VUNJA JUNGU : WAMEMFANYA ALLAAH NI WA RAMADHAAN TU

بسم الله الرحمن الرحيم


BismiLlaahi waswalaatu wassalaamu ‘alaa RasuulliLLaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa ba’ad,

Ndugu Waislam,
Tunaukaribia mwezi Mtukufu wa Ramadhaan. Mwezi wenye fadhila tele zisizohesabika idadi yake. Mwezi ambao ndani yake utakapofunga Swawm yake kwa Iymaan ya dhati na kuitakidi kuwa kuna malipo, basi utasamehewa madhambi yako yaliyotangulia. Mwezi ambao haufananishwi na miezi mingine kwa mavuno na ujira, du’aa ya mfungaji haikataliwi, anapofunga Muislam huwa na furaha mbili; furaha wakati anapofungua na furaha wakati anapokutana na Mola wake. Mwezi ambao Swawm itamuombea shufaa mja siku ya Qiyaamah, itakaposema siku hiyo kumuambia Allaah, “Ee Mola, nimemzuia chakula chake, na matamanio yake ya kimwili mchana kutwa, basi niache nimwombee Shafa'ah.” *

Mwezi ambao ni hifadhi na kinga nzito kabisa ya mja kutokana na moto, na harufu ya mdomo wa aliyefunga (japo atakuwa anapiga mswaki) itakuwa ni bora kuliko harufu ya misk mbele ya Allaah. Atakayefunga siku moja katika mwezi huo akitaka radhi za Allaah na ikiwa hiyo itakuwa ndio siku ya mwisho ya maisha yake, basi ataingia peponi. Kuna mlango wa pepo maalum kwa wale wafungao uitwao Ar-Rayyaan, ambao wataingia wao tu, na watakapoingia mlango huo utafungwa na hatoingia yeyote mwengine. Huo ndio mwezi ambao ni nguzo ya Uislam, ndani yake kunapatikana usiku mtakatifu ambao ni bora kuliko miezi elfu moja, katika mwezi huo milango ya pepo huwa wazi, milango ya moto hufungwa na mashetani hufungwa minyororo. Mwezi utakapofunga wote, Swawm yake ni sawa na kufunga miezi kumi. Na katika kila wakati wa kufutari, Allaah Huchagua watu wa kuwaweka huru na moto.*

Ndugu Muislam, baada ya kujua fadhila zote hizo za mwezi huu Mtukufu, badala ya watu kujiandaa kwa mambo mema ya kheri kama kuanza kujizoesha na Swawm za Sunnah kama zile za Jumatatu na Alkhamiys, masiku meupe n.k., au kutoa Swadaqah kwa maskini ili nao wapate maandalizi mazuri ya mwezi huo wenye baraka, au kujiandaa kwa kufanya mengi ya kheri ambayo yametanawai, kinyume chake kumekuwa kuna wengi wenye majina ya Kiislam ambao huukaribisha mwezi huu Mtukufu kwa kila aina ya maasi kwa jina la ‘Vunja Jungu’ kama ijulikanavyo katika maeneo mengi Tanzania, au ‘Mfungo’ kama inavyojulikana katika maeneo ya Sawaahil (pwani) ya Kenya.

