004-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Je, Manii Ni Twahara Au Najisi?

Wanachuoni wametofautiana katika hilo juu ya kauli mbili:
Kauli ya kwanza:
Inasema kwamba manii ni najisi. Kauli hii ameisema Abu Haniyfah na Maalik. Nayo ni riwaya iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo kwa Hadiyth ya 'Aaishah alipoulizwa kuhusu manii yaliyoingia katika nguo akasema: "Nilikuwa nikiyaosha kwenye nguo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kisha yeye hutoka moja kwa moja kwenda kuswali huku athari ya doa la maji  ikiwa katika nguo yake". Na kuosha hakuwi ila kwa kitu kilicho najisi.

Kauli ya pili:
Wenye kauli hii wamesema kuwa manii ni Twahara. Kati ya waliolisema hilo ni Ash-Shaafi'i na Daawuud Hii ni riwaya sahihi zaidi kati ya riwaya mbili iliyopokelewa toka kwa Ahmad. Wamelitolea dalili hilo kwa Hadiyth ya 'Aaishah kuhusu manii, amesema: "Nilikuwa nikiyakwangua toka katika nguo ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)"

Na kwa Hadiyth yake vile vile kwamba mgeni alishukia kwa 'Aaishah na akawa anaiosha nguo yake. 'Aaishah  akamwambia: "Bila shaka ilikuwa inakutosha ikiwa utayaona, uoshe mahala pake, na ikiwa hukuyaona, basi utanyunyizia maji kuzungukia hapo. Na bila shaka umeniona nikiyakwangua mkwanguo mmoja toka katika nguo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na yeye akaiswalia". Na kutosheka kukwangua, kunaonyesha juu ya utwahara wake.

Wenye kusema kuwa ni najisi, wamejibu kuwa kukwangua  hakuonyeshi kuwa manii ni Twahara, bali kunaonyesha namna ya kutwaharisha kama inavyokuwa katika kuvitwaharisha viatu kwa kuvipangusa katika mchanga.

Hili linajibiwa kwa kusema kuwa 'Aaishah  kuyakwangua manii mara hii na kuyaosha mara nyingine, hakuhukumii unajisi wake, kwani nguo inaoshwa kwa kuingiwa na makamasi, mate na uchafu. Na hivi ndivyo walivyosema Maswahaba wengi kama vile Sa'ad bin Abi Waqqaasw, Ibn 'Abbaas na wengineo: "Bila shaka manii ni kama makamasi na mate, jisafishe nayo japokuwa kwa kijiti."

Na kwa hili, imedhihiri kuwa kitendo cha 'Aaishah (Radhiya Allahu 'anhaa) si jingine bali ni katika mlango wa kuchagua (namna ya) usafi.

Hukumu ya utwahara wa manii inapata nguvu kwamba Maswahaba walikuwa wakiota wakati wa enzi ya Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kwamba manii ilikuwa ikiingia katika mwili wa mmoja wao na nguo yake. Na hili ni kati ya matatizo makubwa. Na lau kama yangelikuwa ni najisi, basi ingelikuwa ni lazima kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) awaamrishe wayaondoshe kama alivyowaamrisha wastanji. Na hakuna yeyote aliyelinukuu hili, na kwa hivyo imejulikana kwa yakini kuwa kuyaondosha hakukuwa ni jambo la lazima.
Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

0 Comments