015-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Mlango Wa Pili -Twahara Ya Kihukumu

Aina za maji
 
Maji juu ya kutofautiana sampuli zake, hayatoki nje ya aina mbili:
 
1- Maji Mutwlaq (Maji Twahara)
 
Ni yale yenye kusalia katika asili ya maumbile yake. Na haya ndiyo yale yaliyochimbuka toka ardhini au yaliyoteremka toka mbinguni. Allaah Mtukufu Anasema:
 
«وينزل عليكم من السماء ماء ليطهركم به»                                  
«..Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni ili kukusafisheni kwayo»([1])
 
Katika aina hii, yanaingia maji ya mito, theluji, umande, na visima, hata kama yatabadilika kwa kukaa sana au kwa kuchanganyika na kitu twahara ambacho ni vigumu kuepukana nacho. Vile vile maji ya bahari, kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa kuhusu maji ya bahari alisema:
 
((هو الطهور ماؤه الحل ميتته))                                   
((Maji yake ni twahara na mfu yake ni halali)).([2])
 
Maji haya yote inafaa kutawadhia na kuogea bila hitilafu yoyote kati ya Maulamaa na hata kamayatachanganyika kidogo na kitu twahara lakini yakaendelea kubebajina la maji. Katika Hadiyth ya Ummu Haani ni kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alioga yeye na Maymunah katika kijibeseni kimoja chenye athari ya kinyunya.([3]) Na (ushahidi mwengine ni) kwa amri ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam kwa wanawake waliomwosha binti yake Zaynab alipowaambia:
 
((Mwosheni mara tatu; kwa maji na mkunazi, na fanyeni osho la mwisho kwa kafuri)).([4])
 
Ama kama yatachanganyika na kitu twahara kikaondosha jina la maji na kuwa jina jingine kamachai kwa mfano, basi haijuzu kujitwaharisha kwayo. Aidha, haijuzu kujitwaharisha hadathi na vimiminika vilivyokamuliwa toka vitu twahara  kama maji ya waridi na mfano wake, kwani hayo si maji halisi.
 
Ibnu Al-Mundhir([5]) anasema: “Maulamaa wote tuliohifadhi kauli zao, wamekubaliana kwa kauli moja kuwa wudhuu haufai kwa maji ya waridi, maji ya miti na maji ya m’asfara. Na haifai kujitwaharisha ila kwa maji yenye kuitwa maji..”
 
 
2- Maji yaliyonajisika
 
Ni maji yaliyochanganyika na najisi ikaathiri moja kati ya sifa zake kwa kubadilisha harufu yake, au rangi yake au ladha yake, kwa namna ambayo mtu akiyatumia, ataona kwa yakini kwamba anatumia najisi (badala ya maji).
 
Maji haya haijuzu kutawadhia kwa vile ni najisi katika kiini chake.
 
 
 
KUTAWADHA KWA MAJI YANAYOCHURUZIKA TOKA KWENYE VIUNGO VYA WUDHUU
 
Maji yanayochuruzika toka kwenye viungo vya mwenye kutawadha na mfano wake, huitwa maji yaliyotumika. Na bila shaka Maulamaa wamehitalafiana kuhusu maji hayo kama yanapoteza sifa ya kuwa ni yenye kutwaharisha au la. 
 
Rai yenye nguvu ni kuwa maji hayo yanabakia ni yenye kutwaharisha madhali hayajapoteza jina la maji mutwlaq na wala hayajachanganyika na najisi ikaathiri katika moja ya sifa zake.
 
Haya ndio madhehebu ya ‘Aliy bin Abi Twaalib, Ibn ‘Umar, Abuu Umaama na watangu wema wengi. Ni mashuhuri pia katika madhehebu ya Maalik. Aidha, ni moja kati ya riwaya mbili zilizopokelewa toka kwa Ash-Shaafi’iy na Ahmad. Pia ni madhehebu ya Ibn Hazm na Ibn Al-Mundhir. Mwelekeo huu pia umechaguliwa na Shaykh wa Uislamu (Ibnu Taymiyah).([6]) Kauli hii inatiliwa nguvu na dalili zifuatazo:
 
1- Kwamba asili ni kuwa maji ni twahara wala hayanajisiwi na chochote. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
 
((الماء طهور لا ينجسه شيئ))                                        
((Maji ni twahara, hayanajisiwi na chochote))([7])
 
Isipokuwa kama sifa yake moja itabadilika au yakapoteza jina la maji mutwlaq kwa kuchanganyika na kitu twahara.
 
