018-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Ni Lazima Kusukutua Na Kupaliza

Kusukutua ni kuosha mdomo na kuyazungusha maji ndani yake. Ama kupaliza, ni kuyafikisha maji mpaka ndani ya pua na kuyavuta kwa pumzi hadi mwisho wake. Na kupenga, ni kuyatoa maji puani (kwa mpumuo) baada ya kuyapaliza.
Kusukutua na kupaliza maji, ni mambo ya lazima kwa mujibu wa kauli sahihi zaidi za Maulamaa. Ni kwa dalili zifuatazo:

1- Ni kwamba Allaah Mtukufu Ameamuru kuosha uso kama ilivyotangulia. Na pua na mdomo ni sehemu ya uso, na wala hakuna chenye kuwajibisha kuhusisha nje yake bila ndani yake, kwani vyote hivyo viwili vinaitwa uso katika Lugha ya Kiarabu. Na kama utasema: “Tundu ya pua na pua yenyewe vimeitwa kwa majina haya maalumu, kwa hivyo havihesabiki kuwa ni sehemu ya uso katika Lugha ya Kiarabu.
Tunajibu tukisema: “Vilevile vitefute viwili, kipaji, nje ya pua, nyusi mbili na sehemu nyingine za uso zimepewa majina maalumu, na kwa hivyo haviitwi uso!” ([1])

2- Ni kwamba Allaah Mtukufu Ameamuru kuosha uso kiujumla, na Mtume alilifasiri hilo kwa kulifanya kivitendo na kulifundisha. Akasukutua na akapaliza maji katika kila wudhuu aliotawadha. Na hakuna yeyote aliyenukulu kuwa aliacha kufanya hayo pamoja na kufupishia kwake juu ya kichache chenye kutosheleza . Na ikiwa kitendo chake kimefanyika kwa ajili ya kufuata amri, basi hukumu yake inakuwa ni hukumu ya jambo hilo katika kuhukumia ulazima.([2])

3- Amri ya kupaliza na kupenga imethibiti kutokana na neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

((من توضأ فليستنثر))
 ((Mwenye kutawadha, basi apenge)).

Na katika riwaya nyingine:

  ((  إذا توضا أحدكم فليجعل في أنفه ماء ثم ليستنثر))
  ((Anapotawadha mmoja wenu, basi aingize maji puani mwake kisha apenge)).([3])

(( إذا توضأ أحدكم فليستنشق..))
 ((Anapowatadha mmoja wenu, basi apalize maji puani…))([4])

(( وبالغ في الاستنشاق إلا أن تكون صائما..))
((….na ubalighishe katika kupaliza isipokuwa kama umefunga)).([5])

Shaykh wa Uislamu([6]) anasema: “…Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutoa amri maalumu ya kupaliza, hakumaanishi kwamba ni muhimu zaidi kuliko kusafisha mdomo. Itawezekana vipi nailhali mdomo ndio sehemu tukufu zaidi ya kufanyia dhikri na kusoma, na mara nyingi hubadilika na kuwa na harufu mbaya?! Lakini kinachofananishwa hapa - na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi – ni kuwa, mdomo ulipowekewa usheria wa kupigwa mswaki na jambo hilo likasisitizwa, na pia kuuosha kabla na baada ya kula, itakuwa imejulikana kuwa Allaah Mtukufu Ametoa kipaumbele zaidi cha kuusafisha kinyume na pua ambayo imetajwa kwa ajili ya kubainisha hukumu yake ili isipuuzwe…”.

4- Ni kwamba amri ya kusukutua imekuja vile vile katika Hadiyth nyinginezo zenye uhakika zaidi. Ni kama Hadiyth ya Laqyt bin Swabrah kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:


(( إذا توضأت فمضمض))
((Ukitawadha, sukutua)).([7])

Ninasema: “Na lau kama mtu atasema kwamba dalili za kuwajibisha kusukutua na kupaliza zimebadilishwa na kuelekezwa katika uSunnah kutokana na Hadiyth ya Rifa’a bin Raafi’i katika kisa cha mwenye kuswali vibaya ambaye Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

 (( إنها لا تتم صلاة أحدكم حتى يسبغ الوضوء كما أمره الله تعالى، فيغسل وجهه ويديه إلى المرفقين ويمسح رأسه ورجليه إلى الكعبين...))
((Hakika haikamiliki Swalah ya mmoja wenu mpaka akamilishe wudhuu wake kamaAlivyoamrisha Allaah. Aoshe uso wake na mikono yake miwili hadi kwenye vifundo, na apake kichwa chake, na (aoshe) miguu yake miwili hadi kwenye vifundo…)) ([8])
Hapa hakutaja kusukutua au kupaliza katika hayo ambayo Allaah Amemwamuru, na kwa hivyo amekwenda sambamba na aya tukufu.


