MASWALI MBALIMBALI KUHUSU SWALAH YA TARAWIYH, WITR NA DU'AA YA LAYTUL-QADR

SWALI:
Assalaam 'Alaykum Warahmatullah,
Inshalla Allah atuwezeshe kuifunga Ramadhan kwa Iman na Ikhlas na wingi wa Rehma zake, Amin.
1)  Nilikua na maswali kidogo tu kuhusu dua hii: "ALLAHUMMA INNAKA 'AFUWUN TUHIBUL-'AFUA...... Jee ina wakati maalum wa kuiomba dua hii au wakati wowote?? 
2)  Na vipi katika taraweh kama ilivyozoeleka husomwa kila baada ya salam ni sunna au haina neno au sio pahala pake. 
3) Jee kuna dua yeyote iliyosunniwa katika tareweh au.
4)  Ikitokezea kuswali Witri mara tu baada tareweh, bahati ukaamka usiku kusali kuna ubaya wowote?  Ukizingatia kwamba witri ni kama kifungio cha sala za usiku.
5)  Mwisho naomba unifahamishe sala za usiku kisunna ni rakaa ngapi, unatoa salam kila baada muda gani na sura gani inazopendekezwa kissuna kusomwa.
Inshallah Allah atatuwafikisha kwa haya.
JIBU:
Bismillahi Waswalaatu Wassalaam 'Alaa Rasuli-Llah صلى الله عليه وآله وسلم
SWALI LA KWANZA:
Nilikua na maswali kidogo tu kuhusu dua hii:"ALLAHUMMA INNAKA 'AFUWUN TUHIBUL-'AFUA...... Jee ina wakati maalum wa kuiomba dua hii au wakati wowote?? 
Kuhusu Du'aa uliyoitaja 'Allahumma Innaka 'Afuwwun Tuhibbbul-'afwa Fa'fu 'Anniy'
Dua hii unaweza kuomba wakati wowote ule unaopenda kwani ni dua'a mojawapo ya kuomba msamaha kutoka kwa Mola Mtukufu, na khaswa kuiomba siku za Laylatul-Qadr kwani ndivyo ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:
 عن عائشة رضي الله عنها أنها قالت يا رسول الله أرأيت إن وافقت ليلة القدر ما أدعو قال ((تقولين اللهم إنك عفو تحب  العفو فاعف عني)) ابن ماجه و صححه الألباني
Imetoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها kwamba alisema "Ewe Mtume صلى الله عليه وآله وسلم je, nitakaposimama usiku wa Laylatul-Qadr niombe nini?" Akasema, ((Sema Ee Mwenyeezi Mungu Hakika Wewe Ndiye Mwenye Kusamehe Unapenda Kusamehe basi nisamehe))  Ibn Maajah na kaisahihisha Albaniy
SWALI LA PILI:
Na vipi katika taraweh kama ilivyozoeleka husomwa kila baada ya salam ni sunna au haina neno au sio pahala pake
Kuombwa Du'aa hiyo na kuifanya mahsusi  katika Tarawiyh kila baada ya salaam au kuifanya mahsusi wakati ma'aalum sio Sunnah, bali kama tulivyosema kuwa wakati wowote mtu anaweza kuiomba na wakati wake maaluum ni  katika Usiku wa Laylatul-Qadr  kama ilivyothibitika katika Hadiythi hiyo ya juu.
SWALI LA TATU:
 Jee kuna dua yeyote iliyosunniwa katika tareweh au?
Hakuna Du'aa iliyokuwa Sunnah kuomba wakati wa Tarawiyh kama wanavyofanya baadhi ya watu katika kila mapumziko ya Raka'ah nne husoma tasbiihi fulani na kuzifanya mahsusi za Tarawiyh.  Hili ni jambo lisilokuwa na dalili katika Sunnah, kwa hiyo inapasa Muislamu kujiepusha nalo.
Ama katika Swalah ya Witr ikiwa ni katika Tarawiyh ya Ramadhaan au miezi mingine, dua zilizothibiti katika Sunnah ni du'aa zinazosomwa katika Qunuut, ambayo ni katika Raka'ah ya mwisho ya Witr, nazo utazipata katika kiungo hiki kifuatacho ambazo zote zimo katika Kitabu cha Hisnul-Muslim kilichokuweko katika AL HIDAAYA katika 'Duaa na Adhkaar'
Bonyeza hapa :
SWALI LA NNE  
Ikitokezea kuswali Witri mara tu baada tareweh, bahati ukaamka usiku kusali kuna ubaya wowote?  Ukizingatia kwamba witri ni kama kifungio cha sala za usiku
Hakuna ubaya wowote kuswali Swalah za baada ya kuamka usiku (Tahajjud) hata kama ulikuwa umeshaswali Witr kabla ya kulala.  Lakini ukimaliza kuswali Swalah mbili mbili utakazojaaliwa, basi haikupasi tena uswali Witr kutokana na kauli ya Mtume صلى الله عليه وآله وسلم
((لا وتران في ليلة)) رواه الترمذي
 ((Hakuna Witri mbili katika usiku)) [At-Tirmidhiy]
Maulamaa wanasema kuwa unaweza kuswali witr tena au Qiyaamul-Layl baada ya Tarawiyh (ingawa pia Tarawiyh ni Qiyaamul-Layl vilevile) usiku zaidi karibu na alfajiri kwa anayetaka lakini kwanza aswali raka’ah moja kuivunja ile witr aliyoswali na Imaam kisha ndipo aswali tena mwisho witr ya kufungia.
