005-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Je, Pombe Ni Katika Vitu Najisi?

Wanachuoni wamehitilafiana juu ya hukumu ya pombe katika kauli mbili:

Kauli ya kwanza:
Ni najisi.
Haya ni madhehebu ya karibu Maulamaa wote. Kati yao ni Maimamu wanne, na Shaykh wa Uislamu amelichagua. Na hoja yao ni neno Lake Subhaana:
«Enyi mlioamini! Bila shaka ulevi, kamari, kuabudu masanamu na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya shetani. Basi jiepusheni navyo ili mpate kufanikiwa».

Wamesema: Uchafu "Rijsu" ni najisi, wakahukumu unajisi wa pombe yenyewe kama ni najisi ya kihisia.

Kauli ya pili:
Ni Twahara.
Kauli hii wameisema akina Rubay'i, Al-Layth, Al-Muzany na watangu wema wengineo. Na imetiliwa nguvu na Ash-Shawkaany, As-Swan'aany, Ahmad Shaakir na Al-Albaaniy (Allah Awarehemu) . Na hii ndio yenye nguvu kwa dalili zifuatazo:

1- Ni kwamba katika aya hakuna dalili juu ya unajisi wa pombe. Na hii ni kwa njia zifuatazo:

(a) Ni kwamba neno uchafu "rijsu", ni katika maneno ya visawe, kwani linabeba maana nyingi. Kati ya maana hizo ni kitu kichafu, kitu kilichoharamishwa, kitu kibaya, adhabu, laana, ukafiri, shari, dhambi, najisi na kadhalika.

(b) Ni kwamba "sisi hatujakuta" au kugundua kauli ya mwanasalafi yeyote aliyefasiri "Ar-Rijsu" katika aya hii kwa maana ya najisi, bali Ibn 'Abbaas amesema: "Ar-Rijsu" ni hasira". Na Ibn Zayd amesema: "Ar-Rijsu ni shari".
  
(c) Kwamba neno "rijsu", mbali na aya hii, limekuja katika Kitabu cha Allaah katika pahala patatu, na hakuna pahala popote kati yake ambapo "rijsu" ina maana ya najisi. Katika neno LakeSubhaana: 
«Namna hivi Allaah Anajaalia uchafu (adhabu) juu ya wasioamini»,
neno "Ar-Rijsu", maana yake ni adhabu. Na katika neno Lake Subhaana kuhusu wanafiki:
 Hakika hao ni najisi, na makazi yao ni Jahannam.
Makusudio ni kuwa vitendo vyao ni vichafu, yaani ni vibaya.
Na katika neno Lake Subhaana:
«Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu».
Masanamu yameitwa uchafu kwa vile yenyewe ndio  sababu ya makamio na adhabu, na wala makusudio sio najisi ya kihisia. Kwani mawe yenyewe na masanamu si najisi.

(d) Na ilipotukia pombe katika aya kuwa imeambatana na masanamu na upigaji ramli, hilolimekuwa ni kiashirio chenye kuengua maana ya uchafu kupelekea katika unajisi usio wa kishariy'ah. Na ndivyo hivyo hivyo katika kauli Yake Subhaana: Hakika washirikina ni najisi.
zilipokuja dalili sahihi zenye kuhukumia kutokuwa najisi miili ya washirikina.

(e) Kwamba kuharamishwa pombe, hakuwajibishi unajisi wake. Ama najisi, ni lazima iharamishwe, kwani ni haramu kuvaa hariri na dhahabu ingawa vyenyewe ni Twahara ikiwa ni udharura wa kishariy'ah na kwa makubaliano ya wote.

(f) Kwamba neno "Ar-Rijsu" katika aya limezungushiwa mpaka (muqayyad)  kuwekwa ndani ya (kati ya kazi ya shetani). Kwa hiyo ni uchafu wa kivitendo, kwa maana ya kibaya au kilichoharamishwa au dhambi, na wala si uchafu wa kiini cha kitu wa kuvifanya vitu hivi kuwa ni najisi.

2- Na kati ya vinavyotolewa ushahidi juu ya utwahara wa pombe ni aliyoyasema Anas katika kisa cha kuharamishwa pombe. Anasema: "…Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwamrisha mwenye kunadi atangaze: Jueni kwamba pombe imeharamishwa,…". Akasema: "Nikatoka nikaimwaga ikatiririka katika barabara za Madiynah.

3- Na katika kisa cha mtu aliyekuwa na mapipa mawili ya pombe.
(…Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Hakika Allaah Aliyeharamisha kuinywa, Ameharamisha kuiuza)).
Na mtu yule akayafungulia mapipa mawili mpaka vikamalizika vilivyomo ndani yake…). Na laukama pombe ingelikuwa ni najisi, basi Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angeliamrisha kumwagia maji juu ya ardhi ili kuitwaharisha kama alivyoamrisha kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui, na angeliwaamuru kujikinga nayo pombe.

4- Kwamba asili yake ni Twahara. Na wala hanukuu kuhusu utwahara huo ila kinukuu sahihi. Na hakuna dalili yoyote juu ya unajisi wake na kwa hivyo, inabakia juu ya asili.

0 Comments