014-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kutahiri

Maana na hukumu yake

Kutahiriwa (katika Lugha ya Kiarabu) ni kisoukomo cha kitenzi  ,(ختن)yaani amekata. Na kutahiriwa ni ima kukata ngozi inayofunika kichwa cha uume, au kukata ngozi iliyopo upande wa juu wa utupu wa mwanamke (ukeketaji) ([1]).

Ama kwa upande wa hukumu yake, Maulamaa wana rai tatu:

1- Kwamba ni lazima kwa mwanamume na mwanamke.
2- Kwamba ni jambo linalopendeza kwao.
3- Kwamba ni wajibu kwa mwanamume lakini kwa mwanamke inapendeza.

Ibn Qudaamah katika kitabu cha “Al Mughny” (1/85) anasema: “Ama kutahiriwa, hilo ni wajibu kwa wanaume na ni ukirimio kwa upande wa haki ya wanawake na wala si lazima kwao. Hii ndio kauli ya Maulamaa wengi….”

Naye An-Nawawy katika kitabu cha “Al Majmu’i” (1/301) anasema: “Na madhehebu sahihi kwa matini ya Ash-Shaafi’iy na yaliyokubaliwa kwa sauti moja na Jamhuri ya Maulamaa ni kuwa kutahiriwa ni wajibu kwa wanaume na wanawake…”

Ninasema (Abuu Maalik): “Ama kutahiriwa mwanamume, inavyoonekana ni kuwa jambo hilo ni la lazima kutokana na dalili zifuatazo:

1- Kwamba hiyo ni mila ya Ibraahiym (‘Alayhis Salaam). Kwani imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 أختتن إبراهيم خليل الرحمن بعد ما أتت عليه ثمانون سنة                       
((Kipenzi cha Ar-Rahmaan Ibraahiym alitahiriwa baada ya kufikisha miaka 80)).([2])

Na Allaah Mtukufu Anamwambia Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

ثم أوحينا إليك أن اتبع ملة إبراهيم حنيفا                                            
« Kisha Tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibraahiym mwongofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina ».([3])

2- Ni kwa yale yaliyopokelewa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia mtu mmoja aliyesilimu:

ألق عنك شعر الكفر واختتن                                                  
 ((Jitakase na taka za ukafiri na utahiriwe)) ([4])

3- Kwamba kutahiriwa ni katika ibada za Waislamu na ni sifa yao maalumu inayowapambanua na Mayahudi na Wakristo.

4- Ni kwamba kutahiri ni kukata sehemu ya mwili, na hili ni haramu, na la haramu halihalalishwi ila kwa lile la wajibu.

Haya ndio madhehebu ya Maalik, Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Lakini Maalik amelichukulia msimamo mkali na kusema: “Mtu ambaye hakutahiriwa, basi hafai kuwa Imaam na ushahidi wake haukubaliwi”. Na Maulamaa wengi wamenukulu toka kwa Maalik akisema kuwa hilo ni Sunnah. Lakini kuacha Sunnah kwa mujibu wa Maalik, ni dhambi.

Ama kwa mwanamke, bila shaka sheria ya kutahiriwa imewekwa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

إذا التقى الختانان وجب الغسل                                            
((Zinapokutana tupu mbili zilizotahiriwa, ni lazima kukoga))  ([5])

Na “Al-Khitaanaan” ni mahala pa kukatwa katika uume wa kijana na utupu wa kijakazi. Na hii yaonyesha kuwa wasichana walikuwa wakikeketwa.