SWALI LA TANO:
Mwisho naomba unifahamishe sala za usiku kisunna ni rakaa ngapi, unatoa salam kila baada muda gani na sura gani inazopendekezwa kissuna kusomwa
a)   Idadi ya Swalah za Sunnah za usiku
Jumla ya Swalah za usiku za Sunnah  ni Raka'ah kumi na moja kutokana na Hadiythi ya Bibi 'Aishah ضي الله عنها
كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يصلي من الليل عشر ركعات يسلم من كل  اثنتين ثم يوتر بواحدة  مسلم
 وقالت رضي الله عنها :   ما كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يزيد في رمضان   ولا في غيره على إحدى عشرة
 ركعة يصلي أربعا فلا تسال عن  حسنهن وطولهن ثم يصلي أربعا فلا تسأل عن حسنهن وطولهن ثم  يصلي
 ثلاث    متفق عليه
Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiswali usiku Raka'ah kumi na akitoa  salam baada ya kila Raka'ah mbili kisha akiswali Witr Raka'ah moja) Muslim
Na akasema vile vile Hajapata Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuzidisha katika Ramadhaan wala miezi mingine zaidi ya Raka'ah kumi na moja, akiswali nne, wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali nne wala usiulize uzuri wake na urefu wake, kisha akiswali  tatu)) Al-Bukhariy na Muslim
 b)     Namna zinavyoswaliwa Swalah za usiku
Unatoa salam kila baada ya Raka'ah mbili kama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo:
((صلاة الليل مثنى مثنى فإذا خشيت الصبح أوتر بواحدة))" أخرجه البخاري 
((Swalah ya usiku ni (raka’ah) mbili mbili na   ukiogopa  kukukuta asubuhi  basi Swali Witr [Raka'ah] moja))  Al-Bukhariy
   c)          Sura za kusoma katika Swalah ya usiku
Hakuna Sura Maaluum ya kusomwa katika Swala za usiku, bali ni vizuri sana kusoma sura ndefu kwani kama hadithi ya Bibi 'Aishah iliyotajwa hapo juu kuwa alisema 'wala usiniulize uzuri wake'akikusudia kuwa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akiswali Swalah kwa utulivu kabisa kwa kusoma mara nyingine sura ndefu,  Rukuu ndefu, sujuud ndefu na kadhalika.
Ifuatayo ni Hadiyth inayoonyesha fadhila za kusoma aya nyingi katika Swalah ya usiku:
 ((من قام بعشر آيات لم يُكتب من الغافلين، ومن قام بمائة آية كتب من القانتين، ومن قام بألف آية كتب
 من المقنطرين (( رواه أبو داود وصححه الألباني -(والمقنطرون هم الذين لهم قنطار من الأجر)
((Atakayesimama (usiku) na aya kumi hatoandikiwa katika miongoni mwa walioghafilika, na atakayesimama kwa aya mia ataandikiwa ni miongoni mwa wanyenyekevu, na atakayesimama kwa aya Alfu ataandikwa miongoni mwa wenye mirundi)) Abu Dawuud na amesahihisha Albaniy (Maana ya mirundi ni wale walio na mrundi wa thawabu)
Ama katika Raka'ah tatu za mwisho imethibitika kuwa alikuwa akisoma sura hizi:
حديث عائشة رضي الله عنها قالت :  كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يقرأ في الركعة الأولى
 بـ { سبح اسم ربك الأعلى } وفي الثانية بـ { قل ياأيها الكافرون } وفي الثالثة بـ { قل هو الله أحد } والمعوذتين  
  أخرجه الترمذي.
Hadiyth kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها ambaye amesema ((Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akisoma katika Raka'ah ya mwanzo ya (Swalah) Witr 'Sabbihisma Rabikal-A'ala' na Raka'ah ya pili 'Qul-Yaa-Ayyuhal-Kaafiruun' na Raka'ah ya tatu 'Qul- Huwa-Allaahu Ahad pamoja na Qul-A'udhu mbili (Al Falaq na An Naas)' At Tirmidhiy
Raka'ah hizi tatu za mwisho vile vile ziswaliwe mbili kwanza kisha umalizie na moja pekee, na katika hiyo raka’ah ya mwisho bada ya kuinuka katika ruku'u usome du'aa ya Qunuut. Au ziswaliwe zote tatu kwa tash-shahud moja tu ya mwisho na kisha kutoa salaam, yaani bila kusoma At-Tahiyaat kwenye raka’a ya pili, na kufanya huku wanasema Ma'ulamaa ni kuitofautisha na Swalah ya Maghrib ambayo unakaa At-Tahiyaat kwenye raka’ah ya pili.

Wa Allaahu A'alam.

0 Comments