Jambo hilo licha ya kuwa halipo katika Dini yetu hii Safi, Tukufu, bali ni jambo ambalo haliwezi kufanywa na Muislam mwenye Iymaan na khofu ya Mola wake na ndio maana tukawaita hao wayafanyao hayo kuwa ni Waislam jina.
Katika masiku ya mwisho ya Sha’abaan, na haswa zaidi siku ile ya mwisho, watu hao hukusanyana na kufanya sherehe (party) kwa kusikiliza nyimbo na kucheza muziki na kunywa vinywaji vya haramu. Pombe siku hiyo kwa wale walevi ndio inanywewa kama kisasi, wengine ndio siku ya uzinzi kwa kuwa Ramadhaan wanaogopa kuyafanya hayo, wale wavuta sigara ambao kidogo wanachelea kuvuta katika mwezi wa Ramadhaan nao paketi zitavutwa kwa mfululizo, wala unga hali kadhalika na mengi mengineyo machafu huwa ndio siku yake rasmi hiyo. Bila kuwasahau wenye kwenda mapkniki na kutumbua.
Watu hao kwa kufanya hivyo, wanamkebehi na wamemfanya Allaah kuwa ni Mungu wa Ramadhaan! Ama miezi kumi na moja iliyobaki, huyo Mungu anakuwa kama hana thamani, au kuwepo kwake kumekuwa si kiutendaji!
Wengine ndio wanaukaribisha kwa kufanya manunuzi (shopping) ya mikeka ya kuswalia – maana miezi yote iliyopita, kwao mungu hakuwepo, kanzu hununuliwa kwa wingi, Misikiti huanza kushehena hadi inakuwa kero badala ya furaha kwa wale wenye kudumisha Swalah za Jama’aah kwa miezi yote ya mwaka kwani hata nafasi za mbele walizozoea kuzipata huwa ni adimu au hata kukosa kabisa kwa hao wavamizi wa Ramadhaan. Vilevile kina dada waliokuwa hawajui hata kuvaa Hijaab, basi utawaona wanaanza kununua leso za kujitanda, kanga zimeongezeka biashara, wanaojitahidi zaidi baibui nazo zimekuwa ni pato kwa wauzaji. Nyumba mbalimbali utaanza kusikia Qur-aan zikisomwa kwenye maredio, kofia na kanzu zimeanza kushamiri kwenye miili ya wengine.Hayo yote ni dhana ya wayafanyayo kuwa ni ‘heshima’ na ‘taadhima’ kwa mwezi huu. Ila walichoghafilika ndugu zetu hao, ni kuwa mafuhumu hiyo, ni mafuhumu inayoonyesha kuwa katika miezi iliyobaki, hakuna kinachowapasa wao kufanya hayo, hivyo, kumfanya Allaah Mtukufu, kuwa Kuwepo Kwake na Uwezo Wake, Nguvu Zake na Amri Zake hazina uzito wowote ila Ramadhaan tu. Nayo ni mafuhumu potofu na dhana iliyo ovu.
Ni wajibu wa jamii linapoonekana jambo lolote ovu, kulizuia, kulikemea au kulikasirikia/kulisusia endapo tutakuwa tupo katika udhaifu wa kutumia njia mbili za awali. Na hii ni amri ya Allaah(Subhaanahu wa Ta'aalaa) kama Anavyosema:
{{Na Waumini wanaume na Waumini wanawake ni awliyaa (marafiki walinzi) wao kwa wao, wanaamrisha ma-aruwf na wanakataza munkari na wanasimamisha Swalaah na wanatoa Zakaah na wanamtii Allaah na Rasuli Wake. Hao Allaah Atawarehemu. Hakika Allaah ni ‘Aziyzun-Hakiym (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika - Mwenye hikmah wa yote}} At-Tawbah: 71

Vile vile Hadiyth kutoka kwa Mtume wetu mpenzi (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) iliyosimuliwa na Abu Sa'iyd Al-Khudriy (Radhiya Allaahu  'anhu) ambaye amesema: Nilimsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akisema: "Yeyote yule atakayeona kitendo kiovu basi akiondoe (akibadilishe) kwa mkono wake, ikiwa hawezi basi kwa ulimi wake (alikemee au kukataza), na ikiwa hawezi basi kwa moyo wake (achukie) na huo (yaani kuona baya na kunyamaza) ni udhaifu wa Imani)) Muslim

UONGOFU NI ULE WA MTUME NA UPOTOFU NI KUZUSHA NA KUFANYA MAASI
Muislamu inampasa afuate mafunzo yaliyo sahihi na kujiepusha na yasiyo sahihi kwani kufuata uzushi ni kumpotosha mtu na hatari yake ni kama alivyosema  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kila khutbah yake:
Akisema katika Khutbah za Ijumaa,
((Amma Ba'ad, hakika lililokuwa bora kabisa la kuhadithia ni Kitabu cha Allaah, na uongofu ulio bora ni uongofu wa Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jambo la shari kabisa ni uzushi wake na kila uzushi ni upotofu)) [Muslim] na katika riwaaya nyingine ((na kila upotofu ni katika moto))

Na pia alieleza katika Hadiyth nyingine:
((Atakayezusha katika mambo yasiyokuwa (katika Dini) yetu basi itarudishwa [haitopokelewa]))Al-Bukhaariy na Muslim

Uzushi huu wa Vunja Jungu ambao ni mchafu na ovu, ni jambo linalopaswa kukemewa na Waislam wote wa hali zote; Mashaykh, Maimaam, Maustaadh, walinganiaji na watu wa kawaida. Katika kila mnasaba na kila khutbah kukemewe hayo hadi jamii ifahamu ubaya wake na madhara yake na mwisho mbaya ambao unaoweza kumfika mtendaji wa tendo hilo.

