016-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: WUDHUU - Fasili Yake Na Dalili Za Ushari'ah Wake

Wudhuu katika lugha ya kawaida, ni neno lenye asili ya Kiarabu(الوضاءة)  ambalo lina maana ya usafi na mng’aro. Na neno (الوضوءُ) kwa “dhwamma” juu ya “waw” (al-wudhu-u), ni kitendo chenyewe cha kuwatadha. Ama kwa fat-ha(الوضوءَ)  (al-wadhu-a), ni yale maji ya kutawadhia. Pia ni kisoukomo au lugha mbili.([1])

Ama kiistilahi (kitaaluma), ni kutumia maji kwenye viungo maalumu; uso, mikono miwili, kichwa na miguu miwili, ili kuondosha kwayo kinachozuia kuswali na mfano wake.


Ushari'ah wake umeashiriwa na Qur-aan, Hadiyth na Ijma’a.

Ama katika Qur-aan, Allaah Mtukufu Anasema:

يآ أيها الذين آمنوا إذا قمتم إلى الصلاة فاغسلوا وجوهكم وأيديكم الى المرافق وامسحوا برؤوسكم وأرجلكم إلى الكعبين                                                                                                                     
«Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalah, basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni»([2])

Ama katika Hadiyth, tunakuta kama vile:

1- Hadiyth ya Abuu Hurayrah (Radhi za Allaah ziwe juu yake) aliyesema: “Amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((لا تقبل صلاة أحدكم إذا أحدث حتى يتوضأ))                                                                          

((Haikubaliwi Swalah ya yeyote kati yenu anapokuwa na hadathi mpaka atawadhe)).([3])

2- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Umar (Radhi za Allaah ziwe juu yake na baba yake) akisema: “Hakika nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

 ((لا يقبل الله صلاة بغير طهور، ولا صدقة من غلول))                                                           
((Allaah Haikubali Swalah bila twahara, wala SwadaqaH inayotokana na mali haramu)).([4])

3- Imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhi za Allaah ziwe juu yake na baba yake) akisema: “Amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((إنما أمرت بالوضوء إذا قمت إلى الصلاة))                                                                             


((Hakika mimi nimeamrishwa kutawadha ninaposimama kuswali)).([5])

4- Imepokelewa toka kwa Abuu Sa’iyd kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((مفتاح الصلاة الطهور، وتحريمها التكبير، وتحليلها التسليم))                                                       


((Ufunguo wa Swalah ni kujitwaharisha, uingio wake ni Takbiyr, na utokaji wake ni kusema “Assalaamu ‘alaykum wa RahmatuLlaah”)).([6])

Ama kwa upande wa Ijma’a, ni kuwa Maulamaa wa Ummah wamekubaliana kwamba Swalah haikamiliki ila kwa twahara kama itakuwa ni wepesi kufanya hivyo.([7])


FADHILA ZA WUDHUU

1- Unazingatiwa kama ni nusu ya imani

Ni kama katika Hadiyth ya Abuu Maalik Al-Ash‘ariy (Radhi za Allaah ziwe juu yake) aliyesema: “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((الطهور شطر الايمان))                                                                                                   
((Twahara ni nusu ya imani…..))([8])


2- Hufuta madhambi madogo madogo

(a) Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((إذا توضأ العبد المسلم – أو المؤمن – فغسل وجهه خرج من وجهه كل خطيئة نظر إليها مع قطر الماء – أو مع آخر قطر الماء-، فإذا غسل يديه خرجت من يديه كل خطيئة كان بطشتها يداه مع الماء – أو مع آخر قطر الماء – فإذا غسل رجليه خرجت كل خطيئة مشتها رجلاه مع الماء – أو مع آخر قطر الماء – حتى يخرج نقيا من الذنوب))                                                                                                      

 ((Anapotawadha mja Muislamu – au Muumini – akauosha uso wake, hutoka katika uso huo kila kosa la kuangalia na matone ya maji – au pamoja na tone la mwisho la maji - , na anapoosha mikono yake miwili, hutoka katika mikono hiyo kila kosa ambalo mikono yake imetumilia nguvu na maji – au pamoja na tone la mwisho la maji - , na anapoosha miguu yake miwili, hutoka kila kosa ambalo miguu yake ililiendea na maji – au pamoja na tone la mwisho la maji - , mpaka hutoka akiwa ametakasika kabisa na madhambi.)).([9])

(b) Imepokelewa toka kwa ‘Uthmaan (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:((من توضأ هكذا غفر له ما تقدم من ذنبه، وكانت صلاته ومشيه إلى المسجد نافلة))                             

 ((Mwenye kutawadha hivi, husamehewa dhambi zake zilizopita, na Swalah yake na kwenda kwake msikitini huwa ni thawabu ziada.([10])

Fadhila na thawabu hizi hupatikana kwa uhakika zaidi kwa mwenye kuswali moja kwa moja Swalah ya faradhi au ya Sunnah baada ya kutawadha.


