013-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Baadhi Ya Adabu Za Kustanji

Kati ya adabu ambazo inatakikana mtu ajipambe nazo wakati wa kustanji ni:

1- Asistanji kwa mkono wa kulia
Ni kutokana na Hadiyth ya Abuu Qataadah, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((لا يمسكن أحدكم ذكره بيمينه وهو يبول، ولا يتمسح من الخلاء بيمينه، ولا يتنفس في الاناء))

((Asikamate kabisa mmoja wenu uume wake kwa mkono wake wa kulia wakati wa kukojoa, wala asijisafishe haja kwa mkono wake wa kuume, wala asipumulie ndani ya chombo)).([1])

Na imepokelewa toka kwa Salmaan, amesema: “Mtu mmoja aliniambia: “Hakika mwenzenu huyu anawafundisheni hata kwenda haja kubwa”. Akasema (Salmaan): “Ndiyo. Ametukataza kuelekea Qiblah wakati wa kukidhi haja kubwa au ndogo, ametukataza kustanji kwa mikono yetu ya kulia, au kustanji kwa chini ya vijiwe vitatu”.([2])

2- Asiuguse utupu kwa mkono wake wa kulia

Ni kwa Hadiyth ya Abuu Qataadah iliyotangulia.

3- Ausugue mkono wake ardhini (kwenye udongo), au auoshe kwa sabuni na mfano wake baada ya kustanji

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa akiingia msalani, nilikuwa nikimpelekea maji katika kijindoo kidogo, halafu hustanji na kisha huupangusa mkono wake juu ya ardhi”.([3])
Hili linatiliwa nguvu na Hadiyth ya Maymuna isemayo: “Kisha Mtume alijimwagia maji juu ya utupu wake, akauosha kwa mkono wake wa kushoto, kisha akaupiga mkono wake juu ya ardhi, halafu akauosha”.([4])

4- Aunyunyizie utupu wake na nguo yake maji baada ya kukojoa ili kuondosha shaka na wasiwasi


Imepokelewa na Ibn ‘Abbaas kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitawadha mara moja, halafu akaunyunyizia maji utupu wake.([5])

NAMNA MGONJWA WA KICHOCHO AU MFANO WAKE ANAVYOSTANJI

Aliyepatikana namtihani wa kupatwa na kichocho, atastanji na kutawadha kwa kila Swalah. Na vile vinavyomchuruzika havina madhara yoyote kwake madhali wakati wa Swalah nyingine haujaingia. Na hii ndiyo kauli sahihi zaidi kati ya kauli mbili za Maulamaa. Kauli hii imesemwa na Abuu Haniyfah, Ash-Shaafi’iy, Ahmad, Ishaaq, Abuu Thawr na wengineo.

Aliyepata mtihani wa ugonjwa huu, atakuwa na hukumu ya damu ya istihaadha. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelizungumzia hilo aliposema:

((انما ذلك عرق، وليست بالحيضة، فاذا أقبلت الحيضة فدعي الصلاة، فاذا ذهب قدرها، فاغسلي عنك الدم وصلي))                                                                                                                        
((Hakika hiyo ni damu ya mshipa na wala si damu ya hedhi. Na hedhi inapokujia, basi acha kuswali. Muda wake unapomalizika, oga ujitwaharishe na damu, kisha swali)). ([6])

Na kwa upande wa Al-Bukhaariy, amesema: Na akasema Ubayy: “Kisha tawadha kwa kila Swalah mpaka uje wakati huo”.([7])

Ninasema (Abuu Maalik): Hukumu hii bila shaka ni kwa mwenye udhuru kwa ajili ya kumwondoshea uzito. Na hakuna shaka kuwa sheria imekuja kwa ajili ya kuuondoshea umma uzito. Allaah Mtukufu Anasema:

«  يريد الله بكم اليسر ولا يريد بكم العسر »                                     
«Allaah Anawatakieni wepesi na wala Hawatakieni uzito»([8])

Maalik na wengineo wanaona kwamba haimpasi mgonjwa huyo kustanji wala kutawadha ila tukama atapata hadathi nyingine.

