NDIMI ZETU ZINASEMA : TUNAITAKA RAMADHAAN NA TUNAIPENDA, LAKINI VITENDO VYETU NI KINYUME CHAKE!

:
Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa)
 أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنْ تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ وَكَثِيرٌ مِنْهُمْ فَاسِقُونَ 
Je, haujafika wakati kwa walioamini kwamba zinyenyekee nyoyo zao kwa dhikri[1] ya Allaah na (kwa) yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawarefukia muda, kisha zikawa ngumu nyoyo zao? Na wengi miongoni mwao ni mafasiki. (Al-Hadiyd: 16)
Ramadhaan inakaribia! Umefika wakati kwa wale waliozama katika shirki, ulevi, (kila aina ya) madhambi na bid’ah, kujirekebisha na kujitakasa kwa Tawhiyd, utiifu kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kufuata Sunnah ya Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo:

  • Tujirekebishe kuanzia sasa ili itakapoingia Ramadhaan, nyoyo na viungo vyetu viwe vinamwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Pekee bila ya kumshirikisha.

  • Tujirekebishe sasa ili itakapoingia Ramadhaan, viungo vyetu vitende amali zenye kumridhisha Allaah!

  • Tujirekebishe sasa ili inapoingia Ramadhaan, vitendo vyetu viendane sawa na Sunnah ya mpenzi wetu Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ili tuwe ni wenye kuwafuata Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) ambao ni viumbe bora kabisa baada ya Mitume.

Kujirekebisha na kujitakasa kunahitaji muda, na hakuna muda mzuri kama huu unaokaribia mwezi wa Ramadhaan!
Salafus-Swaalih walikuwa wakiitarajia Ramadhaan na wakijitayarisha mapema mno. Walikuwa wakiiomba du’aa kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Awawezeshe kuifikia Ramadhaan.
Vipi basi wewe? Umefikia wapi katika kutarajia, kujitayarisha na kuomba du’aa?
Au utakuwa miongoni mwa wale wajinga wanaosubiri siku ya kwanza ya Ramadhaan ndio uanze kupapatika kurekebisha nafsi yako hali ya kuwa bado umezamia katika shirki, madhambi na bid’ah? Matokeo yake basi ni kwamba mwezi utakapomalizika utakuwa bado una athari za maovu. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):
وَاتَّقُوا يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللَّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ
Na iogopeni Siku mtayorejeshwa humo kwa Allaah, kisha kila nafsi italipwa kamilifu iliyoyachuma nao hawatodhulumiwa. (Al-Baqarah: 281)
Na Anasema pia:   
وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَى فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَى 
Ama yule aliyekhofu kisimamo cha Mola wake, na akaikataza nafsi yake na matamanio. Basi hakika Jannah (itakuwa) ndio mahali pake pa kukimbilia. (An-Naziaat: 41)
Na Anasema pia:
أَلَمْ يَأْنِ لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنْ تَخْشَعَ قُلُوبُهُمْ لِذِكْرِ اللَّهِ وَمَا نَزَلَ مِنَ الْحَقِّ وَلَا يَكُونُوا كَالَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِنْ قَبْلُ فَطَالَ عَلَيْهِمُ الْأَمَدُ فَقَسَتْ قُلُوبُهُمْ وَكَثِيرٌ مِنْهُمْ فَاسِقُونَ 
Je, haujafika wakati kwa walioamini kwamba zinyenyekee nyoyo zao kwa dhikri[2] ya Allaah na (kwa) yale yaliyoteremka ya haki, na wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla, ukawarefukia muda, kisha zikawa ngumu nyoyo zao? Na wengi miongoni mwao ni mafasiki. (Al-Hadiyd: 16)

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Atuongoze sote na ndimi zetu zinazosema: “Tunaitaka Ramadhaan na tunaipenda” huku (niyyah zetu na) vitendo vyetu ni kinyume chake. Na uhakika wenyewe ni kwamba wako wanaosema: “Hatupendi Ramadhaan! Isitufikie! Hatutaki kuzindukana madhambi yetu na maasi! Hatutaki kuathirika tukatoka kwenye shirki, bid’ah na dhambi na hali tumeshaizoea! Tafadhali msitukere!
 Ndugu yetu Muislamu! Anza haraka kujitakasa ili Ramadhaan itakapoingia, moyo wako na viungo vyako viweze kukubali kwa sahali kutekeleza kheri nyingi. Hivi ndivyo mtu anavyojitayarisha kikweli na ndipo atakapofaidika na mwezi mtukufu wa Ramadhaan.


[1]Kumdhukuru Allaah kwa kila aina; kukumbuka Utukufu Wake, neema Zake, ihsani Yake kwa kutaja jina Lake; kumsabbih, kumpwekesha, kumshukuru, kumsifu, kumtukuza, kuomba maghfirah, kusoma Qu-raan, kumswalia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), na kwa kuzingatia na kuyataamali Majina Yake Matukufu.

[2]Kumdhukuru Allaah kwa kila aina; kukumbuka Utukufu Wake, neema Zake, ihsani Yake kwa kutaja jina Lake; kumsabbih, kumpwekesha, kumshukuru, kumsifu, kumtukuza, kuomba maghfirah, kusoma Qu-raan, kumswalia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), na kwa kuzingatia na kuyataamali Majina Yake Matukufu.

0 Comments