Kila mwenye kuvunja jungu angepaswa ajiulize wakati anapofikiria kufanya uovu wake, kuwa kufanya hivyo ni kufuata mafundisho ya nani? Ikiwa hayo hayapo katika Dini, achilia mbali kumuudhi Muumba. Ajiulize pia, ana uhakika gani wa kuwa ataishi hadi kuikuta hiyo Ramadhaan?Je, akichukuliwa katikati ya tendo lake ovu kama hilo anafikiria khatima yake ni nini? Kuna uhakika gani wa kuufika huo mwezi na kuumaliza na hata kughufuriwa madhambi hayo aliyoyatenda? Nani anayemiliki uhai mikononi mwake? Wangapi wenye siha wameondoka na siha zao? Wangapi vijana wameondoka na ubarubaru wao? Je, hawajiulizi yote hayo?

Na hao ndugu zetu wanapofikiwa na mawaidha haya, au wakapata kujua ubaya wa wayafanyayo, basi wasiwe wenye ukaidi wa kuyafuata na kuyafanyia kazi. Wasiwe kama watu wa zamani walivyokuwa wakipelekewa Mitume kuwatoa katika kiza cha kuabudu masanamu na kumshirikisha Allaah na kuwaingiza katika mwanga ya uongofu ulio na hoja za wazi, ikawa kila wakipewa mawaidha, wao hutaka kubakia katika ujinga na ukaidi wao,
{{Na haiwafikii Aayah (na ishara, dalili, hoja n.k) yoyote ile katika Aayaat zaRabb (Mola) wao isipokuwa huwa ni wenye kuipuuza.}} Al-An’aam:4

Na Ndiyo maana pia wameambiwa baada yao na sisi pia kuwa tuende tukaone hizo athari za kuangamizwa kwao ili iwe funzo kwetu:

{{Sema: “Nendeni katika ardhi, kisha mtazame vipi ilikuwa mwisho wa waliokadhibisha}} Al-An’aam:11

Athari zao hizi nyingi zimejulikana kwetu kutokana na mafunzo haya ya Qur-aan lakini ni nani mwenye kutaka kutafakari na kujitoa katika upotofu na kupata uongofu? Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kuwa hao wasiotaka kupata uongofu ni vipofu wa moyo:

{{Je, basi hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo za kutia akilini kwayo, au masikio yasikilizie kwayo; kwani hakika hayapofuki macho, lakini zinapofuka nyoyo ziliomo vifuani}} Al-Hajj:46

Naam ndugu Waislamu, mwenye kupofoka macho anaweza kuwa na iymaan ya dini, kwani wangapi waliokuwa vipofu lakini wamepata alhidaaya, wangapi wameweza kuhifadhi Qur-aan na hata kuwa ni Maulamaa wakubwa wa Ummah na mifano ni mingi. Lakini wangapi waliokuwa na macho kamili lakini wakawa ni vipofu wa nyoyo; wakiwa wametawaliwa na upotofu na ufisadi?

KUACHA MAOVU NI KUFANYA JIHAAD YA NAFSI AMBAYO NI JIHAAD BORA KABISA
Aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaaba, "Je, Hijrah gani iliyo bora?"  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu:   
 ((Ni kuhama yale Anayochukia Mola wako Mtukufu)) Swahiyh Al-Albaaniy kutoka kwa An-Nasaaiy

Hivyo mwenye kuacha maovu kama haya ya uzushi wa Vunja Jungu bila shaka atakuwa amepata daraja ya kufanya Jihaad.

