008-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Nini Hukumu Ya Majimaji (utoko) Yanayotoka Kwenye Utupu Wa Mwanamke Na Kile Kiitwacho Unyevunyevu Wa Utupu Wa Mwanamke?

Maulamaa wana mielekeo miwili kuhusu unyevunyevu wa utupu wa mwanamke: [1]   


WA KWANZA

Ni najisi, kwa vile mtoto haumbwi katika utupu kufananisha na madhii. Wametolea dalili kwa maelezo ya Zayd bin Khaalid kwamba alimuuliza 'Uthmaan bin ‘Affaan (Allaah Amridhie) akisema: "Nieleze, (nini hukumu) mtu anapomwingilia mkewe na wala hakumwaga manii? Akasema 'Uthmaan: "Atatawadha kama anavyotawadha kwa ajili ya Swalah, na ataiosha dhakari yake". 'Uthmaan akasema: "Nimeyasikia toka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)….". [2]  

Na maelezo ya Ubayy bin Ka'ab kwamba yeye alisema: "Ewe Mtume wa Allaah! Mtu akimwingilia mkewe na wala hakumwaga? Akasema:

(يغسل ما مس المرأة منه ثم يتوضأ ويصلي)

((Ataiosha sehemu aliyomgusa nayo mwanamke, kisha atatawadha, na ataswali)) [3]
Wamesema: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuamrisha kuiosha sehemu iliyogusana na utupu wa mwanamke ni dalili juu ya unajisi wa unyevu wa utupu wa mwanamke.

Mimi ninapinga (Abuu Maalik) nikisema kwamba Hadiyth hizo mbili zimefutwa [4]   na Hadiyth nyingine zenye kuamrisha kuoga kama itakavyokuja katika sehemu yake in shaa Allaah.

Na pia kuna uwezekano wa kuwa amri ya kuosha ni kutokana na madhii yanayomtoka mwanamume au mwanamke.

Vile vile wametolea ushahidi juu ya unajisi wa (majimaji hayo) kwa kuwa kwake yanatoka katika moja ya njia mbili. Na kanuni inasema:
"Chenye kutoka katika njia mbili, basi ni najisi isipokuwa manii".


WA PILI

Kwamba majimaji ya utupu ni twahara [5]   Mwelekeo huu unatolewa dalili kwa yafuatayo:

1-      Kwamba 'Aaishah - Allaah Amridhie,- alikuwa akiyakwangua manii kutoka katika nguo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yakiwa yametokana na kukutana kimwili, kwani Mtume kamwe hakuota [6]  nailhali yeye anakutana na umajimaji wa utupu. Na kwa vile sisi, lau kama tungelihukumia unajisi wa utupu wa mwanamke, basi tungelihukumu unajisi wa manii yake. Kwani manii hayo yanatokea kwenye utupu wake, na kwa hivyo yananajisika kwa unyevunyevu wake.

2-      Kwamba majimaji haya ni jambo ambalo liko wazi, nayo huwatoka sana wanawake. Na hakuna shaka kwamba jambo hili lilikuwepo kwa wanawake katika enzi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ilivyo kwa wanawake wa zama zetu hizi. Na wala haikupokelewa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha kuoga (kuosha) au kutawadha kutokana na hali hiyo.

3-      Kwamba kauli ya Maulamaa isemayo "Kila chenye kutoka kwenye njia mbili ni najisi isipokuwa manii", basi hii si kauli iliyopokelewa toka kwa Aliyehifadhiwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wala kauli hii haijafanyiwa ijmaa ya Ummah. Bali imepokelewa kwamba baadhi ya vinavyotoka toka kwenye njia mbili havitengui wudhuu, kama vile damu ya istihaadha kama itakavyokuja katika mahala pake inshaAllaah.

Ninasema (Abuu Maalik): Ninaloliona mimi ambalo lina nguvu, ni kwa ufafanuzi huu:

"Ikiwa majimaji haya yanamtoka mwanamke wakati wa kuchezeana na mumewe, au wakati ana hamu ya kujamiiana na mfano wa hili hasa, basi hayo ni madhii. Na mimi nimejua kwamba madhii ni najisi ambayo ni lazima ioshwe, na ni yenye kutengua wudhuu.

Ama ikiwa majimaji haya yanatoka kwenye utupu wa mwanamke takriban nyakati zote, na yanazidi wakati wa ujauzito, au wakati anapofanya kazi kwa bidii, au anapotembea mwendo mrefu, basi majimaji hayo ni twahara kiasili kwa kutokuwepo dalili juu ya unajisi wake. Na Allaah Ndiye Mjuzi zaidi
 
[1]   Al-Mughny (2/88), na Al-Majmu'u (1/570).

[2]   Isnad sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (292), na Muslim (347), lakini imefutwa (mansuukh).

[3]  Isnad sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (293), na Muslim (346), nayo imefutwa (mansuukh).

[4]  Angalia kwenye "Fathul Baary" (1/473).

[5]    Angalia kwenye "Jaami'i Ahkaamu An-Nasaaiy" (1/68).

[6]   Hivi ndivyo alivyosema katika "Al-Mughny" (2/88). Na Shaykh wetu amesema: "Hili linahitajia matini toka katika Qur-aan au Hadiyth, na wala hatukuikuta matini katika mfano wa hili"

0 Comments