Ninasema (Abuu Maalik): Ama kutokupasa kutawadha kwa kila Swalah endapo kama hajapata hadathi, huenda hilo lina mwono kwa wale waliotia udhaifu katika kuongezwa neno “na utawadhe kwa kila Swalah” katika Hadiyth iliyotangulia. Na lenye nguvu hapa ni kutawadha kwa kila Swalahkama itakavyokuja katika mlango wa hedhi. Ama kutopasa kustanji, basi hilo halina cha kuzungumziwa, kwani anaweza kutokwa na kinacholazimisha kustanji na akawa na wasaa wa kufanya hivyo kabla ya Swalah bila ya uzito wowote. Anachosamehewa ni kile tu kinachomtoka wakati wa Swalah kwa ajili ya kuepuka uzito. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 ADABU ZA KUKIDHI HAJA

Mwenye kutaka kukidhi haja ndogo au kubwa, inatakikana ajipambe kwa adabu zifuatazo:
 1.   Ajisitiri na ajiweke mbali na watu na hasa hasa uwandani. 
Imepokelewa na Jaabir (Radhi za Allaah ziwe juu yake), amesema: “Tulitoka na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika safari. Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa hafiki uwandani, isipokuwa hupotea asionekane”.([9])

2- Asiwe na kitu chenye utajo wa Allaah Mtukufu([10])

Ni kama vile pete iliyotiwa nakshi ya Jina la Allaah na vinginevyo. Hii ni kwa vile kulitukuza Jina la Allaah Mtukufu ni jambo ambalo kidini linajulikana na wote. Allaah Mtukufu Anasema:

 ((ذلك ومن يعظم شعائر الله فانها من تقوى القلوب))   

«Ndivyo hivyo! Na anayetukuza ibada za Allaah, basi hayo ni katika unyenyekevu wa moyo»([11])

Hii ni kwa yaliyopokelewa toka kwa Anas kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiivua pete yake anapoingia msalani.([12]) Lakini hii ni Hadiyth Munkar iliyotiwa doa.

Na linalojulikana ni kwamba pete ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilikuwa imetiwa nakshi iliyoandikwa “Muhammad Mtume wa Allaah”.([13])

Ninasema (Abuu Maalik): “Ikiwa pete hii au mfano wake imesitiriwa kwa kitu kama kuwekwa mfukoni au sehemu nyingine kama hiyo, basi itajuzu kuingia nayo. Ahmad bin Hanbal anasema: “Akitaka ataifumbata katika kiganja chake”.
Ikiwa atahofia kupotea kama ataiacha nje, basi itajuzu kuingia nayo kwa vile imelazimu. Na Allaah Ndiye Ajuaye Zaidi.

3- Apige BismiLlaah na ajilinde kwa Allaah wakati wa kuingia msalani
Atafanya hivi kama ataingia sehemu iliyojengwa (choo). Lakini kama itakuwa ni uwandani, basi atafanya hivyo wakati anapoinyanyua nguo yake. Hii ni kwa neno lake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((ستر مابين الجن وعورات بني آدم اذا دخل أحدهم الخلاء أن يقول: بسم الله))
                       
((Sitara iliyoko kati ya jini na utupu wa wanaadamu anapoingia mmoja wao msalani, ni kusema BismiLlaah)).([14])

Na imepokelewa na Anas (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapoingia msalani husema:

  ((اللهم اني أعوذ بك من الخبث والخبائث))

((Ewe Mola! Hakika mimi ninajilinda Kwako na majini wa kiume na majini wa kike)).([15])  

4- Atangulize mguu wa kushoto wakati wa kuingia, na mguu wa kulia wakati wa kutoka
  
Abuu Maalik: Sikupata katika hili matini husika toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Ash-Shawkaaniy amesema katika “As-Saylu Al-Jarraar” (1/64): Ama kutanguliza mguu wa kushoto wakati wa kuingia na mguu wa kulia wakati wa kutoka, basi hili lina hekima yake. Ni kuwa vitu vitukufu huanziwa kwa kulia na visivyo vitukufu huanziwa kwa kushoto. Na bila shaka yenye kuonyesha hilo yamekuja katika sentensi….”

5- Asielekee Qiblah au kukipa mgongo wakati anapokaa kukidhi haja

Ni kwa Hadiyth ya Abu Ayyuub Al-Answaariy (Radhi za Allaah ziwe juu yake) aliyepokea toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), amesema:

اذا أتيتم الغائط فلا تستقبلوا القبلة ولا تستدبروها، ولكن شرقوا أو غربوا 
              
((Mnapokwenda haja kubwa, msikielekee Qiblah wala msikipe mgongo, bali elekeeni mashariki au magharibi)).

