012-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kustanji (kuchamba)

MAANA YA KUSTANJI

Kustanji ni neno la Kiarabu lililo katika mizani ya "istif'aal". Limetokana na kitenzi: (نجوت الشجرة)yaani: "Nimeukata mti". Ni kana kwamba amejiondoshea adha.

Na katika istilahi ni kuondosha chenye kutoka kwenye njia mbili
(القبل و الدبر)   (mbele na nyuma) kwa jiwe au karatasi na mfano wake.

Pia huitwa (Al-Istijmaar) kwa vile mtu hutumia vijiwe vidogo katika kuchamba. Pia huitwa (Al-Istitwaabah), kwa vile mtu huutakasa mwili wake kwa kuuondoshea uchafu  [1]  HUKUMU YAKE

Kustanji ni lazima kwa kila kilichozoeleka kutoka katika njia mbili kama mkojo, madhii na kinyesi - kwa mujibu wa jamhuri ya Maulamaa kinyume na Abuu Haniyfah [2]      kwa neno lake Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 ((إذا ذهب احدكم إلى الغائط فليستطب بثلاثة احجار فإنها تجزيء عنه))((Anapokwenda mmoja wenu haja, basi astanji kwa vijiwe vitatu, kwani humtosheleza))[3]   


Na hii ni amri, nayo ni amri ya lazima. Kisha neno lake:

((فإنها تجزيء))

((kwani humtosheleza))


Na neno kutosheleza hutumika katika wajibu. Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((لا يستنجى أحدكم بدون ثلاثة أحجار))

((Asistanji mmoja wenu kwa chini ya vijiwe vitatu)).[4]   

Na kukataza kupunguza chini ya vijiwe vitatu, kunahukumia uharamu. Na itakapokuwa ni haramu kuacha baadhi ya najisi, basi kuiacha yote ni vibaya zaidi.NI KWA KITU GANI HUSTANJIWA?

Inatosha kustanji kwa moja ya vitu viwili:

1-                  Mawe na mfano wake kati ya kila kitu kigumu chenye  kuondosha najisi na kisichothaminika.

Ni kama karatasi, vitambaa, mbao na vile ambavyo utakasifu wa najisi unapatikana.

Imepokelewa toka kwa mama wa waumini 'Aaishah kwamba (Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:


((إذا ذهب احدكم إلى الغائط فليستطب بثلاثة احجار فإنها تجزيء عنه))

((Anapokwenda mmoja wenu haja, basi astanji kwa vijiwe vitatu, kwani hivyo humtosheleza)) [5]


Na wala haijuzu kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu kutokana na haya yafuatayo yenye uzito:

(b)  Ni kwa Hadiyth ya Salmaan, amesema:

"Hakika alitukataza sisi (yaani Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuelekea Qibla wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, au kuchamba kwa mkono wa kulia, au kuchamba kwa chini ya vijiwe vitatu, au kuchamba kwa kinyesi au mfupa".    [6]

                                                                                                                                             
(b) Imepokelewa toka kwa Jaabir, amesema:  

Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((إذا استجمر أحدكم فليستجمر ثلاثا))

((Anapochamba mmoja wenu kwa vijiwe, basi achambe mara tatu))  [7]    


(c) Imepokelewa toka kwa Khilaal bin As-Saaib toka kwa baba yake ikiwa ni marfuu'i:

((إذا  دخل أحدكم الخلاء فليتمسح بثلاثة أحجار))

((Anapoingia mmoja wenu msalani, basi ajipanguse kwa vijiwe vitatu)) [8]  
Ninasema (Abuu Maalik): "Ikiwa patasafika kwa vijiwe vitatu, basi ni vyema. Na kama si hivyo, itabidi kuongeza zaidi ya vitatu mpaka pasafike".


Na wala haijuzu kuchamba kwa mifupa au kinyesi cha mnyama kutokana na Hadiyth ya Ibnu Mas'uud kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((لا تستنجوا بالروث، ولا بالعظام، فإنه زاد إخوانكم من الجن))

((Msistanji kwa kinyesi cha mnyama wala mifupa, kwani hivyo ni masurufu ya ndugu zenu (katika majini)) [9]  


Na imepokelewa toka kwa Ibnu Masu'ud, amesema:

"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda haja, akaniamuru nimletee vijiwe vitatu. Nilivipata vijiwe viwili na nikakitafuta cha tatu lakini sikukipata. Nikachukua kinyesi cha mnyama nikamletea. Alivichukua vijiwe viwili na akakitupa kinyesi. Akasema:
((هذا ركس))

((Hii ni najisi))[10]    


2- Maji

Imepokelewa toka kwa Anas, amesema:

"Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiingia msalani, na mimi na kijana pembeni mwangu tunabeba ndoo ya maji na kiegemeo, na yeye (Mtume) akistanji kwa maji" [11]

Na kustanji kwa maji ni bora zaidi kuliko kustanji kwa mawe, kwani Allaah Mtukufu Amewasifu watu wa Qubaa kwa kustanji kwao kwa kutumia maji.

