh-laasw ndani yake, hiyo haina njia ya kukubaliwa na kutakabaliwa, na huenda ikawa ina Ikhlaasw lakini sio sahihi, hiyo pia huwa haina njia ya kukubaliwa wachilia mbali kutakabaliwa; sasa ipi yenye harufu ya kukubaliwa na kutakabaliwa ni ile pekee itayokuwa imekusanya mambo yote mawili; sahihi na Ikhlaasw.

Ndugu yangu katika iymaan, ni vyema tuwe na kawaida –kama tulivyoshauri nyuma- ya kujitathmini na kutathmini yale tunayoyatekeleza, kwani kila tulifanyalo au tunalolitekeleza au fikiria kulitekeleza huzaa na kuzusha maswali mawili:

Swali la kwanza: Kwanini umekifanya? Kuhusu sababu ya kutenda kitendo hicho na niya yako. Ikiwa niya ilikuwa kwa ajili ya madhumuni miongoni mwa madhumuni ya kidunia kama vile kutafuta kusifiwa au cheo au kuchaguliwa kuwa mbunge au mwakilishi au malengo yoyote yale ya kidunia, (kitendo) hicho kitakuwa ni kitendo kiovu na kitarembewa kwa yule aliyekifanya. Ikiwa niya yako kufanya hicho kitendo ni kutekeleza Haki ya Allaah ya kujiweka katika hali halisi ya utumwa Kwake na kutafuta njia ya kumkurubia, basi kitakuwa ni kitendo chema na kitimiza sharti la kwanza.Swali la pili: Vipi [namna] umekifanya? Kuhusu utekekezaji wa hicho kinachotekelezwa; je, kuna chenye kuonyesha na kuthibitisha kufuatwa na kuigizwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).Ndugu yangu katika iymaa, kwa kumalizia napenda kujikumbusha nafsi yangu na yako swali jingine nalo ni hili; kwanini nafunga?

Ndugu yangu katika iymaan, jawabu la suala hili ni kuwa funga ni Amri na Maagizo Yake Mola na muislamu huwa hana uchaguzi isipokuwa kumtii Mola wake; Allaah Anasema:“Enyi mlioamini! Mmefaradhishiwa Swawm, kama waliyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Allaah…” [Al-Baqarah: 2:183]

Ndugu yangu katika iymaan, kwa kumaliza ni vyema tuelewe kuwa Ramadhaan inakuja kwa lengo la kutusafisha, kutufunza heshima, utii na kadhalika, tuwe wavumilivu katika kupata mafundisho yake na tuwe wastahalimivu katika kukabiliana na mitihani inayotukuta kila siku. Ramadhaan haiwi Ramadhaan kama hatutokuwa tayari kusameheyana, kukumbushana, kuwaidhiana, kuusiana na kuamrishana mema na kukatazana maovu katika shughuli zetu zote za kila siku, kurekebishana kwa namna itakayoheshimu kila mmoja utu wake.Ndugu yangu katika iymaan, kila amali tuifanyayo tuwe na kawaida ya kuomba ikubaliwe na itakabaliwe, hivyo kwa kumaliza waraka wangu huu, napenda kumuomba Ar-Rahmaan Atuwafikishe katika kuikaribisha na kuipokea Ramadhaan, tumuombe Atuwafikishe katika kuishi na kukaa na Ramadhaan kwa kuifunga, kutekeleza Ayatakayo Muumba, na kuachana na makatazo Yake, pia twamuomba Muumba Atupe uwezo wa kuyatekeleza yatakiwavo kila tunayoyataka kuyatekeleza, Atutie mapenzi baina yetu, mapenzi yatayotupelekea kuwa tayari kusameheyana, kuhurumiana, kuvumiliana, kuheshimiana na kukosoana na kurekebishana, mapenzi yatayopelekea kuwa chini ya kivuli cha Ar Rahmaan Siku ya Qiyaamah.

0 Comments