Abuu Ayyuub anasema: “Tukafika Shaam, tukakuta vyoo vimejengwa kuelekea Ka’abah, tukawa tunakiepa na kumwomba Allaah Mtukufu maghfira”.([16])

Lakini hata hivyo, imepokelewa kwa njia sahihi toka kwa Ibn ‘Umar kwamba amesema: “Siku moja nilipanda juu ya paa la nyumba yetu, nikamwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya matofali mawili akikidhi haja na ilhali ameelekea Baytul Maqdis”.([17])

Na ikiwa ameelekea Baytul Maqdis na yeye yuko Madina, basi atakuwa ameipa mgongo Ka’abah!!

Ninasema (Abuu Maalik): Na ili tuzifahamu Hadiyth hizi mbili, hebu tuziangalie kauli nne mashuhuri za Maulamaa ([18])

1- Ni kuwa katazo la kuelekea Qiblah na kukipa mgongo ni kwa hali zote sawasawa ikiwa ndani ya jengo au uwandani.

Haya ni madhehebu ya Abuu Haniyfah, Ahmad na Ibnu Hazm. Shaykh wa Uislamu pia ana msimamo huu. Ibnu Hazm amelinukulu hili toka kwa Abuu Hurayrah, Abuu Ayyuub, Ibn Mas’ud na Suraaqah bin Maalik. Pia amepokea toka kwa Atwa’a An-Nakh’i, Ath-Thawriy, Al-Awzaa’iy na Abuu Thawr.([19]) Wametoa hoja yao kwa kuitumia Hadiyth ya Abuu Ayyuub iliyotangulia.


2- Ni kuwa katazo hilo linahusiana na sehemu wazi tu lakini si ndani ya jengo.

Hili limesemwa na Maalik na Ash-Shaafi’iy. Kwa kauli yao hii, wao wamepitia mkondo wa kukusanya baina ya dalili mbili. Wamesema: “Kanuni isemayo “Kauli hutangulizwa kabla ya kitendo”, bila shaka hutumiwa katika hali ya kuthibiti umahususi, na umahususi huo hauna dalili yoyote”.

3- Ni kuwa inajuzu kukipa mgongo Qiblah lakini haifai kukielekea.
Hili limehadithiwa toka kwa Abuu Haniyfah na Ahmad, wakiuchukulia udhahiri wa Hadiyth ya Ibn ‘Umar na Hadiyth ya Abuu Ayyuub.

4- Ni kuwa inajuzu kuelekea Qiblah na kukipa mgongo katika hali zote.
Hii ni kauli ya ‘Aaishah, ‘Urwah, Raby’a na Daawuud. Hoja yao wanasema kuwa Hadiyth zimegongana, na kwa hivyo suala linarejea katika asili yake ya uhalali.

Ninasema (Abuu Maalik): Huenda kauli ya kwanza ya kuharamisha kabisa hali zote mbili, ndiyo dalili yenye nguvu zaidi na yenye kinga zaidi kuitumia. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

6- Ajiepushe kabisa na maneno ila kwa dharura

Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema kwamba mtu mmoja alimpitia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ilhali anakidhi haja ndogo, akamsalimia na wala Mtume hakujibu.([20])

Na kurejesha maamkizi ni jambo la lazima. Na Mtume alipoacha kujibu, inaonyesha kuwa ni haramu kuzungumza na hasahasa kama ni kumtaja Allaah Mtukufu. Lakini ikiwa atazungumza kwa ajili ya haja isiyoepukika kama kumwongoza mtu, au kuomba maji au mfano wa hayo, basi itaruhusika kutokana na dharura. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

7- Ajiepushe kukidhi haja njiani wanamopita watu, sehemu wanapopumzikia kupata kivuli na mfano wa sehemu hizo

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((اتقوا اللاعنين))، قالوا: وما اللاعنان يا رسول الله؟ قال: (( الذي يتخلى في طريق الناس أو في ظلهم))