FAIDA:
Fahamu kwamba Wanazuoni wamehitalifiana juu ya hukumu ya kusukutua na kupaliza katika wudhuu na kuoga katika kauli nne.([9])

Kauli ya kwanza:
Ni wajibu kusukutua na kupaliza wakati wa kuoga tu, lakini kwa wudhuu haipasi. Yamesemwa haya na Ath-Thawriy, Abu Haniyfah na wengineo.

Kauli ya pili:
Ni Sunnah wakati wa kuoga na kutawadha. Haya yamesemwa na Maalik, Ash-Shaafi’iy, Al-Layth, Al-Awzaa’iy na jama‘ah.

Kauli ya tatu:
Yote mawili ni wajibu wakati wa kuoga na kutawadha. Haya yamesemwa na ‘Atwaa, Ibn Jurayj, Ibn Mubarak, Is-Haaq na riwaya iliyonukuliwa toka kwa Ahmad. Suala hili ni mashuhuri katika madhehebu ya Hanbali.

Kauli ya nne:
Kupaliza ni wajibu wakati wa kuoga na kutawadha, lakini kusukutua ni Sunnah. Yamesemwa haya na Ahmad katika riwaya, Abu ‘Ubayd, Abu Thawr na jopo la Maulamaa wa Hadiyth. Ibn Al-Mundhir ameichagua kauli hii. 


KUOSHA NDEVU NA NYWELE NYINGINEZO ZA USO([10])Ikiwa nywele zilizoota usoni (ndevu, masharubu, kilambamchuzi, kope na nyusi) ni nyingi kiasi ambacho ngozi inakuwa haionekani, basi itatosheleza kuosha juu yake tu. Na kama ngozi inaonekana, basi itabidi ipate maji. Na ikiwa baadhi ni ndogo na nyingine ni nyingi, basi ni lazima ngozi ya nywele ndogo ipate maji na yenye nywele nyingi ioshwe juu tu.
Ama ndevu refu za singa, si lazima kuziosha zile zilizoshuka, bali inatosheleza kuosha zile tu zilizo katika mpaka wa uso, kwa vile kinachokusudiwa katika uso ni ngozi basi. Hii ni kwa mujibu wa kauli ya Abuu Haniyfah na riwaya toka kwa Ahmad.

Ama kwa mujibu wa Ash-Shaafi’iy na madhehebu ya Ahmad, ni lazima kuosha nywele singa vyovyote zitakavyokuwa zimeshuka, kwani nywele hizo zimeota katika mahali pa faradhi, na kwa ajili hiyo zinaingia katika wigo wa vyenye kuonekana. Na rai hii ina nguvu zaidi. Na Allaah Ndiye Mjuzi Zaidi.  

 
([1]) Angalia katika “Nayl Al-Awtwaar” (1/174) chapa ya Al-Jiyl na “Ahkaam Al-Quraan” cha Ibn Al-‘Araby (2/563).
([2]) “Sharh Al-‘Umdah” cha Ibn Taymiyah (1/178) na “At-Tamhiyd” cha Ibn Abdul Barri (4/36).
([3]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (161), Muslim (237) na wengineo.
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (237).
([5]) Hadiyth Sahihi: Itakaririwa mara nyingi.
([6])“Sharhu Al-‘Umdah” (1/179 – 180).
([7]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (140), At-Tirmidhiy (38), An-Nasaaiy (1/66) na Ibn Maajah (448).
([8]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Abuu Daawuud (859), At-Tirmidhiy (302), An-Nasaaiy (2/20, 193), Ibn Maajah (460) na wengineo.
([9])“Hitilafu za Maulamaa” cha Al-Muruuziy (uk. 23-24), “Attamhiyd” (4/34), “Al-Awsat” (1/379), “Attahqiyq” cha Ibn Al-Jawziy (1/143) na “Al-Muhalla” (2/50).
([10])“Sharh Fath Al-Qadiyr” (1/12), “Al- Mughniy” (1/87) na “Al-Majmuu’i” (1/380).

0 Comments