010-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Namna Ya Kuzitwaharisha Aina Mbalimbali Za Najisi Ambazo Matini Imekuja Kuzibainisha

1- Kuitwaharisha nguo kutokana na damu ya hedhi

Inakuwa ni kwa kuikwangua na kuigandua, kisha kuisugua kwa ncha za vidole iachiane na itoke, kisha ataiosha kwa maji. Ni kutokana na maelezo ya Asmaa binti Abuu Bakr, amesema: "Mwanamke mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Mtume wa Allaah! Mmoja wetu nguo yake ikiingiwa na damu ya hedhi, afanyaje"? Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((تحته, ثم تقرصه بالماء ثم تنضحه, ثم تصلي فيه))
((Ataipikicha, kisha ataikwangua kwa ncha za vidole na maji, kisha atainyunyizia maji, na kisha atasali nayo))  [1]

Na kwa maelezo ya 'Aaishah, amesema: " Mmoja wetu alikuwa akipatwa na hedhi, kisha huikwangua damu toka kwenye nguo yake wakati anapotwaharika, kisha huiosha, na hunyunyizia maji sehemu iliyobaki, kisha huswali nayo". [2]

Na kama mwanamke atataka kutumia kijiti au kinginecho  ili aondoshee damu, au aioshe nguo kwa maji na sabuni na mfano wake katika madawa ya kusafishia, basi itakuwa ni vizuri zaidi.

Hii ni kwa maelezo ya Ummu Qays binti Muhaswan, amesema: "Nilimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu damu ya hedhi iliyoingia kwenye nguo. Akasema:

((حكيه بضلع، واغسليه بماء وسدر))

((Ikwangue kwa ujiti, na uioshe kwa maji na mkunazi)).  [3]


2- Kuitwaharisha nguo kutokana na mkojo wa mtoto mchanga

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((يغسل من بول الجارية, ويرش من بول الغلام))

((Huoshwa ikiingia mkojo wa mtoto wa kike, na hurashiwa maji ikiingia mkojo wa mtoto wa kiume)).[4]   


3- Kuitwaharisha nguo kutokana na madhii

Na  kwa vile madhii ni kitu kinachokithiri kutoka na  kuenea kwa wengi, kuyatwaharisha kumefanywa ni kwepesi na Mwekaji shariy'ah. Kwa hiyo, inatosha kuinyunyizia nguo maji sehemu iliyoingia madhii. Kwa Hadiyth ya Sahl bin Hunayf kwamba yeye alikuwa akipata tabu na uzito kutokana na madhii. Akamwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Ni vipi kwa yale yanayoingia katika nguo yangu? Akasema:

((يكفيك أن تأخذ كفا من ماء فتنضح به ثوبك حيث ترى أنه قد أصاب منه))

((Inakutosha kuchukua teko la maji, ukanyunyizia kwalo nguo yako pale unapoona yameingia)).[5]   


4- Kuitwaharisha sehemu ya nguo ya mwanamke inayoburuzika

Inaponajisika sehemu ya nguo ya mwanamke inayoburuzika, basi hutwaharika kwa kugusana na ardhi iliyo twahara. Mwanamke mmoja alimuuliza mke wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ummu Salamah akimwambia: "Hakika mimi ni mwanamke ninayerefusha ncha za nguo yangu na ninatembea sehemu chafu". Ummu Salamah akamwambia: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((يطهره ما بعده))

((Huitwaharisha (ardhi) iliyo baada yake)).[6]          


5- Kuitwaharisha soli ya viatu

Imepokelewa na Abuu Sa’iyd Allaah Amridhie kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((اذا جاء أحدكم المسجد فليقلب نعليه ولينظرفيهما, فان رأى خبثا فليمسحه بالأرض, ثم ليصل بهما))

((Anapokuja mmoja wenu msikitini, basi avigeuze viatu vyake na aangalie vina nini. Ikiwa ataona najisi, basi aipanguse kwa ardhi, kisha aswali navyo)) [7]


6- Kukitwaharisha chombo mbwa anapokilamba

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((طهور اناء أحدكم اذا ولغ فيه الكلب أن يغسله سبع مرات أولاهن بالتراب))                     


((Kukitwaharisha chombo cha mmoja wenu anapokilamba mbwa ni kukiosha mara saba, moja kati ya hizo kwa mchanga)). [8]    


7- Kuitwaharisha ngozi ya nyamafu

Ni kwa kuitia rangi. Kwa neno lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((اذا دبغ الاهاب فقد طهر)  
((Inapotiwa rangi ngozi ya nyamafu, basi imetwaharika))  [9]

8- Kuitwaharisha ardhi iliyoingia mkojo na mfano wake

Inakuwa ni kwa kumiminia (maji) juu yake. Kama alivyomrisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwagia maji juu ya mkojo wa bedui msikitini [10]   Bila shaka aliamuru hilokwa ajili ya kuharakia usafi. Na kama si hivyo, lau kama angeliacha mpaka ukakauka na athari ya najisi ikaondoka, basi (ardhi) ingetwaharika.


9- Kukitwaharisha kisima au samli inapoingia ndani yake najis

Inakuwa ni kwa kuichota na kuiondosha najisi na sehemu za pambizoni mwake, na iliyosalia inabakia twahara. Ni kwa Hadiyth ya Ibnu ‘Abbaas kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu panya aliyeangukia katika samli akasema:

((ألقوها, وما حولها فاطرحوه, وكلوا سمنكم))
((Mtupeni, na sehemu za pambizoni mwake ziondosheni, na samli yenu kuleni)) [11]  
 
[1]   Hadiyth sahihi: Ameitoa Al-Bukhaariy, na Muslim (291).

[2]   Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (308), na Ibnu Maajah (630).

[3]   Hadiyth hasan: Imetolewa na Abuu Daawuud (363), na An-Nasaaiy (1/195), na Ibnu Maajah (268).  
[4]   Hadiyth sahihi kwa nyingineyo: Imetolewa na Abuu Daawuud (376), na An-Nasaaiy (1/158), na Ibnu Maajah (526).  
[5]   Hadiyth hasan: Imetolewa na Abuu Daawuud (383), na At-Tirmidhiy (143), na Ibnu Maajah (531).

[6]   Hadiyth sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (383), na At-Tirmidhiy (143), na Ibnu Maajah (531).
[7]    Hadiyth sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (646). 
[8]    Hadiyth sahihi: Imetolewa na Muslim (279), na Abuu Daawuud (71). 
[9]   Hadiyth sahihi: Imetolewa na Muslim na mwingine.

[10]   Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (219), na Muslim (284).

[11]   Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (Vichinjwa – Mlango wa 34).

0 Comments