(c) Katika Hadiyth ya ‘Uthmaan (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akizungumzia namna wudhuu wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ulivyo, anasema: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:


((من توضأ مثل وضوئي هذا ثم قام فصلى ركعتين لا يحدث فيهما نفسه، غفر له ما تقدم من ذنبه))          

 ((Mwenye kutawadha kama ninavyotawadha mimi hivi, kisha akasimama akaswali rakaa mbili haizungumzishi nafsi yake ndani yake, ila hufutiwa dhambi zake zilizotangulia)).([11])  


3- Hunyanyua daraja za mja

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:((ألا أدلكم على ما يمحو الله به الخطايا ويرفع به الدرجات؟)) قالوا: بلى يا رسول الله! قال:(( إسباغ الوضوء على المكاره، وكثرة الخطا إلى المساجد، وانتظار الصلاة بعد الصلاة، فذلكم الرباط، فذلكم الرباط، فذلكم الرباط))                                                                


((Je, niwaambieni lile ambalo kwalo Allaah Huyafuta makosa na Hunyanyua kwalo daraja? Wakasema: “Tuambie, ewe Mtume wa Allaah! Akasema: Kutawadha kikamilifukama ipasavyo pamoja na kuwepo uzito na ugumu, kukithirisha kwenda msikitini, kusubiri Swalah baada ya Swalah, basi hayo ni mambo ya mtu kujifunga nayo, basi hayo ni mambo ya mtu kujifunga nayo, basi hayo ni mambo ya mtu kujifunga nayo)).4- Ni njia ya kuelekea peponi

(a) Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhi za Allaah iwe juu yake) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia Bilaal:

(( يا بلال! حدثني بأرجى عمل عملته فى الاسلام، إني سمعت دف نعليك بين يدي في الجنة)). قال : ((ماعملت عملا أرجى عندي من أني لم أتطهر طهورا في ساعة من ليل أو نهار إلا صليت بذلك الطهور ما كتب لي أن أصلى))                                                                                                          


((Ewe Bilaal! Nielezee amali yenye matarajio zaidi uliyoifanya katika Uislamu, kwani mimi nimesikia mtaharuki wa viatu vyako mbele yangu huko peponi)).
Bilaal akasema:
“Sikufanya amali yoyote yenye matarajio makubwa kwangu zaidi ya kuwa sikupata kujitwaharisha wakati wowote wa usiku au mchana, ila huswali kwa twahara hiyo kile nilichoandikiwa kukiswali”.([12])

 (b) Imepokelewa toka kwa ‘Uqbah bin ‘Aamir (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema: “Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((من توضأ فأحسن الوضوء ثم صلى ركعتين، يقبل عليهما بقلبه ووجهه، وجبت له الجنة))                   
  
((Mwenye kutawadha, akaukamilisha vyema wudhuu wake kama inavyotakikana, kisha akaswali rakaa mbili, akafanya khushui kwa moyo wake na uso wake (viungo vyake), basi ni lazima aingie peponi)).([13])


(5) Utakuwa ni alama itakayoupambanua Ummah huu wakati wa kuipitia hodhi

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikwenda makaburini akasema:
((السلام عليكم دار قوم مؤمنين وإنا- إن شاء الله- بكم عن قريب لاحقون، وددت لو أنا قد رأينا إخواننا)) قالوا: أو لسنا إخوانك يا رسول الله؟ قال: ((أنتم أصحابي، وإخواننا الذين لم يأتوا بعد)) فقالوا: كيف تعرف من لم يأت من أمتك يا رسو ل الله؟ قال: (( أرأيت لو أن رجلا له خيل غر محجلة بين ظهري خيل دهم بهم ألا يعرف خيله؟)) قالوا: بلى يا رسول الله، قال: ((فإنهم يأتون غرا محجلين من الوضوء، وأنا فرطهم على الحوض، ألا ليذادن رجال عن حوضى كما يذاد البعير الضال أناديهم ألا هلم فيقال: إنهم قد بدلوا بعدك، فأقول:  سحقا سحقا))                                                                                                          
   