Na thawabu hizo ambazo usawa wake pia ni wa Hijrah pamoja na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anaweza kuzipata mtu atakapokuwa katika twaa'a wakati wa fitnah, nao ni kama wakati wetu huu uliojaa fitnah (mitihani, misukusuko, Uislam kukabiliwa na Uadui ndani na nje n.k.) kila aina, khaswa kwa zama hizi ni mkorogo ulio katika Dini wa yale yaliyo sahihi na yaliyo ya uzushi (Bid’ah). Kwa hiyo, anapojikita mtu katika msimamo thabiti na kujiepusha na fitnah hizo, bila shaka atakuwa amepata fadhila hizo za Hijrah iliyokusudiwa:
Kutoka kwa Ma'qil bin Yasaar (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema:  Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Kufanya ibada wakati wa fitnah, ni sawa na kufanya Hijrah kwangu))Muslim

Basi na tujiepusha na yote Aliyokataza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na kuzidisha ibada kwa wingi khaswa katika miezi mitukufu na mwezi kama huu wa Sha’abaan ambao una fadhila na pia ni ni mwezi ambao tunategema kughufuriwa madhambi yetu. Kwa nini tujiongezee madhambi baada ya kughufuriwa? Tumekosa hata chembe cha shukurani kwa Mola Muumba!
Nyakati hizi ndugu Waislamu tuzitumie katika ibada ili tujichumie mema mengi, kwani ni nyakati ambazo kwa neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) zinatumiminikia kila kukicha, angalau tuzingatie na kushukuru kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
{{Naye Ndiye Aliyejaalia usiku na mchana ufuatane kwa atakaye kukumbuka au atakaye kushukuru}} Al-Furqaan:62 

Ndugu Waislam, kama wanataka kuvunja jungu kama waitavyo hao wavunjaji, basi kwanini wasifanye kama Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ambao walikuwa kila ukikaribia kuingia kwa mwezi wa Ramadhaan wakizidisha kusoma Qur-aan na wale wenye uwezo kimali wakitoa mali kuwapa maskini ili kuwapa nguvu (Kujiandaa na mfungo wa Ramadhaan). 

Ni muhimu kwa Waislamu kufanya maandalizi ya Ramadhaan kwa kujielimisha juu ya namna ya kuukabili mwezi mtukufu hasa kuelewa maana na makusudio ya funga, namna ya kufunga kwa kuzingatia masharti, mambo yanayobatilisha Swawm, pamoja na Sunnah zilizokokotezwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha namna iliyo bora ya kukaribisha funga ya Ramadhaan, hivyo tunapaswa kufunga Sunnah za Jumatatu na Al-Khamiys pamoja na kuisoma Qur-aan kwa wingi kama alivyotuagiza. 

Vilevile Ramadhaan inapoingia Waislam wanatakiwa wajiepushe kabisa na mambo yote ya laghwiambayo hupoteza Swawm kama vile kuangalia mpira, sinema za kipuuzi, misalsalaati, kucheza bao, karata, usoro, dhumna, drafti, keramu n.k. Laghwi  ni jambo lolote la kipuuzi ambalo hupoteza muda na kumsahaulisha mja kumkumbuka Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). 

Katika zama hizi Sunnah zimetengwa mbali na bid’aah ndizo zenye kufuatwa na kuwa ndio mwendo wa Waislamu wengi, kwa sababu ya ujinga wa kuigiza tu watu bila ya dalili, na kutopenda kujifunza mafunzo mema yaliyo sahihi ya Kiislamu. Mafunzo ambayo yamekamilika na kumfaa kila binaadamu popote na wakati wowote.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
{{Leo Nimekukamilishieni Dini (yenu), na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe (ndio) Dini yenu}} Al-Maaidah:3

Tunamuomba Allaah Atuthibitishe mioyo yetu katika Iymaan, na Atuongeze kwenye hidaaya, na Atughufurie madhambi yetu makubwa na madogo. Aamiyn
--------------------------------------
* Maelezo yote hayo yametolewa katika Hadiyth Sahihi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka katika vitabu vifuatavyo:
  • Swahiyhul-Bukhaariy
  • Swahiyhu Muslim
  • Musnad Ahmad
  • Swahiyhut-Targhiyb
  • Sunnan An-Nasaaiy
  • Al-Bayhaqiy
  • Silsilatus-Swahiyhah
  • Swahiyhul-Jaami’i
  • Fat-hul-Baariy

0 Comments