019-Swahiyh Fiqhis-Sunnah - Mlango Wa Twahara: Kuosha mikono miwili hadi kwenye vifundo

2- Kuosha mikono miwili hadi kwenye vifundo

Allaah Mtukufu Anasema:

 .« يا أيها الذين آمنوا إذا قمتم إلى الصلاة فاغسلوا وجوهكم وأيديكم إلى المرافق»
«Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalah, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifundoni »([1])

Maulamaa wamekubaliana kwa sauti moja kuwa ni lazima kuosha mikono miwili wakati wa kutawadha.
  
Fahamu kuwa herufi ya ))  (( إلى katika Neno Lake Allaah Mtukufu:
  «  أيديكم إلى المرافق »

Ina maana ya “pamoja” kama ilivyo katika Neno Lake Allaah Mtukufu:
  « ولا تأكلوا أموالهم إلى أموالكم »
« Na wala msile mali zao pamoja na mali zenu » ([2])

Na Neno Lake:
 « ويزدكم قوة إلى قوتكم »
« Na Atawaongezeeni nguvu pamoja na nguvu zenu » ([3])

Na kwa yaanisho hili, ni lazima vifundo viwili vijumuishwe wakati wa kuosha mikono. Na haya ndio madhehebu ya Jamhuri ya Maulamaa kinyume na baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Maalik.([4])

Msimamo huu wa Jamhuri ya Maulamaa unatiliwa nguvu na kitendo cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Imenukuliwa toka kwa Abuu Hurayrah kwamba yeye alitawadha, akaosha mikono yake hata akaingia katika kipanya, na akaosha miguu yake mpaka akaingia katika miundi miwili. Kisha alisema: “Hivi ndivyo nilivyomwona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akitawadha.([5])

Kisha kaida ‘qaaidah’ (kanuni) inasema: “Lile ambalo wajibu hautimu ila kwalo, basi linakuwa ni wajibu”. Na kuosha mkono kikamilifu hakutojulikana ila kwa kuyazungusha maji kwenye vifundo viwili. ([6])
([1]) Surat Al-Maaidah : 6
([2]) Surat An-Nisaai : 2
([3]) Surat Hud : 52
([4])“Al-Mabsuut” (1/6), “Bidaayat Al-Mujtahid” (1/11), “Al-Majmuu’i” (1/389), “Al-Mughniy” (1/90).
([5]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (246).
([6])“Ikhtiyaarat Ibn Qudaamah” cha Al-Ghaamidiy (1/164).

0 Comments