((Amani iwe juu yenu nyumba ya jamaa ya Waumini. Na sisi bila shaka Apendapo Allaah tutawafuateni hivi karibuni. Ningependa lau sisi tungeliwaona ndugu zetu)). Wakasema: “Ewe Mtume wa Allaah! Je, sisi sio ndugu zako”? Akasema:
((Nyinyi ni Maswahaba zangu. Ama ndugu zangu, hao ni wale ambao hawajakuja bado)).
Wakasema: “Ni vipi utamtambua yule ambaye bado hajakuja katika umati wako ewe Mtume wa Allaah?”. Akasema:
((Niambieni, lau kama mtu ana farasi wenye alama usoni na miguuni wakawa baina ya farasi weusi wasio na mabaka, je hawezi kuwatambua farasi wake?
Wakasema: “Ndio, atawatambua ewe Mtume wa Allaah”. Akasema:
((Basi wao watakuja nailhali wana nuru nyusoni, miguuni na mikononi kutokana na wudhuu. Na mimi ndiye nitakayewatangulia kwenye hodhi. Basi jueni kwa yakini kwamba watu watazuiliwa na kufukuzwa wasije kwenye hodhi langu kamawanavyozuiliwa ngamia wasio na mchunga. Nitawaita: Haya njooni! Patasemwa: “Hakika hao walibadili baada yako”. Nitawaambia: Poteleeni mbali kabisa)). ([14])


(6) Ni nuru kwa mja siku ya Qiyaamah

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhi za Allaah ziwe juu yake) akisema: “Nimemsikia Kipenzi changu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

     ((تبلغ الحلية من المؤمنين حيث يبلغ  الوضوء))  


((Nuru (kipambo) za Waumini zitafikilia pale wudhuu unapofikilia)).([15])


(7) Unafungua kifundo cha shetani

Imepokelewa toka kwa Abuu Hurayrah (Radhi za Allaah ziwe juu yake) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:((يعقد الشيطان على قافية رأس أحدكم إذا هو نام ثلاث عقد يضرب كل عقدة: عليك ليل طويل فارقد، فإن استيقظ فذكر الله انحلت عقدة، فإن توضأ انحلت عقدة، فإن صلى انحلت عقدة، فأصبح نشيطا طيب النفس،   وإلا أصبح خبيث النفس كسلان))                                                                                           


((Anapolala mmoja wenu, shetani hufunga kisogoni mwake vifundo vitatu. Hupiga kila kifundo (kumwambia): Umebakiwa na usiku mrefu, basi lala. Anapoamka akamtaja Allaah, kifundo kimoja hufunguka. Anapotawadha, hufunguka kingine, na anaposwali cha tatu hufunguka. Hapo huwa mchangamfu na mwenye nafsi nzuri, na kama si hivyo, huwa na nafsi mbaya na mvivu)).([16])

 
([1])“Al-Qaamuus” (1/33), “Mukhtaar As-Swihaah” (575) na “Al-Majmuu’i” (1/355).
([2]) Surat Al-Maaidah : 6
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (135), Muslim (225) na wengineo.
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (224).
([5]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na At-Tirmidhiy (1848), Abuu Daawuud (3760) na An-Nasaaiy (1/73). Angalia “Swahiyh Al-Jaami” (2333).
([6]) Hadiyth Hasan kwa nyingine: Imetolewa na At-Tirmidhiy (3), Abuu Daawuud (60) na Ibn Maajah (275). Al-Albaaniy amesema ni sahihi katika kitabu cha “Swahyh Al-Jaami’i” (5761).
([7]) Kitabu cha “Al-Awswat” cha Ibn Al-Mundhir (1/108).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (223) na wengineo.
([9]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (244).
([10]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (229).
([11]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (6433), Muslim (226) na wengineo.
([12]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (1149) na Muslim (2458).
([13]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (234), An-Nasaaiy (1/80) na wengineo.
([14]) Hadyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (234) na An-Nasaaiy (1/80). Pia kitabu cha “Sharhu Muslim”cha Al-Imaam An-Nawawy (3/100).
([15]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (250) na An-Nasaaiy (1/80).
([16]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (1142) na Muslim (776).

0 Comments