2- Imethibiti kwamba Maswahaba walikuwa wakitumia mabaki ya maji aliyotawadhia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). (Hii ni kwa dalili zifuatazo):
 
(a) Imepokelewa toka kwa Abuu Juhayfah akisema:
“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitutokea mchana wa jua kali, akaja na maji ya kutawadhia kisha akatawadha. Hapo watu wakaanza kuchukua mabaki ya maji aliyotawadhia na kujipangusa nayo”.([8])
 
Al-Haafidh katika “Al-Fat-h” (1/353) anasema: “Inawezekana kuwa walichukua yale yaliyochuruzika toka kwenye viungo vya wudhuu vya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni dalili wazi kuwa maji yaliyotumika ni twahara.
 
(b) Na katika Hadiyth ya Al-Masuur bin Makhramah: “…na anapotawadha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), walikuwa wakikaribia kupigana kugombea maji aliyotawadhia”.([9])
 
(c) Imepokelewa na Abuu Musa Al-Ash’ary kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliagizia bilauri yenye maji. Akaoshea mikono yake na uso wake humo na akatema. Kisha akamwambia yeye (Abuu Muusa) na Bilaal:
 
 ((إشربا منه، وأفرغا على وجوهكما ونحوركما))                               
((Kunyweni humo na yamalizieni kwenye nyuso zenu na shingo zenu)).([10])  
 
3- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar akisema: “Katika enzi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), wanaume na wanawake walikuwa wakitawadha wote pamoja”.([11])
 
Na katika riwaya: “Katika enzi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), tulikuwa sisi na wanawake tukitawadha katika chombo kimoja tukiingiza mikono yetu ndani”.
 
4- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiogea kwa mabaki (ya maji) ya Maymunah.([12])
 
5- Imepokelewa toka kwa Al-Rubayyi’i bin Mu’awwadh kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipangusa kichwa chake kwa mabaki ya maji yaliyokuwa mkononi mwake.([13])
 
6- Ibn Al-Mundhir katika “Al-Awswat” (1/288) amesema: “Na katika ijmai ya Maulamaa ni kwamba matonetone yaliyobakia katika viungo vya mwenye kutawadha au mwenye kuoga, na yale maji yaliyotona kwenye nguo zao, ni twahara. Na hii ni dalili kuwa maji yaliyotumika ni twahara. Nakama ni twahara, basi hakuna maana kuzuia kutawadhia maji hayo bila ya hoja wanayoirejelea wale wenye rai kinyume na kauli…”.
 
Na wakati huo huo, mjumuiko wa Maulamaa umesema: “Haijuzu kutawadha kwa maji yaliyotumika”. Yamesemwa haya na Maalik, Al-Awzaa’iy, Ash-Shaafi’iy – katika riwaya moja kati ya mbili – na wenye rai.([14])
 
Maulamaa hawa hawana dalili yakinifu za kuridhisha. Mwenye kutaka, azirejee katika rejea zilizotajwa.
 
 
 
INAJUZU KWA MWANAUME KUOGA KWA MABAKI YA MWANAMKE
 
Maulamaa wana mielekeo miwili katika hukumu ya mtu kujitwaharisha kwa maji yaliyobakia baada ya mwanamke kutawadhia au kuogea.
 
Mwelekeo wa kwanza:
Haijuzu kwa mwanaume kujitwaharisha kwa mabaki ya mwanamke. Na haya ni madhehebu ya Ibn ‘Umar, Abdullaah bin Sarjas, mama wa Waumini Juwayriyah bint Al-Haarith, Al-Hasan, Ahmad bin Hanbal, Is-haaq, Ash-Sha’abiy na Daawuud Adh-Dhaahiriy.([15]) Hoja zao ni:
 
1- Yale yaliyopokewa toka kwa Al-Hakam bin ‘Amr kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kutawadhia mabaki ya maji aliyojitwaharishia mwanamke.([16])
 
2- Imepokelewa toka kwa Haamid Al-Humayriy akisema: “Nilikutana na mtu aliyesuhubiana na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) miaka minne kama alivyosuhubiana Abu Hurayrah. Alisema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mwanamke kuogea mabaki ya mwanaume, au mwanaume kuogea mabaki ya mwanamke. (wachote wote kwa pamoja)”.([17])
 
3- Ni yale yaliyopokelewa toka kwa ‘Aliy bin Abi Twaalib aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na ahli wake, walikuwa wakiogea katika chombo kimoja, na wala haogei mmoja wao kwa mabaki ya mwenzake”.([18])
 
 
Mwelekeo wa pili:
 
Inajuzu mtu kujitwaharisha kwa mabaki ya mwanamke. Yamesemwa haya na “Umar, Abu Hurayrah, ‘Abdullah ibn ‘Abbaas, Ibn ‘Umar, Sa’ad bin Abi Waqqaas, mjumuiko wa watangu wema, Abu ‘Ubaud na Ibn Al-Mundhir. Haya pia ndio madhehebu ya Hanafi, Maalik, Ash-Shaafi’iy na riwaya ya Ahmad.([19]) Wametoa hoja kwa yafuatayo:
 
1- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiogea kwa mabaki ya Maymuunah.([20])
 
2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas akisema: “Ahli mmoja wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliogea kwenye beseni. Na Mtume alipokuja alimwambia: Ewe Mtume wa Allaah! Mimi nilikuwa na janaba. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:
 
((إن الماء لا يجنب))                                                 
((Hakika maji hayaathiriwi na janaba)).([21])
 
3- Imepokelewa toka kwa mama wa waumini ‘Aaishah aliyesema: “Nilikuwa mimi na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) tukioga katika chombo kimoja nailhali wote tuna janaba)).[22] Na katika riwaya nyingine: ((…wote tunachota humo)).
 
