007-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Je, Matapishi Ya Mwanaadamu Ni Najisi?

Tumetangulia kusema mara nyingi kwamba asili ya vitu vyote ni twahara, na kwamba havihamishwi toka kwenye asili yake ila kwa kihamisho sahihi cha kutolea hoja, kisichopingana na kile chenye kutiliwa nguvu au kuwa sawa nacho. Na ikiwa tutalipata hilo, basi ni vizuri. Na kamahatukulipata hilo, itatulazimu tusimame msimamo wa kumpinga anayedai kuwa ni najisi. Kwani kudai huku kunamaanisha kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewajibisha kwa waja Wake kuviosha vitu hivyo vinavyodaiwa kuwa ni najisi, na kwamba kuwepo kwake kunazuia kuswali navyo. Basi ni ipi dalili ya hilo?!

Na matapishi na mfano wa vitu kama hivi, hakikuthibiti kwa njia sahihi (ya kuaminika) chenye kuyahamisha toka kwenye utwahara wa asili.

Na imepokelewa kuhusu matapiko kauli ya  'Ammaar akisema: "Hakika utaosha nguo yako iliyoingiwa na mkojo, kinyesi, matapishi, damu na manii".

Lakini kauli hii ni dhaifu haitolewi hoja. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi.

Na imethibiti toka kwa Abu Ad-Dardaai akisema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitapika, akafungua na akatawadha  [1]  

Katika maelezo haya, hakuna kiashirio chochote  juu ya unajisi wa matapishi, na wala hakuna dalili juu ya ulazima wa kutawadha akitapika mtu, na wala hayaonyeshi kuwa wudhuu unatenguka kwayo, bali lengo lake ni kusunisha mtu atawadhe anapotapika. Kwani kwa kitendo tu cha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakuonyeshi kuwa ni wajibu.

Pamoja na hayo, si kila chenye kutengua wudhuu kinahesabiwa kuwa ni najisi. Na Ibnu Hazmi amelielekea hili na akalichagua Shaykh wa Uislamu katika (Al-Fataawaa).[1]  Hadiyth sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (2381), na At-Tirmidhiy (87), Ahmad (6/443) na wengineo.

0 Comments