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah – Allaah Amridhie – ikiwa marfu'u:
"Aya hii iliteremka kwa watu wa Qubaa:
(( فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُواْ))

« Humo wamo watu wanaopenda kujitakasa » [12]  

Akasema: "Walikuwa wakistanji kwa maji, na aya hii  ikateremka kuwazungumzia wao"[13]        

At-Tirmidhiy anasema (1/31): Huko ndiko kunakotumiwa na Wanachuoni. Wanachagua kustanji kwa maji ingawa kustanji kwa mawe kunatosha kwao. Hakika wao wamependelea kustanji kwa maji na wamelionelea hilo ni bora zaidi. Na hayo hayo ameyasema Sufyaan Ath-Thawriy, Ibnu Al-Mubaarak, Ash-Shaafi'iy, Ahmad na Is-haaq.


MTU HASTANJI KWA KUJAMBA, WALA SI LAZIMA KUSTANJI KABLA YA KUTAWADHA

Mwenye kutokwa na upepo au akaamka toka usingizini, basi si lazima astanji. Ibnu Qudaamah anasema:
" Hatujui katika hili mahitilafiano yoyote".
Abuu Abdillah anasema:
"Hakuna katika Kitabu cha Allaah wala katika Hadiyth za Mtume Wake, kustanji (mtu) kwa kujamba, bali ni juu yake atawadhe".
Na imepokelewa toka kwa Zayd bin Aslam katika neno Lake Allaah Mtukufu:

((إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلاةِ فاغْسِلُواْ وُجُوهَكُمْ))

« Mnaposimama kwa ajili ya swalah, basi osheni nyuso zenu »: [14]

"Mnapotoka usingizini, na wala Hakuamuru kwa jinginelo. Kwa  hivyo basi, inaonyesha kwamba hailazimu, na kwa vile jambo la wajibu (linaelezewa) na sheria. Na hapa aya haikutaja kustanji, wala kustanji huko hakuko katika maana iliyoelezewa, kwani kustanji kumewekwa kwa ajili ya kuondosha najisi, na hapa hakuna najisi.."[15]   

Na si lazima kustanji kwanza kabla ya kutawadha (yaani kuunganisha). Hilo halikusuniwa na wala halikupendezeshwa kama wanavyodhani watu wengi, bali hiyo ni ibada peke yake kando. Na makusudio yake ni kupatakasa mahali kutokana na najisi. Na wala hakuna yeyote aliyenukuu kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akistanji kila anapotawadha au aliamuru hilo.
 
[1]  Al-Mughniy (1/205).
[2]    Mahanafi wamesema: "Kustanji ni Sunnahh iliyokokotezwa madhali najisi haikupetuka sehemu ya haja. Wametolea ushahidi Hadiyth isemayo: ((Mwenye kuchamba kwa mawe, basi afanye kwa witiri. Atakayefanya (hivyo), basi amefanya vizuri, na ambaye hakufanya, basi hapana ubaya)). Na hii ni Hadiyth dhaifu. Tazama kwenye "Dhwa'iyfu Al-Jaami'i" (5468).
[3]   Hadiyth Hasan kwa vishuhudilio vyake: Ameitoa Abuu Daawuud (40), An-Nasaaiy (1/18), Ahmad (6/108-133) kwa sanadi dhaifu. Ina vishuhudilio vinavyoitilia nguvu. Tazama kwenye "Al-Irwaa" (44).

[4]    Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (262), An-Nasaaiy (1/16), At-Tirmidhy (16) na Abuu Daawuud.

[5]    Hadiyth Hasan kwa vishuhudilio vyake: Imetolewa na Abuu Daawuud (40), An-Nasaaiy (1/18), Ahmad (6/108-133) kwa sanadi dhaifu. Ina vishuhudilio vyenye kuitilia nguvu.
[6]    Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (262), An-Nasaaiy (1/16), At-Tirmidhiy (16) na Abuu Daawuud.
[7]   Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Ahmad, Ibnu Abuu Shaybah na Ibnu Khuzaymah. Na Al-Huwayny (Allah Amhifadhi) amesema kwamba sanadi yake ni sahihi katika "Badhlu Al-Ihsaan" (1/351).
[8]    Hadiyth Hasan kwa yaliyotangulia: Imetolewa na At-Twabaraaniy katika "Al-Kabiyr" (7/6623). Angalia "Al-Badhlu" (1/352). 
[9]    Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (682), At-Tirmidhiy (18) na Ahmad (1/436).
[10]   Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (156) na wengineo. Imekwishatangulia.
[11]   Imetolewa na Al-Bukhaariy (151), Muslim (270, 271) na wengineo.

[12]    Surat At-Tawbah aya ya 108.
[13]    Hadiyth Hasan kwa vishuhudilio vyake: Imetolewa na Abuu Daawuud (44), At-Tirmidhiy (3100), Ibnu Maajah (357) kwa sanadi dhaifu. Ina vishuhudilio vinavyoitilia nguvu. Angalia kwenye "Al-Irwaa" (45).
[14]   Surat Al-Maaidah aya ya 6.

[15]    "Al-Mughny" ya Ibnu Qudaamah (1/206) chapa ya Hajar

0 Comments