Kuna Hadiyth zilizopokelewa juu ya wajibu wa kumkeketa mwanamke. Hadiyth zote hizo zimekosolewa. Kati ya Hadiyth hizo ni ile ya Ummu Atwiyya aliyesema kwamba kuna mwanamke fulani aliyekuwa akikeketa mjini Madiynah. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

لا تنهكي، فإن ذلك أحظى للمرأة وأحب إلى البعل                                 
((Usikate sana, kwani hilo linampa hadhi zaidi mwanamke na linapendeza sana kwa mume)) ([6])

Na katika riwaya:

إذا خفضت فأشمي ولا تنهكي، فإنه أنضر للوجه، وأحظى عند الزوج                 
((Unapokata, basi bakisha kidogo wala usikate chote, kwani hilo linapendeza zaidi usoni na linapewa hadhi zaidi na mume)) .([7])
Hadiyth hizi sanadi yake ni dhaifu ingawa Mwanachuoni Mkubwa Al-Albaaniy amesema kuwa ni sahihi katika “As-Silisilat As-Swahiyha” (722).

Na kama mambo ni hivi, basi mwenye kusema anaweza kusema: “Kutahiri ni wajibu kwa wanawake kama ilivyo kwa wanaume ingawa Hadiyth hizi ni dhaifu. Kwani asili ni kuwa wote wawili wako sawa katika hukumu isipokuwa kama kuna dalili ya kuwapambanua. Na dalili hiyo haipo.

Na mwingine anaweza kusema: “Bali hilo ni jambo linalopendeza, na ni ukirimio kwa mwanamke, lakini si wajibu. Na picha ya kupambanua([8]) hapa kati ya mwanamume na mwanamke ni kuwa kutahiriwa kwa upande wa mwanamume kuna maslaha kwake yanayofungamana na utwahara ambao ni moja kati ya sharti za Swalah. Kwani endapo kama govi hilo litabakia, basi mkojo hubaki na hujikusanya ndani.

Ama kwa upande wa mwanamke, faida kubwa kwake ni kuwa kukeketa humpunguzia matamanio yake. Na hii ni kutafuta ukamilifu na wala si katika mlango wa kuondosha adha.

Ninasema (Abuu Maalik): “Kukeketa wanawake kunazungukia kati ya mustahabu na wajibu. Na imepokelewa toka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

الختان سنة للرجال مكرمة للنساء                                           
((Kutahiriwa ni Sunnah kwa wanaume na ukirimio kwa wanawake)).

Lakini Hadiyth hii ni dhaifu. Na lau kama ingelikuwa ni sahihi, basi ingemaliza mzozo. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.

 
([1])   Tazama kitabu cha Ibn Al-Qayyim cha “Tuhfat Al-Mawduwd” (Uk. 106, 132), na kitabu cha “Al-Majmuu’i” cha Imaam Ah-Nawawy (1/301).
([2])   Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (6298) na Muslim (370).
([3])   Surat An-Nahl : 123.
([4])   Al-Albaaniy ameifanya kuwa ni Hadiyth Hasan kwa vishuhudilio vyake. Imetolewa na Abuu Daawuud (356) na Al-Bayhaqiy (1/172). Katika sanadi yake kuna wapokezi wawili wasiojulikana pamoja na mkatiko. Lakini Al-Albaaniy amesema kuwa ni Hadiyth Hasan kwa vishuhudilio vyake ambavyo amevinasibishia katika Sahihi ya Abuu Daawuud (383). Na katika “Al-Irwa’i” (79), mimi sikuiona. An-Nawawiy na Ash-Shawkaaniy wamesema kuwa ni dhaifu.
([5])   Hadiyth Sahihi: Ibn Maajah ameitoa kwa tamko hili (611). Na katika sahihi mbili, imekuja kwa tamko la ((Na utupu kuugusa utupu, hakika imepasa kuoga)).
([6])   Hadiyth dhaifu: Imetolewa na Abuu Daawuud (5271). Amesema kuwa ni dhaifu.
([7])   Hadiyth Munkar: Imetolewa na Al Khatiyb katika kitabu cha “At-Taariykh” (5/327). Tazama pia “Jaami’ul Ahkaam An-Nisaa’i” (1/19).
([8])   Muono huu ameuelezea Mwanachuoni Mkubwa Ibn ‘Uthaymiyn (Allaah Amrehemu) kama ilivyo katika “Al-Mumti’i” (1/134).

0 Comments