IDADI YA RAKAA ZA TARAAWIYH, MWISHO WAKE, NA JINSI YA KUSWALI RAKAA TATU ZA WITR

SWALI:
Asalaam aleykum wa rahmatullah waabarakaatuh,

nina swali lingine mwenzangu anauliza yeye ni mvivu wa kuswali taraweh kwa muda wake maana akishashiba anakua amechoka sasa huwa anaswali usiku akiamka kama saa 8 au 9 sasa je taraweh mwisho wake ni hadi karibu na alfajiri au? mimi nikidhsani mwisho ni saa 6 tu.

Pia sasa hivi ktk kusoma soma alhidaaya nimeona kwamba MTUME swalalahu aleyhiwasalam alikua hazidishi rakaa 11 ktk swala za usiku khasa ktk mwezi wa ramadhan sasa hiyo idadi ni pamoja na witri 3 jumla ndio ziwe 11 au?na kama nikizidisha 11 ni vibaya au?
pia wamesema witri usiswali 3 pamoja yaani uswali 2 kisha 1 isaliwe pekeyake hapo imenichanganya kwani mimi siku zote huwa naswali 3 kwa pamoja.
Jazaakallahu kheir
JIBU:


Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.


Kuhusu mwisho wa kuswali Taarawiyh, ni kabla ya Alfajr ukimalizia na Witr.

Swalah ya Taarawiyh ndio hiyo hiyo Qiyaamul-Layl na kwa mwezi huu wa Ramadhaan inaitwa Qiyaamur Ramadhaan au Taarawiyh. Mazoea yaliyojengeka ni kuiswali baada ya 'Ishaa, lakini wakati wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake (Ridhwaanu Allaahu 'alayhim) walikuwa wakiswali 'Ishaa kwa kuichelewesha kabla kidogo ya katikati ya usiku na baada ya hapo wakiendelea na Qiyaam (Taarawiyh). Ilijulikana kwa jina la Taarawiyh kwa sababu Maswahaba walikuwa wakiswali na hupumzika kila baada ya Rakaa nne au mbili, na kipumziko hicho kikaitwa Taarawiyh na ndio hiyo Swalah ikachukua mkondo wa jina hilo wakati wa Maswahaba.

Ama kuhusu Rakaa alizoswali Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ushahidi waHadiyth ya Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) iliyopokelewa na Al-Bukhaariy na Muslim ni kuwa alikuwa hazidishi Rakaa 11 wakati wa Ramadhaan na usio wa Ramadhaan katika Swalah zake za usiku. Na hizo ni 8 Taarawiyh (Qiyaamul-Layl) na 3 Witr hivyo jumla ni 11.

 
Ama kuzidisha zaidi ya hizo hakuna ubaya kwani inasemekana kuwa wakati wa Maswahaba walipokuwa Waislam wanaongezeka na kuwa na mchanganyiko wa wazee na watoto, walikuwa wakiswali 20 hadi 36 wakizifanya Rakaa fupi fupi lakini nyingi kwa sababu ya watu kuchoka na kisimamo kirefu.

Kuna Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo anasema: "Swalah ya usiku ni Rakaa mbili mbili, na ukikhofu kuingiwa na Alfajr basi malizia kwa Witr japo moja" Al-Bukhaariy

Hadiyth hiyo inaonyesha kuwa mtu anaweza kuswali Rakaa nyingi azitakazo lakini mwisho amalizie kwa Swalah ya Witr ambayo ndio Swalah ya mwisho wa usiku.

Lakini mtu kubakia katika yale yaliyothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ndio bora zaidi na salama.
Hivyo kushikamana na Rakaa 11 ni vizuri zaidi japo Sunnah hiyo imekuwa haitekelezwi na wengi na hata huko katika miji miwili mitakatifu tunaona kila mwaka katika Ramadhaan Sunnah hiyo imeachwa!

Na kuhusiana na swali lako la namna ya kuswali hiyo Swalah ya Witr, ni hivi:

Kuswali Rakaa mbili kwanza kisha utoe salaam. Kisha unamalizia na Rakaa moja na kutoa salaam.
Au kuswali Rakaa zote tatu kwa tashahhud (kikao) moja ya mwisho tu na kutoa salaam.
Haifai kuswali Rakaa tatu zote pamoja kwa kuleta Tashahhud mbili kama vile Swalah ya Magharibi, bali ni kuitofautisha na Swalah ya Magharibi kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
(( ولا تشبهوا بصلاة المغرب))


 ((… wala msiifananishe (hiyo Witr) na Swalah ya Magharibi)) [Al-Haakim, Al-Bayhaqiy, Ibn Hibbaan, Ad-Daraaqutniy]  

0 Comments