 
Lenye nguvu:
Lenye kuridhisha na kuondosha shaka katika dalili za mwelekeo wa kwanza ni ile Hadiyth ya mtu aliyesuhubiana na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) miaka minne (ingawa Al-Bayhaqiy ameitia ila) pamoja na dalili zote za mwelekeo wa pili. Na dalili hizo zinaweza kuoanishwa kwa moja ya mawili:
 
1- Hadiyth zinazokataza zichukuliwe juu ya maji yanayochuruzika toka kwenye viungo, na Hadiyth za kujuzisha zichukuliwe juu ya maji yenye kubaki ndani ya chombo. Hivi ndivyo Al-Khatwabiy alivyooanisha.
 
2- Katazo lichukuliwe juu ya ukaraha pamoja na kujuzu yote mawili.
Ninasema (Abuu Maalik): “Na huenda hili la pili ndilo bora zaidi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
 
([1]) Surat Al-Anfaal: 11.
([2]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (83), At-Tirmidhiy (69), An-Nasaaiy (1/176) na Ibn Maajah (386).
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na An-Nasaaiy (240) na Ibn Maajah (378).
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (1253) na Muslim (939).
([5]) Al-Mughny (1/11) na Al-Muhallaa (1/199).
([6]) “Al-Mughny” (1/31), “Al-Majmuu’i” (1/205), “Al-Muhallaa” (1/183), “Majmu’u Al-Fataawaa” (20/519) na “Al-Awsatw” (1/285).
([7]) Hadiyth Hasan: Imetolewa na Abuu Daawuud (266), At-Tirmidhiy (66) na An-Nasaaiy (1/174).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (187).
([9]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (189).
([10]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (188).
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (193), Abuu Daawuud (79), An-Nasaaiy (1/57) na Ibn Maajah (381). Riwaya baada yake ni ya Abuu Daawuud kwa sanadi sahihi.
([12]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (323). Katika Sahihi mbili imekuja kwa tamko la “Walikuwa wakiogea katika chombo kimoja”.
([13]) Hadiyth Hasan: Imetolewa na Abuu Daawuud (130) na Ad-Daaraqutwniy (1/87).
([14]) “Al-Istidhkaar” (1/253), “Attamhiyd” (4/43), “Al-Mughny” (1/19), “Al-Awswat” (1/285).
([15])“Al-Awswat” (1/292) na “Al-Mughny” (1/282).
([16]) Maulamaa wameitia ila. Imetolewa na Abuu Daawuud (82), At-Tirmidhiy (64), An-Nasaaiy (1/179), Ibn Maajah (373) na Ahmad (5/66). Al-Bukhaariy, Ad-Daarqutwniy na An-Nawawy wameitia ila. Ama Ibn Hajar na Al-Albaaniy, wao wamesema ni sahihi katika “Al-Irwaa”i (1/43).
 ([17]) Isnadi yake ni sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (81), An-Nasaaiy (1/130) na Al-Bayhaqiy (1/190).
([18]) Hadiyth dhaifu: Imetolewa na Ibn Maajah (1/133).
([19])“Muswannaf” ya Abdur-Razzaak (1/110), Ibn Abi Shaybah (1/38), “Al-Awswat” (1/297), “Attahuwr” cha Abu ‘Ubayd (236), “Al-Mabsutw” (1/61), “Al-Ummu” (1/8) na “Al-Mughny” (1/283).
([20]) Hadiyth Sahihi: imekwishagusiwa.
([21]) Imetolewa na Abuu Daawuud (68), At-Tirmidhiy (65), An-Nasaaiy (1/173) na Ibn Maajah (370). Baadhi ya Maulamaa wameitia ila kwa riwaya ya Simaak toka kwa ‘Ikrimah. Riwaya hii imekorogeka. Lakini Al-Haafidh katika kitabu cha “Al-Fat-h” amewajibu kwamba Shu’ubah amepokea toka kwake, na yeye hapokei toka kwa Mashaykh zake isipokuwa Hadiyth sahihi. Na Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
[22] Hadiyth sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (299) na Muslim (321).

0 Comments