((Waogopeni wawili waliolaaniwa)). Wakasema: Ni nani hao wawili waliolaaniwa ewe Mtume wa Allaah? Akasema: ((Ni yule anayejisaidia njiani wanamopita watu au katika kivuli chao)).([21])

8- Ajiepushe kukojoa mahala pa kuogea

Na hasahasa kama maji yanajikusanya mahala hapo kama kwenye hodhi (bath tub) na kadhalika. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kukojoa mahala anapoogea.([22])

9.- Ajiepushe kukojoa katika maji yaliyotuama tuli

Ni kwa Hadiyth ya Jaabir aliyesema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza watu wasikojoe katika maji yaliyotuama.([23])

10- Akusudie sehemu laini wakati wa kukojoa na ajiepushe sehemu ngumu ili kujikinga najisi isije kumrukia

11- Ashikamane na adabu za kustanji tulizotangulia kuzitaja.

12- Aseme wakati anapotoka: “Ghufraanak”.
Imepokelewa toka kwa ‘Aaishah akisema kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa anatoka msalani, alikuwa akisema: “Ghufraanak”.([24])

  JE, INAFAA MTU KUKOJOA KWA KUSIMAMA?

Katika mlango huu, kuna Hadiyth tano toka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Tatu kati ya hizo, ni sahihi. Katika Hadiyth ya kwanza, ‘Aaishah anakanusha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kusimama. Na katika Hadiyth ya pili, inaelezwa kuwa alikojoa kwa kusimama. Ama Hadiyth ya tatu, inaelezwa kuwa alikojoa kwa kukaa (kuchuchumaa).

Ama Hadiyth mbili dhaifu, moja inakataza kukojoa kwa kusimama na nyingine inakuelezea kukojoa kwa kusimama kama ni utovu wa heshima. Hadiyth zenyewe ndizo hizi:

1- Hadiyth ya ‘Aaishah, amesema: Atakayewaambieni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikojoa kwa kusimama, basi msimsadiki. Hakuwa akikojoa ila kwa kukaa”.([25])

2- Hadiyth ya Hudhayfah, anasema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda mwishoni mwa jalala akakojoa kwa kusimama. Mimi nilijivuta kando, lakini aliniambia nikurubie. Nilikurubia mpaka nikasimama nyuma yake, akatawadha na kupukusa juu ya khofu zake.([26])

3- Ni Hadiyth ya Abdur-Rahmaan bin Hasanah, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea akiwa ameshika mkononi mwake kitu kama ngao. Alikiweka kitu hicho, kisha akakaa nyuma yake na kukojoa”.([27])

4- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar, amesema: “Alisema ’Umar: Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniona nikikojoa kwa kusimama akaniambia:

((يا عمر، لا تبل قائما))    
((Ewe ‘Umar! Usikojoe kwa kusimama))
Akasema: “Sikukojoa tena kwa kusimama”.([28])

5- Imepokelewa toka kwa Buraydah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((ثلاث من الجفاء: أن يبول الرجل قائما، أو يمسح جبهته قبل أن يفرغ من صلاته، أو ينفخ في سجوده))

((Mambo matatu ni utovu wa adabu: Mtu kukojoa kwa kusimama, au kuupangusa uso wake kabla hajamaliza kusali, au kupuliza wakati yuko katika sijdah)).([29])

Ninasema (Abuu Maalik): Kutokana na Hadiyth hizi, Maulamaa wametofautiana juu ya hukumu ya kukojoa kwa kusimama katika kauli tatu. ([30])

1- Ni karaha bila ya udhuru

Haya yamesemwa na ‘Aaishah, Ibn Masu’d na Umar katika moja ya riwaya mbili. Pia Abuu Muusa, Ash-Sha’abiy, Ibn ‘Uyaynah, Hanafiy na Shafi’iy.

2- Kunajuzu kwa hali yoyote
  
Haya yamesemwa na ‘Umar (katika riwaya ya mwisho), ‘Aliy, Zayd bin Thaabit, Ibn ‘Umar, Sahl bin Sa’ad, Anas, Abuu Hurayrah na Hudhayfah. Hii ndiyo kauli ya wafuasi wa madhehebu ya Hanbali.

3- Kama mtu yuko sehemu laini ambapo mkojo hauwezi kumrukia itajuzu, lakini kama si hivyo ajizuie.

Ni madhehebu ya Maalik. Kauli hii imeungwa mkono na Ibn Al Mundhir.

