KUANDAMA KWA MWEZI : AFAUATE NCHI ANAYOISHI AU UNAPOANDAMA NCHI YEYOTE?

SWALI:
Assalaamu alaikum,
Je nifunge lini,pale mwezi unapoandama sehemu yoyote ya dunia   au mpaka utangazwe na viongozi wa kidini katika Nchi yangu. Kwa leo ni hayo tuu.
Ndugu yenu katika uislam 

JIBU:
Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kauli iliyo sahihi na yenye nguvu ni kufunga kwa kuonekana popote mwezi. Hadiyth mbalimbali zimeonyesha kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alifunga kwa taarifa za mwezi kutoka sehemu mbalimbali na vile alifungua kutokana na taarifa zilizomjia bila hata yeye kuuona mwezi. Suala hili ni refu na dalili ni nyingi.

Uislam hauna mipaka, na popote duniani Muislam atakapouona mwezi, basi anapaswa Muislam aliyesikia taarifa hizo kufunga bila kujali yuko nchi gani au mji gani. Yasemwayo kuhusu kufunga kwa kiwango cha masafa au kipimo cha vitongoji au ukaribu wa majimbo, miji na nchi, hili halina dalili katika sheria bali ni jitihada za wanachuoni.

Na mojawapo ya fadhila za kutekeleza matendo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ya kufunga kwa kuonekana mwezi popote, ni kupatikana kwa umoja na mshikamano baina ya Waislam kila sehemu duniani. Na ndipo panapoweza vilevile kupatikana siku moja ya 'Iyd duniani na Waislam wote wakawa katika furaha na sherehe pamoja.

Khitilafu na fitna tunazoziona leo hii za kufunga tofauti na kula 'Iyd tofauti hadi kufikia wengine wakila 'Iyd mwanzo hupigwa na kudhibitiwa na dola, ni matunda ya kutofahamika na kutofuatwa matendo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    na pia baadhi ya Waislam kushikamana na masimulizi ya Kurayb yenye utata na kuacha matendo ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  yasiyo na shaka wala khitilafu.

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments