KUPANA HINA NDEVU NI SUNNAH YA KUKARIBISHA MWEZI WA RAMADHAAN?

SWALI
Assalam Aleykum
Kuna kaka mmoja alikutana na mzee fulani kapaka hina ndevu zake na alipo muuliza alijibiwa kuwa eti ni njia ya kuukaribisha mwezi mtukufu wa ramadhani. Huyu kaka aka uliza mbona wengine sijaona wakipaka ndevu zao hina na yeye akajibu kuwa pengine hawatekelezi jambo hilo. Nilipo kuja kuulizwa mimi kama ni kweli kupaka hina ni kuukaribisha mwezi wa ramadhani nilikana kwa vile sikuwahi kusikia hadithi yoyote au aya ya qur an ikisema hivyo. Pengine labda ni ufinyu wa elimu nilo nayo. Naomba msaada wako. Je ni kweli kupaka hina ndevu ni kuukaribisha mwezi wa ramadhani na kama ni kweli tafadhali nipe vithibitisho ili nami nipate funuka. Nashukuru kwa majibu yako.


JIBU:


Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kupaka hina ndevu ili zigeuke rangi ya dhahabu au nyekundu ni Sunnah. Makatazo yapo ya kutokupaka rangi nyeusi, ikiwa ni ndevu au nywele. Na makatazo haya ni kwa wote wanaume na wanawake. Dalili za kuruhusiwa na makatazo ni kutokan na baadhi ya Hadiyth zifuatazo:
1-Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kwamba: Alipita mtu mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) aliyepaka rangi nywele zake kwa hina, akasema: ((Uzuri ulioje huu)). Kisha akapita mwengine aliyepaka rangi kwa hina na *katam akasema: ((Hii uzuri zaidi)). Akapita mtu mwengine aliyepaka rangi ya manjano akasema ((Hii uzuri zaidi kuliko nyingine)). [Abu Daawuud na Shaykh Al-Albaaniy amesema ni Hadiyth Hasan]
*Katam ni mti ambao unapochanganyishwa na hina hukozesha rangi ya hina, na unapotumiwa pekee unatoa rangi ya baina nyekundu na nyeusi)

2-Kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) alipoona ndevu za Abu Quhaafah ambaye ni baba yake Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimwambia ((Badilisha lakini epukana na nyeusi)) [Muslim]
3-Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) amesema: ((Watakuja watu mwisho nyakati za mwisho watakaopaka nywele zao rangi nyeusi kama lundo la njiwa. Hawatasikia hata harufu ya Pepo))  [Ahmad, Abu Daawuud, An-Nasaaiy na Shaykh Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh]
Ama kupaka ndevu kwa hina kwa ajili ya kukaribisha mwezi wa Ramadhaan, hakuna dalili ya jambo hili, hivyo inabakia kuwa ni jambo la kuzushwa na halipasi kutendwa bali likemewe ili lisiendelee kuleta mafunzo yasiyo sahihi kwa wengine kwa sababu kila ibada au jambo lolote linalohusiana na dini linahitaji dalili, bila ya dalili huwa ni jambo la kuzushwa lisilokubalika wala kuwa na thamani mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).
Kujitayarisha kwa ajili ya mwezi Mtukufu wa Ramadhaan sio kwa kujipamba mwili au kudhihirisha uzuri wa mtu, bali inahitajika kupamba nafsi kwa kuiongezea taqwa, kwa kumdhukuru sana Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), kwa kufunga Sunnah mwezi huu wa Sha’abaan  iwe mazoezi ya kujitayarisha Swawm, kuomba du’aa na kufanya mema yoyote mtu anayoweza na kujiepusha na maovu. Maswahaba walikuwa wakikaribisha mwezi wa Ramadhaan kwa matendo mema kama hayo na wakiomba du’aa. Kwa hiyo Muislamu naye anatakiwa afuate nyendo za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake na sio kufuata wanayozusha watu bila ya dalili.

Na Allaah Anajua zaidi

0 Comments