Ninasema (Abuu Maalik): Lenye nguvu ni kwamba hakuna ukaraha wowote wa kukojoa kwa kusimama madhali mtu ana uhakika kwamba mkojo hauwezi kumrukia. Hii ni kwa sababu zifuatazo:

1- Ni kwamba hakuna Hadiyth yoyote sahihi iliyopokelewa toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyokataza hilo.

2- Ni kuwa yaliyopokelewa kuhusu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kukaa (kuchuchumaa), hayapingani na kujuzu kukojoa kwa kusimama, bali hilo linaashiria kujuzu kwa yote mawili.
3- Ni kwa kuthibitika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikojoa kwa kusimama.

4- Ni kuwa ‘Aaishah kukanusha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kukojoa kwa kusimama, kumejengewa juu ya kile anachokijua yeye kwa mujibu wa yale ambayo Mtume anayafanya akiwa nyumbani. Kwa hiyo kukojoa kwake nje ya nyumba yake kwa kusimama, hakukanushiki. Na aliyejua kama vile Hudhayfah na wengineo, ni hoja kwa yule ambaye hakujua, na kwamba jambo yakinishi hutangulizwa kabla ya kanushi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 SUNNAH ZA HULKA ASILI

Nini maana ya Sunnah za hulka asili? Ni zipi Sunnah hizo?
Sunnah za hulka asili ni mambo ambayo mtu akiyafanya, huipata hulka asili ambayo Allaah Amewaumbia kwayo waja, Atawakusanya (Atawafufua) juu yake, na Amewapendelea kwayo, ili wawe juu ya ukamilifu wa sifa na utukufu wa sura.

Mambo haya ni mwenendo wa kale ambao Manabii waliuchagua na sheria zote zikakubaliana juu yake. Inakuwa ni kama jambo la kimaumbile waliloumbiwa kwalo watu.([31])

Maslaha ya kidini na kidunia hufungamana na mambo ya hulka asili ambayo hudirikiwa kwa ufuatiliaji. Kati ya mambo hayo ni kuliweka umbo katika picha nzuri na kuutakasa mwili ndani na nje.([32])

Baadhi ya mambo haya yamepokelewa katika haya yafuatayo:

1- Hadiyth ya Abuu Hurayrah, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((الفطرة خمس: الختان، والاستحداد، وقص الشارب، وتقليم الأظافر، ونتف الآباط))
          
((Hulka asili ni mambo matano: Kutahiri, kunyoa kinena (mavuzi), kunyoa sharubu, kukata kucha na kunyofoa nywele za vikwapa)).([33])

2- Hadiyth ya ‘Aaishah, amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((عشر من الفطرة: قص الشارب، واعفاء اللحية، والسواك، واشتنشاق الماء، وقص الأظفار، وغسل البراجم، ونتف الابط، وحلق العانة، وانتقاص الماء))
                                                                   
((Mambo kumi ni katika hulka asili: Kunyoa sharubu, kuziachilia ndevu, kupiga mswaki, kupaliza maji puani, kukata kucha, kuosha vifupachanda, kunyofoa nywele za kwapa, kunyoa kinena na kustanji)).

Mus’ab mmoja wa wapokezi wa Hadiyth anasema: “Nimelisahau la kumi kama halitakuwa ni kusukutua”.([34])

Kutokana na Hadiyth mbili tunafahamu kuwa mambo ya hulka asili hayaishilii kwenye haya kumi tu, lakini yako mengineyo. Kwa ufupi mambo haya ni:
1- Kutahiri.
2- Kustanji.
3- Kupiga mswaki.
4- Kukata kucha.
5- Kukata sharubu.
6- Kuachilia ndevu.
7- Kunyoa kinena (mavuzi).
8- Kunyofoa kikwapa.
9- Kuosha vifupachanda na sehemu ambazo uchafu hujikusanya kama kwenye mibano ya vidole, makunjano ya masikio na kadhalika.
10- Kusukutua na kupaliza maji puani.

 
([1])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (153), Muslim (267), na wengineo.
([2])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (262), Abuu Daawuud (7), At-Tirmidhy (16), An-Nasaaiy (1/16) 
([3])  Hasan kwa nyingine: Imetolewa na ….(45), Ibnu Maajah (678), An-Nasaaiy (1/45),  na angalia katika kitabu cha “Al-Mishkaat” (360).
([4])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (266), na Muslim (317).
([5])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Ad-Daaramy (711), Al-Bayhaqy (1/161). Na Al-Albaany katika kitabu cha “Tamaam Al-Minnah” uk. 66 anasema kuwa sanadi yake ni sahihi juu ya sharti ya Mashaykh wawili.
([6])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (228), Muslim (333) na wengineo. 
([7])  Hii inawezekana ikawa ni Hadiyth Marfu’u kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Inawezekana pia ikawa ni kauli ya ‘Urwah bin Az-Zubayr mpokezi wa Hadiyth toka kwa ‘Aaishah. Aliwajibu kwa kauli hiyo wanawake waliomuuliza kuhusu suala hilo kama ilivyo kwa Ad-Daaramy (1/199).
([8])  Surat Al-Baqarah : 185.
([9]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (2), Ibn Maajah (335) na tamko ni lake.
([10]) Angalia katika vitabu cha “Al-Majmu’i” (2/87), Al-Mughniy (1/227) na Al-Awsat (1/342).
([11]) Surat Al-Hajj : 32.
([12]) Hadiyth dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud, At-Tirmidhy, An-Nasaaiy na Ibnu Maajah. Al-Albaaniy amesema kuwa ni dhaifu.
([13])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (5872), Muslim (2092) na wengineo.
([14]) Al-Albaaniy amesema kuwa ni Hadiyth Sahihi. Imetolewa na At-Tirmidhiy na Ibnu Maajah. Angalia kitabu cha “Swahyhu Al-Jaam’i” (3611).
([15]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (142) na Muslim (375).
([16]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (394), Muslim (264) na wengineo.
([17]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (145), Muslim (266) na wengineo.
([18]) An-Nawawy amezitaja katika kitabu cha “Al-Majmu’i” (2/82). Al-Haafidh ameziongeza kauli nyingine  tatu katika kitabu cha “Al-Fath (1/296).
([19]) Al-Muhallaa (1/194), Al-Fath (1/296), Al-Awsat (1/334), As-Saylu Al-Jarraar (l/69) na Al-Ikhtiyaaraat Al-Fiqhiyyat (8).
([20])  Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (370), Abuu Daawuud (16), At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy (1/15) na Ibn Maajah (353).
([21]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (68) na Abuu Daawuud (25).
([22]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na An-Nasaaiy (1/130) na Abuu Daawuud (28).
([23]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (281) na An-Nasaaiy (1/34).
([24]) Hadiyth Nzuri kwa nyingine: Imetolewa na At-Tirmidhiy (7), Abuu Daawuud (30), na Ahmad (6/155).
([25]) Hadiyth Nzuri kwa nyingine: Imetolewa na At-Tirmidhiy (12), An-Nasaaiy (1/26), Ibn Maajah (307) na Ahmad (6/136).
([26]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (226), Muslim (273) na wengineo.
([27]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (22), An-Nasaaiy (1/27), Ibn Maajah (346) na Ahmad (4/196).
([28]) Hadiyth Dhaifu: Imetolewa na Ibn Maajah (308), Al-Bayhaqy (1/202) na Al-Haakim (1/185). At-Tirmidhiy amesema kuwa ni Hadiyth Mu’allaq na Dhaifu (1/67).
([29]) Hadiyth Munkar: Imetolewa na Al-Bukhaariy katika kitabu cha “At-Taariykh” (496), Al-Bazaaz (1/547). Al-Bukhaariy na At-Tirmidhiy wamesema kuwa ni Hadiyth Munkar. Lakini imethibiti kwa kauli ya Ibn Mas’ud.
([30]) “Al-Majmu’u (2/98) na Al-Awsat (1/333).
([31]) “Nayl Al-Awtaar” (1/109) na “’Umdat Al-Qaar’i” cha Al-‘Ayniy (22/45).
([32]) “Faydh Al-Qadyr” cha Al-Minaawy (1/38).
([33]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (5891) na Muslim (257).
([34]) Hadiyth Hasan: Imetolewa na Muslim (261), Abuu Daawuud (52), At-Tirmidhiy (2906), An-Nasaaiy (8/126) na Ibn Maajah (293).

0 Comments